Chadema sasa hali si shwari waendesha vikao vya siri kuwajadili wanachama
Na Fidelis Butahe
HALI ya kisiasa ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) inaonekana kuyumba baada ya Mwananchi kupata habari kwamba Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe juzi aliongoza kikao cha siri mjini Dodoma kilicholenga kuwajadili baadhi ya wanachama akiwemo mama mzazi wa Zitto Kabwe, Shida Salum.
Habari hizo kutoka ndani ya chama hicho, zilieleza kuwa waliohudhuria kikao hicho ni Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa, Hemed Sabula, John Mrema, Erasto Tumbo, Benison Kigaila, Halima Mdee, Lucy Owenya na Anna Komu.
Habari hizo zilifafanua kuwa Mbowe aliwasilisha ajenda ya kufukuzwa uanachama kwa afisa habari wa chama hicho, David Kafulila, mama mzazi wa Zitto Kabwe, Shida Salum ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho na Danda Juju ambaye ni afisa Mwandamizi kwa kuwa wanakichafua chama kwa kuchochea mgogoro kutokana na kuvujisha siri za chama kwenye vyombo vya habari.
Habari hizo, zilieleza kwamba baada ya Mbowe kuwasilisha hoja yake, ilipingwa na wajumbe wa kikao hicho kwa maelezo kuwa, Zitto Kabwe hatakubaliana na jambo hilo na kusisitiza kuwa linaweza kukipasua chama, lakini katika majumuisho Mbowe alisisitiza kuwa hataweza kufanya kazi na Kafulila hivyo alisisitiza kuwa Kafulila apewe barua ya kufutwa uanachama.
Kutokana na kusimamia uamuzi huo, ilidaiwa kuwa wajumbe wa mkutano huo walikubali kwa shingo upande umauzi huo.
Baada ya tarifa hizo Mwananchi liliwatafuta wahusika ambao walikiri kuwepo kwa taarifa za kikao hicho na kusisitiza kuwa wanasubiri kuona kama watapatiwa barua za kufutwa uanachama au la.
"Mimi hizo taarifa nimezisikia na nilikuwa najua kuwa kulikuwa na kikao kisicho rasmi kilichokaa Dodoma ila mpaka sasa sijapata barua yeyote, nasikia kuwa wanataka kunitimua uanachama, lakini ngoja tusubiri tuone wakinipatia barua kila kitu kitakuwa wazi," alisema Kafulila ambaye hivi karibuni alitangaza nia ya kuwania Ubunge mwaka 2010 Kigoma Kusini
Kafulila pia aliwahi kuwania nafasi ya Uenyekiti wa Baraza la Vijana la Chama hicho, (Bavicha) katika uchaguzi uliofanyika mwishoni mwa Agosti mwaka huu, lakini mshindi hakupatikana baada ya mpinzani wake, John Heche kupinga matokeo kwa madai kuwa kura 20 zilikuwa zimeongezeka.
Naye Danda Juju alisema taarifa hizo, amezisikia ingawa hana uhakika nazo na kusisitiza kuwa kwa kiasi fulani anaweza kuziamini kwa kuwa alikuwa na taarifa kuwa Mbowe anafanya kikao kisicho rasmi mkoani Dodoma. Mama mzazi wa Zitto, Shida Salum hakuweza kupatikana kuzungumzia sakata hilo.