*MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN -- 036*
*Simulizi za series*
"Nimemwona huko kusini karibu mwa himaya yako. Kwenye ile nyumba aliyokuwa anaishi Zura, mwanamke aliyemlelea na kumkuza!"
.
.
"Lakini una uhakika na si mawenge?" "Haki mfalme wangu, macho yangu yamemwona na kumtambua kabisa!" Punde likatumwa jeshi kwenda kumtafuta Malkia huko iliposemekana. Jeshi la wanaume sita na farasi zao wakafanya msako wa udi na uvumba, ila hawakutoka na jambo.
.
.
Hawakumuona Malkia kabisa ingali walimtafuta kwa masaa. Waljirejesha kwenye himaya ya mfalme, wakamtaarifu mfalme Phares. "Tumezunguka kote ewe mfalme, ila hakuna tulilopata!"
.
.
"Mmeuliza hata watu wanaoishi huko?" Mfalme akauliza. "Ndio, mfalme. Tuliuliza wote. Hakuna aliyemuona!" Mfalme Phares akashusha pumzi akishika kiuno. Alikosa cha kunena kwa muda.
.
.
"Mfalme, je tukamlete yule aliyekuongopea?" "La hasha! Mnaweza mkaenda." Wanajeshi wakaenda. Phares akabakia akiwaza na kuwazua. Alijiendea zake chumbani lakini bado akiwa ametingwa na mawazo.
Kutakuwa kuna namna! Alijisemea. Hii ni mara ya pili sasa anakumbana na hili jambo. Mara ya kwanza akiwa kwenye uwanja wa vita wakijiandaa, na mara ya pili hii sasa.
Ina maana yote hii ni mizengwe? Hapana!
Kuna mchezo gani hapa unaendelea? Huyu Malkia yupo wapi? Alitaka kujua zaidi. Aliadhimia kufanya jambo apate majibu ya maswali yake haya.
Akaona ni busara akimngojea Rhoda wapate kujadiliana. Pengine anaweza kumshauri kitu ukizingatia hana washauri wa karibu.
Alijituliza kabla ya muda kidogo hajatoka kwenda kupata chakula cha jioni. Aliandaliwa chakula kizuri na kingi na wajakazi wake.
Akiwa anakula, mwenyewe kwenye meza kubwa, mara anakuja kijakazi wake na kumwambia: "Mfalme una ugeni!" Akastaajabu. Alijaribu kufikirisha akili yake kama ana miadi, lah! Hakuwa nayo. Akauliza: "Ugeni wa nani?" "Wa mzee wa baraza!" Akajibiwa na kijakazi. Akatoa ishara ya kichwa kuruhusu ugeni huo.
Kijakazi akaenda na punde akarejea akiongozana na mzee wa baraza. Mzee huyu alikuwa ni mmojawapo wa waliomuunga mkono, ila baada ya kupewa presha na Rhoda.
Alikuwa amevalia joho refu rangi ya kahawia lenye kola ndefu lililosimama na kuziba kisogo chake.
Pembezoni mwa joho hilo kulikuwa kumedariziwa na nyuzi za madini ya silva. Joho lilikuwa la thamani, ila pia lililoonyesha hadhi yake ndani ya himaya kama mzee wa baraza.
Miongoni mwa watu wenye ushawishi wa maamuzi himayani. "Karibu." Phares alimkaribisha mzee. Mzee akainama kutoa heshima kwa mfalme.
.
.
"Nimekaribia mfalme," akasema kisha kuketi. "Umekuja na baraka za chakula. Karibu ule."
.
.
"Nimefurahi sana kukuta unakula. Huwa tunaamini mgeni amkutaye mwenyeji anakula, basi ameleta baraka." Mfalme Phares akatabasamu.
"Bila shaka utakuwa umekuja na falsafa ya mgeni njoo, mwenyeji apone." Mzee wa baraza akatanasamu akiyafinyanga mashavu yake yaliyokula chumvi za kutosha.
.
.
"Wala hujakosea mfalme, upo sahihi kabisa." Mfalme Phares akamminia kinywaji kwenye kombe, akamsogezea.
.
.
"Sikutarajia ugeni wako. Unastahili mapokezi zaidi ya haya."
.
.
"Usijali. Usihangaike na mzee anayeenda kufa hivi karibuni, mfalme wangu. Raha yangu ni kukuona ukiwa hai, na furaha pia."
.
.
"Nashukuru sana."
.
.
"Wa kushukuru ni mimi mfalme. Niliyetoka huko mbali kuja kukuhudumia mfalme wangu kwa kukupatia sababu ya kufurahi." Mfalme Phares akanywa kwanza mvinyo mafundo mawili kabla hajauliza;
.
.
"Sababu gani hiyo mzee wangu?" Uso wake ulishikwa na hamu ya kutaka kujua. Na yule mzee akiwa amelijua hilo, akanyanyua kombe la mvinyo na kugida huku mfalme Phares akingoja mzee amalize na kukata kiu yake.
.
.
"Huna haja ya kuwa na papara mfalme, nipo hapa kwa ajili yako," mzee akasema na kisha akatabasamu.
.
.
"Mfalme, utanisamehe kama nitakuwa nimekukwaza, ila inabidi ujue lengo langu ni kukufanya uwe na furaha." "Usijali. Karibu, waweza ukanieleza."
.
.
"Ni kwa muda sasa nimekuona ukiwa mpweke. Umekuwa ukiishi ndani ya jengo hili kuubwa mwenyewe ukizingirwa na wanajeshi, ama vijakazi.
Mfalme wangu, huoni kama ni wasaa wako sasa wa kuwapa wananchi wa Goshen malkia?"
Mfalme Phares akatabasamu. Hakujibu kwa haraka, akanywa kwanza mvinyo wake na kisha kuketisha kichwa chake juu ya tama akimtazama mzee wa baraza.
.
.
"Ni haramu kwa himaya yetu mfalme kutokuwa na malkia maana kasri itageuzwa kuwa pango la wahuni. Tulifanya makosa kutokukueleza hilo mwanzoni, lawama ni juu yetu."
.
.
"Usijali, mzee wangu," akasema mfalme. "Nitalifanyia kazi hilo uliloniambia." Mzee akatabasamu na kuinamisha kichwa chake kuonyesha ishara ya heshima.
.
.
"Sasa naweza nikaenda kwenye jambo langu la pili."
.
.
"Una lingine?"
.
.
"Ndio, mfalme. Siku zote unapoonyeshea tatizo, ni lazima pia uonyeshe suluhisho," akasema mzee kwa kujiamini kisha akapiga makofi mawili.
Punde wakatokea mabinti watatu warembo, wakaenda kusimama mbele ya meza ya mfalme.
Binti mmoja alikuwa mrefu kuliko wote, nywele ndefu nyeusi akivalia gauni rangi ya buluu iliyochoka. Uso wake ulikuwa mwembamba uliochongoka, kidevu chake kama ncha ya mkuki.
Mwingine wa pili alikuwa saizi ya wastani. Nywele zake zilikuwa ndefu nyeupe. Uso wake ulikuwa mfupi wenye mashavu na lips ndogo rangi ya pinki.
Alikuwa amevalia gauni jeupe, refu lililofunika miguu.
Wa tatu na wa mwisho alikuwa analingana kimo na wa pili, ila yeye mwili wake ulikuwa mwembamba zaidi. Shingo yake ndefu ilikuwa imepokelewa na mifupa.
Uso wake pia ulikuwa mwembamba wenye kidevu cha duara. Lips zake zilikuwa nyembamba zilizojichanua. Rangi nyeusi.
Wote waliinamisha vichwa vyao kumsalimu mfalme. Ila hakuna aliyediriki kuinua macho yake kumtazama. Wote walikuwa wanatazama chini kwa soni. "Mfalme wangu, hawa unaowaona hapa ni mabinti toka familia bora za wafanyabiashara waliojiwekeza na kulipa kodi serikalini.
Wana tabia njema na wanavuma kwa uzuri wao. Basi kwa macho yangu yaliyoona mengi nikaona pengine hapa kuna malkia wetu.
Pengine kuna atakayevutia macho na moyo wako mfalme, ukamfanya awe mama wa himaya." Mfalme alinyamaza kimya akiwatazama mabinti hao. Macho yake yalitembea kuwakagua, kushoto na kulia.
Ila yalikwama kwa binti mwenye nywele nyeupe. Alimvutia. Alitazama namna binti huyo anavyong'ata lips zake za pinki akitazama chini.
Namna anavyofinyanga vidole vyake kwa aibu. Akahisi moyo wake unapooza. Mzee wa baraza akaling'amua hilo, akajikuta ametabasamu.
Akauliza kwa sauti ya chini: "Vipi, je umempenda huyo?" Akaonyeshea kwa kichwa chake binti amuongeleaye.
Mfalme akahofia kutoa jibu la wepesi. Akasafisha koo lake akijilaza kwenye kiti. "Usiumize kichwa mfalme wangu. Ujio wangu huu ulikuwa wa kushtukiza. Ningependa kukupa muda wa kufikiri," akasema mzee wa baraza kisha akapiga tena makofi mawili, mabinti wakaondoka.
.
.
"Yule ni binti wa Melkizedeki, mfanyabiashara mkubwa wa chuma himayani. Anaitwa Tattiana. Ni mtaalamu wa mahesabu kama baba yake.
Ni mwerevu sana na mjuzi wa biashara pia."
"Nashukuru sana, mzee. Ningeomba unipe muda wa kufanya maamuzi kabla sijajitutumua kuchagua jambo." Mzee akasimama.
.
.
"Pasipo na shaka lolote, mfalme wangu. Kama nilivyosema hapo awali, ujio wangu ulikuwa wa ghafla. Naomba msamaha kwa usumbufu, lakini pia nikupe chumba upate kufikiria." Mzee akaaga na kumwacha mfalme Phares akibakiwa na mawazo zaidi. Sasa si tu juu ya taswira za Malkia Sandarus kwenye himaya yake, bali pia mwanamke wa kuoa.
Hakuwa na mawazo hayo ya mwanamke, ila sasa akawa amelewa kwa kuchambua.
Kitu kilichomfanya awe njia panda ni Rhoda. Aliwaza na kuwazua kama mwanamke huyo atakuwa tayari kuwa naye.
.
.
Lakini pia alihofia kujiingiza kichwa kichwa kwa mwanamke aliyeletwa na mzee wa baraza. Mbali na maneno ya mzee huyo kumhusu huyo mwanamke, yeye mwenyewe alihitaji kumjua kwa undani.
Basi akaamua kumuita mwanajeshi wake mmoja na kumpa maagizo: "Kamfuatilie yule binti wa Melkizedeki aitwaye Tattiana. Nataka kujua kila jambo kumhusu." Mwanajeshi akabeba agizo hilo na kutokomea kwenda kulitekeleza.
.
.
.
.
.
****
.
.
.
.
.
Sauti ya miguu ya farasi ilisikika nje ya nyumba. Punde mlango ukafunguliwa, akatoka mwanamke, alikuwa mama Fluffy.
Alikuwa amevalia kiremba kikubwa kichwani na gauni rangi ya udongo.
Mbele yake aliona farasi wanne wakiwa wamebebelea wanaume wanne wenye majambia marefu, na mwanamke mmoja aliyevalia kimapambano.
Alimtazama vema mwanamke huyu, akagundua ni mwanaye. Moyo ukamlipuka!
Haraka akamkimbilia akamkumbatia na kumpatia mabusu kedekede. Macho yake yalishikwa na maji ya machozi.
Tabasamu lake lilikuwa pana kuonyesha namna moyo wake ulivyoguswa. "Mwanangu, nilijua umeshakufa!" akasema akibubujikwa na machozi.
Waliingia ndani wakaketi, mama akiwa na kimuhemuhe cha furaha.
Fluffy akamueleza mama yake yale yote yaliyotukia. Kila jambo akamuweka wazi. Hakika hayo yakamshangaza mamaye.
.
.
"Uliwezaje kufanya yote hayo pasipo kuniambia?" "Nisamehe mama. Kila muda na kila wakati nilikuwa nahitajika kutimiza majukumu. Hivi sasa hali ilivyotulia nikaona nije sasa kukwambia."
.
.
"Nimefurahi sana kukuona mwanangu. Nilikuwa na donda kubwa sana moyoni. Nilikuwa nashindwa kulala kila usiku kwasababu ya kukuwaza wewe.
Sikujua kama upo hai. Hata nilipotaka kuja kukufuatilia, tukazuiwa maana vita zilikuwa zinaendelea huko. Himaya baada ya himaya!" Fluffy akatabasamu na kumshika mamaye mkono. "Nipo hai mama. Bado nipo hai." Wakakumbatiana.
.
.
"Ngoja nikakupikie chakula kitamu unachokipenda, mwanangu. Bila shaka usiku huu utakuwa nami. Tuna mengi ya kuongea," mama akasema akielekea zake jikoni.
Baadae, usiku ukiwa umeshika , wakiwa pamoja wanakula, wakawa wanaongea. "Sikudhania kama kuna siku itakuja kutokea himaya za wanyang'anyi zikafa," alisema mama. "Zilikuwa ni himaya zenye nguvu, zenye kuogopeka. Japokuwa zilikuwa ni za wahalifu, na kila mtu alijua, hakuna aliyediriki kuchukua hatua.
Nimefurahi sana mwanangu kuwa miongoni mwa walioziua himaya hizo. Pia mgeni wangu kuwa shujaa na hatimaye kuwa Malkia. Naona nyumba yangu imebarikiwa."
.
.
"Sasa mama ndiyo ufanye twende huko. Kule ndiyo nyumbani kwetu sasa!" Mama akatabasamu.
.
.
"Hapana mwanangu, siwezi kwenda huko. Usijali mie kwa sasa ni mzee, sihitaji kuhaha huku na kule tena na maisha. Kifo kitapata shida kunitafuta na kunipata.
Wewe endelea na majukumu yako, ila uwe unakuja kunipa salamu mama yako.
Na vipi? Umeshapata mchumba wa kukuoa?" Fluffy akacheka. "Hapana mama!"
.
.
"Unakawia nini? Au mmeadhimia himaya yenu kuwa vikongwe mkiwa mabinti?" Walitaniana na kufurahi. Kesho yake asubuhi na mapema, Fluffy akadamka na kumuaga mama yake anarejea Sawaridi.
.
.
Mama akamkabidhi karatasi fulani chakavu yenye rangi ya bati lenye kutu.
Alimminyia karatasi hiyo kiganjani na kisha akaificha kwa kuvifunga vidole vya binti yake. "Nimeihifadhi kwa muda mrefu sana hiyo karatasi. Niliipata mbali sana kipindi nikiwa binti kama wewe. Ila sikupata wasaa wa kufuatilia yale yaliyopo ndani.
Hivi sasa ni mzee, sina tena nguvu hizo. Nakukabidhi wewe. Na nakusihi usije ukawa kama mimi. Usipuuzie kilichomo humo ndani.
Abadani!"
.
.
.
.
.
*NINI HICHO KIMO NDANI YA KARATASI HIYO KUUKUU?*
.
.
.
*NINI MFALME PHARES ATAFANYA JUU YA NJIA PANDA YAKE?* *NA RHODA JE?*
.
.
.
*KARIM YUPO WAPI? AMEMRUDISHA DADA YAKE ULIMWENGUNI? NA SULTAN AMEPATA HABARIZE?*