Na Mwandishi Wetu
WIKI mbili tu baada ya kuanza kwa hatua za mwanzo za uchaguzi mkuu wa ndani ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), kampeni za "kuchafuana" majina miongoni mwa wanachama wanaokusudia kugombea Uenyekiti wa Taifa wa jumuiya hiyo muhimu kisiasa nazo zimeanza.
Hatua hiyo inakuja licha ya Baraza Kuu la Taifa la UVCCM lililokutana Dodoma Februari 9, mwaka huu, kuwaonya mapema wanachama wanaotaka kugombea uongozi katika uchaguzi huo "kutopakana matope", msimamo uliosisitizwa tena hivi karibuni na Mwenyekiti wa Taifa anayemaliza muda wake, Dk. Emmanuel John Nchimbi.
Wiki iliyopita, gazeti moja la kila wiki lilibeba makala ndefu iliyoandikwa na mtu aliyedai kuwa mwanachama makini wa UVCCM, ile ambayo ilikuwa "ikimshambulia" kwa mafumbo na hata waziwazi Naibu Katibu Mkuu wa Umoja huo (Tanzania Bara), Beno Malisa.
Hata hivyo, vyanzo vya habari vya kuaminika vinaeleza kuwa kuna kundi limezindua kampeni maalum ya "kumpaka matope" Malisa pamoja na mtoto wa Rais Jakaya Khalfani Mrisho Kikwete, Ridhiwani Jakaya Kikwete, ambaye ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Malisa amesema kwamba kuna lengo la "kumchafua" kisiasa kutokana na kinyang'anyiro cha uchaguzi mkuu wa UVCCM na kushangaa ni kwa nini.
"Wanasema uanachama wangu katika UVCCM hauna hata miaka mitatu, hapa ndipo uongo unapoanzia. Mimi nilikata kadi mbili kwa wakati mmoja: Ya CCM na ya Umoja wa Vijana wakati nasoma Chuo Kikuu (cha Dar es Salaam) mwaka 2001 na zote nilikabidhiwa na (aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Philip) Mangula", anasema Malisa na kuongeza:
"Kwa hiyo, yeyote anayejaribu kudanganya vinginevyo ana nia yake mwenyewe na hili kwangu siyo tatizo. Mimi naijua siasa, nafahamu kwamba siwezi kukubaliwa na watu wote maana hata Mitume walioleta dini kama Muhammad (SAW) na Yesu nao pia wanapingwa hadi leo. Kwa nini iwe ni ajabu kwangu ambaye ni binadamu wa kawaida kabisa?"
Lakini wakati kiongozi huyo wa juu wa UVCCM akiyasema hayo, vyanzo vingine vya habari vimeeleza kwamba anayetajwa kwa kisingizio cha minong'ono mitaani kuwa mwanasheria na mtoto wa "kigogo" wa CCM aliyejipa jukumu la kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni ya rafiki yake waliyesoma naye kuanzia shule ya msingi mpaka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam siyo mwingine isipokuwa Ridhiwani Jakaya Kikwete.
"Huyo anayelengwa ni Ridhiwani Kikwete na yule anayetajwa kuwa rafiki yake mkubwa waliyesoma pamoja huko kote ni Beno Malisa", kinasema chanzo kimoja cha habari hizi.
Akizungumza kwa simu yake ya mkononi, Ridhiwani amethibitisha kuwa amesoma na Beno Malisa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, lakini akakanusha tuhuma kuwa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni ya Naibu Katibu Mkuu huyo wa UVCCM na wala hajui kama anataka kugombea uongozi wa kuchaguliwa.
"Mimi siyo mwendawazimu nifanye kampeni za Uenyekiti unaosemwa wakati nafasi hiyo yenyewe hadi sasa bado haina mgombea", amesema.
Amesema Mwenyekiti wa Taifa wa UVCCM atachaguliwa Desemba 14, mwaka huu, na wale wanaotaka kugombea nafasi hiyo watachukua fomu miezi minne ijayo, kisha vitafuatia vikao vya mchujo ili hatimaye Kamati Kuu ije kuteua wagombea watatu watakaopigiwa kura na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa, hivyo haelewi tuhuma za yeye kumfanyia mtu kampeni hivi sasa zinatoka wapi.
Alipouliuzwa kuhusu kwenda katika mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara kuendesha mikutano ya kampeni, Ridhiwani amesema kila uongo unaotengenezwa juu yake unajengewa mazingira yanayoweza kukubalika.
Kwa mfano, amesema mkoa wa Pwani anakwenda muda wowote kwa vile ni kwao ambako kuna babu zake, bibi zake, baba zake, shangazi zake, kaka zake, dada zake, binamu zake, watoto wa ndugu zake na hata marafiki aliocheza nao alipokuwa mtoto.
"Hivi mtu anawezaje kupangiwa vipindi vya kwenda kwao? Mimi ninatoka Pwani na huko ndiko sehemu kubwa ya ndugu zangu kwa baba wanakoishi. Utaniambiaje nikienda Bagamoyo au Chalinze ninakwenda kufanya kampeni wakati ni nyumbani kwetu?" Amehoji.
Ameeleza kuwa hata baba yake mzazi alikuwa akienda Chalinze na Bagamoyo muda wowote alipokuwa hayupo chini ya itifaki kama sasa kwa vile ni kwake, na pia siku nyingine alikuwa akilala na kutokea huko asubuhi wakati akienda ofisini kwake Dar es Salaam, hivyo haiwezi kuwa "ishu" kwa yeye naye kwenda wakati ni kwao ambako ataishi hata baada ya kustaafu kazi za utumishi anazofanya hivi sasa.
Kuhusu Lindi na Mtwara, Ridhiwani amesema huko pia kuna babu zake, bibi zake, wajomba zake, mama zake wakubwa na wadogo, kaka zake, dada zake, binamu zake, watoto wa ndugu zake na marafiki aliocheza na kusoma nao, hivyo amekuwa akienda mara kwa mara katika mikoa hiyo miwili kuwatembelea ndugu wa ukoo wa mama yake anayetokea huko na pia Mkuranga katika mkoa wa Pwani.
Mbali na safari anazokwenda peke yake, nyingine amekuwa akifuatana pamoja na wadogo zake au mama yake, na kwamba katika miaka iliyopita alikuwa pia akienda na baba yake kabla "hajabanwa" na itifaki alipochaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kana kwamba haitoshi ameshangazwa na madai kwamba anafanya kampeni wakati hata Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa UVCCM watakaopiga kura za kumchagua Mwenyekiti na viongozi wengine nao bado hawajajulikana.
Amesema zaidi ya asilimia 75 ya wajumbe wanaomaliza muda wao hawana sifa za kugombea tena, hivyo kamwe hawatakuwepo katika uchaguzi huo huku waliobaki kama watawania tena ujumbe huo pia hakuna anayejua kwa uhakika endapo atashinda.
"Hivi anayetuhumu wenzake kwamba wameanza kampeni anaijua vizuri Kanuni ya Umoja wa Vijana au tumwelewaje?" Amehoji na kusema yeye ameiva kisiasa kwani amekuwa ndani ya UVCCM tangu akiwa mtoto mwenye umri wa miaka sita akianzia uanachama na uongozi wa Chipukizi.
Amewataka wanachama wanaotaka kugombea uongozi katika Umoja wa Vijana kuheshimu maadili pamoja na kanuni za uchaguzi na siyo kuogopana na kuanza "kuchafuana" majina.
"Kama mtu unataka kugombea Uenyekiti wa Taifa, Mkoa, Wilaya au nafasi nyingine kwa nini uanze kuchafua wenzako? Mimi ninadhani hiyo siyo njia sahihi ya mtu kushinda ila ni kujipotezea ushindi.
"Ukitaka kugombea uongozi wowote unaangalia kanuni na vigezo vilivyowekwa. Ukiona unakidhi vyote unaeleza kuwa mimi ninataka na sifa zangu ni hizi ili wapiga kura nao wakupime, wakutathmini na wewe uwaambie mikakati yako kuwa ukichaguliwa utafanya moja, mbili, tatu na kadhalika", amesema.
Akionyesha kiasi gani alivyo makini, Ridhiwani ametahadharisha kuwa yeyote "anayewapaka matope" wenzake iwe kwenye vyombo vya habari na hata vinginevyo ili kutaka uongozi ajue anajaribu kulima shamba kwa kutumia wembe badala ya kulimia jembe.
Naye kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM (Tanzania Bara), Beno Malisa amesema uongozi wa kisiasa siyo sawa na uongozi wa kitaaluma kama vile Ugavana wa Benki Kuu, Udaktari Mkuu wa Mkoa, Uhasibu Mkuu wa Wizara, Ujaji wa Mahakama Kuu ama Uhandisi Mkuu wa Kiwanda.
Malisa ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM amesema kabla hajateuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu alikuwa Katibu Msaidizi Mkuu wa Idara ya Utumishi katika Makao Makuu ya UVCCM, na pia amekuwa mwanasheria wa kujitolea wa jumuiya hiyo na amefanya kazi inayoonekana.
Ili kuepuka majungu amewataka wenye mashaka naye waende ofisini kwa Katibu Mkuu wa UVCCM na kupata maelezo ya kesi alizoutetea mahakamani Umoja wa Vijana na kushinda zote, hatua iliyouepusha kulipa mamilioni ya fedha kwa walalamikaji waliokuwa wameushtaki ili kudai fidia kwa namna moja ama nyingine.
Pamoja na mifano mingine, kiongozi huyo wa juu wa UVCCM amesema kupanda au kushuka kwa madaraka ya kisiasa ni tofauti na yale ya kitaaluma kama Ukuu wa Kitivo cha Chuo Kikuu ambako mfanyakazi hupanda ngazi moja baada ya nyingine kwa mpangilio wa lazima.
"Katika siasa hakuna hayo. Leo unaweza kugombea ubunge na kuchaguliwa, kesho ukiapishwa tu unateuliwa kuwa Waziri na kuwaacha Wabunge waliokaa bungeni kwa miaka ishirini hata ishirini na tano na huwezi kusema eti huyu amechaguliwa jana.
"Asiyejua hilo atuambie ni kwa nini Mbunge kama (Chrisant Majiyatanga) Mzindakaya ambaye amekuwepo bungeni tangu mwaka 1965 siyo Waziri, lakini Lawrence Masha aliyechaguliwa kuwa Mbunge mwaka 2005 tu hapa tayari ni Waziri, au aseme ni kwa nini Dk. Maua Daftari amekuwa Naibu Waziri kwa zaidi ya miaka 12 mfululizo lakini William Ngeleja amekaa na wadhifa huo kwa takriban miezi 14 tu na kupanda kuwa Waziri kamili", amesema na kuendelea:
"Ni polisi gani aliyeanza kazi mwaka 2005 ambaye sasa ni Kamanda wa Mkoa? Ni daktari gani ameajiriwa mwaka 2005 ambaye sasa ni Mganga Mkuu wa Mkoa? Hiyo ndiyo mifano ya tofauti ya madaraka ya kisiasa na kitaaluma".
Kuhusu kuchaguliwa kwake kuwa Mjumbe wa NEC, kijana huyo amesema anashangazwa na madai kwamba "alibebwa" na UVCCM wakati nafasi hiyo hakuipata kwa kuteuliwa isipokuwa kwa kupigiwa kura na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM huku zaidi ya asilimia 99 miongoni mwao akiwa hafahamiani nao hata kidogo.
"Katika uchaguzi ule unakutana na wajumbe karibu 2,000 kutoka nchi nzima palepale ukumbini. Unaitwa jina lako na Mwenyekiti (wa Taifa wa CCM), unakwenda mbele na kupewa dakika tatu za kujieleza kwao ili wakujue wewe ni nani na kwa nini unadhani unafaa kuwa Mjumbe wa NEC. Wao ndio wanakutathmini na kuamua kila mmoja katika nafsi yake mwenyewe kama akupe ama akunyime kura. Hapo unawezaje kusema eti nilibebwa?" Amehoji.
Habari zilizolifikia gazeti hili muda mfupi kabla ya kuingia mitamboni jana usiku zinaeleza kuwa mbali na kuzinduliwa kwa kampeni maalum za "kumpaka matope" Beno Malisa anayeonekana kuungwa mkono na wengi katika UVCCM, jina la Ridhiwani Kikwete limekuwa likitumiwa bila yeye kujua ili "kumchafulia" Naibu Katibu Mkuu huyo kama ana nia ya kuchukua fomu ya kuwania Uenyekiti wa Taifa.
Vyanzo vya habari kutoka mikoa ya Pwani, Morogoro na Tabora, vinasema mkakati huo unasimamiwa na kugharamiwa kifedha na kundi la wafanyabiashara wenye asili ya Somalia ambao ndugu yao ni miongoni mwa vijana wanaotajwa kuwa na mipango ya kuisaka nafasi hiyo.
"Hao ndio wanatumia jina la mtoto wa Kikwete kuwatengenezea fitina walengwa hasa Beno Malisa kwa kumtungia uongo", vimedokeza vyanzo hivyo na kumtaja anayesaidiwa kwa njia "chafu" na kundi hilo ambaye hata hivyo jina lake hivi sasa tunalihifadhi.
SOURCE: GAZETI LA TAZAMA