*MKUFU WA MALKIA II -- 59*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Lakini kabla hawajatoka humo wakagundua huko nje wanajeshi walikuwa wanarandaranda huku na kule, wengine wakiwa juu ya farasi na wengine kwa miguu.
Na haikuwa sayansi ngumu hii kuitambua, kuwa wao ndio walikuwa wakitafutwa!
ENDELEA
Wakajawa na hofu sana na pengine sasa vichwa vyao vikakubaliana kuwa kamwe hawataishi kwa amani ndani ya himaya ile ya kigeni.
Toka wameingiza mguu wao humo maisha yao yamekuwa ya kuhaha. Kuhangaika na kurandaranda. Swala hili liliwaumiza sana.
Na wakafikiria kama kuna haja ya kukimbilia himaya nyingine pengine huko watapata ahueni. Lakini vipi napo pakawa hapana unafuu? Watakimbilia kwenye himaya za watu mpaka lini? Swala hili likawaumiza vichwa haswa.
Baadae walipoona hali ni shwari, wakaaga na kwenda zao. Kwa tahadhari kubwa wakatembea mpaka kurejea kule kwa majamaa zao. Walipofika hawakuwakuta, nyumba ilikuwa tupu.
Wakatulia na kungoja. Wakarafuta kama kulikuwa na chochote cha kutia mdomoni maana matumbo yalikuwa matupu, napo wakakosa. Vyombo vilikuwa vichafu na vikavu!!
Tangu asubuhi walipoamshwa na kuwajibishwa kwenda kwa Rabis hawakuwa wametia kitu mdomoni mpaka muda huo, achilia mbali vitumaji na vituchakula walivyovipata toka kwa msamaria mwema aliyewasitiri.
Njaa ilikuwa inawaum na kadiri muda ulivyokuwa unasonga ndivyo hali ikazidi kuwa mbaya zaidi.
"Tunafanyaje sasa?" Ottoman akauliza. Alikuwa amekunja sura kulalama na njaa ikwanguayo tumbo.
"Sijui," Oragon akamjibu kaka yake akipandisha mabega. "Tungoje, labda wanaweza wakaja na chakula."
Wakangoja lakini wakijua jambo hilo ni la uwezekano mdogo tu. Wale majamaa kurejea na chakula, haikuwa kitu cha kuipa kipaumbele, ila hawakuwa na namna zaidi ya kungoja.
Wakakaa humo mpaka wakaanza na kusinzia. Majira ya jioni kabisa, jua likiwa limeshafifia wakasikia sauti ya tangazo huko nje. Wakakurupuka toka katika usingizi wao wa njaa na kuangaza dirishani.
Wakawaona wanajeshi wawili wakiwa juu ya farasi wakitangaza juu ya sherehe ya unyongaji inayoenda kufanyika hapo karibuni baada ya kufanikiwa kumkamata mhalifu mkubwa himayani.
Hivyo wananchi wote walikuwa wanakaribishwa kuhudhuria sherehe hiyo itakayoanza dakika chache mbele kwenye uwanja wa halaiki!
Wakina Oragon wakataman sana kwenda kushuhudia lakini wakaogopa. Waliona ni kama kujipeleka kwenye mdomo wa mamba. Huko wakionekana wanaweza wakakamatwa na wao kunyongwa pia!
Basi wakaendelea kutulia humo ndani lakini katika hali ya kushangaza, baada tu ya dakika chache mtaa wote ukakauka!! Hakuonekana mtu hata mmoja akikatiza, wala sauti ikisemaza.
Oragon na kaka yake wakatazama nje kupitia dirishani. Huku na huko. Hapa na pale. Kimya!!
Hakukuwa hata na ishara ya binadamu. Laiti kama mtu angekuja hapo muda huo basi angesema mji huo ni maghofu tu ya watu wa kale.
"Otto," Oragon akaita. "Twende tukatafute chakula sasa!'
"Wapi?" Ottoman akashangaa. Uso wake ulieleza hofu.
"Huko majumbani!" Oragon akamjibu. "Watu wote wameondoka, wameenda kutazama unyongaji. Twende tukapekue vyakula sasa!"
Ottoman akasita. Ila atakula nini endapo akigoma?? Akajiuliza. Hakuwa ma budi kukubaliana na kakaye.
Kwa tahadhari wakatoka ndani, wakachungulia njia. Kulikuwa salama. Wakajongea ado ado na kuzama ndani ya nyumba moja iliyokaribu baada ya kuhakiki usalama wake.
Humo kulikuwa giza wakawa wanatumia milango yao ya ufahamu kusonga.
Wakapekua huku na huko. Kweli wakapata chakula. Wakala na kushiba, na hapo ndipo wakapata wazo jingine. Wasile tu chakula bali watazame na kubeba vitu vingine vya thamani!
Lengo lao likiwa ni kutengeneza tena fedha zao zilizoibiwa kisha watazame ustaarabu mwingine.
Wakaanza kukomba kila walichokiona kinang'aa na kukitia kifurushini. Walipomaliza ndani ya nyumba hiyo wakaenda nyingine na nyingine mchezo ukiwa ni huo huo, somba na uweke ... somba na uweke.
Nyuso zao zikajawa na matabasamu.
Walipozama kwenye nyumba ya nne, nyumba waliyoapa kuwa itakuwa ya mwisho kisha waende zao, wakasikia sauti ya mtu humo. Haki wakashtuka na kutepeta hofu!!
Sada wakajua mwisho wao umewadia. Endapo mwenye nyumba yu ndani, basi ni hilo ni komo.
"Nyie ni wakina nani?" Sauti iliulizia gizani. Jua lilikuwa limeshaanza kupotea sasa hivyo hizi nyumba zilimezwa na kiza.
"Nyie ni wezi enh?" Sauti ikauliza tena. Oragon na kaka yake wakatazamana. Macho yao yalikuwa yanang'aa kana kwamba paka gizani. Walijawa na woga. Hawakuwa na cha kujibu.
Mara wakasikia vishindo vya mtu, na punde akatokea yule aliyekuwa anawauliza. Kumbe alikuwa ni miongoni mwa wale majamaa zao!!
Yule mtu mfupi.
Akacheka sana kisha akawapongeza wakina Oragon.
"Sasa mmekwiva haswa! Tunaweza tukafanya kazi pamoja."
"Ulikuwa unafanya nini humu?" Oragon akamuuliza. Jamaa akatabasamu kisha akatoa jiti lake mfukoni na kuanza kusugulia nalo meno.
"Unamuuliza mwizi anafanya nini ndani ya nyumba? ... nilikuwa natekeleza kazi yangu kama nyie mfanyavyo!"
"Sisi sio wezi!" Akasema Ottoman.
"Ni wakina nani basi kama sio wezi? Mnafanya nini hapa marafiki zangu?" Jamaa kafupi akauliza.
"Sisi sio marafiki zako!" Oragon akafoka. Kisha akamtazama Ottoman na pasipo kuongea wakatoka ndani ya nyumba hiyo.
Nyuma yao yule jamaa mfupi akawafuata.
"Leo hamnitaki? Na kuwasaidia kote huko?" Mgongoni mwake naye alikuwa ana kafurushi ila si kikubwa kama kile cha wakina Oragon. Pengine yeye alikuwa ameanza kazi muda mfupi hapo nyuma na ile nyumba ndiyo ilikuwa nyumba yake ya kwanza.
Wakina Oragon wasimjali wakanyoosha miguu yao kujiendea.
"Naweza nikawasaidia zaidi. Mtaenda wapi ndani ya himaya hii kama hamtanisikiliza?" Akaendelea kuongea. Mara ghafla Ottoman akageuka na kumkunja nguo.
"Achana na sisi! Mlitarajia tutakufa mlivyotutoa sadaka kwa Rabis? Mmekosea sana. Haujui ni mangapi tumepitia na hili si la mwisho!"
Aliposema hayo akamsukumiza jamaa huyo, akadondoka chini wakaendelea na safari yao.
"Hamuwezi kuishi ndani ya himaya hii pasipo sisi!" Akaropoka jamaa huyo akiwatazama wakina Oragon wanaishia. "Mtakamatwa na kuuawa muda si mrefu!"
Wakina Oragon hawakumjali. Wakaendelea kukazana wakiwa sasa wamepata kiburi na mali walizonazo.
Lakini wasifike mbali, wakasikia sauti za farasi!! Mioyo ikakita. Walikuwa ni wanajeshi!!!
Kabla hajawafanya lolote, mara yule jamaa mfupi akapaza sauti kuwaita.
"Njooni huku!"
Akielekea upande wake wa kushoto kwa kasi. Hawakuwa na budi zaidi ya kumfuata jamaa huyo upesi!
**
"Nimeipata!" Lucy alipaza sauti yake kwa furaha. Alimkumbatia Bella kwanguvu zake zote kisha akambusu shavuni mara tatu!
"Nini kimekupata??" Bella akashangaa. Lucy akarudishia mlango wa chumba chao baada ya kutazama usalama alafu akamketisha Bella kitako juu ya kitanda.
"Kazi yetu sasa imekwisha!" Akasema kwa furaha. "Nimepata moyo wa mfalme!"
"Lucy, nini wasema?" Bella akatahamaki.
"Nilikuwa nakwambia mfalme si mtu wa kawaida, ukawa huamini. Leo nimeupata moyo wake chupani kabatini!"
"Hakika?" Bella akauliza akikodoa macho.
"Ndio, hakika! Nimepata moyo wake kule kabatini umo ndani ya chupa!"
"Sasa?" Bella akauliza. "Mbona umeuacha huko?"
"Usijali," Lucy akamtoa hofu. "Nimeuhifadhi mahali salama kabisa. Leo majira ya usiku wa kutosha tumwite mkuu na tumwambie kila kitu kipo tayari sasa!"
Bella akamnyaka Lucy na kumkumbatia.
"Hatimaye tutarudi kwenye miili yetu," akasema kwa tabasamu pana. "Hatimaye tunarudi nyumbani!"
"Hapana!" Lucy akatikisa kichwa. "Sio tu tunarudi nyumbani bali na hapa tunapafanya kuwa nyumbani!"
Wakacheka haswa.
Sasa walikuwa wamefikia kwenye komo tamu. Kukusanya tu taarifa za Goshen na kuzifikisha kwa Jayit hakukuwa kunatosha. Leo imekuwa bahati iliyoje kupata kitu cha zaidi mbali na matarajio yao!!
Kitu cha thamani, aghalabu, amali! Hakika walitegemea kingemfurahisha mkuu wao.
Baadae baada ya kutengenezea madhabahu yao vema, wakamwalika mgeni wao kukaimu. Wakamweleza kinaganaga kuwa vita imeshakwisha. Hawana tena haja ya kumwaga damu.
GOSHEN IPO MIKONONI MWAO!!
Basi Jayit akiwa mjawa wa tabasamu, akawaambia wajiandae kesho karamu yaja!
***