*MKUFU WA MALKIA II -- 63*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
"Kila kitu??" Venim akatoa macho.
"Ndio," Rhoda akajibu kwa maringo. "Kila kitu ... nami nitakupa kila kitu."
ENDELEA
Hicho ndicho alikuwa anahitaji Rhoda kwa Venim na si kingine. Kujua kila kitu anachokijua mwanaume huyo. Hilo ndilo lilikuwa lengo lake hapo na kingine kile.
Na alikuwa anaomba ayajue hayo kabla hajamkabidhi mwili wake Venim. Hakuwa anataka kabisa. Na kichwani mwake alishapanga kuwa akishafahamu hayo yote anayoyataka, basi Venim asahau kabisa kuhusu kumpata.
Utalalaje na mwanaume asiyekusisimua wala kukuvutia kwa lolote lile?? Alijisemea kifuani. Venim hakuwa na sababu hata punje ya kumfanya ahamasike kufanya tendo.
Kila mwanaume huyo alipomuwekea mkono mwilini alihisi kutetemeka. Alikuwa ni wa baridi kama chura. Na kila anapomtazama anaogopa. Hajaizoea sura yake kabisa japo wanaishi chini ya paa moja.
Atawezaje kumpa mwili mwanaume wa hivi??
Lakini zaidi ya hapo, alikuwa anajikinga asije kujikuta anabeba mimba ya Venim pasipo kutaka. Kwa mbingu ama kwa ardhi, hakuwa anataka jambo hili litokee kamwe!!
Kubeba mimba ya Venim kutakuwa ni agano ambalo litamuwia vigumu kulivunja. Hakutaka kabisa kuwa na familia na mwanaume huyu wa ajabu, na aliapa kujitahidi kuzuia hilo.
"Basi kuanzia sasa, tutabadili ratiba," alisema Venim. "Nitakuwa nakufundisha jua linapochomoza, linapokaa katikati na linapozama kila siku!"
Rhoda akafurahi.
"Upo tayari?" Venim akamuuliza akitabasamu.
"Ndio, nipo tayari muda wowote."
"Lakini," Venim akampa tahadhari. "Mafunzo mengine tutayafanya nyakati za usiku wa manane peke yetu ndani ya misitu. Na mengine yakihusisha kuua viumbe hai kama binadamu. Utakuwa na moyo wa kustahimili hayo??"
Rhoda hakufikiria mara mbili akasema:
"Nipo tayari!" Kwa uso wa ujasiri. Venim akatabasamu.
"Sawa," akamshika Rhoda mkono. "Lakini pia kuanzia sasa itabidi uanze kubadili vyakula unavyokula. Hauwezi kuwa mlozi kamili kama waendelea kula vyakula vya binadamu!"
"Vyakula gani hivyo?" Rhoda akauliza kwa macho ya kidadisi.
Venim akamwambia ataanza kwanza kwa kunywa damu ya watu. Kisha baada ya hapo, ataanza kula nyama zao pia. Rhoda akaridhia.
"Nitajitahidi."
Hakika hapo Venim akashangazwa na ujasiri huo wa Rhoda. Hakusita kabisa kukubali yote hayo. Hakuonyesha hata chembe ya woga machoni mwake!!
Lakini Venim akashindwa kujua dhamira halisi ya Rhoda. Mapenzi yalimpofusha macho na kuzubaisha akili. Kila kitu kuhusu Rhoda alikiona chema na kisicho na shida.
Aliamini Rhoda ameamua kubadilika ili aendane na mumewe. Jambo ambalo lilimfanya awe na furaha sana moyoni.
Akamfundisha Rhoda ulozi siku hiyo nzima kabla jioni hawajapumzika na kutia chakula tumboni.
Katika meza ya chakula, Rhoda akakabidhiwa bilauri kubwa lililojaa damu.
"Leo utaanza na hilo," Venim akamsihi.
Rhoda akala chakula na kumaliza, kisha taratibu akaanza kunywa damu aliyojaziwa bilaurini. Kabla hajanywa, harufu ikamkereketa. Akataka kutapika!
Haraka akaliweka bilauri chini akikunja uso. Venim akatabasamu. Akamtia moyo ni mara yake ya kwanza hivyo ni kawaida. Atazoea tu hivi karibuni.
"Taratibu taratibu, usijali."
Rhoda akanyanyua tena bilauri la damu na kulipeleka mdomoni. Akajitahidi kupambana na harufu. Akaria mara moja.
Ila sasa akashindwa kuzuia kutapika. Haraka akanyanyuka na kukimbilia kando akatapika chakula chote akichokula.
Venim akahofia. Akamtaka aache hilo zoezi kwa siku hiyo, atalifanya hivi mbeleni. Rhoda akatulia kwanza kuvuta hewa. Alipotosheka akarudi kitini na kushika tena bilauri.
Alitaka ajaribu tena!!
Lakini Venim akamzuia. Hapa akagiza vijakazi wake waondoshe bilauri hilo mbali.
"Pengine tujaribu njia nyingine," akapendekeza.
"Njia gani hiyo?" Rhoda akauliza upesi.
Venim akafikiria kidogo kisha akamtahadharisha njia hiyo ni fupi, ila hatari zaidi. Na endapo akiifuata njia hiyo basi atatoka katika mfumo wake wa binadamu moja kwa moja na kuwa kama yeye.
Hata mtu atakapomuona popote pale basi atajua kuwa yeye ni mlozi - mtu mwenye nguvu za kilozi ndani yake!!
"Ni njia ipi hiyo??" Rhoda akauliza kwa shauku.
"Njia ya ubatizo!" Venim akamjibu. "Utakapobatizwa utapewa jina lako la kilozi na mwili wako wa kipekee. Upo tayari?"
"Ndio, nipo tayari," Rhoda akatikisa kichwa.
"Sawa. Basi keshokutwa pindi mwezi utakaposimama kamili angani, tutaenda huko kaskazini ya mbali kwa ajili ya shughuli hiyo."
Rhoda akatabasamu. Mapigo yake ya moyo yalienda mbio kwa furaha.
**
"Nefil njhami khatu habab? ... Nefil njhami khatu habab?" Sauti hii ilikuwa inaongea huku ikififia.
"Nefil njhami khatu habab?" Ilivuma. Ikashuka mawimbi ... "Nefil njhami khatu habab?" Ikaishilia kwa mbaali ... "Nefil njhami khatu habab?"
Sauti hii ilifanya hivi mara tatu lakini hakuna mtu aliyekuwa anasikia wala kuijali. Iliishia kusema hivyo na mwishowe ikapotea kabisa!
Ulikuwa ni usiku mzito. Huko gerezani wengine walikuwa wanateta, wengine walikuwa wamelala, wengine walikuwa wanalia.
Kila mmoja alikuwa amejazwa na hofu kifuani mwake. Ungeliona hilo usoni. Hakuna aliyekuwa anajua kuhusu kesho yake. Mambo yaligeuka, tena upesi! Hakuna aliyepewa hata muda wa kufikiria.
Ni kama vile kufumba na kufumbua macho, A ikawa Z!!
Kwenye chumba kimoja cha gereza, mama Tattiana alikuwa amekaa akiegemea nondo. Uso wake ulikuwa mkavu, macho yaliyolegea kwa kuchoka kulia. Mashavu yalikuwa na michoro kadhaa ya machozi.
Amekuwa akimlilia mwanae aliyemwacha kasrini. Hajui hatma yake ni nini huko kama yu hai au mzima. Wakati wengine wakipata usingizi, hata wakajilaza, yeye hakuwa nao hata lepe!
Wakati wengine wakiwa wanateta, yeye alikuwa anagugumia na moyo wake. Ni bora angekuwa naye mule gerezani akamwona na kumshika.
Alijua hata angeomba akamwone mwanae asingeruhusiwa hata kidogo. Hakuwa na namna. Japo walikuwa ndani ya himaya moja, alijihisi ametupiwa himaya ya mbali mno.
Nini mama pasipo mtoto??
Kong! Kong! Kong!!
Nondo zikagongwa na kumshtua kila mmoja ndani ya chumba. Wote wakatazama langoni. Walikuwa ni vijakazi wawili wa Jayit, sura mbaya za kuogofya. Mikononi wamebebelea jambia ndefu zinazong'aa. Walisimama hapo na kuwakagua kwa macho yao yanayotisha!!
Kisha wakatazamana na kuteta katika lugha ambayo hakuna mwingine aliyewaelewa. Na mara wakafungua lango na kuwabeba wanawake wawili.
Wanawake hao wakalia kwa hofu kuu. Wakalia wakiwaomba wenzao wawasaidie lakini nani atathubutu??
Kila mmoja alikuwa anatetea uhai wake. Waliishia kuwatazama wanawake hao waliobebwa kwa macho ya hofu mioyo ikiwaenda mbio.
Hawakujua wenzao walipelekwa wapi na walienda kufanywa nini. Lakini majambia yale mikononi mwa wale vijakazi yaliwatisha. Pengine wameenda kutolewa sadaka!!
Hata wale waliokuwa na usingizi ukakoma, wote wakabaki macho wakilia na kuomboleza. Wakanena na kuelezana.
Lakini tofauti na mawazo yao, baada ya dakika kadhaa, wanawake wale waliobebwa wakarejeshwa tena chumbani. Walikuwa hoi wanalia!!
Wakatupiwa ndani na lango likafungwa!
"Ni nini kimewakumba huko?" Wenzao wakawauliza. Wakaeleza kuwa wamebakwa kwa zamu. Na haikujalisha ni kwa namna gani walilia kwa maumivu makali waliyoyasikia, hakuna aliyejali.
Wakiwa wanaongea hapo, mara wakashtushwa tena na sauti ya lango likigongwa!!
Kong! Kong! Kong!
Wakatazama.
Huko wakawaona vijakazi wengine wawili wa Jayit. Kabla vijakazi hao hawajafungua lango, wakamtazana mama Tattiana kisha wakaongea katika lugha yao ya pekee.
Mama Tattiana akapata hofu nzito. Sasa akajua zamu yake imewadia!!
**