Kauli ya Waziri wa Mawasiliano na Miundo mbinu wa SMZ, Rashid Seif Suleiman ya kuvilaumu vyombo vya habari vya Tanzania BARA ilinishangaza sana.
Ni kweli kabisa kuna kitu viongozi wetu waasisi wa 'muungano' walikiona kama kilikuwa ni cha muhimu sana kuziunganisha nchi zetu, lakini vile vile makosa ya kutokuelimishwa na kutoshirikishwa kwa wananchi wengi katika kufikia uamuzi huo ndiyo yamechangia kwa kiasi kikubwa kuwa chanzo cha mitikisiko na utegemezi katika 'muungano'.
Imedhihirika kuwa viongozi wakuu waliokuja baada ya marehemu Sheikh Abeid Amani Karume na pia Wazanzibari wengi hawakutaka kuendelea kuwepo muungano na kwa sababu hiyo ilibidi viongozi wetu wawabembeleze kihoja na ilipobidi pia yalitumika mabavu ili waendelee kuwepo mwenye 'muungano' . Hii ilipelekea wananchi wengi wa Zanzibar na pia wachache wa bara kuamini kama viongozi wakuu wa bara walikuwa na ajenda fulani za siri ambazo kuzitimiza ilibidi tuwaombe na kuwashinikiza Wazinzibari waendelee kuwepo kwenye 'Muungano'.
Fikra na mitazamo hii imekuja kujisimika zaidi pale badhi ya viongozi wakuu wa Zanzibar walipotiwa misukosuko pale walipohoji uwepo wa muungano na manufaa yake.
Kwa sasa wanafanya kila wanachotaka bila kujari mshikamano, sheria na taratibu za nchi wakidhani kuwa Tanganyika inawahitaji sana zaidi ya wao kuihitaji Tanganyika.
Hata kujitoa kwao katika sheria za Jamhuri ya muungano zinazohusu usafiri wa majini za mwaka 2003 na kuunda sheria zao za bahari na usafiri na kuwa chini ya Zanzibar Maritime authority((ZMA) mwaka 2006 ilikuwa ni katika mwendelezo wa fikra hizo.
Waswahili wanasema, mdharau mwiba mguu huota tende!.
Tumezidharau na wakati mwingine kuzipuuzua chokochoko za 'muungano' kwa muda mrefu huku tukiwadekeza Wazinzibari kwa kuwapa kila kile wanalichokuwa wanakitaka na matokeo yake kwa sasa tunayaona. Kwa sasa imekuwa chao ni chao lakini chetu pia ni chao na wakati mwingine wanataka wakichukue chote.
Tulianza muungano vibaya na inavyoonekana pia tutaachana nao vibaya, na kwa maana hii, dawa ya muungano kwa sasa siyo serikali tatu kama baadhi ya watu wanavyodhani, bali ni kuachana kabisa na muungano ili pande zote zipate ukweli halisia kama kuna umuhimu katika muungano. Hatutakuwa wa kwanza wala wa mwisho katika kuvunja muungano kwa sababu kuna nchi zimevunja muungano na zikapiga hatua zaidi za kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Hata katika ndoa, watu wanapokinzana sana, huwa wanafikia maamuzi ya kuachana ili kujipima na kuona umuhimu wa wao wakiwa pamoja au wakiwa single (space) na wakipatwa na reality, wengi wao hurudiana tena.