Simulizi: Mimi na Mimi

Simulizi: Mimi na Mimi

Jamn mnasema ndoto mpak episode inaenda ya tano MBNA JC alikuwa anaota na tunajua ni ndoto hiyo nikweli amekufa sio yye yye tu mpka adellina bobo kwahyo tuwaombee watakuja wengne
 
MIMI NA MIMI 3

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Siri, Tamaa, Hila, Usaliti, Ukatili, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★★★★★★

SEHEMU YA KUMI NA TISA

★★★★★★★★★★★★★★★★★



Ilikuwa ni Tesha. Nikabaki nikimwangalia kwa umakini alipokuwa akinikaribia, na alikuwa ameweka uso makini.

"JC... mbona umekuja hapa? Huyo alikuwa nani?" Tesha akauliza.

Nikaacha kumwangalia na kusema, "Twende turudi. Nimeemaliza kupunga upepo."

Nikataka kumpita, lakini akasimama mbele yangu kama kunizuia na kusema, "Ngoja JC."

Nikamwangalia usoni.

"JC nini kinaendelea?" akaniuliza hivyo.

"Kuhusu nini?" nikamuuliza pia.

"JC... mimi siyo mgeni kwako kaka. Nakujua. Nakuangalia... ninaona kabisa kuna kitu kinakusumbua. Sisi wote tuna huzuni, lakini... wewe... sijui tu hata nisemeje uelewe..." akasema hivyo.

Nikaendelea tu kumwangalia.

"Nakuangalia, lakini ni kama vile sikujui. Kama vile kuna kitu unaficha JC," Tesha akaniambia.

Nikamtazama kiumakini na kuuliza, "Kwa nini useme hivyo?"

"We' ndo' uniambie. Nini kinaendelea? Huyo mtu alikuwa nani?" akauliza.

"Hamna umuhimu wowote kukuambia kuhusu..."

"We' niambie, kama hamna jambo unaficha..."

"Nina..." nikaishia hapo tu baada ya kutaka kuongea kwa hisia kali.

Akatulia na kuendelea kuniangalia kwa macho yenye huzuni.

Nikafumba macho na kukaza hisia zangu, nami nikasema, "Unaona nini Tesha? Kwa nini unafikiri... unahisi kuna jambo gani naficha?"

Akasema, "Labda nakosea. Na sitaki niwe sahihi, maana... kama kweli kuna jambo unaficha kuhusu haya yote yaliyotokea kaka... sijui kama nitaweza kuelewa sababu zako za kutosema endapo kama hautaniambia."

Nikamwangalia usoni, nami nikamshika begani na kusema, "Nisamehe Tesha."

Akabaki kunitazama kwa hisia.

"Nisamehe... sikuwepo nanyi haya yote yalipotokea... najua jinsi unavyoumia," nikamwambia hivyo kwa hisia.

Akaangalia pembeni, huku machozi yakimjaa, naye akasema, "Sielewi JC. Yaani... bado sielewi. Hh... inawezekanaje yaani... da' Mimi... Bobo... afe namna ile, yaani... ah aisee..."

Alionyesha jinsi alivyoukaza uchungu mwingi moyoni wake, nami nikaona nimkumbatie tu.

"Ah! JC! Sss... inauma sana kaka, yaani... dah!" akaongea kwa hisia sana na kunikaza mgongoni.

Ni wazi Tesha pia alihitaji sana kutiwa moyo, na mimi ndiye mtu wa karibu zaidi kwake ambaye alitegemea kuipata faraja ingawa nami nilikuwa kwenye maumivu ya kihisia. Lakini nikashindwa kujua hata nimwambie nini. Alihisi kuna vitu nilikuwa sisemi, na hakujua ni mengi kadiri gani nilikuwa nimebeba moyoni mwangu yaliyosababisha nisiseme. Kumbatio ndiyo likabaki kuwa faraja pekee ambayo ningeweza kumpatia mdogo wangu huyu, na baada ya sekunde kadhaa za kushikiliana namna hiyo nikamwachia na kumwangalia alipokuwa akijifuta machozi.

Nikamwambia, "Kila kitu kitakuwa sawa Tesha. Tumepitia mengi. Najua tulitavuka na hili."

Tesha akatikisa kichwa kama kukataa na kusema, "Sijui kama nitaweza JC. Yaani... sijui kwa kweli..."

Machozi yakakaribia kunitoka, nami nikajizuia na kuangalia pembeni.

Tesha akashusha pumzi na kusema, "Sometimes nahisi ni kama vile naota yaani."

Nikatikisa kichwa kukubaliana na hilo na kusema, "Mimi pia."

"Bado naona kama kuna mchezo hapa JC. Haiwezekani Bobo na Adela wauawe... ndani ya siku moja... vibaya yaani... nani angeweza kufanya kitu kama hicho? Yaani naona ni kama mpango kaka... na ninahofia... hayo matukio yanaweza kuendelea...." akaishia hapo tu.

Nilikuwa nikimtazama kwa hisia sana.

"Hauna wazo lolote... juu ya nani angeweza kuwafanyia hayo JC?" akauliza hatimaye.

Nikaangalia pembeni tu.

"Kaka..." akaniita.

Nikatikisa kichwa kukanusha, nami nikasema, "Sina idea. Ngoja tuone tu mapolisi watapata nini Tesha. Sisi... kilichopo sasa hivi ni kuwa pamoja. Tuwe pamoja na wengine Tesha... wanatuhitaji sana."

Akaangalia chini tu.

Nikamshika begani tena na kusema, "Najua yaliyotokea ni mazito Tesha. Lakini nakuomba uniahidi kitu kimoja. Naomba uniahidi kwamba utakuwa imara sana. Uwe imara hasa kwa ajili ya Mariam. Alichokuwa Miryam... kimebaki kwako sasa. Niahidi kwamba utakiendeleza Tesha."

Aliniangalia kwa njia yenye mkazo kiasi, naye akauliza, "Kwa nini unaniambia hivi?"

Nikafumba macho na kusema, "Just... tafadhali niahidi. Niahidi mdogo wangu."

Nilipomwangalia, Tesha alikuwa ametazama chini sasa, naye akatikisa tu kichwa kukubaliana nami.

Nikamwachia na kusema, "Asante. Twende turudi ndani."

Nilisema tu hivyo na kumpita, naye akaanza kufata nyuma yangu pia. Hisia zilinikaba sana muda huo, yaani nilijihisi kuwa mnafiki wa hali ya juu mno. Mpaka tumerudi pale ndani sikumsemesha tena Tesha, na nilikuta mazingira yakiwa vile vile nilivyoyaacha. Inaonekana baada ya mimi kuondoka muda mfupi nyuma walianza kuongea baada ya kumaliza chakula, kwa kuwa nilikuta wakina Bi Jamila, Bi Zawadi, Mariam na Ankia wakiwa wanalia kwa sauti za chini na kupewa faraja na wengine. Hali ya maumivu na hisia ya unafiki niliouhisi kutoka kwangu zikamilemea pia kiasi kwamba nikashindwa kuvumilia kukaa hapo, nami nikaelekea tu huko juu kujaribu kuwa peke yangu kwanza.

Niliingia tu kwenye chumba ambacho alitumia Nuru kabla ya kuondoka hapa nyumbani ile juzi, nami nikakaa kwenye kitanda huku nikiinamisha uso kwa huzuni. Kuna sehemu ndani yangu ilitamani hii iwe ndoto, kila mara nilipofikiria, yaani nilitamani tu nifumbe na kufumbua macho kukuta pamekucha na kila kitu kipo sawa kabisa. Lakini uhalisia haungeweza kunipa tena zawadi hiyo. Hili lilikuwa ni picha halisi, nitake nisitake, Miryam tayari alikuwa amenitoka. Nikaitoa mfukoni laini ambayo yule mwanaume alinipatia na kuiangalia kwa umakini, nikiwa naelewa kwamba mambo mazito zaidi yangefuata kuendana na kile alichoniagiza nifanye kutoka kwa Bertha.

Nilizama kwenye fikira nzito hadi nikawa sijatambua kwamba kuna mtu aliingia chumbani humo, hadi alipofika karibu kabisa na nilipokaa na kusimama mbele yangu, kisha akanishika kidevuni kwa vidole vyake viwili na kunifanya ninyanyue uso wangu kumtazama. Ilikuwa ni dada yangu, Jasmine, na kumwangalia usoni kulinionyesha hali yenye kujali sana kunielekea, akiwa anataka kunipa faraja bila hata kutumia maneno. Nikalemewa na huzuni zaidi baada ya kumwangalia hivyo, machozi yakanijaa kwa kasi sana, nami nikakikumbatia kiuno chake hapo hapo na kuanza kuitoa huzuni yangu kuu kwa kilio. Nilimkaza Jasmine na kuendelea kulia, yeye akifanya "shhh" na kukibembeleza kichwa changu kwa upendo.

Nilikuwa kwenye maumivu ambayo hakuna mtu yeyote hapo angeweza kuelewa uzito wake, lakini kitulizo kidogo nilichoweza kupata kutoka kwa dada yangu kikanipa uwezo wa kujipa nguvu za kuvumilia. Ni muda mfupi kutokea hapo na Jasmine akaitoa mikono yangu kwake taratibu, akanifuta machozi na kunitia moyo akisema asingeacha kuwa pamoja nami kwa sababu alielewa ni jinsi gani niliumia sana, nami nikamshukuru sana kwa hilo. Lakini nikamsihi tu aelekee kujipumzisha kando ya wanaye kwa kuwa sote tungehitaji mapumziko, hivyo kwa pamoja tukatoka humo ili kweli kwenda kupumzika.


★★★


Usiku huo ulionekana kusonga taratibu hadi sote tulipoweza kupata nafasi za kuipumzisha miili yetu, wageni wakipata vyumba vya kushiriki na hata wengine kulala sebuleni pia, na kwa upande wangu pia nikaweza kupata usingizi niliohitaji kuupa mwili nguvu. Siyo kwamba nilienda tu na kufumba macho shwaa, usingizi ukaja, la. Ilinichukua muda kuupata usingizi huo kwa kuwa bado huzuni yangu ilikuwa nzito. Nilijikuta namkumbuka sana Miryam wangu, nikawa naangalia picha zake nilizotunza kwenye akaunti ya simu yangu na kujikuta nikitokwa na machozi kila nilipokumbukia mambo yote tuliyokuwa tumepitia. Na nadhani nikasinzia huku bado simu ikiwa mkononi kutokana na uchovu kuulemea mwili wangu.

Nililala kwenye gari langu pamoja na Simba, ambaye kwangu pia alikuwa sehemu muhimu ya kupata kitulizo kwa kiasi chake. Kwa hiyo nilikuja kuamshwa na Jasmine kwenye mida ya saa tatu asubuhi, ili nikapate chai, nami nikaenda kufanya hivyo pamoja na wengine pia. Wengine wote walikuwa wamekwishaamka. Mzee Manyanza hakwenda kazini, akiwa amechukua muda wa siku chache nje ya kazi kushughulika na msiba huu, hivyo wanaume tukakaa kwenye masofa sehemu ya varanda hapo nje kupata chai na kuzungumza kwa ufupi. Wanawake walikuwa huko ndani au wakitoka kwenda hapa na pale na kuendelea kuonyeshana ushirikiano wenye amani, na sisi; mzee Manyanza, Tesha, Simba, marafiki zake mzee watatu aliofanya nao kazi, na mlinzi wa wazazi wetu pia, tukawa tunazungumza kiufupi.

Tayari maaskari wale walikuwa njiani kufika huku kama walivyoahidi jana ili kuja kunihoji. Simba, akiwa ni mwanajeshi, angeweza kutumia ujuzi wake kuonelea kwamba visa vya Adelina na Bobo vilikuwa vyenye utata mkubwa uliolenga shabaha ya kitu kimoja kuwa ndiyo sababu ya mambo yaliyowapata kuwapata, ingawa wawili wale hawakuwa na ukaribu. Yalikuwa maongezi yenye utulivu tu kujaribu kuweka mambo haya au yale bayana, na mimi kiukweli sikuwa na mengi ya kuchangia ingawa nilijua mambo yote kwa undani. Nilikuwa nikifikiria tu kuhusu maneno ya yule mwanaume aliyetumwa jana, ambayo najua ningetakiwa niyaseme pindi ambapo maaskari wangefika.

Tesha sasa akawa anaongea, akisema mambo fulani kumhusu Bobo. "Asa' ile juzi yake, akawa ameniambia... tufanye kitu ili kumfurahisha nani, Ankia. Maana bado alikuwa amemnunia... na huyo Ankia anajua kudeka kweli..."

Akawafanya wakubwa watabasamu kidogo.

"Nikampa mawazo na nini, akaona kumpeleka Mlimani City kule ndo' wazo zuri. Tena ilikuwa kuangalia movie ile ya Eonii... tukakubaliana kumshawishi Ankia twende wote ili aka-enjoy. Hiyo movie yenyewe hata huwa siyo nzuri kihivyo..." akasema Tesha.

"Eeh, wanaipaga hype sana, eti mapinduzi ya filamu, lakini Bongo kwa movie bado..." Simba akasema kiutani.

"Hahah... bora tu waendelee kutamba na tamthilia hizi," akasema rafiki yake mzee.

"Yeah, angalau tamthilia," mzee akasema.

Tesha akasema, "Eeh, sema... Ankia anapenda sana movie hizi za wabongo, lilikuwa wazo zuri kwa sababu hakuwahi kuiona hiyo movie... tena ingekuwa siyo kwa sababu tu ya movie, yaani kumpa ile experience kwenda sehemu kama theater yaani... halafu na mambo mengine mazuri yafate... kama hivyo."

Wengine wakatikisa vichwa kuonyesha uelewa

"Bobo alikuwa anapenda sana kushirikisha rafiki akiwa kwenye... dilemma... yaani, alipokuwa hana uhakika afanye nini, angeniuliza, angeniomba ushauri, halafu ndiyo angeamua la kufanya. Ni mambo yaliyomfanya awe mwana sana, yaani alijali sana maoni ya marafiki zake... na alikuja kumjali sana Ankia hapa mwishoni, alimpenda mno... akawa tofauti kabisa na tulivyomzoea mwanzo, ile uhuni na nini... ukapotea. Yaani alitaka kufanya kila kitu ili amfurahishe Ankia..." Tesha akaeleza.

Nilimwangalia kwa uelewa mwingi, nikijua hayo aliyosema kuwa kweli kabisa.

Akaendelea kusema, "Alikuwa serious, alianza kufanya na maandlizi kesho yake tu, me ningetakiwa nisubirie, halafu nimpange Ankia kutoka bila kumwambia tunaenda kukutana na Bobo huko..."

"Ili iwe surprise," rafiki yake mzee akasema.

"Eeh. Asa'... nilikaa kumngojea kama hivyo, akabaki kimya tu, na ni siku ambayo niliwahi kumaliza shift yangu kazini, kwa hiyo nilipoona anachelewa kunitafuta nikaona nimpigie. Tafuta, tafuta, tafuta, wapi. Mpaka siku ikapita. Ndiyo taarifa za dada zikaja, hatujakaa sawa na zake Bobo zikafata. Tsk... iliuma sana," Tesha akaongea hivyo.

Nikaangalia chini kwa huzuni.

"Tulikuwa kwenye mshtuko baada ya kupewa... taarifa za dada. Imekuja na ya Bobo... nilichoka yaani. Yaani kuona kilichompata iliogopesha. Mpaka nikawa nawaza ingeweza kunipata mimi pia, maana tulikuwa karibu mno..." Tesha akasema.

"Vipi kuhusu ndugu zake Bobo?" mzee akamuuliza.

"Mtsk... hatukuwahi hata kuongea sana kuhusu familia yake, lakini... nafikiri walikuwa watu wa huko Mbeya. Sijui hata kama watakuwa wamezipata hizi taarifa.... sijui kama... inawezekana kuna mtu huko anamuwaza sana..." Tesha akasema.

"Tutajua. Tutawatafuta ndugu zake wote pia na kuwapa pole," mzee akasema.

Tesha akatikisa tu kichwa kukubaliana naye.

"JC..." Simba akaniita.

Nikamwangalia.

"Mara ya mwisho umemwona Adelina ilikuwa lini?" Simba akaniuliza.

Nikaangalia chini tu na kubaki kimya.

"Si ni ile siku umetoka kwake baada ya kukutana na Miryam? Hukuonana naye tena?" Simba akaniuliza kwa mara nyingine.

Nikatikisa kichwa kukubali.

"Inabidi uwe mwangalifu sana kuhusu utakachowaambia mapolisi kaka," Simba akasema.

"Una maana gani?" mzee akamuuliza.

"Jinsi tu mambo yalivyo, mapolisi wanaweza wakamchanganya JC kwenye mahojiano yao. Si unajua wakiwa wanafanya uchunguzi wanapendaga ku...."

"Hamna haja ya kuwa mwangalifu na chochote. Siyo JC aliyefanya hayo mambo, ataongea ukweli wake, na mapolisi wataendelea na uchunguzi wao kuwakamata waliofanya hayo," akasema mzee.

"Ni kweli. Ila huwa wana njia za kuzungusha tairi lirudi nyuma kumgonga ambaye hakulisukuma Frank, JC anapaswa tu kuwa makini. Wanaweza kuanza kumgasi yeye asipoeleza vizuri alikuwa wapi hayo yalipotokea," rafiki yake mzee akasema.

Nilikuwa nimeangalia chini tu bado.

"Sina maana mbaya lakini..." rafiki huyo akasema.

"Hapana, umesema kweli. JC analijua hilo, nilikuwa namkumbusha tu pia," Simba akaongea.

"Kwa hiyo aandae cha kusema?" Tesha akauliza.

"Watauliza maswali simple tu. Atasema ukweli, lakini siyo lazima azame sana kusema kila kitu. Majibu ya kweli, kifupi tu. Basi. Wamalize, waondoke, waendelee na mambo mengine," Simba akasema hivyo.

"Ila watawakamata tu. Vipimo vikishamalizika, lazima watawajua tu waliohusika," akasema yule mlinzi, aliyeitwa Omari.

"Watakuwa wameshamaliza. Tutawauliza tujue wamefikia wapi, kama watakuwa tayari kusema," Simba akaongea.

"Jayden..." mzee akaniita.

Nikamwangalia.

"Kevin alikuwa ametuma salamu mapema, anasema amekutafuta leo ila hamjaweza kuongea. Simu imezima au?" akaniuliza.

Najua ilikuwa njia ya kunitaka nizungumze angalau, nami nikasema, "Hapana. Sijaiangalia toka asubuhi."

"Alienda Arusha mara moja, ikiwa Jas alikwambia," mzee akasema.

"Ndiyo, nafahamu. Nitamtafuta baadaye," nikasema tu hivyo na kutazama chini.

Ukimya mfupi ukafuata, nikiwa nimeonyesha wazi kwamba bado sikuwa mwepesi wa kufanya mazungumzo zaidi, na kabla hawajajitahidi kuyaendeleza wanawake wawili wakafika hapo kutoa vyombo na kutusafisha mikono kienyeji; yaani kwa kutunawisha kutumia jagi na kibeseni, ikiwa ni Deborah na msaidizi mmoja wa kazi. Wakatusafisha kwa heshima na kurudi ndani, na kutokea huko ndani tuliweza kusikia sauti za watoto wa Jasmine wakiwa wanalia, labda kuogeshwa, ndipo mama pia akawa amekuja hapo na kusimama usawa wa kiti alichokalia mzee.

"Vipi suala la viti Omari?" mama akasema hivyo.

Alikuwa akiongea na mlinzi, naye akasema, "Vipo njiani."

"Inabidi viwahi, maana kuna ndugu wengine wanakuja huku mapema leo. Vilitakiwa kufika saa mbili, sa'hivi ishafika saa nne," mama akasema.

"Viti vya kukodi?" akauliza rafiki ya mzee.

"Eeh, na chuma za turubai. Mvua inaweza kunyesha," akasema mama.

"Wanakuja. Kuna kikwazo nafikiri sijui shauri ya sikukuu... ndo' maana wamechelewa," akasema Omari.

"Nilikuwa sina hata habari kama kwa wengine kuna Krismasi," akaongea Tesha.

"Haina maana yoyote," akasema Simba.

"Wasiliana nao basi, ujue wamefika wapi," mama akamwambia Omari.

"Sawa mama," Omari akajibu.

"J, Mariam anataka akuone," mama akanisemesha.

Nikamwangalia, nami nikatikisa kichwa kukubaliana na hilo kisha kusimama, nikiwa tayari kwenda ndani. Lakini ni hapa ndiyo tukasikia honi ya gari kutokea huko nje, naye Omari akanyanyuka upesi na kuwahisha huko huku simu ikiwa sikioni.

"Sijui itakuwa wajomba ndiyo wamefika?" mama akauliza hivyo kumwelekea Tesha.

"Sijajua, labda..." Tesha akajibu na kusimama.

"Hapana, ni maaskari," Simba akasema.

Wote sasa wakasimama isipokuwa mzee Manyanza na rafiki zake tu, na kutokea kule getini kweli tukaona gari la maaskari likiingia hadi lilipofikia sehemu iliyowezekana kuegesha.

"Mtaingia kuongelea ofisini, si ndiyo?" mama akamuuliza mzee.

Akanyakuka kitini hatimaye na kusema, "Ndiyo."

Wenzake wakanyanyuka pia, naye mama akaniambia, "Namwambia Mariam utaenda kumwona baadaye... ukimaliza."

Nikatikisa kichwa kukubaliana na hilo, na ikiwa wazi kwamba maaskari walikuwa wameshashuka na kuanza kuja upande wetu, ndiyo sasa nikawatazama na kubaki nimekaza uso kwa njia makini zaidi. Hii ilitokana na kwamba maaskari hao niliwatambua, wakiwa watatu. Wawili walikuwa wale wale ambao walinitoa barabarani ile jana, na mwenzao, mwenzao alikuwa ni yule mwanaume niliyekutana naye usiku wa jana pale nje hadi akanipa maelekezo niliyojua yalitoka kwa Bertha.

Ilinishtukiza kusema kweli. Alikuwa amevalia kwa namna ya kiaskari zaidi, na hilo likanielewesha kwamba alikuwa askari aliyenunuliwa na madam Bertha kumsaidia kufanya madhambi yake. Aloo! Pesa za yule mwanamke zilikuwa changamoto, siyo poa. Kwa hiyo Bertha alikuwa na watu kila mahali, hadi aliweza kuwashikilia maaskari kama huyo pia. Sikujua ikiwa ni wote aliwaweka kwenye kiganja chake, lakini kwa mwendo huu nilielewa haingekuwa rahisi hata kidogo kupata haki ya kweli kwa maafa aliyoyasababisha; ukitegemea na mimi nilikuwa kiganjani mwake pia.

Kwa hiyo hapa sikuwa na namna ila kuendelea kuwa mbwa wa Bertha pro max. Maaskari hao wakatufikia hapo varandani na kutupatia salamu vyema, naye mzee akawaambia tuelekee ndani ili wafanye mahojiano yao kwangu vizuri zaidi. Nilikosa amani kila nilipomwangalia huyo askari wa Bertha na kuona namna alivyonitazama kwa yale macho ya kujuana, nami nikajitahidi kuacha kabisa kumwangalia kutokana na hisia mbaya nilizopata.

Tukaingia ndani hatimaye, ikiwa ni mimi, mzee, Simba, na maaskari hao pekee ndiyo tulioelekea kwenye ofisi ndogo ya mzee Manyanza huko ndani. Ujio wa maaskari sikuzote huinua macho ya wengi, kwa hiyo niliona waliokuwemo wakitutazama hadi tulipofika ndani ya ofisi na kwenda kukaa. Mimi nikakaa kwenye sofa moja la humo pamoja na mzee wangu, maaskari wale wawili wakikaa kwenye lingine, huku mwenzao yule feki akisimama pembeni. Simba alikuwa amesimama pia pembezoni mwetu.

"Tunajua bado mna mambo mengi ya kufanya, kwa hiyo hatutatumia muda mrefu sana," askari wa kwanza akasema hivyo.

"Haina shida Alfred," mzee akamwambia.

"Jayden..." askari huyo akaita.

"Naam..." nikaitika.

"Jana najua tulikutana ghafla, hatukuwa na muda hata wa kujitambulisha. Naitwa Alfred, huyu ni Inspector Musa... na huyo ni detective Idris," askari huyo akanijulisha.

Nikatikisa kichwa kuonyesha uelewa na kumwangalia huyo "detective" Idris, ambaye alinitazama kwa umakini. Kumbe alikuwa mpelelezi.

Askari Alfred, akiwa anaonekana kuwa na cheo fulani kikubwa kwa hao wawili, akasema, "Kwa hiyo jana ulisema kwamba ulikuwa Bunju, tokea upate habari za kifo cha mchumba wako?"

Nikatikisa kichwa kukubali.

"Zilikufikiaje?" akaniuliza.

Nikatulia kidogo, kisha nikasema, "Mtandaoni. Mitandao ya kijamii, nili... niliona taarifa ya gari lililopinduka... nili... nilijua ni lake kwa... nilipoona namba za usajili."

"Mara ya mwisho umemwona ilikuwa lini?" akauliza.

"Jana yake," nikasema hivyo.

Maaskari wakatulia kidogo.

Nikajiwahi kwa kusema, "Oh, hapana... aa... ni hiyo hiyo siku."

"Wapi?" akauliza tena.

"Hospitali, kule Tegeta. Tulikuwa wote... mwanangu alikuwa anaumwa. Yeye akaondoka kwanza maana alikuwa hajisikii vizuri, ndiyo...."

Nikaishiwa hapo baada ya kitu chenye kuchoma sana kuniingia moyoni. Nilikumbuka vingi!

"Ikawaje?" akaniuliza yule aliyeitwa Musa.

Nikajikaza na kusema, "Tuliwasiliana baadaye. Alinitaka tu... tukutane... sehemu fulani, sa'..."

Nilikuwa nashindwa kuzungumza vizuri kutokana na kichwa changu kuchanganya habari nyingi kutokana na hisia nzito kunilemea.

Simba akasema, "Ana... anajikusanya bado..."

"It's okay, tunaelewa. Well, wacha niende kwenye point ili nikuulize tu moja kwa moja. Inspector Idris ndiye anadili na uchunguzi wa kina juu ya jambo lililompata mchumba wako. Kwa uchunguzi aliofanya, inaonyesha ni kweli uliwasiliana na mchumba wako masaa machache kabla ya ajali kutokea... lakini ni kama kuna jambo lililopelekea... au kusababisha itokee. Sehemu aliyodondokea haikuwa kutoka barabarani moja kwa moja, yaani aliingia changarawe na kuendelea kuendesha hadi kufikia hilo bonde... ndiyo gari likadondokea huko. Hiyo inaonyesha motive, Jayden. Unafikiri ni nini kingemsukuma mchumba wako... mpaka afanye jambo la namna hiyo?" askari Alfred akaniuliza.

Mzee akaniangalia, naye Simba akauliza, "Unataka kusema kwamba Miryam alijiua?"

Nikafumba macho baada ya kupandwa na hisia mbaya moyoni.

"Ndiyo tunataka kujua," askari Alfred akamwambia.

Mzee akamwangalia na kusema, "Miryam hakuwa mwanamke reckless. Alijijali, na aliwajali wapendwa wake. Hangekuwa mbinafsi kufikria kufanya jambo kama hilo."

Nikamwangalia yule Idris kwa namna yenye hasira kiasi, yeye akinitazama kwa kiburi tu.

"Labda kuna vitu vipya vilitokea ambavyo vilifanya nia yake ibadilike. Ndiyo sababu namuuliza Jayden ili atuambie kama anafikiri ni mchumba wake mwenyewe ndiye aliyejiongoza huko, au kama kuna mtu alimsababishia," askari Alfred akasema.

"Mtu mwingine kivipi?" akauliza Simba.

Huyo Idris akasema, "Hakukuwa na mtu mwingine ndani ya gari lake isipokuwa yeye. Lakini angeweza kuwa amepewa stress na mtu mpaka kupelekea iwe hivyo. Hatuwezi kujua kama alikuwa amelewa, au kama ni breki zilifeli tungegundua hilo, lakini inaonyesha gari lilikuwa ni zima kabisa. Tena jipya. Kwa hiyo ni wazi huyo mwanamke angeweza kuwa...."

"Jina lake ni Miryam!" nikajikuta naongea hivyo kiukali kumwelekea mwanaume huyo.

Sikupenda kabisa alivyomsema Miryam kama "huyo mwanamke" kwa njia iliyoonyesha dharau iliyofichwa, na wengine wakabaki kunitazama kwa njia makini baada ya kuona nimepandisha hisia. Na nilikuwa namwangalia kwa hisia kali sana.

Mzee akanishika begani na kusema, "Jayden... usiwe hivyo. Wanajaribu tu kusaidia."

Nikafumba macho kwa ufupi nikiwa nazikaza hisia zangu, kisha nikamwangalia askari Alfred na kusema, "Miryam aliniita hotelini. Lakini nilipofika nikakuta hayupo. Aliniachia... aliniacha hospitali na mama wa mwanangu, na hali haikuwa nzuri sana kati yetu. Sisemi kwamba ni mama wa mwanangu ndiyo alisababisha, ila... nilihisi Mimi alikuwa... alikuwa na wivu, ndiyo maana, nikawa namtafuta lakini sikumpata..."

Niliongea upesi huku pumzi zangu zikitetemeka. Wote walikuwa wakiniangalia kwa utulivu.

"Nilihisi hatia yaani... nilijilaumu sana ndiyo maana nikaenda mbali kwanza... s-sikuamini kilichotokea... nili... hhniliona ni makosa yangu mpaka yeye ku... kupatwa na hiyo ajali..."

Iliniuma sana kuongea uwongo huo. Nilitaabika rohoni, na sikuweza kuzuia maumivu yangu hapo hadi machozi yakaanza kunivizia. Simba pia akanishika begani.

Mzee akawaambia maaskari, "Bado hili ni jambo zito sana kwa mwanangu, Alfred. Anahitaji muda, sisi wote. Natumaini hayo yatakuwa yamewatosha kwa wakati huu."

Askari huyo akasema, "Ni sawa, haina shida. Asante kwa ushirikiano wako Jayden. Na nyie wote."

"Asante pia," mzee akamwambia.

Nilikuwa nimetazama chini tu, nikiendelea kuzidhibiti hisia zangu.

"Vipi kuhusu vifo vya Adelina na Bobo?" Simba akawauliza.

Askari Musa akajibu kwa kusema, "Uchunguzi unaendelea bado. Hatuchoki mpaka tuwapate waliohusika."

"Fanyeni kweli, hao wajinga hakikisheni mnawapata kabla huu mwaka haujaisha. Yaani mkimpata hata mmoja, nijulisheni. Hao wenzao wote wanaonekana kufanya hivyo wakiwa na nia fulani, tunatakiwa tujue kama ilikuwa kinagaubaga ama kama kuna mtu aliwatuma. Tuwakomeshe," akasema Simba kwa mkazo.

Nikamwangalia machoni yule Idris, ambaye alikuwa akinitazama kwa umakini.

"Ndiyo, tutajitahidi sana. Basi, Mr. Manyanza wacha sisi tuage. Shughuli nyingi inatungoja," akasema hivyo askari Alfred huku akianza kusimama.

Sisi pia tukasimama, na mzee akampatia mkono wa shukrani.

"Pole sana Jayden. Jikaze tu kiume, haya ndiyo maisha," askari Alfred akaniambia hivyo kwa kutia moyo na kunipa mkono.

Nikaupokea kishukrani huku nikitikisa kichwa kukubali kitia moyo chake, na Musa pia nikatikisa mkono pamoja naye. Nikakosa umakini kwa maneno ya mzee wangu alipokuwa akiongea na askari Alfred kuhusu kuwapa chai sijui, baada ya yule Idris kunisogelea ili kunipa mkono pia. Kwa sekunde chache nilibaki nimeangalia kiganja chake tu kwa umakini, na kisha nikamwangalia usoni bila kuonyesha jitihada yoyote ya kutaka kukipokea. Wengine walikuwa wameanza kuuelekea mlango huku Simba akiwa ananiangalia kwa umakini, na askari huyo akatabasamu kidogo na kukishusha kiganja chake, halafu alipoanza kunipita, akanifanyia "moja" kwa ishara akitumia midomo yake bila kutoa sauti.

Baada ya kunipita, nikatafakari neno hilo aliloniachia hapo na kuelewa kwamba alimaanisha imebaki siku moja ili nifanye kile alichokuwa ametumwa aniagize kufanya. Zoezi la kwanza kwake lilikamilika, nikiwa nimetumia maneno aliyoniambia niyaseme ili kuwadanganya maaskari wenzake juu ya mambo yaliyompata Miryam. Simba akaniambia angewasindikiza pia wageni, na mimi hata sikumjibu na kurudi kukaa tu hapo hapo sofani nikiwa nimeghafilika sana moyoni. Ni nini ambacho kingefuatia baada ya kuiweka laini ile kwenye simu siku hiyo niliyopangiwa kufanya hivyo? Niliwaza sana.






★★★★★★★★★★

ITAENDELEA

★★★★★★★★★★


Whatsapp +255 678 017 280
 
Wapendwa na wapenzi wa simulizi ya MIMI NA MIMI, ninataka kuwafahamisha kwamba kutakuwa na badiliko kubwa la kupost story hii hapa. Sehemu ya kumi na tisa ndiyo itakuwa sehemu ya mwisho kutua hapa, na hii ni kutokana na hitilafu nyingi sana zinazoninyima budi ya kuendelea kuipost, ikiwemo ubebaji wa kazi bila idhini ya mwandishi kutoka kwa watu mbalimbali. Nitaunda grp special ambalo wapenzi wa story hii wataweza kuimalizia, hivyo wanaweza kunicheki kwa namba ile ile ambayo huwekwa chini ya kila sehemu za hadithi hiyo ili niwaunge. Asanteni sana 🙏
 
Wapendwa na wapenzi wa simulizi ya MIMI NA MIMI, ninataka kuwafahamisha kwamba kutakuwa na badiliko kubwa la kupost story hii hapa. Sehemu ya kumi na tisa ndiyo itakuwa sehemu ya mwisho kutua hapa, na hii ni kutokana na hitilafu nyingi sana zinazoninyima budi ya kuendelea kuipost, ikiwemo ubebaji wa kazi bila idhini ya mwandishi kutoka kwa watu mbalimbali. Nitaunda grp special ambalo wapenzi wa story hii wataweza kuimalizia, hivyo wanaweza kunicheki kwa namba ile ile ambayo huwekwa chini ya kila sehemu za hadithi hiyo ili niwaunge. Asanteni sana 🙏
Shukrani mkuu, ila ungeeleza kama ni group la kulipia au la. Na kama na kulipia ni kiasi gani
 
Wapendwa na wapenzi wa simulizi ya MIMI NA MIMI, ninataka kuwafahamisha kwamba kutakuwa na badiliko kubwa la kupost story hii hapa. Sehemu ya kumi na tisa ndiyo itakuwa sehemu ya mwisho kutua hapa, na hii ni kutokana na hitilafu nyingi sana zinazoninyima budi ya kuendelea kuipost, ikiwemo ubebaji wa kazi bila idhini ya mwandishi kutoka kwa watu mbalimbali. Nitaunda grp special ambalo wapenzi wa story hii wataweza kuimalizia, hivyo wanaweza kunicheki kwa namba ile ile ambayo huwekwa chini ya kila sehemu za hadithi hiyo ili niwaunge. Asanteni sana 🙏
Pole sana ndugu Elton watu wa hivyo hawakosekani Dunia hii ya leo tamaa zimetujaa wewe unapost bure mwingine anaibeba na kwenda kujipatia ujira pasipo na kuumiza kichwa,ahsante kwa sehemu hizi ulizotupatia nimejifunza mengi kupitia riwaya hii nimejuta nimekuwa mpya na ninaweza kupenda tena bila mipaka.
 
Pole sana ndugu Elton watu wa hivyo hawakosekani Dunia hii ya leo tamaa zimetujaa wewe unapost bure mwingine anaibeba na kwenda kujipatia ujira pasipo na kuumiza kichwa,ahsante kwa sehemu hizi ulizotupatia nimejifunza mengi kupitia riwaya hii nimejuta nimekuwa mpya na ninaweza kupenda tena bila mipaka.
Asante ndugu yangu
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom