SEHEMU YA TISINI NA SABA
Ilikuwa ni usiku wakati wa chakula karibu watu wote walikuwa meza moja kasoro Mzee Mgaya ambaye alikuwa ndani kwake, mara baada ya kumaliza kula mama yake Samson aliomba aitiwe shemeji yake Mzee Mgaya akiwa na maongezi ambayo yalihusu familia nzima.
Mzee Mgaya alikuja huku akiwa na kitabu fulani kidogo kinachohusu biashara zake, ilionekana alikuwa anapitia pitia mambo fulani akiwa kule ndani.
Eeeh Naam shemeji nasikia una maongezi na Mimi, vipi ni faragha au inakuwaje? Mzee Mgaya aliuliza.
Hapana ni mazungumzo ya wazi kabisa na yanatuhusu wote tuliokaa hapa ndani, ni kwamba kwanza nitumie nafasi hii kuwashukuru wote wewe shemeji pamoja na dada yangu hapa, kwa moyo mliokuwa nao na mpaka sasa nashindwa nawezaje kulipa fadhila zote ambazo mmemtendea kijana au mtoto wangu, najua mwenyezi MUNGU atalipa. Kwanza kitendo Cha kuishi na binti ambaye mmesema Hana undugu na nyinyi na mkampatia huduma zote inaonesha ni jinsi gani mna mioyo ya kipekee kabisa hakika nimejifunza kitu kutoka kwenu. aliongea kwa hisia kali mama Samson huku Mzee Mgaya na mkewe wakitabasamu na kuitikia Amina.
Kisha akaendelea.........
Lakini pia nichukue nafasi hii kumuombea msamaha mwanangu, licha ya kuwa mlishamsamehe, lakini Kuna haja ya Mimi kumuwakilisha tena, hebu Samson naomba uinuke uwaombe msamaha walezi wako. aliamuru mama Samson.
Samson alipiga magoti kwa mama Kulwa na kumuomba msamaha kwa dhati kabisa, huku mama Kulwa akionesha kasamehe bila kinyongo.
Kisha Samson akainuka na kutaka kupiga magoti mbele ya Mzee Mgaya lakini kabla hajafanya vile alizuiwa na kuambiwa akae chini.
Mwanangu Samson , Mimi Nina Nia ya dhati kuhakikisha wewe unafika sehemu sahihi ambayo nataka, najua kwasasa huelewi lakini, baada ya muda utajua na kutambua umuhimu wa shule. Huna haja ya kupiga magoti mwanangu. aliongea kwa sauti ya chini yenye utulivu Mzee Mgaya huku akimpigapiga Samson mgongoni.
Mama Samson akaendelea .......
Lakini pia naomba nitumie nafasi hii kuyamaliza mambo yangu na huyu Binti mwenye mtoto najua muda mwingi ananiogopa kutokana na yale yaliyotokea lakini niseme tu kuwa wala asiwe na wasiwasi na Mimi,
Tumeshakuwa ndugu au wamoja kwakuwa amezaa na mwanangu,
Si halali , Wala si sheria, lakini hakuna namna imeshatokea, mtoto hana hatia namuombea ukuaji mwema na natoa baraka zangu kwa dhati.
Binti yangu naomba nisamehe Mimi mama yako yaliyotokea ni hasira tu. aliweka kituo mama mzazi wa Samson.
Rahma alibaki akiona aibu kwani alikosa hata jibu la kumwambia mama Sam akajikuta anamwangalia mama Kulwa ambaye kamzoea zaidi,
Unaniangalia nini, kwani unaongea na Mimi ongea na mkweo na huyo ndiye mwenyewe Mimi Sina mjukuu bado Jose mwenyewe hata simuelewi Kila siku yeye ni kusoma tu mara asomee hiki mara hiki haridhiki yule mtoto, sijui anadhani atajua ya ulimwengu wote.alitania mama Kulwa Kisha akaendelea..........
Dada kwanza nikushukuru kwa kuamua kufunga mjadala huu huku tukiyamaliza mambo kwa amani na niseme tu kuwa Mimi Hawa watoto wote nilishawasamehe, na Kuna muda Sam alihisi nina roho mbaya lakini si kweli yeye bado ni kijana mdogo hivyo panapotakiwa alisemwa vizuri lengo si kumnyanyasa bali kumrudisha kwenye mstari wa maadili mazuri. Kuhusu huyu Binti hawezi kuzungumza nadhani aibu nayo si unajua tena, lakini kuwa na amani Kila kitu kitakaa sawa tu. alifafanua mama Kulwa.
Stori ziliendelea huku kila mmoja akiwa radhi na mwenzake kifupi mambo yaliisha.
Asubuhi na mapema baada ya breakfast watu watatu walikuwa kwenye gari la Mama Kulwa safari ikiwa ni kwa Tausi, walifika na kupokelewa vizuri huku mama Kulwa akionesha kuzungusha macho huku na huko kuiangalia nyumba ya Tausi namna ilivyo kuwa ya kisasa baada ya kupandishwa Kuta na kuwekwa bati zingine za kisasa , rangi nzuri ya kuvutia lakini pia fence nayo ilikuwa si haba. Samson aligundua namna mama Kulwa alivyochukia ghafla, yaani zile chuki za wazi.
Walishuka kwenye gari huku Tausi akikumbatiana na mama Kulwa, lakini licha kukumbatiana vile macho ya Jackline (Mama Kulwa) yalikuwa kwenye Kuta za nyumba ya Tausi, Samson aligundua hali ile akatabasamu akijisemea kimoyomoyo kazi ipo.
Jamani dada zangu karibuni ndani, yaani kidogo nije hukohuko maana Jana hamjaja jamani mama Samson, aliongea Tausi huku wakikumbatiana na mama yake Samson kwa muda.
Hapana mdogo wangu, muda wenyewe hautoshi, lakini pia tumeamua kuongeza siku moja kwaajili yako maana niliona si vema kuondoka bila kuonana na wewe na pia shemeji alifikisha salamu kuwa ulitualika. aliongea mama Sam.
Samson wewe ni mwenyeji hapa hebu tuandalie glass na pia toa na juisi kwenye........Kabla hajamalizia sentensi yake Mama Kulwa alidakia kuwa yeye hajisikii kula Wala kunywa chochote.
Vipi dada kwani unajisikia vibaya, aliuliza Tausi huku akigundua jambo kutoka kwa mama Kulwa. lakini Samson naye aligundua Nini kinamsumbua mama Kulwa.
Mama yake Sam yeye aligundua mabadiliko toka kwa mama Kulwa kwani alimuona mnyonge ghafla lakini hakujua nini kinasababisha awe kwenye hali ile.
Baada ya muda kidogo mama Kulwa aliaga kuwa anaondoka, Kuna mahali anaenda akiahidi kuwa atarudi kuja kuwachukua mama yake Samson na mwanaye. ni jambo liliwashangaza wote lakini hakuna aliyemzuia asiende atakako.
Dada yangu wewe acha tu huyu mama Kulwa kaondoka hapa kwasababu ya wivu unamsumbua, najua hiki kibanda alichokiona ndicho kimechafua hali ya hewa kwa upande wake yaani janamke lina roho mbaya dada wewe acha tu, muulize Samson atakwambia unadhani yule kachukia nini. aliongea Tausi huku akionesha naye kachukia.
Sasa kama ni hii nyumba,mbona nyumba yake ni kubwa kushinda hii ndugu zanguni. aliongea mama yake Samson kwa mshangao.
Ndiyo hapo jiulize ndugu yangu alitaka Mimi niishi mazingira gani? ana zaidi ya miaka nane hajawahi kuja kwangu Lakini leo kukuta nyumba imebadilika tofauti na anavyoifahamu, basi moyo wake umeumia mno. alilalamika Tausi.
Mama Sam na mwanaye waliangaliana bila kutia neno kisha wakashinda pale kiasi cha lunch kupata pale, lakini wakaanza kumsubiri mama Kulwa lakini hakutokea. Ndipo Samson aliposhauri wapande daladala warudi tu, ni jambo ambalo Tausi hakuliafiki ikabidi awasiliane na Taxi driver ili awarudishe akina Sam na mama yake.
**************************************
Mmmmh mwanangu kama maisha yenyewe watu wanaishi hivi, nimeshachoka ingekuwa amri yangu ningeondoka hata Leo bahati mbaya hata stendi yenyewe sijui ilipo maana tunaonekana kama sisi tumesababisha. aliongea mama Sam huku wakigonga geti na kuingia ndani, wakakuta gari la Mama Kulwa lipo parking wakapata jibu kuwa bila kufanya maamuzi mengine wangesubiri hadi wachoke.
Mzee Mgaya naye aliingia jioni ile huku akisalimia juu juu na kuingia ndani na kuacha gari likiunguruma nadhani kwa kusahau, Samson. alizima lile gari na kumrudia mama yake kuwa asijisikie vibaya sana kwani mama Kulwa ndivyo alivyo.
Mama yake Sam alikuwa kampakata mtoto wa Rahma huku akiongea mambo fulani na mwanaye Samson, huku Rahma akiwa jikoni na Sarah wakiandaa dinner kwa siku ile.
Makelele toka ndani kwa mama Kulwa yalianza kidogo kidogo huku sauti za mtu na mkewe zikipanda Kila baada ya muda fulani, baadaye matusi na malalamiko kibao yalisikika toka kwa mama Kulwa huku watu wote waliokuwa nje wakiwa hawana la kufanya, ndipo kiunyonge mama yake Samson alikabidhi yule mtoto akajifunga nguo zake vizuri Kisha taratibu akaingia ndani ambako amani ilikuwa ni sifuri.
Itaendelea..............................