*MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN – 44*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
“Sasa niachieni kazi mimi. Najua vile n’takavyofanya,” alisema kabla hajashika mlango na kuyoyoma.
“Mke wangu u …”
“Nini? Tumeshamaliza majadiliano. Twende ule tulale.”
Mke akatangulia kwenda akimwacha mumewe nyuma akisita na roho.
ENDELEA
***
“Nimemkuta mfalme? Rhoda alimuuliza mlinzi getini. Alikuwa amekuja hapo makaoni akiwa mwenyewe. Alikuwa amevalia gauni rangi nyeupe iliyofifia likipambwa na maua maua madogomadogo.
Ulikuwa ni usiku, kwa majira ya sasa tungesema ni mishale ya saa nne. Kuja hapo mwenyewe njia nzima ilikuwa si jambo la kawaida, ila kwake wala halikumwia vigumu. Dhamira ndani ya nafsi yake ilikuwa kubwa.
“Ndiyo yupo, ila huwezi kumwona muda huu,” alisema mlinzi.
“Siwezi kumwona? Unaniambia kama nani?”
“Mam, muda sasa umeenda. Mfalme atakuwa amepumzika na ahitaji bughdha. Rhoda akasonya, akamsukumia mlinzi kando kisha akazama ndani. Mlinzi hakusumbuka naye tena, akabaki anamshuhudia tu mwanamke huyo akizama ndani.
Rhoda akaita mara mbili, na mara mfalme akatoka tokea chumbani. Alikuwa amevalia nguo za kulalia, shati na suruali nyepesi. Alikutana na Rhoda wakaketi sebuleni.
“Kuna shida gani Rhoda?” Phares akauliza.
“Nina ombi dogo kwako, mfalme,” Rhoda akasema akifinyanga vidole vyake.
“Rhoda, tafadhali niite Phares. Una ombi gani hilo lililoshindwa kungoja?”
“Phares, kuna mtu ambaye anaweza kutusaidia kujua wapi Malkia alipo!”
“Malkia?”
“Ndio, namaanisha Sandarus!”
Phares akatabasamu.
“Rhoda, kuna jambo ulilowahi kuliacha likakupita kwa jema?”
“Phares, hili jambo kwako ni dogo?”
“Hapana si dogo, ila juhudi zako ni za kushangaza. Tuachane na hayo, nani huyo anaweza kutusaidia?”
“Kuna mzee anaitwa Tretho.”
“Ndiyo nani huyo?”
“Ni mfugaji fulani hivi anaishi ng’ambo ya mto.”
“Umeshindwa kumalizana naye? – au shida ni nini?”
“Sijashindwa kumalizana naye, tatizo hayupo. Askari wako walimkamata na kumtia ndani.”
“Askari wangu? Bila shaka ana makosa?”
“Ndio, na sijaja hapa kumwombea msamaha ila kukuomba niweze kuongea naye na tumsikilize nini anachoweza kutupatia.”
Phares akashusha pumzi. Alifikiria kwa muda wa dakika moja kabla hajakata shauri la kumuita askari wake na kumwagiza amlete Tretho mbele yake. Asakri akatii na punde Tretho akaletwa.
Akasimamishwa mbele ya mfalme.
Alikuwa ni mzee mfupi mwenye ndevu nyingi nyeupe. Alikuwa amevalia joho la kaki linalomfikia chini kidogo ya magoti.
Hakuwa na viatu, na mikono yake ilikuwa imefungwa kamba maalum wanazofungiwa wafungwa. Alikuwa ananuka ng’ombe, yeye pekee akionekana kutokujali harufu hiyo.
Aliinamisha kichwa chake kumsalimu mfalme kabla hajatazama kinyenyekevu.
“Unaweza ukaongea naye,” Phares akamwambia Rhoda akimwonyeshea mkono mzee Tretho. Rhoda akatabasamu na kuinamisha kichwa chake kutoa shukrani kisha akamgeukia mlengwa.
“Tretho, unaweza kunisaidia kumtafuta mtu ambaye sijui yupo wapi?”
Tretho akatikisa kichwa.
“Hapana, siwezi,” alijibu kwa sauti yake kavu ya chini.
“Tretho hakuna mtu anayetaka kukujeruhi. Nataka tu kufahamu ili unisaidie. Ninashida kubwa sana na nimeambiwa wewe unaweza kunisaidia.”
Tretho kimya.
“Unaweza ukanisaidia tafadhali?”
“Siwezi kufanya hicho kitu. Aliyekwambia amekudanganya.”
Rhoda akasaga meno kwa ghafira. Alimtazama Phares, Phares akamtikisia kichwa na kumnong’oneza:
“Tumia busara,”
Rhoda akahema kwanza kupunguza fukuto la hasira kifuani, alafu akamrudia Tretho na tabasamu.
“Nitakupa chochote unachotaka endapo ukinisaidia. Unataka nini?”
Tretho kimya. Alitazama chini.
“Usiogope, sema wataka nini?”
“Nataka mnitoe lupango,” hatimaye Tretho akanena. Rhoda akatabasamu.
“Siyo hilo tu, bali pia msinitoze tena kodi kwa wanyama wangu. Sina kodi ya kulipa mara kwa mara. Ninafuga ng’ombe wale kwasababu ndiyo familia yangu pekee iliyobakia.”
Wakati akisema hayo, macho yake yakawa mekundu. Rhoda akamtazama Phares na kumshika mkono. Akamnong’oneza:
“Naomba umsikilize.”
“Kutokulipa kodi?”
“Tafadhali nakuomba. Ni huyu mmoja tu.”
“Endapo wengine wakijua unadhani italeta picha gani? Vipi nao wakigoma?”
“Haitatokea, tafadhali naomba,” alisema Rhoda akilegeza macho na kuuminya minya mkono wa Phares.
Phares akatikisa kichwa mara moja. Rhoda akatabasamu, akamwambia Tretho kwamba amekubaliwa ombi lake. Tretho akawa radhi sasa kumsaidia.
“Ili kufanikisha shughuli, kunahitajika vitu kadhaa: Majina matatu ya mlengwa anayetafutwa, na kitu chake chochote kile, aidha nguo, nywele ama kiatu.”
Hili tena likawa jaribio kwa Rhoda. Atavitolea wapi hivyo vitu?
“Kama hivyo vitu havipo?” akauliza.
“Kazi inakuwa ngumu zaidi. Mahitaji mengine ni makubwa na yanagharimu,” akasema Tretho.
Kabla Rhoda hajasema jambo, akamtazama kwanza Phares. Kuna vuguvugu la hofu lilikuwepo kati yao.
***
“Una uhakika ndiyo hapa?” aliuliza mkuu wa kikosi cha wanajeshi wa Sultan. Walikuwa tayari wamewasili eneo la Karim lakini hawakuona chochote hapo.
Kulikuwa ni msitu wa miti na vichaka virefu. Hakukuonekana kama kuna dalili yoyote ya makazi ya watu, labda wanyama tu.
Giza lilikuwa limeshamiri na sauti za wadudu zikitambaa kujaza anga.
“Ndiyo hapa hapa mkuu!” akajibu mwanajeshi aliyeulizwa. “Huwa natumwa kuja hapa, napafahamu. Hapa ndiyo penyewe!”
“Sasa Karim anaishi msituni?”
“Hapana, mkuu! Kulikuwa kuna nyumba hapa.”
“Sasa ipo wapi?”
“Nashindwa kuelewa ipo wapi! Ila ni hapa.”
Mkuu wa vikosi akaamrisha wanajeshi wake wapekue eneo zima la tukio. Zoezi likaenda kwa takribani dakika ishirini pasipo mafanikio. Hakuna kilichoonekana.
“Hatujaona kitu, mkuu! Hamna mtu.”
“Inawezekanaje?” mkuu wa vikosi akauliza.
“Karim ni mlozi, mkuu. Atakuwa ametumia ulozi wake kujikinga,” akasema mwanajeshi mmoja. Hilo jambo likaonekana lina mantiki ndani yake.
“Sasa tunafanyaje?” mkuu akauliza. “Sultan hawezi kutuelewa tukienda kumweleza haya. Kuna yeyote mwenye wazo?”
Mwanajeshi mmoja akanyoosha mkono. Kabla hajasema alichonacho, mara akakakamaa kama mti. Macho yalimtoka na mishipa ya damu ikamsimama.
Alianza kutikisika kama simu iliyowekwa mfumo wa kutetemesha. Mdomo ukatoa mapovu na macho yakatoa damu. Akadondoka chini na kufa!
Wote wakapata hofu. Kilikuwa ni kitu cha ajabu kutukia!
Kama haitoshi, akafuatia mwingine na mwingine kutengeneza idadi ya watu watatu. Wote wakafa kifo cha aina moja. Wakikakamaa na kutoa mapovu na damu. Kisha wakidondoka kama migomba.
Wanajeshi wakatazama huku na huko. Hakukuwa na mtu waliyemuona. Sasa nani anawaua? Ila swali kubwa lilikuwa nani anafuatia kufa baada ya hao watatu?
Mioyo iliwakimbia wakatota woga. Japokuwa walikuwa wameshikilia silaha zao mkononi, hazikuwa na faida wala kazi. Utapambanaje na kitu usichokijua wala kukiona?
Akafuatia mwanajeshi mwingine … mwingine pia kwa kasi ya ajabu! Wengine wakaanza kukimbia kuokoa roho zao.
Na wao hawakufika mbali, mara udongo ukaanza kutitia! Kila walipokanyaga palimomonyoka na kutengeneza shimo. Hakuna hata mmoja aliyebaki, wote wakamezwa shimoni.
Wakajikuta mahala pa giza. Walikanyagana na kusukumana maana walikuwa hawaonani. Hawakujua wapi pa kwenda wala pa kutokea.
Ilikuwa kizungumkuti!
Wakiwa humo mara kwa mbali ukaonekana mwanga mdogo wa ginga la moto. Mwanga huo ulikimbia na kupotea. Haikujulikana wapi ulielekea.
Ukapita muda mchache, ukaonekana tena mwanga wa ginga la moto ukiwa karibu tofauti na mwanzoni kana kwamba mtu aliyekua ameubebelea moto huo alikuwa amejongea karibu.
Mara ukapotea!
Ulivyokuja kuonekana tena, ukawa upo karibu zaidi ya mara iliyopita. Mara sauti ya panga ikasikika, sauti za watu kadhaa zikalalama kwa maumivu. Mwanga ulipoonyesha walikuwa ni wanajeshi watano wameuawa.
Walikuwa wamelala wanavuja damu za kutosha.
Kufumba na kufumbua mwanga wa ginga la moto ukapotelea mbali kana kwamba aliyeubebelea anakimbia kwa kasi! Pumzi za watu zikaanza kusikika zikihema hofu.
“Mbeba moto ni muuaji!” ikafoka sauti moja.
Haukupita muda mrefu, mara ginga la moto likaonekana tena kwa mbali! Likawa linapotea na kuibuka tena. Linapotea na kuibuka tena.
Pasipo mashaka wanajeshi wakajiandaa kupambana.
Lakini ajabu ginga hilo la moto lilipotea na kuja kutokea karibu na wanajeshi hao likiwa upande tofauti kabisa na ule uliotokea. Hivyo likawa limewapoteza wale waliokuwa wamejipanga.
Likazima na mara sauti za watu wakilalama maumivu zikasikika. Watu wanne wakaenda. Walikuwa chini wakimwaga damu, tayari wamekufa.
Ginga la moto likaonekana layoyoma.
Haukupita tena muda mwingi, yakaonekana maginga mawili ya moto kwa mbali.
WANAJESHI HAWA WATATOKA SALAMA? KARIM YUPO WAPI?
NINI TRETHO AMEMWELEZA RHODA KAMA NJIA YA KUFANIKISHA KAZI YAKE?