*MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN*41*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA…
“Ubaya hakuna anayejua. Kama lingetokea kabla ya kwenda kwa Venin, huenda angetusaidia kujua.”
“Lakini kuna mtu anaweza kutuonyesha njia,” mwanaume aliyeongozana na Bonas alisema. Wote wakamtazama.
“Nani huyo?” Rhoda akauliza upesi.
ENDELEA…
“Kuna mzee mmoja yupo kule ng’ambo ya mto. Yeye huwa ananasibu ana maono japo si maarufu sana kwa walio wengi,” akajibu rafikiye Bonas, Loki kwa jina.
“Una uhakika?” Rhoda akauliza. Macho yalikuwa yamemtoka akiachama mdomo kuonyesha namna gani alivyobamwa na habari hizo.
“Ndiyo, nina uhakika. Hata ninaweza kuwapeleka mkihitaji.”
Rhoda akamtazama Bonas, mwanaume huyo akampandishia nyusi, akarudisha macho yake kwa Loki akisimama na kusema:
“Ngoja, twende!”
Akapandisha zake juu na kuwaacha wanaume peke yao.
“Loki, una uhakika na unachokisema?” Bonas aliuliza. “Unajua hizi habari ni kubwa sana kwa huyu mama na endapo akijua umemlaghai inaweza ikapelekea ngoma nzito na ngumu kuicheza.”
“Sijamdanganya, nimesema kweli tupu, Bonas. Ya nini nidanganye?”
“Ni mzee gani huyo unayemuongelea?”
“Mzee Tretho.”
“Tretho wa kule mambugani? – mchunga ng’ombe?”
“Ndio, unamdharau enh? Mimi namjua maana nilishawahi kukumbana naye mahali.”
“Mbona hukuwahi nambia? Sijawahi kusikia kama ana lolote!”
“Kwasababu Tretho ni msiri na si mjivuni.”
Mara wakasikia mlango unafunguliwa, Rhoda akachomoza toka chumba chake cha juu.
“Tuombe Mungu unachosema kikawe kweli,” Bonas alisema akipachika kiganja chake juu ya bega la Loki. Rhoda aliwakaribia, akawatazama kwa macho yenye bashasha.
“Tunaweza tukaenda!” akasema akitangulia kwenda nje.
Walipanda farasi zao, pasipo kuwa na ulinzi wowote, wakaanza safari ya kuelekea ng’ambo kukutana na Trethro. Ndani ya kama dakiaka ishirini na kitu hivi wakawa wameufikia mto.
Wakavuka na kuchukua mwendo wa robo saa kabla ya kujikuta mbele ya nyumba ndogo chakavu. Fupi na isiyo na mahadhi ya kuvutia. Madirisha yake yalikuwa madogo, na paa lake likiezekwa na nyasi zilizooza.
“Ndiyo hapa,” Loki akamwambia Rhoda. Rhoda akapekua kwanza mazingira kabla hajauliza:
“Kunaonekana kimya, kutakuwa kuna watu kweli?”
“Anaishi mwenyewe,” Bonas akadakia. “Ni yeye na ng’ombe zake tu!”
Loki akashuka na kuusogelea mlango, akagonga na kuita pasipo majibu. Akazunguka nyuma ya nyumba mpaka zizini, hakumuona Loki wala ng’ombe.
“Hayupo!” Loki alimwambia Rhoda aliyekuwa bado yupo juu ya farasi. “Anaweza akawa yupo malishoni.”
“Muda huu?” Bonas akatahamaki kwa swali.
“Hana mahala pengine pa kwenda zaidi ya huko,” Loki akajibu upesi.
“Lakini malisho hufanya nyakati za jioni! Pengine kamuangaze kwa majirani,” Bonas alishauri. Loki akaenenda upesi huko kumtazama na kumuulizia Tretho.
Muda mfupi baadae akarejea. Akamtazama Rhoda na kumwambia:
“Hayupo!”
Rhoda akakunja sura kwa hasira.
“Wamesema amechukuliwa na wanajeshi,” Loki akajazia taarifa. “Ilikuwa ni leo asubuhi wakati anawapatia maji mifugo yake.”
Rhoda akastaajabu.
“Wamekwambia amechukuliwa kwa kosa gani?”
“Hapana!” Loki akatikisa kichwa. Rhoda akashusha pumzi ndefu.
Aliona sasa njia imekuwa ndefu zaidi.
Kama Tretho amekamatwa ina maana atakuwapo lokapu kule karibia na milki ya mfalme. Kumpata mzee huyo maana yake ni kumtoa lokapu, na kumtoa ni mpaka kuwepo na maelezo ya kueleweka, ama amri toka kwa mfalme.
Akimwomba mfalme, ataulizwa kwanini anataka msaidia mzee huyo. Ataweza kusema sababu ni Malkia? Hatompatia tembe za mashaka mfalme juu ya kusumbuka huko na Malkia Sandarus?
Au hataonekana ni mtu mwenye kuamini ulozi kupita kiasi?
Aliguna.
***
Baada ya kuangaza huku na huko na kuhakikisha kwamba yupo mwenyewe tu, Seth akatoa kijidaftari chake na peni ndani ya mfuko akaanza kuandika maneno fulani yenye alfabeti za ishara.
Alfabeti hizi hazikuwa na mpangilio maalum, kuna ambazo aliziandika kwa juu, zingine chini na katikati! Alikuwa makini akiziandika, na fika alikuwa anajua anachokifanya.
Aliandika ukurasa wa kwanza kisha akafungua wa pili na wa tatu, kuna muda aliacha kuandika akawa anafikiria, kisha akaendelea kuandika na kuandika.
Alikuwa amejitenga kabisa na ulimwengu akiwa ameketi juu kabisa mwa jengo kubwa la kijamaa. Pembeni kidogo kulikuwa kuna kachumba kadogo chenye kengele kubwa nyeusi iliyokuwa imetulia tuli.
Hapa ndipo mahala anapopapenda Seth, patulivu na pasipo na bughdha. Kila anapohitaji muda wa kuwa mwenyewe, basi huja huku juu ya paa, huketi na kufanya mambo yake.
Anatazama himaya nzima akiwaza na kuwazua kwa kadiri atakavyo. Ni watu wachache tu ndiyo walikuwa wanajua makazi haya ya Seth. Na hata hao wanaojua huwa wanampatia muda wa yeye kuwa peke yake kwa utambuzi.
Tangu apande huko juu, sasa alikuwa ameshakula takribani dakika ishirini hivi. Ila utulivu wake ulikuja kupotezwa na ujio wa mgeni ambaye hakumtarajia. Kwasababu alikuwa amemezwa na karatasi ya kijidaftari chake, hakugundua kama kuna mtu amemjongea.
“Seth!” Sauti ikamshtua. Haraka akafunga kijidaftari chake na kukirejesha ndani ya mfuko, na peni yake pia.
Akageuka nyuma kumtazama mgeni. Alikuwa bwana Bozi: mzee wa baraza la Sawaridi mwenye heshima zake.
Mzee huyu ndiye aliyempendekeza Seth na Dummy kwa Malkia, kwamba wanaweza kutumiwa na kuleta tija.
“Pole kwa kukushtua!” Alisema Bozi kwa tabasamu akiweka mkono wake begani mwa Seth. Seth akatabasamu lisilotoka moyoni.
“Karibu.”
“Ahsante sana, Seth. Najua haukutarajia ujio wangu, na pengine nitakuaribia mipango yako. Naomba uniwie radhi.”
“Usijali, karibu.”
Bozi akaketi. Alijetengenezea na majoho yake asijiweke uchi.
“Kumbe huku ni pazuri kiasi hiki!”
“Yah! Kuna upepo wa kutosha.”
“Na muono bora kabisa. Ukiwa hapa waweza kuona kila jambo linaloendelea himayani. Si bure wapenda kukaa huku.”
Seth akatabasamu pasipo majibu. Kichwani alikuwa anawaza ni nini kimemleta Bozi pale, na kama ameona kile alichokuwa anaandika na kukielewa.
“Nimekutafuta sana huko chini kabla ya kufikiria kwamba utakuwepo huku,” Bozi aliendelea kulonga kwa bashasha. “Tokea asubuhi sijakuona, ina maana ulikuwepo huku?”
“Hapana,” Seth akajibu kifupi.
“Sawa, nisikupotezee sana muda wako, kuna jambo fulani nilikuwa nataka kuongea na wewe, na jambo hili ningependa liwe siri kati yangu na wewe.”
Siri tena? Seth aliongelea kifuani. Alikuwa tayari ana siri ya Fluffy, na sasa nyingine ilikuwa inataka kuongezwa!
“Vipi, naweza nikaendelea?” Bozi aliuliza. Seth akatikisa kichwa.
“Nakuskiza.”
“Seth, bila shaka unajua mimi ndiye nilikusogeza karibu na Malkia.”
“Najua.”
“Safi sana. Unajua nafasi hiyo ni kubwa sana, na sikuwahi kukuomba fadhila yoyote ile.”
Seth kimya. Alishajua sasa mchezo upi unataka kuchezeka, ila bado hakujua nini kilikuwa nyuma ya mchezo huo. Akawa mpole asikie japo moyo wake tayari ulishachagua kutoshirikiana na Bozi.
“Na sijalenga kupata fadhila yoyote ile toka kwako, Seth. Lakini naona kuna jambo mbele yetu, jambo muhimu na nyeti.”
Seth kimya, anaskiza.
“Seth, naona tunastahili zaidi ya hiki tulicho nacho sasa.”
“Ukimaanisha nini?” Seth akafungua mdomo kuuliza. Alitazama macho ya Bozi yaliyokuwa yamejaa uchu, Bozi akatabasamu.
“Usiwe na haraka, Seth. Taratibu taratibu tutaelewana. Mimi nataka mema kwa ajili yako, yangu na himaya nzima. Naona ni vema sasa tukaanza mipango ya kurejesha himaya yetu mikononi toka kwa hawa wanawake.”
Seth akamtazama Bozi kwa mshangao. Alikosa cha kusema.
“Najua unaweza kudhani ni ngumu, ila hakuna kisichowezekana. Kwa hali na mali inabidi turejeshe himaya yetu mikononi, hatuwezi tukawa tayari kutawaliwa na mgeni, tena mwanamke!
Najua endapo tukiunganisha nguvu, tutalifanikisha hili kwa wepesi pasipo hata kumwaga damu.”
“Ni kweli, lakini mimi si miongoni mwenu. Nashukuru kwa kunishirikisha.”
“Seth …”
“Nimesema nashukuru, sina haja ya kujiunga na upande wowote ule kwa lengo lolote lile! Bila shaka nimeeleweka, na unaweza ukaenda.”
Bozi akabaki ameduwaa. Alishusha pumzi ndefu akanyanyuka.
“Pengine haupo kwenye hali nzuri kihisia. Nitakupatia muda.”
“Hata kama ukinipatia milele, jibu langu litakuwa hilo hilo! Sina nyendo, uroho, wala hitaji lolote la kisiasa.”
Bozi akaguna.
“Hujui usemalo, na hakika utakuwa kujuta.”
“Baada ya kwanza kujuta wewe,” Seth akasema kwa kujiamini. Bozi asitie neno, akaenda zake baada ya kumkata Seth jicho kali na kutabasamu kwa kebehi.
Seth akaendelea na kazi yake ya awali, ila sasa asiifanye vema sababu ya mawazo.
Alikaa kama dakika tano tu, mara wanaume watatu waliovalia magwanda ya jeshi wakawaja na kusimama kandokando yake. Mmoja akamwamuru:
“Simama!”
Kabla hajasema jambo, akanyanyuliwa na kubebwa kama kiroba. Hakujua anapelekwa wapi.
Alihofia uhai wake.
NINI KINAENDA KUMKUTA SETH? NANI AMETUMA AKAMATWE?
VIPI RHODA ATAFANIKIWA KUKUTANA NA TETHRO AMSAIDIE JUU YA MALKIA?
NINI MWISHO WA HARAKATI ZA UPOFU ZA RHODA JUU YA MKUFU?
JESHI LA SULTAN LIPO NJIANI KUELEKEA KWA KARIM, KARIM ATAKUBALI KUTIWA TENA NGUVUNI?
FLUFFY NA SIRI YAKE?
LAKO JICHO......