Simulizi: Mchawi

Simulizi: Mchawi

SEHEMU YA 20:

Yule mtu aliondoka na kuniacha na mke wangu ambaye alionesha kushtushwa na hali yangu.
“Mume wangu vipi?” aliuliza huku akitokwa na machozi.

“Naumwa?” nilimjibu huku moyo wangu ukiniuma mpaka machozi yalinitoka kitu kilichomshtua mke wangu na kuzidisha kilio. “Maskini mume wangu, unaumwa nini baba Zawadi?”

“Malaria.”
Alinichukua hadi bafuni na kunivua nguo zote kisha alinimwagia maji, na kunisaidia kurudi ndani. Alinitengenezea uji haraka na kuninywesha, kila kitendo cha upendo alichonifanyia mke wangu kiliuumiza moyo wangu baada ya kuona ni unafiki.

Lakini mke wangu ugonjwa wangu ulimgusa sana, muda wote alikuwa karibu yangu mpaka nilipopitiwa na usingizi. Nilipoamka nilimkuta pembeni yangu mkono shavuni.

“Mume wangu,” aliniita kwa sauti ya upole.
“Naam.”
“Poleee.”
“Asante.”
“Unaendeleaje kwa sasa?”
“Sijambo kidogo.”

“Nikutayarishie chakula gani?”
“Sijisikii kula,” pamoja na huruma yake ya mamba sikuipenda zaidi ya kumuona mnafiki.

“Mume wangu, kumbuka umemeza dawa kali, unatakiwa kula ili dawa zifanye kazi.”

“Nitakula baadaye.”
“Hapana, kuna ndizi na nyama nimekuandalia, naomba ule kidogo.”
“Hapana sijisikii kula.”

“Mume wangu.”
“Naam.”
“Mimi nani yako?”
“Mke wangu.”
“Unataka nani akubembeleze ili umsikie?”
“Wewe.”

“Kwa nini hutaki kunisikia?”
“Si nimekueleza nitakula baadaye.”
“Ni wazi huna mapenzi na mimi hata kunisamehe kwako kulikuwa kwa uongo.”
“Jamani mi si naumwa?”

“Kuumwa gani, ni wazi najilazimisha kwako huna mapenzi nami.”
Nilishangaa mke wangu akizungumza kitu ambacho hakikuwepo zaidi ya mimi kutojisikia kula. Niliamini kama nitaendelea kukataa naweza kuzalisha mapya, nilikubali kula kitu kilichomfurahisha mke wangu.

Baada ya kula nilijitahidi kulala lakini usingizi uligoma kunichukua, kila nilipofumba macho niliyaona matukio yote yakijirudia toka la mwanangu kuchelewa kutembea na siku niliporudi ghafla na kumkuta mwanangu akiwa katika mazingira mabaya.

Pia nilipomshuhudia mke wangu akiteremka kwenye gari na pia siku aliyorudi siku ya pili na kunidanganya kuwa alikuwa kwenye sherehe ya harusi kumbe alikwenda kulala na mwanaume. Na la siku ile nililoshuhudia kwa macho yangu akiwa na mwanaume kama walivyozaliwa katika kitanda changu
 
SEHEMU YA 21

Kila yalivyojirudia akilini mwangu niliumia nikajikuta nalia peke yangu kitandani. .
Nilipatwa na fikra za kuachana naye lakini moyo ulikataa kwa kuamini sitampata mwanamke mzuri kama yeye.
Niliamua kufa na tai shingoni, niliificha siri ile moyoni mwangu kwa kuamini kama ningeisema basi ningeachana naye kwa mazingira niliyoyaona na mazungumzo niliyosikia.

Kwa kuwa sikupenda kuwepo nyumbani kutokana na kuumia kila nilipomuona mke wangu, niliamua kwenda kazini siku ya tatu japo sikuwa nimepona vizuri.

Baada ya tukio lile nilizidi kuteseka kwenye maisha yangu kila nilipokuwa kazini, nilijua mume mwenzangu atakuja nyumbani. Moyo ulikuwa ukinilipuka kwa kujua muda ule nilikuwa nasalitiwa. Kila nilipokuwa peke yangu nilijikuta nashindwa kufanya kazi na kuhama kimawazo, nikawa nahisi kama dunia nzima nimeibeba kichwani mwangu.

Kutokana na kuwa na wasiwasi wa moyo juu ya vitendo vya mke wangu, hali yangu ilianza kubadilika. Nilikuwa nikipungua mwili kila kukicha. Wa kwanza kunigundua hali hiyo alikuwa mke wangu ambaye alitaka kujua nina tatizo gani.
“Mume wangu mbona upo hivi, una tatizo gani?”

“Nipo sawa,” nilijibu kwa mkato.
“Hapana mume wangu, kuna kitu kinakusumbua.”

“Mbona mimi nipo sawa.” “Si kweli, toka ulipougua hujarudi katika hali yako ya kawaida, pia hata ule uchangamfu wa ndani umepotea. Kama bado unaumwa turudi hospitali tujue una tatizo gani.”
“Hapana nipo sawa,” niliendelea kumkatalia mke wangu.

Nilimkatalia kwa kuamini chanzo ni yeye hata kama ningemwambia kuwa nilimuona akifanya mapenzi na mwanaume mwingine kwenye kitanda changu ningeongeza msumari wa moto kwenye kidonda.

Nilijua lazima angeomba talaka kutokana na kunipa masharti nikirudi nyumbani nimpigie simu japo nilimpigia zaidi ya mara kumi bila kupokelewa.

Pia niliyafuatilia maneno yake aliyomhakikishia yule mwanaume kuwa siwezi kurudi nyumbani kwa vile alinieleza nirudi kwangu kwa taarifa. Niliamini kama ningemueleza ningekuwa nimevunja masharti ya kurudi nyumbani bila taarifa japo simu haikupokelewa.

Kama angeniacha, lingekuwa pigo kutengana naye, pamoja na matatizo yote bado alikuwa mtu muhimu sana kwangu.
 
SEHEMU YA 22

ilipoishia...:

Pia niliyafuatilia maneno yake aliyomhakikishia yule mwanaume kuwa siwezi kurudi nyumbani kwa vile alinieleza nirudi kwangu kwa taarifa. Niliamini kama ningemueleza ningekuwa nimevunja masharti ya kurudi nyumbani bila taarifa japo simu haikupokelewa.
Kama angeamua kuniacha kwangu lingekuwa pigo kubwa kutengana na mke wangu ambaye pamoja na matatizo yote bado alikuwa mtu muhimu sana kwangu.

SASA ENDELEA,...:
“Au bado una yaleyale?” mke wangu aliniuliza kwa sauti ya unyonge.
“Yapi hayo?” nilimuuliza kwa kuhofia ameshtukia kilichokuwa moyoni mwangu.
"Si kuhusu mgogoro wetu wa mi natembea nje ya ndoa.”

“Walaa yote mbona yaliisha.”
“Ndiyo maana nikaja kupanga huku tuishi kwa raha mustarehe, mume wangu toka tuhamie huku nimeisha ondoka bila ruhusa yako?”

“Hapana.”
“Au nimeishafanya jambo lolote baya?”
“Hapana.”
“Au la kutoa mimba bado linakutesa?”
“Walaa.”

“Sasa nini mume wangu?”
“Nina wasiwasi malaria bado haijaisha,” ilibidi nidanganye ili kumfanya mke wangu aachane na mimi kwa vile alikuwa kero mbele yangu.

“Basi mpenzi naomba ukaangalie afya yako kwa kweli hali yako ilivyo hata mimi sina raha,” mke wangu alisema kwa sauti ya huruma.
“Nina imani nitakuwa katika hali ya kawaida muda si mrefu.”

“Fanya hivyo mume wangu,” maneno ya mke wangu bila kumfumania nisingekubali kama anahujumu ndoa yetu, alikuwa na maneno matamu yenye kumfanya maskini kujiona tajiri na asiye na nguvu kujiona anaweza kuibeba dunia nzima peke yake.

Nilikubaliana naye ili kuwa mbali naye, lakini kazini moyo wangu ulikosa raha na kujuta siku niliyokuwa naumwa kurudi nyumbani. Heri ningeendelea kuamini naibiwa bila kuwa na uhakika kama siku ile niliyoshuhudia kwa macho yangu.

Kila nilipokuwa peke yangu tukio la kumfumania mke wangu lilijirudia na kuwa mateso mazito moyoni mwangu.

Kila kukicha mwili wangu ulikuwa ukikongoroka, kila aliyenijua aliniuliza nimekumbwa na kitu gani akiwemo bosi wangu ambaye alinibembeleza nimueleze nasumbuliwa na nini ili anisaidie hata kwa fedha zake za mfukoni.
 
SEHEMU YA 23

Moyoni niliapa kufa na siri yangu kwa kutomwambia mtu yeyote aibu yangu. Hali yangu ya kiafya ilizidi kubadilika, mwili kila kukicha ulipungua uzito kwa mawazo, chakula nilikula lakini sikusikia ladha yake. Kuna kipindi nililaani kuwa maskini kwa kuamini kama ningekuwa na uwezo mke wangu asingechukuliwa na mwenye fedha.

Rafiki yangu wa karibu, Simon alinifuata siku moja baada ya kunikuta nimejisahau huku machozi yakinitoka.
“Kazala,” aliita kwa sauti.
“Ee..eeh?” nilishtuka kama nilikuwa usingizini.

“Kazala una tatizo gani rafiki yangu?” aliniuliza akiwa amenikazia macho.
“Sina tatizo,” nilimjibu huku nikifuta machozi kwa kiganja cha mkono. “Hapana Kazala kuna tatizo zito ulilonalo lakini hutaki kulisema.”

“Nipo sawa rafiki yangu,” nilikataa kwa kuamini kusema linalonisumbua nitakuwa nimejivua nguo hadharani.
“Kalaza unajiona ulivyo?”
“Kwani vipi?” nilijifanya kushtuka japo ukweli niliujua.

“Kazala haupo sawa, usiponieleza mimi swahiba wako utamueleza nani? Kumbuka mimi huku ndiye ndugu yako wa karibu. Japo tangu mlipohamia Uzunguni hutaki nifike kwako kwa kusingizio cha mkeo na kusahau ukifa sisi ndiyo wa kukuzika.”
Kauli ya Simon ilikuwa na ukweli kwani ndiye aliyekuwa mtu wangu wa karibu kwa kuelezana siri zetu za ndani.

Lakini siri ya mke wangu sikumueleza japo ilikuwa ikifahamika mtaani lakini hakukuwa na mfanyakazi mwenzangu aliyekuwa akijua nini kilichokuwa kikiendelea ndani ya nyumba yangu.

Pia mke wangu baada ya kuhamia makao mapya alipiga marufuku rafiki zangu wote akiwemo mtu wangu wa karibu kama Simon wasifike kwetu, nami kutokana na mapenzi mazito nilimkubalia.
“Simon nipo sawa,” bado niliendelea kufa na siri yangu moyoni.

“Kazala nitazame.”
Nilimtazama, tulikaziana macho kwa muda kisha alisema:
“Kazala una tatizo zito, nakwambia utakufa kwa kihoro.”

“Kihoro?” nilishtuka.
“Ndiyo, kila kukicha utapungua mwisho utakufa umelala.”
“Una maana gani?” kauli ya Simon ilinishtua.

“Hujioni, hii ni hali yako?” ajabu Simon alikuwa mkali kama yeye ndiye mwenye tatizo.
“Sasa kipi cha ajabu?” nami nilikuwa mkali.
“Mkeo atakuua.”
 
SEHEMU YA 24:

“Eti?” nilishtuka kusikia vile.
“Unashtuka nini?”
“Umejuaje?”
“Siyo nimejuaje, kila mtu anakuonea huruma, kwa akili yako unaona ni siri kwa vile hutaki ushirikiano na kumuona mkeo ni kila kitu, watu wote wamekuacha waone mwisho wake. Lakini sipo tayari kukuona ukipotea kwa vile unanihusu Kazala.”

Yalikuwa maneno makali yaliyonifanya mwili wangu utetemeke na jasho kunitoka. Kauli ile ilikuwa kama mkuki moyoni mwangu, nilijikuta midomo na koo vikinikauka ghafla na kukosa la kusema, nikajiona kama mtu niliyekuwa nikitembea uchi siku zote na kujiona nimevaa kumbe watu wananiona sina nguo. Moyo uliniuma sana na kujiona kiumbe niliye na bahati mbaya.

Nikiwa nimeinama chini kama mwari machozi yakinitoka, Simon alinishika begani na kuniita jina langu.
“Kazala.”

Sikuitikia kwani midomo ilikuwa kama ina nta, kila nilipojaribu kuifungua ili niitikie iligoma kufunguka. Nilinyanyua uso na kumtazama Simon aliyekuwa akinitazama kwa jicho la huruma huku machozi yakinitoka.

“Kazala,” aliniita tena.
“Na.na..am,” niliitika. “Pole sana, najua kiasi gani mapenzi yanavyotesa.”
“Ninyi mmejuaje?” nilijikakamua na kumuuliza swali ambalo niliamini ni siri yangu.

“Mbona siri ipo wazi, taarifa hizi zilinifikia muda mrefu tangu matatizo ya mwanao kuchelewa kutembea. Pale mtaani kwenu kila nilipokuja kukutembelea nilielezwa tabia chafu za mkeo lakini nilishindwa nianzie wapi kukueleza kutokana na wewe jinsi unavyompenda mkeo.

“Kwa kweli nilihofia kuitenganisha nyumba yako kutokana na wewe kumuamini sana mkeo. Huwezi kuamini kuna mtu mmoja wa nyumba mliyokuwa mnakaa zamani, kila nilipokuja na kuondoka alinifuata njiani na kunieleza unavyopelekwa na mkeo kwa tabia zake chafu na kuniomba nikueleze ili uweze kumdhibiti mkeo.
 
Back
Top Bottom