Salamu za rambirambi zatolewa
Rais Magufuli wa Tanzania ameandika haya katika ukurasa wake wa Twitter
Kwa niaba ya Serikali na Watanzania nakupa pole Mhe. Rais Uhuru Kenyatta na Wakenya wote kwa kuondokewa na Rais Mstaafu Daniel Toroitich arap Moi. Watanzania tutamkumbuka kwa uongozi wake mahiri, jitihada za kuimarisha uhusiano wetu na Kenya na kufufua Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Museveni akumbuka nyakati zao pamoja mwishoni mwa miaka ya 1970 na hadi miaka ya 80.
"Kwanza nilikutana naye wakati alikuwa Makamu wa Rais. Nilikuwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam. Kwa hivyo, tulikuwa tunafuata kile viongozi katika Afrika Mashariki walikuwa wakifanya,”alikumbuka.
Wawili hao walikutana tena katika mkutano jijini Arusha mnamo 1985. Moi alikuwa na mawaziri Charles Njonjo, marehemu Nicholas Biwott na Rais wa kwanza wa Tanzania Mwalimu Nyerere ambaye alifariki mnamo 1999.
"Wakati huo nilikuwa waziri. Aliwahi kuwa mpatanishi kati ya upinzani na serikali ya Uganda. Alikuwa mwana Afrika Mashariki mahiri na aliyeungaunga mkono umoja wa Afrika Mashariki."
Balozi wa Uingereza nchini Kenya Jane Marriott pia ametuma salamu za rambirambi kupitia Twitter.
"Nimesikitishwa na kifo cha Rais wa zamani wa Kenya, Mh. Daniel Toroitich Arap Moi. Kwa niaba ya Serikali ya Uingereza, napenda kufikisha kwa dhati salamu zangu za rambirambi. Mawazo yangu yapo kwa familia yake na marafiki, na watu wa Kenya #RIPMoi, "aliandika kwenye mpango wake wa twitter.
Balozi wa Marekani nchini Kenya Kyle McCarter amesema, "Marekani inasimama na Wakenya wakati huu wa maombolezo.
Mtindo wa mazishi ya Mzee Moi
Mazishi ya Mzee Moi yatakuwa ni mazishi ya sita kufanyika kitaifa, lakini ya pili tu ambayo yatafanyika kwa heshima kamili za kijeshi. Mtu mwingine pekee aliyewahi kufanyiwa maziko ya namna hiyo alikuwa Rais Jomo Kenyatta mnamo mwaka 1978.
Makamu wa Rais wa zamani Kijana Wamalwa, Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Wangari Maathai, Gavana wa zamani wa Nyeri Wahome Gakuru na Mke wa Rais Kibaki, Bi. Lucy Kibaki walizikwa kitaifa lakini bila ya heshima ya kijeshi.
Huduma ya mazishi imepangwa Jumanne kwenye uwanja wa Kasarani, Nairobi.
Kuangalia kwa mwili itakuwa Jumamosi, Jumapili na Jumatatu. Hapo awali, familia yake ilikuwa imetangaza kwamba tarehe ya mazishi ya marehemu itadhihirishwa na serikali.
Wakati wa Kutoa habari, mbunge wa Rongai, Raymond Moi, alielezea kwamba sababu iliyosababisha uamuzi huo ni kutokana na mazishi kushughulikiwa na Serikali.
Raymond alileza zaidi kwamba Moi anatarajiwa kuzikwa nyumbani kwake huko Kabarak.
“Ni mazishi ya ki-serikali sasa. Imechukuliwa na serikali kwa hivyo wanajeshi watashughulikia. Bado hatuwezi kupeana tarehe halisi mpaka tuungane nao. Nadhani tarehe hizo zitatolewa nao, “Raymond Moi alisema.
Februari 8, 2020: Mwili wapelekwa majengo ya Bunge, Rais Uhuru awaongoza Wakenya kutoa heshima za mwisho
Mwili wa Rais Moi umepelekwa katika majengo ya Bunge Februari 8 na unatarajiwa kukaa huko kwa siku tatu ikiwa ni heshima yake kwa Taifa hilo, ambapo Rais wa Taifa hilo Uhuru Kenyatta, ameongoza wageni mbalimbali kuutazama mwili huo katika viwanja hivyo.
Februari 10, 2020: Wakenya wautazama Mwili wa Mzee Moi kwa mara ya mwisho
Mwili wa Rais wa zamani Daniel arap Moi umepelekwa katika Majengo ya Bunge mapema leo Jumatatu asubuhi kwa siku ya mwisho ya umma wa Wakenya kuutazama.
Mamia ya Wakenya walisimama katika foleni wakisubiri wakati wengine wakitiririka ndani ya Majengo ya Bunge asubuhi ili kuuutazama kwa mara ya mwisho.
Huduma ya kumbukumbu ya kitaifa itafanyika Jumanne kwenye uwanja wa kitaifa wa Nyayo kabla ya mwili kusafirishwa kwenda nyumbani kwake Kabarak ambapo utazikwa Jumatano.
Wakenya walijitokeza kwa wingi katika Majengo ya Bunge siku ya Jumamosi na Jumapili ili kutoa heshima zao kwa rais huyo wa zamani.