SIMULIZI: Mkufu wa Malkia wa Goshen

SIMULIZI: Mkufu wa Malkia wa Goshen

Unafanya vema mtoto mzuri....endelea kutupa burudani
 
mwendelezo wenyewe uko wapi mtani?
Tuendeleee
Aah jamani

Aah jamani unauliza makofi polisi? Endelea please
Tuendelee
Tuendelee. Haina kuchoka hiyo
Tuendeleeee shusha nondo mama
tuendelee jamn
Unafanya vema mtoto mzuri....endelea kutupa burudani
Inazidi kunoga [emoji91]
Shunie njoo basi
Abeeeh nimekuja
 
*MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN --- 42*

*Simulizi za series*


ILIPOISHIA

Alikaa kama dakika tano tu, mara wanaume watatu waliovalia magwanda ya jeshi wakawaja na kusimama kandokando yake. Mmoja akamwamuru:

“Simama!”

Kabla hajasema jambo, akanyanyuliwa na kubebwa kama kiroba. Hakujua anapelekwa wapi.

Alihofia uhai wake.

ENDELEA…

Aliingizwa kwenye chumba fulani cha giza, akafungiwa humo. Aliuliza yupo wapi na nani anamfanyia hilo tukio ila hakuna aliyemjibu zaidi ya kurudiwa na mwangwi wa sauti yake.

Chumbani alikuwa mwenyewe na hakuna mtu nje aliyekuwa anamsikia, pasipo kujali ni kelele namna gani alipiga.

“Huyu ni kwanza, na tutawamaliza wale wote watakaokaidi mpango wetu.” Sauti ya kiume ilisikika gizani.

“Lazima mpango wetu ufaulu, lazima turudishe himaya mikononi mwetu.”

“Ndio!” wengine wakaitikia. Ilikuwa sauti ya watu wawili, zote za kiume.


***


Hodi ilibishwa mara moja kabla mlango haujafunguliwa. Alikuwa ni bibi yake Sultana mdogo akiongozana na mlinzi, mwanaume mrefu jabali.

Bibi alikuwa amejitundika kikoi kipana kilichofichama shingo na mabega yake. Gauni refu jeusi na mkoba wa rangi nyekundu mkono wake wa kuume.

Nywele zake ndefu zenye mvi alikuwa ameziviringita na kuzibania vizuri upande wa kushoto. Usoni hakuwa ametia kipodozi chochote hivyo uso wake ukaonyesha umri wake pasipo matatizo.

Hakuonyesha kujali, hakuwa na sababu ya kufichama umri ilhali ni majaliwa ya muumba.

‘umri ni maji ya mto, yakienda hayageuzi shingo’ waenenda vema walishawahi kusema.

Bibi alitazama huku na huko, hakumwona mjuu wake. Akaita akiketi kitini na mlinzi akienda zake baada ya kumaliza kazi.

Baada ya muda kidogo, akatokea msichana, yani mjukuu, akiwa amelewa usingizi. Alipomuona bibiye akatabasamu, akamkumbatia na kuketi karibu yake.

“Mbona kuchelewa hivi?” Sultana akauliza.

“Unajua kulivyo mbali huku kwenu, alafu mimi ni mzee si kama wewe!”

Sultana akapiga makofi mara tatu na mara kijakazi akaja upesi, akamwagiza alete kikombe cha kahawa upesi kwa ajili ya bibi yake.

“Bibi, ulipata barua yangu?” Sultana hakuwa na subra.

“Ndiyo, niliipata na ndiyo hiyo imenileta hapa.”

“Sasa bibi unanisaidiaje?”

“Mjukuu wangu, humwachi mgeni aheme?”

Sultana akajikuta anatabasamu. Kijakazi alifika akamiminia kahawa kwenye kikombe na kumpatia bibi aliyekinyaka na kukipeleka mdomoni kunywa mafundo mawili.

“Sasa mjukuu wangu wataka nini?” Bibi akauliza. “Kama maji tayari yameshamwagika, unataka kuyachota?”

“Kama inawezekana bibi!” Sultana akalipuka kwa hamu.

“Hapana,” Bibi akasema. “Maji yakishamwagika hayawezi kuzoleka kamwe.”

“Basi tufanye mpango wa kuyachota mengine!” Sultana akapendekeza.

Bibi akanywa kwanza mafundo mawili ya kahawa, kisha akatazama kando.

“Mjukuu wangu, nadhani umesahau jambo, na si mbaya nikakukumbusha. Sina ulozi wa kumdhuru mtu, sijawahi kumdhuru yeyote, bali tu kusaidia.”

“Lakini bibi …”

“Hapana! … siwezi nikamuumiza yeyote.”

“Basi naomba unisaidie.”

“Nitakusaidia ila si kwa kudhuru wengine.”

“Inawezekana hilo?”

“Ndio, hakuna lisilowezekana!”

“Lakini bibi, vipi kama sisi tukidhuriwa kwa mioyo yetu ya maua?”

Bibi akamshika mjukuu wake shavu akimtazama machoni.

“Unanikumbusha mbali sana, kipindi kile ulivyokuwa mtoto. Ulikuwa mbishi na mkorofi. Sababu hiyo ukawa unapigana na wenzako kila uchwao … mabaya mawili hayatengenezi jema moja.”

Sultana akatazama chini. Alinywea kana kwamba amemwagiwa maji ya baridi. Bibi akafungua mkoba wake na kutoa chupa moja ndefu yenye mfuniko mweusi, ndani yake kulikuwa kuna unga mzito wa kahawia.

Akaiweka mezani.

Akatoa tena chupa nyingine, ndogo kwa umbo yenye mfuniko mpana mweupe, nayo akaiweka mezani kisha akaufunga mkoba wake.

“Hili ndilo jaribio letu la mwisho,” akasema bibi akishika chupa ile ndefu. Akamwonyeshea mjukuu wake.

“Umeona hii?”

“Ndio, bibi!”

“Utaitia kwenye njia atakayokatiza mumeo.”

Sultana akatikisa kichwa kuafiki.

“Na hii,” Bibi akaonyeshea chupa ndogo. “Utaiweka nguoni mwake.”

“Ahsante bibi.”

“Tahadhari, inabidi uyafanye haya mumeo asijue.”

“Sasa bibi nitawekaje akiwa ananiona?”

“Na inabidi uiweke siku ya tatu baada ya mwezi kuwa mzima.”

“Je kama asipokuja siku hiyo?”

“Basi itakulazimu usubirie tena mpaka utakapopata wasaa huo. Ukiiweka siku tofauti na hiyo, hakuna mabadiliko yoyote yatakayojiri.”

Sultana akazikusanya chupa zake akizijaza kiganjani.

“Hizo hazitamfanya Sultan akupende zaidi,” Bibi akasema. “Bali zitamfanya akumbuke nyumba yako atakapokuwa mbali.”

“Kivipi?” Sultana akauliza.

“Dawa itakayokuwa nguoni mwake, itamfanya asikie harufu yako muda wote. Na dawa atakayoikanyaga kwa mguu wake, itamfanya azunguke koote ila arejee hapa hapa. Kiu ya miguu yake itakuwa hapa.”

Sultana akatabasamu. Akamkumbatia bibi yake kwanguvu.

“Ahsante sana bibi.”

“Lakini mjukuu wangu, kama bwana akirejea kwako mara kadhaa, na akahisi harufu yako mara kede, kama hujampatia cha kumfanya akukumbuke, na hicho kipo kichwani, basi ni kazi bure.”

“Kwa hilo ntajitahidi sana,” akaahidi Sultana.

“Sasa naona utanipa muda wa kumpumzika.”

Sultana akacheka.


***


“Kwahiyo?” Sauti ya mwanamke iliuliza ikitokea ndani ya chumba.

“Sijajua cha kufanya mpaka sasa,” sauti ya kiume ikajibu.

Ni ndani ya nyumba yenye ulinzi wa kutosha, ya mfanyabiashara Melkizedek. Sebuleni walikuwa wameketi watoto: Fanty na Tattiana wakila cha usiku. Walikuwa wakipiga soga na kukenua.

Huko nje walinzi wawili walikuwa wamesimama getini wakibebelea mikuki. Mwingine mmoja alikuwa anazunguka huku na kule kuhakikisha usalama.

Mazingira yalikuwa ya kimya na joto, upepo ukipuliza kwa maringo.

“Una maanisha nini kusema hujajua cha kufanya mpaka sasa?” aliuliza mwanamke, mke wa Melkizedek. Alikuwa amejilaza kitandani pamoja na mumewe.

Alikuwa amevalia gauni jepesi jeupe la kulalia. Nywele zake ndefu rangi nyekundu zilikuwa zimetapakaa kitandani. Uso wake mwembamba mrefu wenye kidevu chenye ncha ulikuwa unatazama dari.

Macho na mdomo wake vilikuwa vinafanana na vya mwanae Tattiana. Mwili wake ulikuwa mwembamba ukiingia kama mara mbili na nusu ya mumewe ambaye alikuwa amejlaza chali , tumbo lake kama kiroba likitazama juu kama kichuguu.

“Unajua uzito wa hilo ombi?”

“Najua, lakini ni zito kuliko mwanao kuwa malkia?”

Kukawa kimya kidogo.

“Mzee wa watu amekupigania, na kuna uwezekano mkubwa wa mtoto wetu kuwa malkia. Nini unataka zaidi ya hicho?”

“Tatizo mke wangu, Cedar si haramu kuuzwa tu kwetu bali kwenye himaya nyingi. Vipi kama mzigo ukikamatwa huko na kuharibu taswira yangu?”

“Kumbuka tayari mtoto wako atakuwa malkia, atakusaidia!”

“Atanisaidia kwenye himaya zingine? Kuficha uhalifu wangu?”

“Melkizedek, nimechoka sasa kuongelea hili jambo karibia kila siku. Fanya utakavyoona wewe ni sahihi!”

“Kwahiyo umesusa?”

“Si kwamba nimesusa, bali nimeona sina msaada wowote, na tayari umeshafanya maamuzi yako binafsi. Mchango wangu ni nini tena kwako?”

Kukawa kimya. Kama dakika moja ikapita, hodi ikagongwa mlangoni.

“Baba, mzee amekuja!” Sauti ya Fanty ilisikika. Melkizedek akamtazama mkewe.

“Ameshakuja!”

“Ndio, si alikwambia atakuja?”

“Sasa nimjibu nini?”

Mwanamke akatikisa kichwa.

“Unavyoona wewe,” akajibu.

“Ebu acha basi kisirani. Mimi namwambia anipatie muda zaidi.”

Mke hakujibu, akanyanyuka na kujivesha gauni lake jekundu maridadi kisha akamtaka mumewe waende kumpokea mgeni. Melkizedek akavalia shati kubwa, akaongozana na mkewe mpaka chini.

Walimkuta mzee akiwa ameketi na watoto. Watoto wakapisha kuwapa faragha.

“Nimekuja kama vile tulivyoahidiana,” alisema Mzee akitabasamu.

“Karibu sana,” Melkizedek na mkewe wakamkarimu.

“Samahani, sitakuwa na muda mwingi wa kukaa na nyie. Kuna mahali natakiwa kupitia nikitoka hapa. Sema niliona nikatize mara moja kupata majibu yangu.”

Melkizedek akatabasamu na kumtazama mkewe. Macho yake yalionyesha yu njia panda.

“Nataka nipate majibu yenu ili basi nijue namna ya kuenenda katika jitihada zangu za kumfanya Tattiana awe malkia.”

“Tumekubali!” akasema mke wa Melkizedek. “Tumekubali, tumejadiliana na mume wangu na tumeona inawezekana.”

Mzee akatabasamu na kutikisa kichwa.

“Nilijua hilo halitakuwa tatizo kubwa kwenu. Mtoto kuwa malkia si jambo dogo!”

Mzee na mke wakatabasamu, Melkizedek akaigiza. Moyoni bado alikuwa na ukakasi.

Mzee hakukaa, akasimama na kuaga.

“Sasa niachieni kazi mimi. Najua vile n’takavyofanya,” alisema kabla hajashika mlango na kuyoyoma.

“Mke wangu u …”

“Nini? Tumeshamaliza majadiliano. Twende ule tulale.”

Mke akatangulia kwenda akimwacha mumewe nyuma akisita na roho.


NINI KITAJIRI KATIKA NJIA YA MZEE NA MELKIZEDEK?

SULTANA MDOGO ATAFANIKIWA KUFANYA VILE ALIVYOELEKEZWA NA BIBI YAKE?

NINI KITAMKUMBA SETH?

LAKO JICHO.....
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom