Monday, 08 August 2011
NA HAMIS SHIMYE,
Gazeti la Uhuru
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imeitoza faini ya sh. milioni 100 CHADEMA, baada ya kubainika inakwepa kodi tangu ilipoanzishwa mwaka 1992. TRA pia imeanza kukata kodi mshahara wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa na watumishi wengine wa CHADEMA.
Habari za kuaminika kutoka ndani TRA zilisema ulipaji faini unaanza mara moja, baada ya uchunguzi kukamilika na kuonyesha chama hicho hakilipi kodi.
Tumemaliza uchunguzi na kubaini CHADEMA hailipi kodi ya mishahara ya kila mwezi ya watumishi wake tangu ilipoanzishwa, kilisema chanzo chetu cha habari.
Imeelezwa kuwa, CHADEMA imekiuka sheria na kanuni za ulipaji kodi, zinazotaka mtu, kampuni au taasisi yoyote kulipa kodi TRA.
Ijapokuwa tangu ilipoanzishwa ilikuwa hailipi kodi, katika uchunguzi tulipata taarifa za kuanzia mwaka 2000 hadi sasa zinazoonyesha hailipi kodi, kilisema chanzo hicho.
Kutokana na hilo, chama hicho kinapaswa kulipa faini ya sh. milioni 100 na kimeamriwa kulipa kodi ya mishahara ya watumishi wake kuanzia mwezi uliopita.
Chanzo hicho kilisema CHADEMA imeiandika barua TRA ikidai wanacholipana ni posho na si mishahara.
Hata hivyo, sheria ya kodi inaeleza kiwango chochote cha posho kinachozidi kima cha chini cha mshahara kinapaswa kukatwa kodi.
Watendaji ambao TRA imeanza kuwakata kodi ni Dk. Slaa, ambaye analipwa mshahara wa zaidi ya milioni 7.4, fedha ambazo ni nyingi kuliko mshahara wa mbunge.
Mshahara huo unatokana na mapendekezo ya Azimio la Kamati Kuu ya chama hicho iliyokutana Januari 29 na 30, mwaka huu, mjini Dar es Salaam, ambapo mshahara huo umegawanya katika sehemu sita.
Sehemu hizo ni posho ya mwezi, fedha za mafuta, majukumu, viburudisho, nyumba na utendaji kazi, ambapo mshahara wa mwezi ni sh. 2,300,000.
Fedha za mafuta ni sh. sh. 1,387,000 kwa wastani wa lita 750 kwa mwezi, huku fedha za majukumu zikiwa sh. 575,000, mawasiliano sh. 460,000 na nyumba sh. milioni moja.
Posho kwa ajili ya viburudisho sh. 462,500 na utendaji kazi sh. 989,000. Mshahara huo umefanywa maalumu kwa Dk. Slaa pekee na iwapo chama hicho kitapata katibu mkuu mwingine hawezi kulipwa mshahara kama huo.
Last Updated ( Monday, 08 August 2011 19:34 )
Ama kweli sikio lakufa halisikii dawa. Ule usemi wa Nyerere kwamba serikali za kifisadi zinawaogopa sana matajiri na badala yake zinafukuzana na walipa kodi wadogo wadogo umedhihirika. Hapa kuna maswali mengi zaidi ya majibu. Je, kati ya vyama vya kisiasa zaidi ya 18 ni CHADEMA pekee ndiyo hawakuwa wakilipa kodi kwa watumishi wao?
Na tukuwapekua CCM tangu kurejelewa mfumo wa vyama vingi; walikuwa wakilipa kodi kikamilifu TRA? Na kwa nini CHADEMA pekee na si CCM, CUF, NCCR, TLP na vinginevyo pia? Huu ndiyo ugonjwa wa asasi zetu.
Tatizo la asasi karibu zote za serikali hii ya kifisadi ni kutumika kama vitengo vya propaganda vya CCM! Inasikitisha sana kuona asasi nyeti kama Usalama wa Taifa, JWTZ, Polisi, TRA, TAKUKURU n.k. zinapokea amri na kutekeleza maamuzi toka kwa mavuvuzela wa CCM. Si vibaya kwa vyama vya siasa kutozwa kodi lakini si sahihi kuchomeka interests za kisiasa kama ilivyo sasa. CCM ni vipofu na hawajui waendako. Ila kuna jambo moja wanapaswa kukumbushwa nalo ni kwamba kamwe hawatatawala milele.
Na sheria gandamizi wanazowatungia wapinzani sasa zitawasakama wenyewe watakapopigwa kumbo na kuwekwa pembeni kama ni kweli TRA ni wazalendo kiasi hicho katika kukusanya kodi mbona hawajatupa takwimu za kiasi walichokusanya toka kwa familia ya Kikwete yenye biashara lukuki zinazosimamiwa na Ridhwani?
Na vipi kodi ya zile nyumba walizokwapua toka milki ya serikali walizozikarabati na kuzipangisha wanalipashilingi ngapi kwa mwezi. Kikwete, Mkapa, Makamba, Maghufuli, kina Mboma, Mahita na mafisadi kibao walifanya vile, tunataka kujua ni kiasi gani nchi hii inakusanya tokana na kupangishwa nyumba hizo.
Mwisho tungependa kuuliza mbona wanawaogopa "Wawekezaji" wanaokamua gesi, dhahabu mpaka mashirika yakiwemo mahoteli makubwa na kampuni za mawasiliano zinazojibadilisha majina kila baada ya kwisha kwa Tax Holidays za jina la awali?