Simulizi: Mchawi

Simulizi: Mchawi

SEHEMU YA 34:

Ilipofika saa tatu bila kumuona mke wangu nilijaribu kupiga tena simu lakini bado haikuwa ikipatikana. Niliamua kwenda kwa wazazi wake kutaka kujua kuna kitu gani kimetokea kiasi cha mke wangu kuondoka haraka na simu yake kutokuwa hewani kipindi kirefu.

Niliamua kumfuata kwao, nilitoka na kuegesha mlango, sikutaka kuufunga kwa kuhofia kupishana naye.

Nilikwenda ukweni kumuulizia mke wangu, nilikodi gari mpaka kwa wakwe zangu. Bahati nzuri nilikuta bado hawajalala, baada ya kugonga hodi mama mkwe alinikaribisha kwa vile aliifahamu sauti yangu.
Karibu baba Zawadi.

Asante mama, shikamoo, niliamkia huku nikiingia ndani na kukaa kwenye kochi.
Marahaba, kwema utokako?
Namshukuru Mungu, sijui mwenzangu amefika huku?

Mmh! Kwa leo sijamuona, kauli ile ilinishtua sana lakini nilificha mshtuko wangu.
Sasa atakuwa amekwenda wapi? nilijikuta nikimuuliza swali mama mkwe lisilomhusu.

Nitajuaje baba, kwani alikuaga anakwenda wapi?
Mama, yaani nimerudi nyumbani nimekuta ufunguo kwa jirani bila maelezo yoyote.

Zawadi yupo wapi?
Ameondoka naye.
Mmh! Sasa atakuwa amekwenda wapi?
Hata mimi nashangaa tena nasikia kaondoka na ile gari ya yule mwanaume wake.

Mmh! Unasema kweli? mama mkwe alionesha kushtuka.
Kutokana na maelezo ya mtu aliyemuona.
Kwa hiyo hukumuona kwa macho yako?
Sijamuona mama nimeambiwa.
Basi usifikirie moja kwa moja kuwa ameondoka na mwanaume wake wa zamani, kwani ameondoka tangu saa ngapi?

Saa tano.
Saa tano, sasa atakuwa amekwenda wapi na mtoto, kwani hali hii imetokea mara ngapi?
Ni leo tu mama toka tumalize yale matatizo yetu.

Nakuomba rudi nyumbani ukapumzike, akirudi atakueleza alikuwa wapi kama maneno yake hayaeleweki mlete kwangu. Nimechoka na upumbavu wake, hawezi kutuchezea akili kiasi hiki, mama mkwe naye alionekana kukerwa na kitendo cha mke wangu kuondoka bila kuaga.
Sawa mama.

Nina imani hakufika mbali angekuwa amekwenda peke yake ningekuwa na wasiwasi, lakini kwa vile ameondoka na mtoto atawahi kurudi tu huenda mmepishana amesharudi nyumbani.
Nitashukuru mama.

Basi baba rudi nyumbani, nina imani mpaka muda huu atakuwa amerudi tu.
Sawa mama, nilikubaliana na mama mkwe na kugeuza kurudi nymbani nikiwa na matumaini ya kumkuta.
 
SEHEMU YA 35

nilikubaliana na mama mkwe na kugeuza kurudi nymbani nikiwa na matumaini ya kumkuta.

Nilikodi gari ili niwahi nyumbani nikiamini huenda mke wangu amerudi na kutonikuta na kumfanya awe na wasiwasi wa kutaka kujua mimi nipo wapi.

Nilikwenda hadi nyumbani na kuingia ndani, nyumba ilikuwa kimya kuonesha hakukuwa na dalili za kuwepo mtu ndani.
Wazo langu lilikuwa labda amerudi na kuingia kulala, nilikwenda chumbani.

Chumba kilikuwa kitupu na hali ilikuwa ileile ya chumba kuwa katika hali ya uchafu. Nilibakia nimesimama kwenye mlango wa kuingilia chumbani kwa dakika kadhaa nikiwa siamini kilichokuwa mbele yangu.

Nilijiuliza mke wangu atakuwa wapi?Nilirudi sebuleni na kukaa kwenye kochi nikiwa sijui mke wangu amekwenda wapi. Hata hivyo, nilikuwa na wasiwasi kwamba mama mkwe alikuwa akijua kila kitu ila alinificha.

Ilikuwa ni mateso juu ya mateso kwani siku ile nilikuwa nimefanya kazi nzito kwa muda mrefu hivyo niliamini nikirudi nyumbani ningepumzika.

Lakini tangu nilipofika nilikuwa juujuu kwa ajili ya kumtafuta mke wangu, tena bila kula.
Njaa iliyokuwa ikiniuma kama kidonda ilitoweka kutokana na mshikemshike wa kuzunguka kumtafuta mke wangu.

Saa ya ukutani ilionesha tayari ni saa sita na nusu usiku, bado hakukuwa na dalili za mke wangu kuonekana. Bado sikukata tama, nilirudia kumpigia simu lakini hali ilikuwa ileile, hakuwa akipatikana hewani.

Nilijikuta nikiwa na wasiwasi kuhusu mke wangu na kujiuliza kipi kimemsibu mpaka muda ule awe hajarudi. Ingekuwa ameondoka peke yake ningejua amerudia matatizo yake.

Lakini alikuwa ameondoka na mwanangu wa pekee Zawadi, nilijiuliza kama kweli ameparama tena na kurudiana na yule mwanaume huenda ikawa hata Zawadi si mtoto wangu wa kumzaa.

Kwa upande wa Zawadi, ningekuwa tayari kufa kama ningeambiwa si mtoto wangu kwani nilifanana naye kila kitu. Kila aliyemuona alijua ni mwanangu bila hata ya kumwambia. Nilikaa sebuleni kumsubiri nikijipa moyo kuwa huenda amekwenda kwenye sherehe na kuchelewa kurudi.

Nilikaa sebuleni mpaka alfajiri ilipoingia bila kumuona mke wangu wala kivuli chake. Nilijiuliza mke wangu atakuwa wapi? Kutokana na kulala usingizi wa mangamungamu niliamka asubuhi kichwa kikiwa kizito.
 
SEHEMU YA 36;

Kwa vile niliacha kiporo cha kazi, niliposhtuka nilioga harakaharaka nikitegemea huenda mke wangu akatokea kabla ya kwenda kazini kama alivyofanya siku za nyuma lakini haikuwa hivyo.

Mpaka naondoka, sikumuona mke wangu na kumuachia funguo jirani nikiamini huenda jioni nikirudi naweza kumkuta.

Nilikwenda hadi kazini nikiwa nimechoka sana, nilificha uchovu wangu na kufanya kazi kwa nguvu japo kila nilipokuwa peke yangu nilisinzia na kuwafanya wafanyakazi wenzangu kunitania eti nilikesha na shemeji bila kujua msiba mzito uliokuwa moyoni mwangu, baada ya bomu lililokuwa limetulia kulipuka upya.

Baada ya kazi nilirudi nyumbani nikiwa na matumaini ya kumkuta mke wangu lakini nilipofika nilikuta mlango umefungwa. Nilikwenda kwa mke wa jirani yangu kuulizia huenda alikuja na kuondoka.

Karibu shemeji, alinikaribisha aliponiona.
Asante, vipi hajarudi mke wangu?
Sijamuona kwani alikwenda wapi? lilikuwa swali juu ya swali.

Hata najua! Mbona huyu mwanamke ananitesa sana, kosa langu nini kila kukicha niwe mimi tu? nilijikuta nikibwabwaja kwa uchungu bila kujielewa.
Kwani kuna nini shemeji?

Yule mwanamke kila kukicha amekuwa akinifanyia mambo yaliyokosa ubinadamu kabisa.
Lakini mbona tumeishi naye vizuri tena mke wako ni mpole na msikivu sana, tatizo nini?

Nilijikuta nikifunguka mwanaume na kuuanika ubaya wa mke wangu, mke wa jirani alinionea huruma na kusema:
Mbona haendani na usemayo?
Mke wangu ni chui ndani ya ngozi ya kondoo.
Pole sana shemeji, na mtoto kampeleka wapi?

Nitajuaje?
Kwani kwao wanasemaje?
Nao hawajui lolote.
Ungesubiri na leo huenda akarudi usiku huu.

Mmh! Sidhani.
Niliagana na mke wa jirani yangu na kuingia chumbani ambako kulikuwa vululuvululu. Baada ya kuoga nilikwenda kununua soda na mkate ili nitulize njaa.

Chakula kilinishinda na kulala na njaa. Usingizi wangu ulikuwa wa kushtukashtuka kila mara kwa kuamini labda mke wangu amerudi.

Kila niliposhtuka usingizini nilitulia na kusikiliza huenda kuna sauti ya mtu ikiniita.

Niliona chumbani kama nikilala akiita naweza nisimsikie hivyo nikaamua kuhamia sebuleni na kukaa kwenye kochi kumsubiri mke wangu. Muda nao ulikuwa umekwenda, ilikuwa tayari imegonga saa saba na nusu usiku...
 
SEHEMU YA 37

Mpaka kunakucha hakukuwa na dalili za mke wangu kurudi, hata bila kunawa uso nilikwenda ukweni kuulizia taarifa za mke wangu, labda amerudi na kuogopa kurudi na kufikia kwa mama yake.

Nilipofika ukweni nilikuta ndiyo kwanza wanaamka.
Vipi baba mbona asubuhi asubuhi? mama mkwe aliniuliza baada ya kuniona asubuhi ile.

Mama, mke wangu yupo huku?
Ina maana alirudi na kuondoka tena?
Hapana mama hajarudi kabisa.
Toka juzi?

Ndiyo mama.
Mmh! Mbona mwana huyo ana matatizo, sasa atakuwa amekwenda wapi?
Kwani huku hajafika?
Sijamuona baba yangu.
Basi lazima atakuwa amekwenda kwa mwanaume wake.

Jamani, yaani ndiyo kafikia hatua hii? Mama mkwe alishika kiuno kuonesha naye kachoshwa na taarifa ile.

Basi mama acha niwahi kazini.
Niliagana na mama mkwe na kurudi nyumbani ili nijiandae kwenda kazini japokuwa nilikuwa katika wakati mgumu baada ya kumkosa mke wangu kwao.

Nilirudi hadi nyumbani kichwa kikiwa kizito, chumba nilikiona kama dunia isiyo na kitu chochote zaidi ya mimi peke yangu. Moyo ulikufa ganzi, nilishindwa kwenda kuoga ili niwahi kazini kwani muda ulikuwa umekwenda sana.

Nilihisi kama mwili unakosa nguvu, kichwa kilianza kuniuma kwa mawazo na mapigo ya moyo yalikwenda kwa kasi. Niliwahi kukaa kwenye kochi kabla sijaanguka, nilijilaza nikiwa na maswali mengi juu ya mke wangu kuondoka nyumbani bila taarifa.

Nilijiuliza tatizo nini hasa ikiwa kila kitu kilikuwa kikienda vizuri, nikiwa bado natafuta sababu ya mke wangu kuondoka bila kuaga na sehemu gani amekwenda, chini ya meza niliona bahasha iliyokuwa imefungwa. Nilijikuta nikipata shauku ya kutaka kujua ile barua ya nani.

Pamoja na mwili kutokuwa na nguvu, nilinyanyuka nilipokuwa nimejilaza na kwenda kuiokota ile bahasha iliyokuwa na jina langu. Moyo ulinilipuka kwani ule ulikuwa mwandiko wa mke wangu.

Nilijikuta nikiingiwa na wasiwasi huenda mke wangu alirudi asubuhi ile na kunikosa wakati nimekwenda kwao kumtafuta na kuamua kuondoka na kuacha ujumbe.

Niliichukua ile bahasha na kuifungua, nikakutana na karatasi iliyokuwa imeandikwa kwa wino mwekundu. Baada ya kuifungua, nilikutana na maneno ambayo kidogo yasimamishe mapigo yangu ya moyo.
 
Back
Top Bottom