*MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN II - 33*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Hawatayapata siku zote hizo, aliamini na kuwaaminisha. Akaenda zake akiwa ameghafirika.
"Uliyajuaje mafumbo yote yale?" Fluffy akamuuliza Seth akiwa na kimuhe. Seth akamwambia baba yake alikuwa akimuuliza sana akiwa mtoto, vile vile vitabu vingi alivyovisoma. Wakampongeza sana kwani alisaidia kupata maji ambayo hawakujua wangeyapatia wapi.
Lakini kwa wakati huo, yule kiumbe, akiwa amepania kwa dhati, akaenda kukesha usiku mzima kupitia mafumbo yake aliyoyaandika kwenye kuta za pango. Hata kula hakutaka.
ENDELEA
Kasrini, Goshen.
Ni asubuhi iliyokuwa inakaribia mchana lakini si muda mrefu watu walitoka kupata kifungua kinywa. Kwa mbali farasi watatu walionekana wanajongea kwenye lango la kuingilia. Farasi hawa wa rangi ya 'brauni' walikuwa wanakimbia kwa kasi.
Walipokaribia karibu na kusimama ikaonekana kumbe migongoni mwao walikuwa wamewapakia Tattiana na Mama yake wakiongozana na mzee wa baraza. Wakajitambulisha kwa ufupi pale langoni, wakaruhusiwa kuingia ndani kuonana na mfalme.
Baada ya dakika kadhaa za kungoja, mfalme akaja kuungana nao mezani na sasa mzee wa baraza akashika hatamu kueleza kilichowaleta hapo.
Kwa heshima yake, akasema wazazi wa Tattiana wameridhia kumleta binti yao aje akae hapo kama mchumba wake mpaka pale atakaporidhia kumuoa.
Wameamua hivyo kwa kuona itakuwa njia nzuri kwa binti huyo kuanzisha mahusiano na mume wake wa baadae na pia itamsaidia kiakili na hata kimwili kwasababu kadhaa kama vile upweke anaokumbana nao hapa karibuni.
Na kama haitoshi itaanza kumjenga na kumwandaa kubeba majukumu yake kama mke wa kiongozi mkubwa ndani ya himaya. Kama Malkia.
Mfalme akalipokea swala hilo kwa mikono yote miwili lakini akastaajabu kwanini imekuwa ghafla hivyo. Limekuwa ni jambo la kushtukiza mno. Alitakiwa aarifiwe kama mhusika.
"Ni kweli," akaafiki mzee wa baraza. "Tumefanya makosa makubwa sana. Lakini fadhila zi juu yetu maana wewe umekuwa mfalme msikivu na unayejali. Nakuomba sana msamaha, mfalme. Na nakuomba ulipokee shauri letu hili kwa mikono yote miwili."
Phares akafikiri kwa muda kidogo. Kisha akauliza:
"Lakini na binti huyu ameridhia? Nami ningependa kumsikia akitia neno kwenye hili."
Basi Tattiana akapewa fursa ya kuongea. Akiwa ameinamisha kichwa chake chini, akasema ameridhia hilo na yupo tayari. Mfalme akajikuta ametabasamu.
"Basi hamna shida. Niko tayari," akasema kwa akimkabidhi mkono mzee wa baraza na hata baadae mama yake Tattiana kisha akawasindikiza kwenda zao wakati wakimuacha binti ndani.
"Muende kwa kheri zote," mfalme akawabariki.
Waliingia farasi watatu ila sasa wakatoka wawili tu. Mfalme akawatazama wageni wake hao wakiishilia akitabasamu, alafu akaenda zake ndani kukutana na mchumba wake.
"Jisikie upo nyumbani," akamkarimu Tattiana lakini akamwambia hatokaa naye kwa muda huo kwani kuna kazi moja ndogo anatakiwa kwenda kuitekeleza nje ya kasri.
Kabla hajaondoka, akapiga makofi matatu wakaja vijakazi wake na haraka vijakazi hao wakagawanywa na kuteuliwa watatu kwa ajili ya kumtazama na kumhudumia Tattiana.
"Nitarejea muda si mrefu, kipenzi," mfalme akaaga na kwenda zake. Tattiana naye akaenda ndani alipoelekezwa kama chumba chake maalumu baada ya chumba hicho kufanyiwa matengenezo na kupambwa inavyotakiwa.
Chumba hichi kilikuwa kikubwa mno, kitanda kipana cha duara, kimejawa na maua yanayovutia na samani zake zilikuwa za gharama kubwa.
Tattiana akajiweka kitandani akilala chali. Asidumu hapo muda mrefu, mawazo yakamkaba koo. Kichwa chake kilirejelea na kuchambua siku nzima ilivyokuwa mpaka yeye kuishia hapo. Alikuwa anaona kila kitu kichwani kwake kana kwamba tamthilia kwenye televisheni.
Wakati mambo hayo anayoyawaza yakitukia hakuwa na muda wa kuyachambua vema, sasa alikuwa mwenyewe kitandani, huu ulikuwa ni muda muafaka kwake kufanya zoezi hilo.
Akakumbuka namna mzee yule wa baraza alipofika nyumbani kwao asubuhi ya mapema, akazungumza na baba na mama yake kisha akaitwa na kupewa maagizo pasipo kuombwa neno.
Ni bayana walikuwa wanamjadili yeye. Lakini mbona wamemuondoa nyumbani haraka kiasi hicho? Ni nini kipo nyuma yake? Akili yake nyepesi ikamwambia sababu ni kile kitu ambacho huwa kinaletwa pale nyumbani.
Hatakiwi kukijua.
Wazazi wake na mzee yule wa baraza walikuwa wamefanya njama aondoke pale ili siri yao ibaki salama.
Lakini kwanini wanashirikiana kwenye hili? Aliamini kabisa mzee yule hakuwa anafanya haya bure. Lazima kuna fadhila anapata hapa, ipi hiyo?
Ule mzigo! Akalipuka kifuani mwake. Fadhila hii ni ule mzigo wanaoleta watoto wa yule mzee kila usiku pale nyumbani.
Mawazo haya yakamwogopesha sana Tattiana. Aliamini kabisa mzigo ule si wa mema, usingefichwa.
Na je mfalme anajua kuhusu hayo?
Akagaragara kitanda kizima akiwaza na kuwazua.
***
"Umezipatia wapi?" Zura akamuuliza Fluffy huku akimpokea mzigo wa kuni kadhaa. Fluffy alikuwa ametoka safari kidogo akiongozana na Alk, jitu pekee la Azeth lililobakia. Watu hao walisafiri kwenda kuangaza kama watapata kuni za kuanzishia moto wa kuwasitiri na baridi la usiku unaokaribia kuingia.
Fluffy akatabasamu akiketi.
"Tumetoa mbali sana," akajibu kwa kujigamba. "Tumezitoa mbali kweli."
Zura akaguna. "Wewe ungeweza kwenda mbali ndani ya jangwa hili?"
"Kwanini nisiweze?" Fluffy akauliza.
"Si ungeanguka kama jana!" Seth akatania wakacheka. Fluffy akaeleza wamezitoa kuni hizo upande wao wa kusini walipokuta miti kadhaa ya tende. Kwa msaada wa Alk wakavunjavunja miti hiyo iliyokauka na kuileta papo.
"Mmefanya jambo la maana sana," Malkia akawapongeza. "Tunaweza sasa tukapasha hata vyakula vyetu vilivyopoa na kuchukiza."
Mara akakumbuka jambo, akamuuliza Seth:
"Vipi yule kiumbe wako hawezi akatoa chakula? Yeye ni maji tu?"
Wakacheka.
"Lakini mimi namhofia sana," akasema Zura. "Anapokuwa karibu yangu nahisi kukosa pumzi. Naomba leo asije akatokea kwani naweza nikazirai."
Malkia akaongezea hapo. Tatizo ni kwamba yeye hamuamini kabisa yule kiumbe. Na anaona hata Seth akifanikiwa kujibu mafumbo yake yote bado atatafuta namna ya kuwamaliza tu.
"Sasa tutafanya nini?" Seth akauliza. Akasema hawana budi kumwamini kiumbe huyo kwani ndilo chaguzi pekee walilo nalo.
"Tofauti kabisa na binadamu, viumbe hawa huwa waaminifu. Cha msingi ni kutumia zoezi lake hili kujikwamua zaidi maana kiuhalisia hatuwezi kupambana naye. Mtu anayeweza kujaza vyombo maji usijue yametokea wapi, ni nini utamfanya?"
Kukawa kimya kidogo. Wakawasha moto kujipa joto na hata kupasha vyakula vyao wapate kutia kitu tumboni.
Muda ukapita, na kidogo yule kiumbe akajiri. Leo alikuwa amewahi kuliko jana. Aliketi asimwongeleshe yoyote yule isipokuwa Seth aliyemtaka waanze zoezi lao mara moja!
Lakini kabla ya kuanza, Seth akwamwambia ana ombi kwake juu ya zoezi lao. Kiumbe yule, pasipo hiyana, akamkaribisha apate kumsikia.
Seth akamwambia anataka waboreshe zoezi lao, leo na yeye apewe fursa ya kumuuliza mafumbo kadhaa kiumbe huyo. Na endapo akifanikiwa kumuuliza akashindwa, basi azawadiwe zawadi kubwa. Si maji.
"Kanji keti na?" Zawadi gani hiyo? Kiumbe akauliza. Seth asifikiri sana akamwambia anataka awasaidie kukamilisha safari yao ndefu ya kwenda Misri.
Kiumbe kile kikatulia kwanza kwa muda mchache kisha kikamwambia Seth kuwa atafanikisha ombi lake hilo kwa makubaliano makubwa pia kwa upande wake.
Endapo Seth akikosa swali lake lolote, basi atawamaliza wote kwa kuwanyonya damu na kukusanya mifupa yao.
Seth akabaki na njia panda. Akawatazama kwanza wenzake kabla ya kujibu.
***