*MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN -- 038*
*Simulizi za series*
Sultan akanyanyuka akitoa macho na kukunja ndita. Alikunja ngumi yake pana nzito, akauliza:
.
.
“Unasemaje?” kana kwamba hakusikia.
Mlinzi akasita hata kurejea alichosema. Akiwa anatetemeka, na uso wake ukiwa mweusi kwa hofu, akasema: “Sultan, Karim ametoroka, na ameua walinzi kadhaa.”
.
.
Sultan akamzaba kofi zito mlinzi huyo kijumbe, kofi likammwaga chini na kumpachika alama nyekundu shavuni.
.
.
“Pumbavu!” Sultan akafoka. “Wazembe wakubwa nyie, wapuuzi msio na faida. Anatorokaje mtu aliye ndani ya lupango?”
.
.Mlinzi alinyanyuka upesi akasimama kiukakamavu akitazama chini. Jicho lake la upande uliozabwa lilikuwa limeiva kuwa jekundu mithili ya nyanya masalo.
.
.
“Tuwie radhi, Sultan. Wanaume waliokuwa zamu walishindwa kumzingatia kwa umakini.”
.
.
Sultan alisaga meno. Alipandwa na ghadhabu sana, hakutaka tena kumskiza mtu na badala yake akaondoka kwenda chumbani aliporejea akiwa amejisitiri na nguoze za thamani, akatoka ndani pasipo hata kuaga.
Akili yake haikuwa pale tena, bali Kasrini. Alikuwa anamuwaza Karim. Alikuwa anawaza namna ya kuenenda na mwanaume huyo aliyempanda kichwani.
Mke wake mdogo aliyeachwa kwenye bumbuwazi, akamsindikiza mumewe huyo ambaye hakuwa na habari juu yake kwa muda huo, akayoyoma na kundi lake la walinzi kuelekea kasrini.
Mwanamke akabaki malangoni akimtazama mume akipotea. Aliona ndoto ya kuelekea kasrini inayeyuka, na sasa amepata tena sababu rasmi ya kuhofia.
“Kama Karim ametoka, ina maana mwanamke yule naye atakuwa amerudishwa duniani?” alijiuliza.
Hakutoka hapo malangoni hata pale mumewe alipokuwa haonekani kabisa. Alikaa hapo akiwaza, macho yake yakionyesha ni namna gani alivyo mbali kifikra.
Alikosa raha kabisa. Alikuja kuokolewa toka kwenye bahari ya mawazo na kijakazi wake aliyeita na kumwambia:
.
.
“Sultana, malango yamekaa wazi sana, si njema kwa usalama.”
.
.
Basi akatoka na kwenda zake ndani. Akaenendea bilauri la mvinyo na kumiminia kwenye glasi akanywa. Glasi ya kwanza, ya pili, ya tatu, ya nne … bilauri likakata.
Kabla hajaongeza bilauri lingine apoteze fahamu vizuri, akachukua peni yake ya kuchovya na karatasi akaandika ujumbe wenye aya tatu kisha akapaza sauti kumuita kijakazi wake.
Upesi kijakazi akaja.
Karatasi yake ya ujumbe akaikunja na kuitia bahashani. Ilikuwa ni bahasha yenye nembo ya kasri na nguvu ya Sultan. Akamkabidhi kijakazi.
.
.“Nimekuita hapa maana wewe wapajua kwa bibi yangu, haya upesi umfikishie ujumbe huu!”
.
.
Kijakazi asiulize jambo, akapotea machoni mwa Sultana wake kwenda kutimiza agizo.
.
.
.
.
***
.
.
.
.
Jioni wakati Jua larembua, limechoka na linaaga uso wa dunia, sauti kubwa ya tarumbeta inavuma ndani ya himaya ya Goshen.
Tarumbeta hii ilikuwa inapulizwa na mwanaume kiongozi aliyekuwa amepanda farasi wa mbele kabisa kwenye msafara wa bibie Rhoda uliokuwa ukirejea nyumbani.
Tarumbeta hii ilikuwa ni ishara, lakini pia shangwe ya wasafiri, wenye heshima na hadhi ndani ya himaya, kurejea wakiwa salama na kufanikisha kile walichokiendea.
Phares, aliyekuwa chumbani kwa muda huo, alijikuta anatabasamu baada ya kusikia tarumbeta hiyo. Zaidi akajikuta anacheka na kutikisa kichwa chake.
Rhoda alikuwa amerejea. Na pia alikuwa ametekeleza lile alilokuwa amelilenga!
.
.
Alitoka ndani akaenda kusimama nje akiwa ameambatana na wafuasi wengine pia na walinzi. Walikuwa wamebebelea maua kadhaa kwa ajili ya kumlaki na kumpongeza Rhoda.
Kama vile malkia, Rhoda akapokelewa kwa matabasamu na makumbato. Phares akaongozana naye kwenda ndani, kwenye sebule kubwa pana, walipojikuta wenyewe na tayari wakishahudumiwa vinywaji aghali.
.
.
“Pole sana kwa safari, Rhoda,” Phares alisema kwa macho yenye furaha. “Nimefurahi sana kukuona tena, lakini nimefurahi sana kwa maana kazi umeifanikisha.”
.
.
Rhoda akatabasamu kidogo na kutikisa mguu wake uliokuwa umebebwa na mwingine kutengeneza umbo namba nne.
.
.
“Nashukuru sana, Phares, japo haikuwa kazi ndogo.”
.
.
“Bila shaka, ila nilijua fika utafanikiwa.”
.
.
“Ulijuaje Phares?”
.
.
“Penye nia hapakosi njia. Ulikuwa na nia kubwa mno kiasi cha kutokushindwa na sababu yoyote mbele yako.”
.
.
Rhoda akatabasamu pasipo kuhangaika na kauli hiyo. Ndani ya moyo wake bado haja yake haikutimizwa. Haja yake itapoa pale atakapoutia mkufu ndani ya kiganja chake na kuivaa shingoni.
Kila alipokuwa anawaza kuhusu mkufu huo, hujikuta anapata nguvu mara mbili asiogope mlima wowote uliosimama mbele yake.
.
.
“Natamani sana kujua yaliyotokea huko kwa Venin,” Phares alichombeza. “Unaweza ukanambia kwa sasa au umechoka taabani ukitaka kupumzika?”
.
.
“Sijachoka kiasi hicho,” Rhoda akatikisa kichwa akimtazama Phares kwa macho yake yang’aayo urembo. Pasipo kusita akamwambia mwanaume huyo yale yote yaliyotukia. Mpaka kufika kikomo Phares akawa ameachwa na bumbuwazi.
Alijua safari hiyo ilikuwa ngumu ndio, ila hakujua kama ni kwa kiasi hicho. Akampongeza tena Rhoda na kumpa pole.
.
.
“Yameshapita sasa hayo, na sasa tutazamie yajayo Phares.”
.
.
“Ni kweli, ila sidhani kwa sasa kama ni muda muafaka. Ningependelea tuongelee hilo kesho.”
.
.
“Hamna shida, Phares. Kweli ni jambo kubwa na pana, na linahitaji tutulize vichwa … Je, kuna lolote jipya lililotukia hapa nikiwa huko mbali?”
.
.
Swali hilo likasafirisha akili ya Phares haraka kwenda kwenye lile tukio la mzee wa baraza na mabinti zake.
.
.
Alikumbuka mabinti wale na sauti ya mzee yule, ila mmh mmh hakuona kama hilo jambo Rhoda anatakiwa kulisikia, basi akalifichia kifuani na kuchakata akili yake upesi kuziba mwanya huo.
Akakumbuka tukio la taarifa ya kuonekana kwa Malkia ndani ya himaya. Hili akaona linastahili katika meza yao ya maongezi.
.
.
“Unasema kweli, Phares?” Rhoda alitahamaki kusikia.
.
.
“Ndiyo, ni kweli tupu.”
.
.
"Laki … lakini imewezekanaje?”
“Sijajua imewezekanaje? Nashindwa kuelewa mwanamke huyu yupo wapi na anafanya nini!” .
.
Rhoda akakosa cha kusema. Alibakia akiwanda wanda ndani ya mawazo yake asijue mlango wa kutokea.
.
.
“Tatizo hili swala si mara ya kwanza kutukia, ni mara ya pili sasa! Ina maana Sandarus yupo mazingira ya karibu? Na je mbona huonekana na kupotea kwenye mazingira ya kutatanisha?”
.
.
Rhoda alihangaika kutafuta neno, akakosa kabisa. Alizidiwa mawazo. Aliona kweli sasa anahitaji kupumzika. Alinyanyuka akamuaga Phares kwamba anaenda nyumbani kwake kupumzika.
Phares alitamani kumwambia mwanamke huyo alale hapo makaoni, ila akakumbuka ni mwiko – hakuna mwanamke anayelala hapo isipokuwa malkia. Basi akashuhudia Rhoda akienda zake.
Mwanamke huyo hakupitia hata mahesabu ya biasharaze, akanyookea ndani ya chumba chake kabatini alipotia chupa ndogo yenye kimiminika rangi ya kahawia, akafunga kabati kwa komeo kubwa kabla hajaenda kuoga na kujilaza juu ya kitanda chake kipana maridadi.
Alijitahidi kuepuka mawazo alale kwa amani, lakini hola! Bahati kwake uchovu ulikuwa mwingi hivyo akajikuta analala, tena vema tu! .
.
Kwa siku kadhaa mwili wake ulikosa kitanda cha kumfanya anyooshe kila kiungo.
.
.
.
***
.
.
.
“Hodi!”
.
.
Kabla usiku haujazidi kuwa mnene, sauti kavu ya kizee inasikika toka kwenye mlango mkubwa, mpana na imara wa mbao.
Mlangoni alikuwa amesimama mzee wa baraza ndani ya joho lake jeusi na viatu vyake vya wazi rangi ya chumvi.
Alikuwa ndani ya eneo kubwa lenye nyumba kubwa kuukuu. Getini kulikuwa kuna wanaume wawili walinzi waliokuwa wamevalia sare na kushikilia mikuki mirefu mikali kwenye mikono yao ya kuume.
Walinzi hawa walikuwa wamemruhusu mzee huyu kupita na sasa alikuwa ana jukumu lingine la kugonga azame ndani ya jengo.
Hakurudia kubisha tena kabla hajasikia sauti ya mlango kufunguliwa kwa ndani, na mara mtu anachomoza kichwa kumtazama. Alikuwa ni kijana mwenye ndevu kiasi rangi ya kahawia sawia na nywele zake fupi.
.
.
Macho yake yalikuwa madogo yenye kiini cha paka. Kwa makadirio alikuwa ana miaka ishirini naa, haipiti ishirini na tano.
Alitabasamu alipomuona mgeni, akatabasamu na kuufungua mlango zaidi.
.
.
“Karibu sana.”
.
.
“Ahsante, nishafika.”
.
.
Mzee akaingia na kuketi kitini. .
.
Sebule ilikuwa ya wastani ila yenye kila kinachohitajika. Kwenye kuta zake kulikuwa kumening’inizwa dhana kadhaa zilizotengenezwa na chuma. Japokuwa dhana hizi zilikuwa za vita, zilivutia sebule.
.
.
“Karibu, mzee wangu. Nikuitie baba?” aliuliza kijana, jina lake Fanty, uso wake ukiwa na tabasamu.
.
.
“Hapana, Tattiana yupo?” Mzee akauliza.
.
.
“Ndio, yupo chumbani kwake.”
.
.
“Mwambie nahitaji kuonana naye.”
.
.
Fanty alipochukua hatua kwenda kumuita Tattiana, mara Mzee akamuita.
.
.
“Au achana naye, niitie kwanza baba, nina maongezi naye.”
.
.
“Sawa!” Fanty akajibu na kwenda zake. Punde akarejea akiwa ameongozana na mwanaume mfupi mnene mwenye nywele na ndevu za kutosha.
Mwanaume huyu alikuwa amevalia nguo za ngozi, mikono yake ikiwa na bangili kadhaa za chuma ila zinazovutia kwa maumbo yake mbalimbali. Macho yake yalikuwa madogo yakimezwa na ukubwa wa mashavu.
Kwa jina alifahamika kama Melkizedek. Mfanyabiashara na mfuaji mkubwa wa chuma.
Alifurahi kuonana na mzee wa baraza, walisalimiana na kujuliana hali kabla hajatesa kiti kwa kukalisha mzigo wake wa mwili.
.
.
“Sikutegemea kukuona hapa karibuni, mzee.”
.
.
“Hata mimi sikutegemea kurudi hapa karibuni.”
.
.
“Ni nini hicho kimekurejesha, tena usiku kama huu?”
.
.
“Ni habari njema, na si kingine.”
.
.
“Habari zipi hizo? Siku yangu leo haikuwa njema, naomba uibadilishe kwa ujumbe wako.”
.
.
Mzee wa baraza akatabasamu kwanza. Alimtazama mwenyeji wake akaona machoni namna gani alivyokuwa na kiu ya kujua.
.
.
“Unaweza ukawa mkwe wa mfalme,” akasema kwa ufupi.
.
.
“Ukimaanisha nini?” Melkizedek akalipuka kwa swali.
.
.
.
.
*MZEE HUYU ANATAKA KUMWAMBIA NINI MELKIZEDEK? ANA UHAKIKA NACHO? NA NINI ADHMA YAKE NYUMA YA HAYA AYAFANYAYO?* .
.
*NINI RHODA ANATAZAMIA KUFANYA HUKU TAARIFA ZA MALKIA ZIKIMPATIA HOFU NA WALAKINI?*
.
.
*NA JE SULTAN ATAMFANYA NINI KARIM? NINI HATMA YA MKEWE WA KWANZA?*
LAKO JICHO.....