SIMULIZI: Mkufu wa Malkia wa Goshen

SIMULIZI: Mkufu wa Malkia wa Goshen

Shunie usinifanyie hivyo mama unajua arosto ilivo haifai eee
[emoji16] [emoji16] [emoji16]
Nitakufa mie
Yan huyu mke mwenzio anataka kunifanya nisilale wakati hapa namuwaza Rhoda,,mlozi mpya in the building[emoji23]
Yaan leo nataka kuwaona mkifa nataka kuwa kama steve jaman hivi si mnajua story bila arosto hainogi kabisa mnajua hizi mambo nyie wapenzi wa story na me sijawahi kuwapiga arosto kabisa
 
*MKUFU WA MALKIA II -- 53*

*Simulizi za series*

ILIPOISHIA

Bella na Lucy, aliyetokea nyuma, wakamtazama. Lucy akabinua mdomo wake na kusema:

"Amekwisha."

Bella akamalizia.

"Tufanye upesi!"

ENDELEA

Baada ya muda mchache, ikagundulikana Tattiana amedondoka chini. Hata mfalme akaamshwa na kujuzwa hilo. Ilikuwa bado ni usiku wa manane. Tattiana hakuwa anajielewa, na kama kuna hatua basi za kuelekea kifoni, yeye alikuwa amebakiza moja tu.

Hakuwa anaelewa chochote kile. Hakuwa hata na punje ya fahamu. Alipoteza damu nyingi. Mifupa yake mingi ilikuwa imevunjikavunjika. Hata kama angelipona, basi kamwe asingeliweza kurejea kwenye hali yake ya kawaida.

Angeweza kupooza mwili ama kuwa mlemavu wa kudumu.

Mfalme akachanganyikiwa sana. Ni nini kilitokea? Tattiana alifika huko kufanya nini? Ilikuwaje akaangukia chini? Vijakazi wote pamoja na walinzi wakaitwa na kuulizwa kilichotokea.

Nani alimwona Tattiana na mpaka anadondoka walikuwa wapi?

Kukawa kimya. Hakuna aliyesema jambo. Kila mtu aliogopa kwani kama ingebainika anahusika, angechukuliwa hatua kali maana mfalme anampenda sana Tattiana.

Lakini baadae, baada ya kubanwa sana wakitishiwa kufungwa maisha yao yote, Bella kwa uoga akasema huwa anamwona Tattiana majira ya usiku akizungukazunguka.

"Sijui huwa anafanya nini," akaeleza. "Ila si mara moja wala mbili."

Kidogo naye mmoja wa wanajeshi walinzi wa kasri akasema pahali pale alipotelezeaTattiana na kudondoka palikuwa pana mafuta. Hicho ndicho kimemwangusha.

Maneno haya yakawa mengi sana lakini ukweli ukabakia kwamba mtu pekee atakayetoa taarifa sahihi ni Tattiana na si mwingine. Mdomo wake ndio pekee utakaoeleza ukweli wa mambo.

Lakini sio leo wala kesho. Mwili wake ulikuwa umekusanyiwa kitandani daktari akihangaika kuokoa uhai wake.

"Itachukua muda mrefu sana kurejea. Amedondoka vibaya na kuathiri uti wake wa mgongo," daktari alieleza.

Mfalme akamsihi arejeshe uhai wa mwanamke huyo kwa namna yoyote ile. Hatamwelewa kabisa mwanamke huyo akifariki. Yupo tayari kwa gharama yoyote na chochote atakachohitaji atampatia.

"Umenielewa?" Mfalme akamkaba daktari.

"Ndio, nimekuelewa," daktari akasema kwa hofu.

Baadae taarifa zikasambaa himaya nzima. Melkizedek na mkewe wakashtushwa mno na habari hizo hata wakafunga safari upesi kwenda kumwona mtoto wao.

Mama alipomwona akalia sana. Akamuuliza mwanaye aliyekuwa hamsikii, nini ilikuwa shida? Kwanini amejiingiza matatizoni hivyo?

Kwa uchungu aliokuwa nao, hakutaka kurudi na mumewe nyumbani. Alitaka kubaki na mwanaye hapo kasrini anapotibiwa. Kwa mfalme hakuwa na shaka, akaona kheri.

Mama huyo akaketi kandokando ya mwanae akimtazama, machozi yanambubujika.

"Nitahakikisha kila kitu kinakuwa sawa," mfalme alimtoa hofu Melkizedek. "Nitampatia kila huduma na ulinzi wa kutosha. Usijali."

"Nashukuru sana," Melkizedek akampatia mkono mfalme. "Natumai mkononi mwako yupo salama."

Mfalme akamsindikiza mpaka nje, bwana huyo akaenda zake.

**

"Sasa tunafanyaje?" Aliuliza Bella akimtazama Lucy aliyekuwa amejilaza kitandani. Walikuwa ndani ya chumba peke yao. Wakati Lucy akiwa amejilaza miguu ipo chini, Bella alikuwa ameketi kitako.

Wote walionekana kutingwa na mawazo. Hawakuwa na raha. Hawakuwa na amani.

"Mimi nilidhani atakufa!" Akalalama Lucy. "Mwanamke ana roho ngumu yule. Kudondoka kote huko!"

"Tunafanyaje sasa?" Bella akarudia swali lake ambalo halikupatiwa jibu. Alikuwa ana hofu mpaka anatetemeka. "Akiamka si atatutaja?" Akaendelea kulonga. "Na akitutaja si ndo mwisho wetu huo!"

"Usijali," Lucy akampoza. "Hawezi amka yule. Hata akiamka atakuwa bubu, si kwa namna alivyodondoka."

"Mmh," Bella akaguna. "Unadhani itakuwa hivyo? Mfalme ameweka madaktari wote nguli ndani ya himaya wamtimbu mtu mmoja. Unajua hilo?"

"Najua!" Lucy akajibu akinyanyuka. "Lakini kifo kamwe hakizuiliki hata uwe na madaktari wangapi. Kikija kinakuja tu. Cha muhimu ni kumtazama kwa jicho makini. Tukimwona anapata ahueni, ama anaelekea kupona, basi tunammaliza!"

"Utaweza kwa namna anavyolindwa vile?" Bella alikuwa na shaka.

"Inawezekana!" Lucy akajibu akibinua mdomo. "Hakuna lisilowezekana, kumbuka tupo chini ya paa moja."

Kisha akauliza:

"Zile maiti umezihifadhi vizuri?"

"Za wale maaskari?" Bella akauliza.

"Ndio, kwani kuna zingine?" Lucy akabweka.

"Nimezihifadhi pazuri hamna shaka," Bella akachonga.

"Sasa inabidi tumalizie lile zoezi letu," Lucy akahusia. "Ila itabidi tutulie kidogo kwani kwa sasa ulinzi utakuwa mkubwa sana."

**

Baada ya kutembea kwa muda mrefu, Waheed akawaasa wapumzike angalau kidogo wavute pumzi. Wakaketi na kunywa maji kulainisha makoo yao.

Kulikuwa na ka giza hafifu kama vile jioni. Walitulia hapo kana kwamba wapo msibani. Hakuna mtu aliyekuwa anamwongelesha mwenzake wala kuongea. Hawakuwa na furaha. Haikuhitaji kusoma vitabu kulijua hilo.

"Tutadumu humu mpaka siku gani?" Fluffy akauvunja ukimya. Aliuliza akiwa amejikunyata kana kwamba anasikia baridi kali.

"Siku tatu," Waheed akajibu. "Vipi kuna tatizo?" Kisha akauliza.

Fluffy akamtazama kama mhaba wa matumaini, alafu akasema:

"Nataka kutoka nje."

Wenzake wote wakamtazama.

"Nataka kwenda nyumbani na kuachana na haya yote," akaongezea. Na punde macho yake yakawa mekundu kama bendera. Mara yakavujisha maji.

"Usilie, Fluffy," Seth akamuasa akimshika bega. "Yote yanakaribia kwisha. Tumeshamaliza."

"Sidhani," Fluffy akajibu akivuta makamasi. "Nimechoshwa na haya. Nini maana ya safari hii kama tunatoka tofauti na tuliongia? Hata tutakapopata hicho tunachokihitaji, nini itakuwa furaha yake?"

Maneno haya yakamgusa kila mmoja isipokuwa Waheed. Alikuwa anamtazama mwanamke huyo kwa mapuuzo akitamani hata kumziba mdomo.

"Tumehangaika mno kufika hapa, alafu tunakuja kupotezea hapa! Yale yote ya mwanzoni yanakuwa bure? Tuliyafanya yanini?" Fluffy aliendelea kumwaga maneno.

Alikuwa na uchungu kifuani mwake na kadiri alivyokuwa anaongea ndivyo akawa anazidi kuupata zaidi. Machozi yalizidi kummiminika na ikafikia pahala akawa hawezi hata kuongea.

Kifua kilimbana. Kwikwi zilimzidi na kuubana ulimi. Seth akahangaika kumbembeleza pasipo mafanikio. Ikafikia kipindi sasa Waheed akashindwa kuvumilia.

Akatamani kuropoka, ila akaona hamna haja hiyo. Akajitahidi sana kudumu na hasira yake. Alisimama akawaambia waondoke kwani muda wa kupumzika sasa umekoma. Alifanya hivyo kukatisha yaliyokuwa yanaendelea.

Basi wakanyanyuka na kuendelea na safari yao. Wakatembea kwa umbali wa nusu kilomita kabla hawajakutana na njia panda. Hapo wakasimama kidogo kutafakari.

Lakini ndani ya Waheed kulikuwa na roho ya kidhalimu. Roho ya kinyama.

Katika hali ya mshangao akachomoa kisu chake kiunoni alafu haraka, kufumba na kufumbua, akamkita Alk kifuani, akamkita pia na Fluffy!

Wakadondoka chini wakiugulia maumivu makali. Waheed, pasipo huruma, akamkita pia na Seth aliyekuwa hawezi kujitetea kwa kujaa na majeraha miguuni.

Wote wakalala chini wakiwa wanavuja damu lukuki, kisu cha Waheed kikichuruza kwa kushiba damu.

Waheed akatabasamu. Sasa alikuwa amekamilisha kazi. Akasimama kuwatazama watu hao wakikata roho. Na walipotimiza zoezi hilo, akaendelea na safari yake roho ikiwa nyeupe.

Hakuwahitaji tena watu hao. Hawakuwa na faida tena kwake. Alikopita huko ndipo alipokuwa anawahitaji kama sadaka. Sasa aendako ni kushuka tu. Anaweza maliza mwenyewe.

***
 
*MKUFU WA MALKIA II -- 54*

*Simulizi za series*

ILIPOISHIA

Waheed akatabasamu. Sasa alikuwa amekamilisha kazi. Akasimama kuwatazama watu hao wakikata roho. Na walipotimiza zoezi hilo, akaendelea na safari yake roho ikiwa nyeupe.

Hakuwahitaji tena watu hao. Hawakuwa na faida tena kwake. Alikopita huko ndipo alipokuwa anawahitaji kama sadaka. Sasa aendako ni kushuka tu. Anaweza maliza mwenyewe.

ENDELEA

Akatembea akiwa ana furaha. Anajihisi mwepesi akifahamu fika, safari yake inakaribia kukoma na hivyo basi ataanza kula matunda ambayo alikuwa anayatamani kwa muda mrefu.

Matunda ambayo alikuwa anayapigia mahesabu tangu alipokuwa kijana.

Nani hataki madaraka bana? Waheed alijiona kichwani mwake akiwa mtu mkubwa mno. Mtu anayesikilizwa na kuheshimiwa. Lakini zaidi mtu anayeogopeka!

Alijiona akiwa ana ubavu, amezungukwa na dhahabu na vitu vya thamani. Akiwa tishio mpaka himaya zingine.

Mate yakamtoka.

Hatimaye ndoto yake hii ilikuwa inaelekea kutimia. Ndoto aliyoivutia subra kwa miaka nemda rudi. Sasa atakapoitia kofia hiyo mikononi kila mtu atajua kumbe hakuwa Waheed.

Kumbe hakuwa punguani bali mtu anayejielewa. Mtu wa maana na mwenye malengo yake!

Alilenga haswa kuuthibitishia ulimwengu juu ya hilo ...

**

"Umekunywa chai nlokuandalia?" Aliuliza bibi akimtazama kwa macho ya huruma.

"Hapana, sijanywa," akajibu kwa sauti ya chini. "Sijiskii kula chochote kile."

Bibi akashusha pumzi alafu akaketi na kumtazama mwanamke huyu, mke mkubwa wa Sultan.

Afya yake bado haikuwa imerejea kama hapo awali japo kidogo ilikuwa kheri. Alikuwa amevaa joho pana na uso wake wake haukuwa umeparwa hata kidogo. Ulikuwa umepooza na kunywea.

"Sasa kama usipokula mjukuu wangu, huoni tutarejea kule kule tulipotokea? Sultan hatapendezwa na hili hata kidogo," bibi alisema akimwekea mkono begani. Japo huyu mwanamke hakuwa mjukuu wake, alijitahidi kumwonyesha upendo.

Alitaka arejee katika hali yake. Lakini si kurejea kule kasrini. Lah! Kule kasrini alikuwa anataka mjukuu wake aendelee kukaimu.

"Sultan!" Akasema mke huyu mkubwa kwa uchungu. "Hanijali tena. Hana muda na mimi. Hanipendi tena. Hajui nimefanya yote haya kwasababu yake. Amesahau nimekuwa hivi kwasababu ya pumzi yake!"

"Usiseme hivyo mjukuu wangu," bibi akambembeleza. "Sultan bado anakupenda. Na hata iweje bado wewe utabakia kuwa mkewe daima."

Sultana mkubwa akajikuta akibubujikwa na machozi. Alihisi upanga unachana moyo wake alipokumbuka mahaba ya Sultan. Namna mwanaume huyo alivyokuwa anamkarimu na kumwonyesha kila aina ya upendo.

Leo yupo hai, ila kamsahau kana kwamba kafariki!

"Tangu alipoondoka hapa hajawahi kurudi hata siku moja kunijulia hali. Hata kutuma vijakazi wake kuja kuniulizia, hakuna! Ni upendo gani huo unaousema?" Sultana akalia. Hata bibi akambembeleza pasipo mafanikio.

Lakini pia ndani ya kifua cha bibi huyu moyo ukamchoma na kumsuta. Alijionea haya kwa kila chozi alilodondosha mwanamke huyo kwani mkono wake uliokuwa unambembeleza nao ulikuwa unahusika kumliza.

Alikuwa anajua kila kinachoendelea hapo. Alikuwa anafahamu fika kwanini Sultan hakuwa anakuja kumsalimu mke wake wa kwanza kwa maana alimpatia mjukuu wake dawa.

Dawa ya kumpumbaza Sultan. Dawa ya kutia kwenye pindo la nguo la mwanaume huyo na ya kumwagilia njiani apitapo.

Sultan akamsahau kabisa mkewe wa kwanza. Si tu yeye bali wanawake wote kwake wamekuwa vinywesi.

Baada ya kushindwa kumbembeleza Sultana, bibi akaenda zake chumbani kuupooza moyo wake. Kadiri alivyokuwa anamwona Sultana akilia kwa uchungu, naye akajikuta anaumia. Alijilaza kitandani na kuwaza.

Akawaza.

Akawaza.

Hakuwa na cha kufanya. Akapiga moyo konde Sultana atazoea hali kadiri muda uendavyo, japo alikiri ilikuwa ni ngumu.

Akadumu humo chumbani mpaka akasikia Sultana amenyamaza. Akajishauri kwenda kumuona, lah! Akaona hamna haja, ngoja atulie avutevute muda kwanza. Pengine akienda huko upesi anaweza akamtifua tena kidonda.

**

"Ameenda!" Alisema kijakazi akitoa macho. Alikuwa ni mwanamke aliyejisitiri mwili wake kwa nguo ndefu na kiremba kichwani.

"Ameenda wapi?" Bibi akauliza upesi. Macho yamemtoka pima. Alikuja hapa upesi baada ya kutomwona Sultana huko chumbani. Gauni lake alikuwa amelishikilia mkononi limpe uhuru kunyanyua miguu.

"Sijui ameenda wapi!" Kijakazi akajibu akipandisha mabega."Hakuongea na mtu!"

Bibi akawafuata walinzi langoni, nao akawauliza. Kweli wakakiri kumwona Sultana akiondoka na farasi lakini hawakujua wapi anaenda. Hakuwashirikisha.

Bibi akachanganyikiwa. Hakutamani kusimama wala kukaa. Alihisi Sultana atakuwa ameenda kasrini. Hakuna mahali kwengine zaidi ya huko.

Akang'ata lips.

Hatakiwi kwenda huko. Akasemea kifuani. Huko atatibua mambo!!

**

"Ana miadi na wewe?" Lilikuwa swali la pili. Mlinzi alikuwa anamtazama kana kwamba uji uliokatika, lango akiliweka nyuma ya mgongo wake.

"We mshenzi," Bibi akafoka akimnyooshea kidole. "Acha kunichosha! Sina muda wa kulumbana na wewe hapa. Unajua mimi ni nani kwa Sultan?"

Kabla mlinzi hajajibu kitu, akasukumiwa kando, Bibi akaingia zake ndani upesi. Akiwa ameshikilia gauni lake, akarusha hatua kubwa na kuzama ndani.

Akaangaza. Kulikuwa kimya!!

Punde kijakazi akaja na kumkarimu.

"Sultan na Sultana wake wapo wapi?" Bibi akauliza pasipo kuchelewa. Kijakazi akamwelekeza wapo wamepumzika uani.

Bibi akauliza tena.

"Sultana mkubwa alifika hapa?"

Kijakazi akakataa, hakumwona. Labda vijakazi wengine kwani hapo wapo wengi. Basi Bibi akaamua kwenda zake huko uani kukutana na Sultan na mkewe.

Alipofika akakuta viti vitupu!

Moyo wake ukaanza kumwenda mbio!! Alihisi kuna jambo haliko sawa. Na jambo hili halikuwa dogo kabisa.

Akiwa ametoa macho ya hofu, akaongoza miguu yake upesi kwenda mpaka chumbani kwa Sultan. Akabisha hodi mara tatu. Hakukuwa na majibu.

Akafungua mlango na kuzama ndani. Kweli akathibitisha ile hofu aliyokuwa nayo haikuwa bure. Kwa macho yake alishuhudia maiti mbili kitandani. Moja ya Sultan na nyingine ya Sultana mdogo, yaani mjukuu wake!

Mashuka yalikuwa yamelowana damu. Walikuwa watupu, wameachama na macho yapo wazi.

Bibi akajawa na machozi lukuki lakini akashindwa kupiga kelele za yowe kwani alijikuta kifua kimembana ghafula!

Hakutaka kuamini alichokiona. Wala hakutaka kusadiki kama ni ndoto. Kwake vyote hivyo vilikuwa ni vibaya asivyotaka hata kujaribu kutokea!

Alimtazama mjukuu wake kisha Sultan. Bado miili yao ilikuwa ya moto. Je, muuaji yupo wapi? Haraka akatazama bafuni na kila eneo ndani ya chumba. Hakuona mtu.

Alijawa na hasira mno mpaka akawa anatetemeka. Hakujua angemfanya nini Sultana pindi angemjaza mkononi.

Pasipo kukawia, akatoa taarifa kwa walinzi juu ya mauaji hayo, wote wakaungana kumsaka Sultana mkubwa alipo. Waliamini bado yupo ndani kwa maana hakuonekana akipita tena langoni. Na ilikuwa wazi yeye ndiye alitekeleza mauaji hayo.

Atakapokamatwa, adhabu yake ni kunyongwa mpaka afe!! Kisha abakizwe hapo mpaka kunguru na tai wambakize mifupa.

Wakamsaka huku na kule. Baada ya muda kidogo, mmoja wa walinzi akapaza sauti:

"Yupo huku!"

Haraka wakenda huko. Ilikuwa ni stoo. Wakamkuta Sultana mkubwa akiwa ananing'inia kitanzini!!

Ameacha ujumbe karatasini ukiwa umeandikwa na damu. Karatasi imeshikizwa na ncha ya kisu ukutani.

**
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom