Simulizi: Mchawi

Simulizi: Mchawi

SEHEMU YA 25

ILIPOISHIA

“Mbona siri ipo wazi, taarifa hizi zilinifikia muda mrefu tangu matatizo ya mwanao kuchelewa kutembea. Pale mtaani kwenu kila nilipokuja kukutembelea nilielezwa tabia chafu za mkeo lakini nilishindwa nianzie wapi kukueleza kutokana na wewe jinsi unavyompenda mkeo.

“Kwa kweli nilihofia kuitenganisha nyumba yako kutokana na wewe kumuamini sana mkeo. Huwezi kuamini kuna mtu mmoja wa nyumba mliyokuwa mnakaa zamani, kila nilipokuja na kuondoka alinifuata njiani na kunieleza unavyopelekwa na mkeo kwa tabia zake chafu na kuniomba nikueleze ili uweze kumdhibiti mkeo.

SASA ENDELEA...

“Lakini bado ningeanzia wapi kukueleza unielewe? Bado kwangu ulikuwa mtihani mkubwa. Baada ya ninyi kuhama nilikutana naye tena yule aliyekuwa akinipa taarifa za mkeo, akaniambia kuwa nyumba uliyohamia umepangiwa na mwanaume mwenzio, bwana wa mkeo.

“Kwa kweli habari zile ziliniumiza sana lakini vilevile sikuweza kukueleza chochote baada ya mkeo kukukataza usitembelewe na rafiki zako nikiwemo mimi mtu wako wa karibu. La kunikataza nisije kwako halikuniumiza kwa vile hata nilipoacha kuja kwako hakuna kilichopungua kwangu.

“Hali yako ya sasa iliwachanganya sana watu wengi, najua uliulizwa na kila mtu akiwemo bosi, hakuna hata mmoja uliyemueleza tatizo lako. Juzi kuna kitu nilisikia sijui mkeo katoa mimba ya mwanaume wa nje na watu kusema huenda imekuchanganya sana.

“Japokuwa nilikuwa najua kila kitu lakini nilitaka kauli toka kwako kwa kujitahidi kukubembeleza lakini umekuwa ukificha ukweli wakati unazidi kuteketea.

“Lakini hali yako kila kukicha imekuwa ikizorota huku ukiwa mtu wa kuhama kimawazo kila dakika, unajisahau kama upo kazini. “Wengi wanakuonea huruma japokuwa matatizo yako wewe unajua ni siri yako, kutokana na kufanya siri wenzako waliamua kukuacha waone mwisho wako, wengi wanakuona mjinga kuendeshwa na mwanamke.

“Hebu naomba unieleze kila kitu usinifiche mimi rafiki yako. Kwa nini umefikia hatua hii ikiwa kila kitu cha mke wako unakijua?” alisema Simon kwa uchungu.
 
SEHEMU YA 26

“Simon, sijui hata nikwambie nini? Kwa kweli vitendo vya mke wangu vinaniumiza na kunitesa sana. Nilimuamini sana lakini aliyonifanyia nashindwa nifanye nini.

Niliona aibu kukueleza mwanzo kwa kuogopa aibu hii, lakini kumbe natembea uchi nikiamini nimevaa nguo,” niliinama kwa uchungu huku machozi na kamasi vikinitoka.
Moyo uliniuma na kujiona kwa hali ile sikuwa na faida ya kuendelea kuishi.

Niliona heri nife kuliko aibu ile ambayo nilijiuliza kazini pale watanielewaje? Baada ya kuwaza na kukosa jibu, nilimuuliza Simon anaweza kunisaidia nini.
“Simon ndugu yangu hapa nilipo najiona kiumbe nisiye na faida duniani.”

“Kwa nini?”
“Hebu nieleze nitaficha wapi sura yangu ikiwa kila mtu anaijua siri yangu, kupungua kwangu si kwa sababu ya yote uliyosema ni kitu kingine kabisa, heri nife.”

“Ufe kwa ajili ya mwanamke?”
“Ndiyo Simon, jambo alilonifanyia kwa kweli limeniumiza sana sana.” “Kitu gani tena rafiki yangu?”

Kwa vile kila kitu changu kilikuwa wazi niliamua kumueleza ukweli nilivyomfumania mke wangu na mwanaume ndani ndipo aliponiuliza huku ameshika mdomo kwa mshtuko.

“Ha! Halafu ukafanyaje? Haki ya nani ningekuwa mimi, sasa hivi ningekuwa nasubiri hukumu ya kunyongwa. Ndani ya nyumba yangu tena kitandani kwangu? Dharau gani hiyo Kazala?”

Simon aliniuliza, macho yakiwa yamemtoka pima.
Nilimueleza nilivyoondoka na homa yangu na niliyoyakuta na jinsi nilivyoshindwa kuingia ndani na kuondoka na kuzidiwa na kuanguka njiani kisha kulala kwenye matapishi.

“Kazala...kazala...Kazala huo ni uanaume gani? Unamuacha mgoni wako chumbani kwako tena kitandani kwako? Hata kama nyumba amepanga bado pale ni kwako. Kibaya umeondoka unaumwa unataka kufia njiani, rafiki yangu hayo ni mateso gani anayokutesa mkeo?”


“Ningefanyaje na mke wangu alinikataza nisirudi nyumbani mpaka nimtaarifu. Kama ningerudi na kumfumania lazima ningekuwa nimevunja makubaliano yetu na angedai talaka.”

“Kazala umeoa au umeolewa?”
“Nimeoa.”
“Kwa nini mkeo akupande hadi kichwani na kukupangia atakavyo?” Simon alisema kwa uchungu.

“Siyo kunipangia ni makubaliano yetu,” nilijikuta nikimtetea mke wangu pamoja na yote aliyonifanyia.
 
SEHEMU YA 27….

“Acha ujinga, mwenye amri kwenye nyumba ni mwanaume, umeona sababu ya kupangiwa kurudi nyumbani? Ilikuwa ili ajiandae usimfumanie. Umerudi mara moja na kukuta yale, hebu jiulize tangu mhamie hapo ni mara ngapi yule mwanaume anakuja kama kwake na kufanya uchafu wake?”

“Nashangaa sasa hivi sijui amekuwaje, lakini siku zote mke wangu alikuwa mtu mwenye heshima, hata sijui kabadilika vipi?” bado niliendelea kumtetea mke wangu.

“Kazala mkeo si mtulivu tangu mwanzo, sema ulikuwa hujui kwa vile jambo usilolijua ni sawa na usiku wa giza. Lakini hafai kuwa mke wa mtu. ”

“Kwa hiyo unanishauri nini kwa hili?”
“Hapa hakuna chochote cha kufanya, kama umeyajua yote mabaya ya mkeo na mengine kushuhudia kwa macho yako unasubiri nini, unataka akuue?”
“Unanishauri nifanye nini?”

“Yule mwanamke hakufai, achana naye ujipange upya bila hivyo atakuua kwa kihoro. Hebu jiangalie, umeshuhudia uchafu wa mkeo mara moja tu, umekuwa hivi kama mgonjwa wa kifua kikuu. Ameshakujua wewe nyoka wa plastiki huumi, ipo siku atakuteremsha kitandani ili alale na mwanaume wake.”

“Wee atawahi?” nilijikakamua mwanaume.
“Utafanya nini?”
“Nitaua mtu.”
“Hukuua mtu ulipofumania watu wapo kitandani hawana nguo mwilini, utaweza kusema kitu mbele ya mwanaume mwenzako aliyewapangia nyumba?”

“Lakini nilimsikia akisema hata yeye hapendi kuja pale nyumbani ila mke wangu ndiye anayemlazimisha,” najua majibu yangu yatakufanya unicheke na kuniona zuzu, nioneeni huruma mwenzenu kweli nilikamatika, kupenda kubaya, nilikuwa zuzu kwisha kazi.

“Kazala majibu gani hayo? Mbona kupenda kumekugeuza zuzu, au umeinamishwa?”
“Sijainamishwa,” nilikataa katakata neno la kuinamishwa na mke wangu zaidi ya kumpenda tu.

“Basi ndugu yangu kwa usalama wako muache yule mwanamke kabla hajakuacha, la sivyo muda si mrefu utakufa au kuwa nwendawazimu.”
“Kwa kweli kuachana na mke wangu siwezi labda unipe njia nyingine ya kumtuliza.”

“Utamtuliza vipi?”
“Kwa vyovyote vile hata kwenda kumueleza yule jamaa aachane na mke wangu.”

“Mimi siwezi kufanya hiyo kazi, labda ukamueleze mwenyewe kwani mbaya wako si unamjua?”
“Basi nakuomba kitu kimoja.”
“Kitu gani,” kauli ile ilinifanya nikae vizuri kumsikiliza.
 
Back
Top Bottom