*MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN II -- 50*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Lakini kwa upande wa Waheed yeye ilikuwa kinyume. Kifuani mwake alikuwa ametunza furaha. Moyoni mwake alikuwa na amani.
Alijikuta anatabasamu mara kwa mara kama mwehu.
ENDELEA
Lakini Zura na Malkia wapo wapi? Nafsi zao zilizotumika kama nauli zimeendea wapi? Kujiunga na jeshi la wafu? Ama ndiyo zimeenda kule pasipo na njia tena ya kurudi?
Hakuna mtu anayejua. Kila mtu, hata wewe unajiuliza maswali haya. Lakini pengine ni wazi una matumaini. Bado unadhani watakuwa huko sehemu fulani. Wapo salama na hawajadhurika.
Si wewe peke yako unayewaza hayo. Kwa kuwafanya wapate amani ya moyo, ndivyo hata wakina Seth walivyokuwa wanawaza. Malkia na Zura wapo sehemu. Wapo salama. Wapo hai.
Japokuwa kila kitu kilikuwa kinapingana na mawazo hayo ila bado tu waliamini. Kama wasingeliamini hivyo hata hii safari wasingeendelea nayo.
**
Juu ya madhabahu pakawekwa mishumaa kumi na mbili, idadi ya mwezi katika ulimwengu wa kilozi, kisha kijakazi, mwanaume jabali, akapaza sauti yake kusema:
"Habti habti habti! Segoth kil vi njham!"
Wenzake wote waliokuwa chini ya madhabahu hiyo wakapaza sauti zao kuitikitia habti! Habti! Habti! Mara tatu.
Wote walikuwa wamevalia majoho meupe na kufanya eneo hilo kuonekana mithili ya anga lililojawa na ndege yange yange.
Baada ya kusema hayo, wakanyamaza kimya kana kwamba hamna mtu hapo. Punde akaonekana Venim akipanda hapo madhabahuni, mkononi alikuwa amebebelea kitabu kipana kikuukuu chenye kava gumu.
Yeye pekee ndiyo alikuwa amevalia joho jekundu. Na pia tena yeye pekee ndiye alikuwa ameachia nywele zake wazi. Wengine wote walikuwa wamejivesha viremba. Rangi nyeupe.
Madhabahu ilikuwa imezungushiwa mabakuli yaliyojaa damu. Kwenye kila kona kiliwekwa kiota chenye mayai matatu matatu ya ndege bundi. Na katikati kabisa ya madhabahu hiyo, kulikuwa na taswira ya mwezi angani.
Venim akaweka kitabu chake mezani, alafu akawatazama vijakazi wake waliokuwa wamejikusanya hapo na kuongea maneno kadhaa akiwataarifu nini wanafanya hapo na kwanini wanafanya hivyo.
Akiwa anateta kwa kujigamba akasema kwa kujiamini ni wakati wa kumrejesha Venet mahali anapostahili kwakuwa ana kisasi nao cha damu. Vijakazi wote wakafurahia wakinyoosha mikono yao juu na kupiga nduru.
Lakini kwanini wanafurahia kiasi hiki? Je hawakutaka mtu na kaka yake warejeshe familia yao?
Simulizi ilianzia mbali kidogo. Wakati Venet akiwa mlozi mbabe mwenye sauti na maamuzi ya kutetemesha anga, kila mtu alimtii na kumuogopa. Hata wale walozi wadogo wadogo walijikuta wakijisalimisha mikononi mwake na kuungana naye kama vijakazi.
Lakini baada ya Venet kudondoka, wote wakahamia kwa mdogo wake, Venim, kwakuwa yeye ndiye pekee aliyebaki mwenye nguvu na mamlaka. Kitendo hiki kikamghafirisha sana Venet. Si tu kwamba akaona mdogo wake amemsaliti, bali pia na wajakazi wake.
Akaapia kwa damu. Siku atakaporejea himayani, kwa mkono wake, atateketeza wote hao. Kila mwili utabakia kama jivu juu ya uso wa dunia. Watang'ata meno na kulia kwa uchungu.
Sasa nani anataka haya yamtokee? Kwa hali na mali inatakiwa Venet abakie Tanashe. Azeekee na kufia huko huko kwa usalama wao!
Venim akafungua kitabu na kuanza kupaza sauti kwa hali ya juu, wajakazi wake nao wakamfuatisha wakitengeneza ala ya muziki. Aliposoma kurasa tatu, mara anga lililokuwa jeupe likawa jeusi ti! Radi zikaanza kunguruma. Mabakuli ya damu yakaanza kutikisika.
Akaendelea kusoma na kusoma. Wajakazi wakaitikia kisomo. Damu zikaanza kukauka mabakulini. Na yale mayai ya bundi yakapiga nyufa!
Ardhi ikatetemeka. Upepo mkali ukakatiza na kuzima mishumaa yote. Na mara kipande cha mwezi kilichokuwepo angani, nacho kikayoyoma isijulikane kimeenda wapi!
Anga likawa jeusi kana kwamba ni usiku ama mvua nzito yataka kunyesha.
**
Akiwa ndani ya shimo, akastaajabu kuona anga likibadilika rangi. Moshi mzito mweusi ilikuwa unatanda angani, ukafanya bluu kuwa nyeusi tena nyeusi totoro.
Nani alikuwa anageuza mchana huu kuwa usiku? Akajiuliza akisogelea nondo na kuzidaka kwa mikono yake mipana. Akataka kujibadili kuwa kundi kubwa la popo, akastaajabu anashindwa.
Akajaribu kadiri ya uwezo wake akastaajabu anafeli. Akatoa macho kwa mshangao. Nini kinatokea? Anga lilikuwa jeusi, kwanini anashindwa kugeuka?
Akiwa kwenye bumbuwazi, akaona bundi wakikatiza angani. Wakilia milio ya ajabu. Wakitanua mbawa zao kana kwamba tai. Wakirandaranda huku na kule!
Hapa alichokiwaza kichwani akajikuta anakikataa. Hapana! Akasema akitikisa kichwa. Haiwezekani. Hapana! Akatikisa nondo kwanguvu.
Akatumia nguvu zake zote kutikisa nondo hizo atoke lakini hakuweza kabisa. Mwishowe akachoka. Akaketi akiwa amejawa na maji machoni.
Alijihisi mdhaifu. Mtupu. Mchovu.
"Zama zimekwisha Venet," akasikia sauti ikimwambia. Akatazama kuangaza lakini hakumwona mtu huyo.
"Zama zako zimeisha, yakupasa urudi ulipotokea."
Punde akamwona Venim! Alikuwa amesimama kandokando na mfalme Phares.
Akasimama akisaga meno. Akamtazama Venet kwa macho ya hasira. Akaukunja uso wake akiminya nondo kwanguvu.
"Ni wewe!" Akafoka. "Ni wewe Venim!"
Akafoka kwa sauti kali. Hakutaka kukubali kuwa mdogo wake amemshinda kwa mara nyingine tena. Hakutaka kuukubali udhaifu huu lakini ndiyo ulikuwa uhalisia!
Akiwa ndani ya mwili wa Rhoda akajimenya na kutoka nje. Akamlilia sana kaka yake amsaidie, asimtupe kama alivyofanya hapo awali lakini vyote hivyo vikawa nyimbo kwenye masikio ya Venim. Macho yake yalikuwa yanatazama mwili wa Rhoda ulioketi pembeni.
Alishajua fika kile anachokiongea Venet hakikuwa kitu akimaanishacho hata kidogo. Hakuwa pale kumsaidia bali kumwangamiza.
Punde Venet akamwona Venim akipokea kikopo kidogo cha chuma chenye mkanda wa chuma. Kikopo hiki kilikuwa kinafuka moshi mzito mweupe. Venim akachuchumaa kisha akaanza kufukizia moshi huo ndani ya shimo alilomo Venet.
Ndani ya muda mfupi moshi ukajaa humo, Venet akasikika akikohoa na akihangaika kuhema. Akitapatapa huku na kule.
"Pole, kaka. Namhitaji huyo mwanamke. Na wewe pia nahitaji urudi Tanashe," Venim akasema akitazama shimoni japo hakuwa anamwona Venet kwasababu ya kuzongwa na moshi mzito.
"Nakulaani, ewe mbwa!" Sauti ya Venet ikasikika moshini. "Nakulaani kwa kushirikiana na binadamu kwasababu ya mwanamke. Nakulaani kwa kufunga anga langu kwa kujaza bundi. Nakulaani kwa kuufunga mwezi angani. Nakulaani kwa usaliti wako.
Binadamu watakuwa anguko lako. Huyo mwanamke atakuwa anguko lako."
Baada ya hayo Venet hakuongea tena. Alikohoa mara mbili kukawa kimya.
Moshi ulivyotoweka, Venet akaonekana akiwa amejilaza chini asionyeshe dalili ya kuwa mzima. Venim akaamuru shimo lifunguliwe na watu hao wawili watolewe. Agizo likatekelezwa.
Venet akaenda kutupiwa ndani ya Tanashe. Rhoda akahifadhiwa vema kwa ajili ya Venim kwenda naye.
"Na mifuko yako ya dhahabu i tayari," mfalme alimwambia Venim.
"Mifuko gani?" Venim akastaajabu.
"Ile uliyosema tukuandalie kama malipo," mfalme akaeleza. Venim akakana kusema kitu hicho. Mfalme akajua kumbe Harid alidanganya.
"Naweza nikaondoka sasa. Nimeshamaliza kazi yangu," akasema Venim akimpatia mfalme mkono wa kheri.
**
Alipokuja kushtuka alijikuta kitandani. Hakukumbuka amelala usingizi huo kwa muda gani na hakukumbuka aliulala akiwa wapi.
Akatazama kando na kando. Chumba kilikuwa kikubwa na ukutani kulikuwa kuna mifupa ya binadamu, mpaka mafuvu.
Akaunyoosha mwili na kupiga mihayo. Akanyanyuka na kuendea dirisha, akatazama nje. Mazingira haya yalikuwa mageni. Hapana! Si mageni! Akalumbana kifuani mwake.
Akakunja uso wake kuangaza vema. Punde, mlango ukagongwa na Venim akaingia.
Rhoda akatoa macho.
Alah!
Alikuwa kwa Venim!
Kwa bashasha la furaha, Venim akamweleza mwanamke huyo kuwa amemrudisha kwenye uhai wake uliobebwa na walozi. Na sasa amekuwa wake. Amekuwa wake kamili!
Rhoda hakuelewa kitu hapa. Au tuseme hakutaka kuelewa kitu hapa. Akauliza:
"Mfalme alikupa ukaenda nami?"
"Ndio, kwa roho nyeupe," Venim akajibu akitabasamu.
Rhoda akatazama dirishani njia ya kuelekea Goshen. Akakamata nondo za dirisha na kusaga meno. Akatazama njia hiyo kwa sekunde kadhaa, alafu akasema kifuani mwake.
"Goshen, hata ukinitupia katikati ya mamba nikaliwe, bado nitarejea nikiwa nawaongoza mamba hao."
**