Simulizi: Mchawi

Simulizi: Mchawi

SEHEMU YA 38:

Barua ile ilinikatisha tamaa na kujikuta kila herufi moja niliyokuwa nikisoma ndivyo moyo wangu ulivyokuwa ukikamuliwa bila ganzi. Siwezi kuelezea maumivu niliyoyasikia, ilikuwa sawa na kung’olewa jino bila ganzi.
Mpaka namaliza kusoma, machozi yalikuwa yamefunika macho yangu na sehemu ya karatasi ilikuwa imelowa upande kwa machozi. Barua ilisema hivi:

Kwako Kazala,
Najua utashtuka kupokea ujumbe huu na kukufanya uchanganyikiwe. Najua wewe ni mwanaume na wanaume wameumbwa kukabiliana na matatizo. Najua unanipenda na utaendelea kunipenda, lakini kutokana na kushindwa kwenda na wakati na kunigeuza mwanamke wa kizamani wa kukaa ndani kama samani nimeamua kuishi maisha yangu ya uhuru kama wanawake wengine.

Nimeamua kuondoka, sitaki unitafute hata mama yangu naye sitaki anitafute, nimeamua kuishi maisha niliyoamua kuishi mimi mwenyewe. Nimekuvumilia mengi Kazala lakini huna shukrani. Nyumba yetu imekuwa ikiendeshwa na watu wa pembeni kuliko sisi wanandoa.

Kazala umekuwa ukiwasikiliza watu wa pembeni kuliko mimi mkeo, nilikueleza tutaachana tukiwa tunapenda nina imani kauli yangu imetimia. Najua utajiuliza kuhusu mtoto, Zawadi ni mtoto wako na ataendelea kuwa mtoto wako nimeamua kuondoka naye ili aendelee kupata malezi mazuri. Ila akitimiza miaka saba nitakurudishia mwenyewe ila naomba unisahau kabisa.

Tangu leo ninapoondoka, mwisho wa wiki hii nafunga ndoa ya kidini tena kanisani na kuwa mke wa mtu anayefahamika mbele za Mungu. Nawe mpenzi wangu wa zamani fanya hivyo, tafuta mwanamke anayeendana na wewe ili ufunge naye ndoa, ukichelewa unaweza kuugua ugonjwa wa akili.

Nakutakia maisha mema wewe na huyo mwanamke utakayemuoa, ila nakuonya kitu kimoja. Nyumba haiendeshwi na watu wa pembeni, ukifanya hivyo kila utakayemuoa atakukimbia.
Ni mimi mzazi mwenzako,
Mama Zawadi.

Barua ile ilikuwa pigo mujarabu moyoni mwangu, ilikuwa sawa na kuupasua moyo wangu kwa kisu butu bila ganzi. Akili yangu haikukubaliana na kutaka kurudia kwa mara ya pili lakini kila nilipotaka kusoma machozi yalizuia nisiyaone maandishi.
 
SEHEMU YA 39:

Nilinyanyuka na kutembea taratibu hadi chumbani na kurudi sebuleni, kichwa kilikuwa kizito hata cha kufanya sikujua na kuona kazi yote niliyoifanya ilikuwa bure. Niliyarudia maneno aliyowahi kuniambia mke wangu na kuyaandika katika barua niliyokuwa nimeishikilia kuwa maneno ya nje yatavunja nyumba yetu tukiwa tunapenda.

Nilijikuta nikianza kumlaumu Simon kwa kuona yeye ndiye chanzo cha nyumba yangu kuvunjika baada ya kukubali ushauri wake ambao mwanzo niliuona kama umenisaidia kumbe ulikuwa bomu lilikuwa likisubiri kulipuka na matokeo yake kuisambaratisha nyumba yangu.

Nilijiuliza nitafanya nini ili kumrudisha mke wangu mikononi mwangu kabla ya mwisho wa wiki haujafika. Nilijiuliza hiyo ndoa itafungwa kanisa gani na siku gani, Jumamosi au Jumapili? Kwangu ulikuwa mtihani mkubwa kujua mke wangu ataolewa kanisa gani ili nikaweke pingamizi.

Mawazo yalinizidi, nikawa naona kichwa kama kinataka kupasuka. Mara giza zito lilitokea mbele yangu, sikujua kilichoendelea hadi nilipokuja kushtuka na kujikuta hospitali, pembeni yangu alikuwepo rafiki yangu Simon ambaye alikuwa akizungumza na daktari.

Nilimsikia akimuuliza:
“Vipi daktari siyo tatizo kubwa?”
“Si kubwa, ni wazi mgonjwa aliwaza sana kufikia hatua mishipa kushindwa kufanya kazi vizuri. Lakini sasa hivi atarudi katika hali ya kawaida ila anatakiwa kupunguza kuwaza sana.”

“Sawa daktari.”
Simon alipogeuka alishtuka kuniona namtazama, hata bila ya kunisemesha nilimuona akigeuka na kumwita daktari:

“Dokta.”
“Unasemaje?”
“Naona mgonjwa ameamka.”
Daktari alikuja kitandani na kunisemesha:

“Pole Kazala.”
“Asante,” nilimjibu kwa sauti ya chini.
“Unaendeleaje?”
“Kichwa kinauma kwa mbali.”

“Punguza kuwaza ndugu yangu, unaki – over load kichwa na kusababisha maumivu makali.”
“Nimekuelewa daktari,” nilimkubalia lakini niliamini bila mke wangu kurudi sitaweza.

“Huna ugonjwa mwingine zaidi ya huo na dawa yake ni kupunguza mawazo na kumeza dawa za maumivu tu.”
Nilidungwa sindano ya maumivu na usingizi tena, nikaambiwa niendelee kupumzika mpaka siku ya pili ili nipate muda wa kulala sana kukifanya kichwa kipunguze mawazo.
 
SEHEMU YA 40:

Nilitoka siku ya pili na kuja kuchukuliwa na Simon ambaye alionesha hakwenda kazini siku ile kwa ajili yangu.
Kabla ya kufika nyumbani tulipitia hotelini na kupata kifungua kinywa kisha tulirudi nyumbani.

Tulipofika nyumbani Simon alinieleza nipumzike na yeye kupanga baadhi ya vitu vilivyokuwa shaghalabaghala, baada ya kuweka baadhi ya vitu vizuri alikuja kukaa karibu yangu na kuniita jina langu.

“Kazala,”
“Naam.”
“Tatizo nini?”
“Shemeji yako ataniua,” nilijibu huku akishika kifua kuzuia presha iliyokuwa ikipanda.

“Tatizo nini?”
“Ameamua kunikimbia.”
“Tatizo nini?”
“Hata sijui, yaani dawa uliyonipa mwenzangu imeharibu kila kitu,” nilianza kumlaumu Simon.

“Acha lawama za kijinga, pale hukuwa na mke kama mkeo anakuletea mwanaume ndani na kulala naye kwenye kitanda chako bado unalaumu watu?

Huu si uzoba?”
“Kama ningemuacha atakavyo asingenikimbia.”
“Ingekuwa mimi nisingeumia, ningeshukuru.”
“Ushukuru nini Simon?” nilishangaa majibu ya Simon.

“Yule mwanamke kuondoka mwenyewe, hukuwa na mke ndugu yangu. Kama angekuwa mwanamke mwenye staha zake angeandika barua kama hii? Kazala aliyekuroga amekufa, si bure kufanyiwa mambo yote haya bado unamlilia mkeo?”
“Ndugu yangu mazoea mabaya, pamoja na yote bado nampenda sana mke wangu.”

“Unampenda? Haya huyo kakukimbia kazi kwako.”
“Utanisaidia vipi?” pamoja na kumnanga mke wangu bado nilimuomba ushauri wa kumrudisha mke wangu.

“Kazala tumekuja kutafuta maisha si wanawake, ujinga wako huo utasababisha ufukuzwe kazi. Hakuna mwajiri atakuvumilia na matatizo yako ya kifamilia yasiyoisha. Kumbuka wazazi wako wanakutegemea matokeo yake unaacha kilichotuleta huku unakuwa bwana penda penda.”

“Nitajitahidi lakini itanichukua muda kumsahau, nilimpenda sana mke wangu.”
Nilikubaliana na Simon niachane na mke wangu kisha nifanye kilichonipeleka kule japo nilijua kwa upande wangu kilikuwa kitu kigumu kumuondoa mke wangu moyoni mara moja.

Nilipanga kwa siri Jumamosi na Jumapili nizunguke makanisa yote kwa pikipiki ili nijue ni kanisa lipi mke wangu anafunga ndoa ili niweke pingamizi. Kwa vile mke wangu alikuwa Mkatoliki niliamini lazima ningejua anafunga ndoa kanisa gani.

NJOO KESHO TUENDELEE KUSOMA.
 
SEHEMU YA 41

Siku ya Jumamosi ilipofika, nilikodi pikipiki kwa ajili ya kuzunguka makanisa yote ya mjini. Kanisa kubwa lilikuwa katikati ya mji pia madogo yalikuwa pembeni kidogo na mji hayakupungua manne.

Niliamini hata kama ningezunguka kutwa nzima nitaweza kufika toka kanisa moja kwenda lingine kwa wakati bila kuchelewa.

Dereva wa pikipiki aliniuliza swali baada ya kuzunguka zaidi ya mara mbili makanisa yote ambayo hayakuonesha dalili zozote za kufungwa ndoa.

“Sikiliza ndugu yangu, tutamaliza mafuta bure, kwa nini tusiende kwenye ofisi za kanisa ili tujue kuna ndoa au hakuna na kama ipo itafungwa saa ngapi? Hiyo itatusaidia kuja kwa wakati kuliko kuzunguka na kukufanya upoteze fedha nyingi.”

Wazo lile nilikubaliana nalo na kuamua kwenda kwenye ofisi za kanisa kuulizia kama kuna ndoa ilikuwa ikifungwa siku ile. Makanisa yote manne yalinieleza kuwa siku ile hakukuwa na ndoa yoyote ila Jumapili kulikuwa na ndoa nne ambazo zote zingefungwa kwenye kanisa kuu tu.
Niliamini katika ndoa zile nne lazima moja itakuwa ya mke wangu kipenzi Suzana, mama Zawadi.

Nilimshukuru dereva wa pikipiki ambaye kwa sasa angeitwa bodaboda. Nilikubaliana naye kunifuata nyumbani siku inayofuata na kunipeleka kanisani ili nikaweke pingamizi ndoa ya mke wangu.

Baada ya kurudi nyumbani nilikuwa na mawazo mengi kuhusiana na hiyo kesho na kujiuliza nitakapotoa pingamizi litakubaliwa au ndiyo nitaabika hasa kutokana na ndoa yetu kufungiwa Bomani.

Upande mwingine niliamini nitakuwa na nguvu ya kuvunja ndoa ya mke wangu kwa vile ilikuwa ikitambuilika kiserikali na vyeti nilikuwa navyo.
Nilipanga kesho nikienda kuweka pingamizi niende na vyeti vya ndoa ili kutia uzito pale mke wangu atakaponikana.

Siri ile sikutaka kumshirikisha Simon kwa kuhofia kunipa ushauri mbaya ambao ungeharibu mipango yangu yote. Ushauri wa Simon mwanzo niliuamini lakini baada ya ushauri wake kusababisha mke wangu kukimbia, sikumuamini tena na kuona ndiye chanzo cha matatizo yangu.

Siku ya pili, baada ya kufuatwa na dereva wa pikipiki niliwasili kanisani saa tatu asubuhi japokuwa ndoa ilikuwa ikifungwa saa saba mchana.

Nilikaa pale mpaka saa nne na nusu ndipo magari ya maharusi na ndugu na jamaa walipoanza kuingia. Muda mfupi kanisani pakawa na watu wengi na magari kutokana na harusi nne kufungwa, nilisubiri kwa hamu nimuone mke wangu akitaka kufunga ndoa na kuweka pingamizi.

Nami nilikuwa mmoja wa watu niliowahi ndani viti vya mbele kanisani kusubiri ibada ya ndoa. Kanisa lilijaa watu wengi sana pamoja na maharusi wote. Kwa vile mabibi harusi walikuwa wameziba nyuso zao, iliniwia vigumu kumtambua mke wangu ni nani kati ya wale wanne.

Baada ya taratibu zote kufanyika ndoa zilianza kufungwa moja moja huku nikisubiri kwa hamu kuiona sura ya mke wangu. Ajabu ndoa zote zilifungwa bila kuiona sura ya mke wangu. Nilijikuta napagawa na kujiuliza nilielezwa ndoa nne au tano?

Baada ya ndoa zote kufungwa bila kushuhudia sura ya mke wangu, watu wote walitoka kanisani na kubakia peke yangu. Nilijiuliza mke wangu atakuwa amekwenda kufunga ndoa wapi.

Nikiwa nado nimesimama kama sanamu nikiwa bado na matumaini huenda kuna ndoa nyingine ingekuja kufungwa, nilishtuliwa na mhudumu wa kanisa.
“Ndugu vipi mbona huondoki na wenzako?”

“Samahani kaka kuna ndoa nyingine zaidi ya hizi?”
“Hakuna, leo kulikuwa na ndoa nne tu hakuna zaidi ya hizi.”

“Mmh! Sijui watakuwa wamekwenda kufunga ndoa wapi?” nilijikuta nikizungumza peke yangu kwa sauti.
“Kina nani?” mhudumu wa kanisa aliniuliza.

“Ooh! Samahani,” nilijikuta nikijibu na kuondoka bila kuaga mpaka nje ya kanisa.

Nje ya kanisa watu walikuwa ndiyo wanamalizikia kuondoka, nilijikuta nimerudi nyumbani kwa miguu na kumsahau dereva wa pikipiki aliyenipeleka. Kwa kweli nilikuwa nimechanganyikiwa na kuamini kama maneno aliyonieleza mke wangu yana ukweli basi atakuwa amefunga ndoa siku ile.

Usiku ulikuwa mrefu kwangu, usingizi ulinikimbia kabisa. Mawazo yote yalikuwa kwa mke wangu na kuona kama kweli ameolewa basi atakuwa amenifanyia ukatili mkubwa sana. Siku ya pili ilikuwa Jumatatu, sikuweza kwenda kazini, nilikuwa kama mtu niliyefiwa, hata chakula kilinishinda.

Jioni Simon alikuja kunitazama na mmoja wa wafanyakazi wenzangu na kunikuta nimejilaza sebuleni mikono kichwani huku pembeni ya macho yangu yakiweka michirizi na kulowesha kwenye mito ya kochi. Simon alinishangaa sana na kuniuliza:

“Kazala una matatizo gani?”
“Simon wewe si wakuniuliza swali kama hilo, unajua vizuri matatizo yangu,” nilimjibu bila kumuangalia.
“Kazala umetoka nyumbani kufuata mapenzi au kazi?”

“Nimefuata kazi.”
“Unaacha kwenda kazini kwa ajili ya mwanamke, nilikueleza toka zamani kuwa huyu mwanamke si chaguo sahihi kwako, lakini ukaona labda nakuchokonoa majibu sasa umeyaona.”

“Simon usiseme hivyo wewe ndiyo sababu ya mke wangu kunikimbia.”
“Mimi?” Kauli yangu ilimshtua Simon.
“Ndiyo.”
“Mimi nimefanya nini?” alionesha kushangaa.

“Ushauri wako ndiyo sababu ya mke wangu kukimbia.”
“Kweli aliyekuroga amekufa, kitendo cha kumfumania mkeo ni mimi? Si ulitaka kufa kwa mawazo nimekusaidia bado huoni msaada wangu?”

“Msaada gani wakati mke wangu kanikimbia.”
“Mkeo yule sawa na kuku aliyelala nje, si kuku tena ni kwale.”
“Lakini umeona lawama zote zinatokana na ninyi watu wa pembeni kuingilia ndoa yangu.”

“Hao watu wa pembeni unaowalaumu ndiyo waliomponya mwanao aliyekuwa fundi majiko.”

“Pamoja na hayo, lakini ninyi ndiyo chanzo cha mke wangu kukimbia.”
“Kwani shemeji kaenda wapi?” Shedu, mfanyakazi mwenzangu aliyeongozana na Simon aliniuliza.

“Hata najua yule mwanamke kaamua kuniua ningali hai,” nilizungumza kwa sauti ya kukata tamaa.
“Kazala wanawake wamekwisha mpaka uchanganyikiwe kiasi hiki?” Shedu aliniuliza.

“Kwani huyo aliyemchukua mke wangu hakuona wanawake wengine mpaka kamchukua mke wangu? Kibaya zaidi jana kamuoa kabisa.”
“Utani huo! Atamuoaje mke wa mtu?” Shedu alishtuka.

“Mpaka kamtoa kwangu atashindwa vipi kumuoa kabisa?”
“Kwa hiyo Kazala bado unampenda mkeo?” Shedu aliniuliza akinikazia macho.
“Tena sana.”
“Na akirudi utakuwa tayari kumsamehe?”

“Ndiyo, najua si akili yake ni ushawishi wa watu wenye fedha wanaoona maskini kama sisi hatuna haki ya kuwa na wanawake wazuri.”

“Mtu mwenyewe unamjua?”
“Kwa sura namjua ila sijui anakaa wapi?”
“Upo tayari kumeza mfupa?”

“Una maana gani?”
“Najua huna uwezo wa kushindana na yule bwana kwa nguvu na fedha, lakini lipo kimbilio la wanyonge nakwambia mkeo atarudi mwenyewe.”
“Kimbilio la wanyonge! Kimbilio gani?” nilishtuka kusikia vile na kutaka kulijua hilo kimbilio la wanyonge.

“Kwa babu.”
“Kwa babu una maana gani?”
“Kwa mganga wa kienyeji.”
“Kweli ataweza?” nilimuuliza kutaka uhakika.

“Bwana wee tena hawa wanaopenda wake za watu kazi yake ndogo sana, nakwambia ndani ya siku mbili mkeo atarudi, ikivuka haifiki wiki.”

“Kweli?”
“Kweli kabisa, unajua taarifa zako nimezisikia toka kwa swahiba wangu hapa, roho iliniuma na kuona umefanyiwa ukatili, kibaya nasikia jamaa ana mke yaani asiridhike na mkewe aje amchukue wako? Tena nitakupeleka mguu kwa mguu hadi kwa mzee wangu, nakuapia mkeo atarudi,” Shedu alinihakikishia kunirejeshea furaha.

“Kama kamuoa?” niliuliza swali ambalo kwangu lilikuwa tata.
“Nimekueleza mkeo atarudi, si mkeo wa ndoa?”
“Ndiyo.”
“Basi atarudi huyo, tukifika kwa babu kazi imekwisha.”

“Gharama zake?”
“Si kubwa sana, utamudu tu.”
“Huyo babu yupo wapi?”
“Tanga katika Wilaya ya Lushoto Kijiji cha Mlalo kisha unaingia ndani zaidi kuna sehemu inaitwa Tewe, hapo temea mate chini kuna kufuru za ajabu, watu wanaweza hata kumfufua maiti akatembea.”

“Nauli yake si kubwa?”
“Ya kawaida utaimudu.”
“Mmh! Nipo tayari hata kesho.”
“Itabidi muombe ruhusa ya siku mbili ili mwende na kurudi,” Simon aliyekuwa kimya muda wote alichangia.
“Lakini Shedu usemacho ni kweli?” pamoja na Simon kuchangia bado sikumuamini Shedu.

“Kwa nini tuandikie mate na wino upo? We twende halafu uniulize swali hilo baada ya kutoka kwa babu.”
Tulikubaliana kesho nikaombe ruhusa kazini ili twende Mkoa wa Tanga kwa mtaalam.
 
Back
Top Bottom