Riwaya: Scolastica Temu

Riwaya: Scolastica Temu

SEHEMU YA 29



TULIPOKOMEA....
Alijitupa sofani na kurudia kukaa kihasarahasara vilevile; aogope nini ilhali yuko peke yake? Akaiwasha runinga na kuangalia chaneli yenye miziki mfululizo. Saa nane kasoro dakika kadhaa, chupa ya pili ikiwa nusu, alipitiwa na usingizi akiwa amekaa vilevile sofani, kihasarahasara!
***ENDELEA***
Alizinduka alfajiri saa kumi kasoro. Usingizi wote ukapaa. Bado hakuwa mtu mwenye utulivu akilini. Akaangaza macho huku na kule. Mara akanyanyuka na kuufuata mlango. Akajaribu kufungua, ukamgomea. Akagundua kuwa alifungua kwa funguo na komeo. Hapo akaridhika kuwa bado alijali hadhari kuhusu usalama wake.
Akarudi sofani na kuiangalia ile bia nusu aliyoiacha mezani usiku wa manane. Hakuwa na haja nayo. Utaratibu wa kunywa pombe alfajiri au kukiwa kumepambazuka kabisa, hakuwa nao. Alikuwa akisikia kuwa kuna watu hunywa bia asubuhi wakisema, ‘wanazimua’ kuondoa ulevi wa jana. Hiyo dhana haikuwamo akilini mwake asilani.
Alichofanya ni kuendelea kujilaza pale sofani na sasa hakuwa na muda hata wa kuendelea kuangalia runinga iliyokuwa bado ikiendelea kuporomosha muziki mfululizo. Hadi saa kumi na nusu alfajiri hiyo alikuwa amejilaza hapohapo sofani.
Aliwawazia wafanyakazi wenzake kule ofisini, akamwazia mkurugenzi wake ambaye alionekana kumjali na kuwa tayari kumsaidia katika kila shida aliyoambiwa. Akajisikia kuwa na hatia kwa uongo alioutengeneza siku aliporipoti ofisini asubuhi ya siku ya pili baada ya kubakwa kule Komakoma.
Je, wakijua kuwa hayupo Kigoma bali yupo hapohapo jijini Dar, watamwelewa vipi? Heshima yake itashuka! Hilo lilikuwa dhahiri, jambo ambalo hakutaka limkute. Kimoyomoyo alikuwa akimwomba Mungu awe naye katika kila hatua anayofikia ili aitimize azma yake.
Kwamba mambo ayafanyayo ni dhambi dhahiri mbele ya Mungu, hilo alilitambua fika, lakini akajiambia, ‘siwezi kuacha. Siachi asilani. Kama ni dhambi na iwe dhambi. Nitatubu mbele ya safari.’
Kelele za wapitanjia, pamoja na ngurumo za magari zilizidi kusikika kadiri muda ulivyokwenda. Hatimaye saa kumi na mbili u nusu ikamkuta akiwa hapohapo sofani. Mara akashtuka na kukimbilia kisengeretua mezani, Akabadili kituo cha runinga. Akaweka kituo fulani cha Tanzania ili ajionee taarifa zozote ziwe za magazetini au zingine.
Alikuta kituo hicho kikitangaza yaliyoandikwa magazetini. Mtangazaji alisoma vichwa vya habari vya kurasa za mbele za magazeti hayo. Nyingi zilikuwa za kisiasa na badhi zilihusu utendaji mbalimbali wa serikali katika kuwahudumia wananchi.
Habari za kurasa za ndani hazikusomwa, bali za kurasa za mwisho zilizozungumzia michezo, ndizo pia zilizosomwa. Akilini mwake aliijua Tanzania kuwa ni nchi kubwa, yenye Watanzania zaidi ya milioni hamsini na tano. Imekuwa ni nchi yenye mambo mengi, matukio makubwa kwa madogo. Kifo cha mtu mmoja aliyekutwa chumbani mwake huko uswahilini, mtu asiye na jina kubwa katika jamii, hakiwezi kuwa habari kwa vyombo vingi vya habari. Aliamini hivyo. Na kama kweli itakuwa habari, basi itakuwa na uzito mdogo kuliko ilivyo.
Zitaandikwa aya nne au tano na habari itaishia hapo.
Kwa hali hiyo, hakujisikia kuwa na hofu yoyote. Laiti angekuwa amemuua waziri, naibu waziri, mkuu wa wilaya, mkoa au mfanayabiashara mkubwa na kadhalika, kwa vyovyote kurasa za juu zingepambwa na habari kuhusu kifo hicho. Pamoja na hayo, aliamua kufungua kwenye blogu maarufu mbili, ambazo huko alizikuta habari za kifo cha Kibutu, zikiwa zimeripotiwa kwa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi.
Kama kawaida ya taarifa za aina hiyo, marehemu inasemekana alitoka baa akiwa na mwanamke ambaye hakujulikana bayana na akaja kugundulika kesho yake asubuhi chumbani mwake akiwa amekufa. Taarifa hiyo Polisi ikasema kuwa bado uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo cha kifo hicho, ambacho pia kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na daktari, mtu huyo alikufa kwa kuvuta hewa yenye sumu kali.
“Wataendelea kufanya uchunguzi mpaka Yesu atarudi na hawajapata kitu,” alinong’ona huku akizima mtandao huo na kuitupa simu sofani.
Umuhimu wa kuendelea kutazama runinga au mitandao kwenye simu, sasa hakuwapo akilini mwake. Akiwa na vazi lake lilelile, kanga tupu, aliitwaa chupa ile ya bia na kwenda kumimina kinywaji kwenye karo nje, kisha akairudisha chupa ndani akisubiri kina Zinduna watakapoihitaji awape. Kisha akatwaa mswaki na kuelekea bafuni.
Dakika kadhaa baadaye, alikuwa ameshaoga na sasa aliihisi njaa. Saa yake ilimwambia kuwa ni saa moja na dakikaishirini. Hakuwa tayari kutoka, aende Pazi Social Club kwa ajili ya kunywa supu. Wala hakuwa radhi kwenda buchani japo ni mtaa wa nyuma kusikowa na watu wengi mtaani.
Kwa asubuhi hiyo, ambayo kila mtu huwa anawaza
kujishughulisha ili apate pesa, anaweza kuwa mtaani akakutana na mtu asiyestahili kukutana naye kwa kipindi hicho. Ikitokea akakutana na yeyote anayefahamiana pia na wafanyakazi wenzake ni kipi kitajiri baadaye? Je, akikutana na yeyote ambaye labda siku ile kule Mood Bar Mtaa wa Togo alikuwapo na akamwona kwa usahihi, itakuwa ni salama kwake?
Hakujua kilichoendelea huko kwenye vyombo vya dola, lakini aliamini kuwa huenda katika upelelezi wao wakaambiwa kuwa marehemu alikuwa Mood Bar. Hapa sasa watafika huko. Hawatakosa watu wawili, watatu wa kuwahoji, na, watu hao wakawapa ushirikiano wa kutosha. Hawatakosa!
Huenda mmoja kati ya hao watakaotoa ushirikiano kwa vyombo vya dola, akakutana naye hapo nje tu wakati akielekea buchani! Kitakachofuata ni nini kama siyo mtu huyo ‘kujitia kimbelembele’ na kwenda kuripoti Polisi? Ni hilo lililomfanya ajisikie kuwa makini zaidi na zaidi.
Akaamua kutoenda buchani. Ndani humo kulikuwa na mayai sita
ambayo hakukumbuka aliyanunua lini. Lakini ni zaidi ya wiki mbili zilizopita. Akawasha jiko na kuyachemsha matatu. Alikuwa pia na kopo kubwa la maziwa ya unga. Akainjika sufuria na kuchemsha maji kwa ajili ya maziwa hayo.
Nusu saa baadaye alikuwa kamili! Hana njaa tena, alijisikia kuwa tayari kwa lolote japo si kwa kupigana ngumi. Akautwaa mkoba na kutoa kila kilichokuwamo. Chupa ya PAK na kipaketi chenye tembe moja ya Olanzapin ni vitu alivyovizingatia sana, akijali uwepo wake humo mkobani.
Lakini kama kuna kitu kilichomtisha na kuhisi kuwa kinaweza kumsababishia hata yeye kifo cha haraka, ni hiyo sumu kali ya PAK. Masharti yaliyowekwa yalikuwa ni makubwa na hadhari ilipaswa kuzingatiwa, vinginevyo inaweza kukuua wewe kabla hujaitumia kwa lengo ulilolikusudia.
Mpaka asubuhi hii alikuwa amejali kuwa makini sana, na aliamini kuwa huenda akakamilisha kazi kwa umakini ikiwa jioni mambo yatakwenda kama anavyotarajia. Baada ya kukamilisha kazi hiyo, ni kwamba hatakaa na chupa hiyo hata kwa robo saa, atahakikisha anapata sehemu yoyote ya kuitupa!
Aliukung’uta mkoba huo na kuvirejesha vitu vilivyokuwamo, simu ile ndogo ya marehemu Kisengo, ikiwa miongoni.
Kujishughulisha kwa hili na lile humo ndani mwake kulimfikisha saa tano. Na bado hakujua sasa atafanya nini ili kuvuta muda hadi hiyo saa kumi na moja jioni. “Ndiyo sababu mtu unajikuta unakwenda kujichimbia sehemu na kuanza kunywa mipombe ili kupoteza mawazo,” alinong’ona na kusonya akilaani kwa muda kwenda poleple.
Hatimaye akaamua kuchukua uamuzi wa kuondoka tu humo ndani. Akili ikamtuma tena kwenda kule Tegeta kwenye baa ya mafichoni, ambako mteja hufichwa ndani, eneo la VIP na kuhudumiwa kinywaji kama vile muda unaruhusu. Lakini pia alitaka akienda huko, asirudi hapa kwake mpaka tu atakapokuwa amekamilisha kusudio lake kule Maranatha Grocery.
Aliivua kanga na kuitupa kitandani. Akaifungua kabati na kutoa gauni refu lililovutikavutika, jekundu lililoiva. Akaliweka sofani. Alitambua kuwa gauni hili lilimshika vilivyo mwilini, na alitaka alivae hilohilo. Kisha akaitwaa miwani yenye weusi wa mbali, iwezayo kuvaliwa hata kama jua linayoyoma. Kisha akafungua saraka na kutoa kofia nyeusi ya kikapelo.
Alipovaa gauni lile, kofia juu ya nywele zake zilizomwagika mgongoni, miwani ya bei ikimkaa vyema usoni, aliamini itakuwa vigumu kwa kila mtu anayemfahamu, kuweza kumtambua. Akajikubali kwa mwonekano huo. Isingekuwa rahisi kwa mtu wa kawaida mwenye macho ya kawaida, kiwango cha kawaida katika uchunguzi na upeo wa kawaida katika utambuzi, kuweza kubaini kuwa anamwona mtu yuleyule, Scolastica Temu,mwanasheria.
Alipojitazama kwenye kioo alihisi kuwa anawona mwanamke mwingine mwenye asili ya Mmarekani. Mmarekani mweusi. Akajipulizia yale manukato yake ya bei ghali, kisha akahesabu kiasi cha shilingi laki tatu na kuziweka mkobani. Akatoka.
Alidhamiria kukaa Tegeta mpaka saa kumi jioni ndipo aende Maranatha Grocery.
*****
SAA kumi jioni, wahudumu wa Maranatha Grocery walikuwa wakipanga meza na viti tayari kwa kuwakaribisha wateja. Kabla ya hapo kulikuwa na wateja lakini walikuwa wameketi tu na kuongea wakisubiri muda rasmi wa mauzo kuanza.
Meza moja iliyokuwa chini ya mwembe, ilikuwa na watu watatu; wanaume wawili na mwanamke mmoja. Meza nyingine ilikuwa na mwanamke mmoja. Meza nyingine takriban saba chini ya paa kubwa hazikuwa na watu.
Kadiri dakika zilivyosogea ndivyo wateja walivyoongezeka. Lakini bado kulikuwa na baadhi ya meza zilizokuwa tupu.
Scolastica Temu alifika hapo saa kumi na moja na dakika kumi. Akawatupia macho wateja hao wachache, kwa zamu na kwa chati, akili yake ikiwa ni kwa mtu mmoja tu; Machemba.
Hakuwapo!
***ITAENDELEA ***

Sent using Jamii Forums mobile app
 
SEHEMU YA 30



TULIPOKOMEA....
Meza moja iliyokuwa chini ya mwembe, ilikuwa na watu watatu; wanaume wawili na mwanamke mmoja. Meza nyingine ilikuwa na mwanamke mmoja. Meza nyingine takriban saba chini ya paa kubwa hazikuwa na watu.
Kadiri dakika zilivyosogea ndivyo wateja walivyoongezeka. Lakini bado kulikuwa na baadhi ya meza zilizokuwa tupu.
Scolastica Temu alifika hapo saa kumi na moja na dakika kumi. Akawatupia macho wateja hao wachache, kwa zamu na kwa chati, akili yake ikiwa ni kwa mtu mmoja tu; Machemba.
Hakuwapo!
***SASA ENDELEA***
Akaiinua simu yake kubwa aliyokuwa kaishika mkono wa kulia, akiwa na dhamira ya kuangalia ni saa ngapi. Hakujiona kuwa kawahi sana au kachelewa. Aliukumbuka ule ujumbe aliouona kwenye ile simu ndogo ya Kisengo, ukimtaka afike huko Maranatha saa kumi na moja.
Aliamini kuwa Machemba atakuwa njiani, hivyo aliamua kuchagua kiti katika meza iliyokuwa pembezoni mwa ukumbi ambako kulikuwa na paa kubwa. Akaketi na mhudumu alipomjia aliagiza chupa ndogo ya maji. Akawa akinywa taratibu huku mara akiwa anachati mitandaoni, mara macho yanakuwa makini kuangalia kila aingiaye.
Hatimaye akaamua kujikita tena kwenye blogu, kuangalia kilichoripotiwa huko. Kama kawaida yake akaifungua blogu maarufu aliyozoea kusoma habari zake. Na kama alivyotarajia, aliikuta habari iliyohusu kifo cha Kisengo.
Katika habari hiyo, mwandishi alidai kuwa marehemu aliingia katika gesti hiyo, akiwa na mwanamke aliyesemekana ni kahaba ambaye baadaye haikujulikana aliondoka vipi.
Taarifa hiyo ikaendelea kudai kuwa habari hizo zimetolewa na mfanyakazi wa gesti hiyo, ambaye jina lake limehifadhiwa. Kwamba, asubuhi ndipo ilipobainika kuwa mpangaji huyo amefariki dunia, na alikuwa peke yake.
Kwa Scolastica, habari hiyo haikuwa ya ajabu wala ya kumtisha. Ilikuwa ni habari nyepesi kuliko ilivyo. Zaidi, aliamini kuwa mwandishi huyo hakufanya utafiti wa kina wakati akiiandaa habari hiyo. Na kwa kuwa hakukuwa na majina ya wapangaji hao, wala uthibitisho wa kamanda wa polisi wa mkoa kuhusu tukio hilo, aliichukulia habari hiyo kama uzushi mtupu.
Hata hivyo, moyoni alimsifu marehemu Kisengo kwa kutochukuan hatua ya kuandikisha majina pale mapokezi. Kwa jinsi alivyojijua, kati ya udhaifu aliokuwa nao, ni pamoja na kuzua uongo wa papo kwa papo; abuni jina lisilo lake na kulitaja pale kuwa ni lake mapokezi.
Jina la Flora alilolibuni wakati alipokutana na Kisengo kule Maseru Bar, Mkwajuni, hakudhani kama angelikumbuka pale mapokezi. Angejikuta akilitamka jina lake halisi. SCOLASTICA TEMU.
Hakufungua blogu nyingine. Aliingia kwenye mtandao wa facebook na kuchati na marafiki huku macho yake yakiwa hayatulii na umakini kwa ule mkoba wake ukiwa umezingatiwa.
Ni wakati akiendelea na utaratibu wa kuinamia simu na mara kuangaza macho kwa wateja waingiiao, ndipo ghafla akamwona mwanamume mfupi, mwembamba kiasi, akitembea taratibu lakini kikakamavu akiingia eneo hilo. Alivaa fulana nyeupe na suruali ya jeans ya kibluu. Ni Machemba Tilo Lembo.
Scolastica hakupata shida kumtambua. Kama ilivyokuwa wakati alipowaona Kibutu kwa siku yake na Kisengo kwa siku yake mara baada ya kumtendea ukatili wa aina yake kule Komakoma chumbani kwa Kibutu, safari hii pia damu ilimwenda mbio, mapigo ya moyo yakiongezeka.
Lakini badala ya kujiwa na fikra za kubatilisha kilichompeleka hapo, ndiyo kwanza shauku ya kutimiza azma yake ilivyozidi kumwingia. Na zaidi, kauli za huyu Machemba, kauli zilizojaa dharau na dhihaka, zilimwongezea kumbukumbu ichukizayo.
Aliyakumbuka yake maneno ambayo Machemba alimwambia siku ile: “Kwa leo inatosha, mtoto mzuri… Vaa twen’zetu. Giza limeingia. Siku nyingine utafaidi zaidi.” Kisha tena akamwambia kwa ukali: “Vaa! Usitarajie kubembelezwa zaidi. Hatuna muda mchafu wa kuendelea kuwa na mwanamke mchafu ka’ wewe! Vaa usepe fasta!”
Yalikuwa maneno ambayo ilikuwa vigumu kufutika katika kumbukumbu zake. Ni Machemba huyohuyo ambaye alimshinikiza kuzivunjavunja laini zake mbili za simu mbele yao! Alijisikia kumchukia kuliko hata alivyokichukia kifo.
*****
MACHEMBA aliangaza macho katika meza zote zilizokuwa na wateja. Wengi wao hawakuonesha kujali uwepo wake eneo hilo, kila mmoja alikuwa akihangaika na kinywaji chake au akiongea na mwenzake. Kila mmoja alimtazama mara moja tu na kuachana naye. Yeye pia alifanya hivyohivyo, na akagundua kila mtu yuko pale kivyake. Kila mtu, lakini sio wale wanaume wawili na mwanamke mmoja ambao walikuwa wameketi katika viti vilivyoizunguka meza moja, kila mmoja akiwa na soda mbele yake.
Aliyaona macho yao yakiwa na kitu cha ziada katika mboni zao. Ile tazama yao ya kiuficho, machoni na akilini mwa Machemba haikuwa siri. Aliwashtukia na kuwahisi kuwa ni watu walio pale kikazi. Zaidi, sura ya mmoja wao ilimletea kumbukumbu ya kumwona kiasi cha miaka miwili iliyopita. Ilikuwa ni sura iliyotangaza uaskari zaidi, watu ambao alikwishavun ja nao uhusiano tangu alipokuwa Kigoma.
Kwa siku hii, kumwona mtu wa aina hiyo, na hao wenzake ambao nao wako kama yeye, sehemu aliyopanga kukutana na rafiki yake, Kisengo, kwa mipango mizito ya pesa, kwake ilikuwa ni dalili ya kuingiliwa na nuksi.
Hata hivyo, hakuwa na hisia za asilimia mia moja kuwa ujio wa mtu huyo mahali hapo unamhusu yeye. Hivyo, aliwavuka na kuendelea kuingia ndani zaidi, akiwapita wateja aliokuta wako wawili, wawili au watatu. Alihitaji kupata meza ambayo ilikwa tupu au labda kuwe na mteja mmoja tu.
Haikuwapo meza iliyokuwa tupu kwa wakati huo bali zilikuwapo tatu ambazo zilikuwa na mtu mmoja, mmoja. Mbili zilikuwa na wanaume na moja ilikuwa na mwanamke. Yeye akaamua kwenda pale alipokuwa kaketi mwanamke yule mwenye mvuto, Scolastica Temu.
Alipoifikia meza hiyo, alimsalimu kwa upole na kumuuliza, “Samahani, shangazi, naruhusiwa kukaa?”
Scolastica ambaye alikuwa ameinamia simu yake, alinyanyua uso kusudi bila ya kujali kama Machemba atamkumbuka au la. Akamjibu, “Sina uwezo wa kukukataza. Mimi ni mteja tu.”
“Nilifikiria labda uko na wenzako ambao labda wametoka kidogo,” Machemba alisema huku akivuta kiti na kuketi.
“Hapana. Niko peke yangu.”
Wepesi wa wahudumu wa grosari hiyo haukuwa wa kawaida; tayari mhudumu wa kike alikuwa kando yake. Machemba akamwagiza bia. Mhudumu alipoondoka sasa Machemba akaamua kuketi vizuri na kumtazama Scolastica sawia, akivutiwa na rihi ya manukato ghali aliyojipulizia sanjari na nywele zzake na ile kofia kichwani bilam kukosa miwani iliyomkaa vyema usoni.
Kama awali, Scolastica hakuwa na woga wala aibu. Aliamua liwalo na liwe. Akaunyayua uso na kuktanisha naye macho. Mshtuko wa mbali ukampata Machemba. Hakuhitaji kutumia zaidi ya sekunde mbili kubaini kuwa huyu mwanamke mwenye mvuto mkali ni yule ambaye yeye na wenza walimbaka kule Komakoma kiasi cha mwezi mzima uliopita.
Hata hivyo, hali ya mshtuko moyoni, kigugumizi, kooni na maluweluwe machoni vilitoweka baada ya muda mfupi na akajipa ujasiri, akijifanya kama hamkumbuki asilani. Kiuchokozi tu, akitaka kumsoma Scolastica kama anaweza kuwa na kumbukumbu kuhusu yeye, akarusha swali, “Ni mwenyeji hapa shangazi?”
“Uenyeji gani unaozungumzia?” Scolastica alijibu kwa swali.
Machemba akaachia kikohozi bandia. “Nina maana, wewe ni mwenyeji wa Kinondoni hii?”
“Hapana. Nimekuja leo tu. Naishi Tabata Kimanga.”
Ulikuwa ni uongo ambao Machemba hakuwa na uwezo wa kuupinga akilini mwake. Tangu siku ile walipombaka, hakujua kama mwanamke huyo ambaye awali Kibutu aliwaambia kuwa alikuwa akiishi eneo la Biafra, bado atakuwa akiishi huko. Huenda alihama siku zilezile.
Dakika kama kumi baadaye Machemba alikuwa ameshajiaminisha kuwa Scolastica hamkumbuki, hali iliyompa ujasiri na kuamua kurusha ndoano. Akilini mwake alijisemea utakuwa ni ubwege wa kiwango gani kama ataishia kujiongelesha kwa hoja hii na ile isiyokuwa na mashiko kama hatamtamkia maneno ya kiume?
Ni mwanamume bwege kiasi gani ambaye ataishia tu kumwangalia mwanamke huyu mzuri, ambaye wakati alipokwenda msalani tu, takribani kila jicho lilimganda kutokana na ujenzi bora wa umbo lake lililokuwa likinyumbulika kwa namna ivutiayo?
“Hachomoki,” Machemba alinong’ona wakati akimtazama Scolastica akirejea kutoka msalani, akitembea taratibu.
Kilichomtia kiburi Machemba ni pesa zilizokuwa mfukoni. Alikuwa na shilingi laki nne na dola mia tatu za Marekani. Hakukiona kikwazo cha kumfanya amkose mwanamke huyu mzuri. Na kwa siku hii alidhamiria kuitumia vizuri zaidi, akitumia ujuzi wake wote pale kitanda kitakapowalaki.
Ili aianze karata yake, aliamua kumshawishi Scolastica anywe bia. Wakati huo yeye alikuwa ameletewa bia ya pili. Scolastica hakukataa. Alitambua kuwa ikiwa wote watakunywa bia, huenda huyu Machemba akaanza kujilengesha kama ilivyokuwa kwa wenzake waliokwishatang
ulia mbele za haki.
Nusu saa baadaye walikuwa wamezoeana. Hoja iliyowaunganisha zaidi ilihusu bajeti kuu ya serikali iliyokuwa ikijadiliwa huko bungeni, Dodoma. Waliongea mengi, wakifafanuliana na wakati mwingine wakibishana. Ni kuzoeana huko kulikomfanya Machemba aamue kurusha ndoana yake bila kusita.
“Mbona mapema sana we’ kaka…sijui kaka nani vile maana tangu tumekutana hapa hakuna anayemjua mwenzie,” Scolastica alisema huku akiachia tabasamu la mbali.
Machemba akaachia cheko dogo, cheko la majidai. “Aisee, kumbe!” hatimaye alisema. Akaongeza, “Hoja ilitukamata sana. Mimi naitwa Machemba Tilo Lembo. Ni mzaliwa wa Kigoma ila nipo huku kikazi. Nafanya kazi bandarini, huu mwaka wa sita. Na ninaishi hapahapa Kinondoni. Na wewe shangazi?”
Ukimya ukapita kidogo. Scolastica akaitwa chupa yake ya bia , hii ikiwa ni chupa ya pili, akaipeleka kinywani. Mafunda mawili yakashuka kooni. Kisha akaitua na kumtazama tena Machemba. Akawaza abuni jina au ataje lake halisi. Akaamua kutopoteza muda kubuni jina. Kwani akimtamkia jina lake halisi litamsaidia nini? Atalipeleka wapi? Zaidi ataenda nalo kuzimu.
“Naitwa Scola,” alisema kwa sauti ya chini.
“Scola?”
“Yeah, Scolastica Temu.”
“Jina zuri kama ulivyo mwenyewe.”
Scolastica hakutia neno. Alikunywa tena bia.
“Ok,” Machemba aliendelea kushawishi kwa namn alivyoona inafaa. “Shangazi kwani tatizo ni nini?”
“Umeniona leo na hapahapa,” Scolastica alimjibu. Hunijua vizuri halafau unataka tukalale wote hii leo!”
“Siyo ajabu, Scola…” Machemba aliitetea hoja yake.
Walizungumza, wakipishana kidogo lakini hatimaye Scolastica alikubali. Wakaamua kuagiza bia moja, moja za mwisho na Scolastica akapendekeza waondoke na bia mbili za kunywea gesti. Hakukubali kwenda nyumbani kwa Machemba japo Machemba mwenyewe alimbembeleza sana. Hakutaka kuwa kwenye mazingira asiyoyajua vizuri.
“Siku nyingine nitakuja kwako, leo hapana.”
***ITAENDELEA ***

Sent using Jamii Forums mobile app
 
SEHEMU YA 31



TULIPOKOMEA....
Walizungumza, wakipishana kidogo lakini hatimaye Scolastica alikubali. Wakaamua kuagiza bia moja, moja za mwisho na Scolastica akapendekeza waondoke na bia mbili za kunywea gesti. Hakukubali kwenda nyumbani kwa Machemba japo Machemba mwenyewe alimbembeleza sana. Hakutaka kuwa kwenye mazingira asiyoyajua vizuri.
“Siku nyingine nitakuja kwako, leo hapana.”
***ENDELEA***
TANGU saa kumi jioni, Inspekta Materu, Sajini Geranija na Sajini Rahma walikuwa Maranatha Grocery. Haikuwa rahisi kuwabaini kwa kuwa walikuwa wamevaa mavazi ya kawaida kama raia wengine, wa kawaida waliokuwa hpo. Walikuwa wakivuta muda huku kila mmoja akishusha kooni soda baridi.
Wakati Scolastica alipoingia walimwona lakini hawakumtilia maanani. Mawazo yao yalikuwa kwa yule aliyeandika ujumbe kwenyte simu ya Kisengo kuwa wakutane hapa jioni hii.
Muda ulizidi kwenda, hali iliyomfanya Inspekta Materu aanze kukata tamaa. “Tunaweza kuwa tunapoteza muda wetu bure?” aliwauliza wenzake huku akiwatazama kwa zamu.
“Kwa nini, afande?” Geranija alimjibu kwa swali, sauti yake ikiwa ya chini.
“Tunaweza kujikuta tunamsubiri mtu ambaye hatakuja.”
“Ni mapema mno kufikiria hivyo, afande,” Geranija alisema kwa kujiamini. “Naamini lazima atakuja. Kwa maisha ya sasa hakuna mtu anayeweza kubatilisha miadi kwa sababu za kipuuzi. Labda apatwe na tatizo kubwa. Ile meseji inaonyesha ni ya dili la pesa, unadhani ataacha kutimiza miadi?”
“Bado hiyo haijalishi. Ikitokea akawa amepata taarifa ya kifo cha jamaa yake, unadhani ni lazima aje tena hapa? Aje kufanya nini?”
Sajini Rahma akachangia, “Afande tufanye hivi. Ikifika saa kumi na mbili kasorobo hajafika, basi tuondoke zetu. Tutafute njia nyingine ya kumpata.”
Walikubaliana hivyo. Na hawakukosa kumtazama kwa makini, mwanamume yeyeote aliyeingia hapo. Na mchakato huo ulikuwa mwepesi kwa kuwa hawakuwa wakiingia watu wengi kwa mkupuo. Ni mmoja, mmoja tena baada ya dakika kadhaa. Hivyo, macho sita ya askari hao hayakukosa kumtazama na kumchunguza yeyote aliyeingia.
Sura ya Machemba waliyoiona katika simu ilikuwa vichwani mwao, hivyo wasingepata shida kumtambua kama angeingia. Na ndivyo ilivyokuwa. Dakika kadhaa baada ya kutimu saa kumi na moja, macho yao yalihamia tena eneo la kuingilia ukumbini humo na wakamwona mwanamume mfupi, mwembamba kiasi, mweusi akiingia kwa mwendo wa taratibu huku akiangaza macho kwa namna ya kujiamini. Macho yao yakamfuata kwa chati hadi alipovuta kiti kwenye meza iliyokuwa na mtu mmoja, mwanamke. Akaketi.
“Ni mwenyewe,” Geranija alisema kwa sauti ya chini huku akiwatazama wenzake kwa zamu.
“Yeah,” Materu alikiri.
Rahma hakusema kitu, alibaki tua akiendelea kumtazama kwa chati vilevile na wakati mwingine kuyahamishia macho kwa watu wengine.
“Ananifahamu,” Geranija alisema. “Mwaka mmoja ambao umepita tangu tulipoonana Kigoma mara kadhaa, hauwezi kumfanya akanisahau. Na hii ajra yetu, kwa watu kama yeye ambao wanatuchukia, haiwezi ikatokea mtu akakusahau kirahisirahisi. Ulimwona alivyokuwa aking’aa macho huku na kule wakati akiingia?”
“Nimemwona,” Materu alijibu. “Na unadhani kukukumbuka kunaweza kutuharibia na akatutoroka kijanja?”
“Sidhani,” Geranija alikataa. “Na hawezi kututoroka. Kwa vyovyote hana wasiwasi wala hajui kuwa tuko hapa kwa ajili yake. Anajisikia huru, na anaonyesha kweli ni mtu wa wanawake. Sijui yule mwanamke aliyekaa naye walikuwa na miadi? Au kajipachika tu?”
“Ni kama kajipachika tu,” Materu alisema. “Huoni alivyokuwa kama anaulizia uhalali wake kukaa pale?”
“Kajipachika kweli kama unavyosema. Na si unakumbuka mipicha ya kwenye ile simu ya Kisengo. Hawa walikuwa ni marafiki na wapenda wanawake. Yaani picha nyingi ni za mikao ya kihasarahasara tu. Wanajichukulia machangu.”
“Kwa hiyo inaonyesha hata huyo mwanamke mwenyewe huenda ni malaya tu; anawinda wanaume hapa. Jamaa kajiliengesha,” Sajini Rahma alisema.
“Nd’o maana’ake,” Materu alikubaliana na Rahma. “Sema tu, tuwaache wajidai kwa muda. Ila wakiondoka , tunamgeuzia kibao huyo jamaa.”
Muda ulizidi kwenda. Soda zilipokatika, hawakuagiza tena, badala yake waliagiza bia. Saa moja ikawakuta hapo.
Moja u nusu!
Mbili kasoro!
“Hatuna muda zaidi wa kukaa hapa,” hatimaye Materu alisema.
“Afande,” Sajini Rahma alisema, “ni vyema tungeendelea kuvuta subira.”
“Subira ya nini zaidi,” Materu alionesha kukerwa na kauli ile. “Kilichotuleta hapa ni kutaka kumpata mtu wetu. Na kishajileta. Ya nini kuendelea kukaa hapa. Kwani na sisi tumekuja kulewa hapa?”
“Naelewa hivyo afande,” Rahma alisema, akionekana kutojali ukali wa mkuu wake.
“Sasa nini tena?”
“Nina shida na yule dada aliye naye?”
Inspekta Materu na Sajini Geranija walimtazama kwa mshangao. Kisha Geranija akamuuliza, “ Unamaanisha yule uliyesema kuwa ni malaya tu?”
“Ndiyo. Kwani mnamwonaje? Hebu mtazameni vizuri. Mnadhani atakuwa ni kati ya malaya wanaozungukia kwenye mabaa wakiwinda wateja?”
Sekunde kadhaa zikakatika, Materu na Geranija wakimtazama huyo mwanamke. Kisha Materu akamrudia Rahma. “Enhe, kwani ana nini huyo mwanamke? Anatuhusu nini katika ujio wetu hapa?”
Ni mzuri sana. Nimempenda. Ana sura nzuri na umbo zuri vilevile. Mliliona umbo lake wakati anaingia? Yuko kama Mtutsi kabisa yaani.”
“Kwa hiyo?” Geranija alimbana. “Mbona haueleweki? Unaeleaelea tu.”
“Nataka awe shoga’angu.”
“Hilo tu?” Geranija alimuulzia.
“Ni hilo tu,” Rahma alisema huku akiachia tabasamu la mbali. Alikuwa na maana yake. Sura ya picha aliyorushiwa kwenye mtandao wa WhatsApp wakati alipotoka Wizara ya Sheria, haikutofautiana na sana na huyu mwanamke aliyekuwa akimzungumzia. Lakini hakutaka kulizibua hilo mapema kwa hawa askari wenzake.
“Unaleta masihara wewe,” Materu alisema.
“Unaweza kuchukulia masihara, afande,” Rahma alisema huku sasa akilikata tabasamu lake na kuwatazama kwa macho ya kikazi zaidi. “Sina masihara mjue. Cha muhimu hapo ni kuwaacha tu waongee. Najua jamaa atakuwa anamsomesha huyo demu. Tuwaache. Hawalala hapa. Wataondoka.
“Kikazi tunamhitaji mwanamume, binafsi namhitaji mwanamke. Kama wataelewana, basi ni kwamba watakapoondoka watakwenda ama nyumbani kwa mmoja wao au watakwenda gesti. Ni huko tutakapowasiliana na yule mwanamume na mimi nitawasiliana na mwanamke. Au mnaonaje?”
Ukimya wa muda mfupi ulitawala, maneno hayo yakizunguka vichwani mwa Materu na Geranija. Hawakuelewa mwenzao kwa nini alikuwa anaingiza suala ambalo linaingilia jukumu lililowaleta hapo. Hata hivyo hawakujali. Wakaamua kumpuuza, wakimwachia huru kwa pendekezo lake huku kila mmoja akijisemea kimoyomoyo vilevile, ‘mambo ya wanawake utayaweza?’
Materu akaagiza bia nyingine, akiwaagizia na wenzake.
*****
MATEMENDE Lodge haikuwa mbali kutoka Maranatha Grocery. Machemba na Scolastica walitoka Maranatha saa tatu kasoro dakika chache usiku na kutembea taratibu wakielekea kwenye gesti hiyo. Wakatumia uchochoro ambao kulikuwa na kijigiza cha wastani, kijigiza kilichomfanya Machemba akose uvumilivu. Mkono wa kushoto ukaanza kumkosea adabu, ukatua mgongoni kwa Scolastica na kushuka taratibu hadi nyongani ulipotulia kwa muda.
Scolastica alishtuka na kusimama, akamgeukia Machemba na kumwachia huru pale alipomvuta zaidi na kumkumbatia, akiongeza utomasaji huku akihema kwa nguvu. Ambacho Machemba hakuruhusiwa ni kupenyeza ulimi kinywani.
Dakika moja aliyoachiwa autalii mwili wa Scolastica, ilitosha kudhihirisha kuwa anahitaji haraka zaidi. Hilo hata Scolastica alilibaini pale mkono wake mmoja ulipogota alipopakusudia na kufanya kile alichokikusudia. “Vumilia,” hatimaye alimwambia.
“Tuna muda wa kutosha. Hapa ni njiani. Usiwe na pupa.”
Machemba alimwelewa. Wakaendelea na safari yao fupi. Mara tu walipoingia gesti na Machemba kuzungumza kidogo na mhudumu bila hata ya kujiandikisha kwenye kitabu cha wageni, wakaonyeshwa chumba cha kujipumzisha.
Wakaingia.
***ITAENDELEA***

Sent using Jamii Forums mobile app
 
SEHEMU YA 32





TULIPOKOMEA....
Dakika moja aliyoachiwa autalii mwili wa Scolastica, ilitosha kudhihirisha kuwa anahitaji haraka zaidi. Hilo hata Scolastica alilibaini pale mkono wake mmoja ulipogota alipopakusudia na kufanya kile alichokikusudia. “Vumilia,” hatimaye alimwambia. “Tuna muda wa kutosha. Hapa ni njiani. Usiwe na pupa.”
Machemba alimwelewa. Wakaendelea na safari yao fupi. Mara tu walipoingia gesti na Machemba kuzungumza kidogo na mhudumu bila hata ya kujiandikisha kwenye kitabu cha wageni, wakaonyeshwa chumba cha kujipumzisha.
Wakaingia.
*****SASA ENDELEA*****
*****
“KWA akili yao nahisi hawatakwenda mbali,” Geranija alisema huku akinywa bia yake. “Watakwenda pale Matemende Lodge.”
“Una hakika?” Inspekta Materu alimuuliza huku akimtazama kikazi zaidi. “Wafuatilie. Kwa uchochoro huo waliopita hawawezi kukushtukia. Hata hivyo, hawana wazo lolote la kufuatwa na mtu. Ukiona wameingia hapo. Basi tuwape dakika tano au kumi. Kama watapitiliza basi itabidi sasa tupindue meza. Tumfuate mtu wetu na kumweka sawa.”
Kwa mara nyingine Geranija alikunywa funda kubwa la bia. Kisha akasimama na kuacha kiwango kidogo cha kinywaji chupani. Akatoka akiifuata njia waliyopita Kisengo na Scolastica. Aliwaacha hatua kama mia moja hivi mbele yake.
Waliposimama naye akasimama na kujitia kuidonoadonoa simu yake kama akisaka mawasiliano fulani. Walipoendelea kutembea naye akawafuata, lakini akiwaacha kwa umbali uleule.
Hatimaye akawaona wakielekea Matemende Lodge.
Akawashuhudia wakiingia. Kuamini kuwa watapewa huduma hapo halikuwa jambo ambalo alilipa asilimia mia moja. Hakutaka kurudi kwa wenzake papohapo kumbe huenda huko ndani wateja hao wakaambiwa hakuna nafasi. Hivyo, alibana kwenye kiambaza cha jengo moja lililokuwa jirani, ambalo ujenzi wake ulikuwa haujakamilika.
Dakika tano baadaye akajenga imani kuwa wahusika wake wamepewa chumba. Akarudi Maranatha.
“Vipi?” Materu alimuuliza mara tu alipomwona mbele yao.
“Walishapewa chumba. Dakika tano nilizosubiri, zinatosha kuamini hivyo. Ukiingia gesti, ni mawili; uambiwe nafasi ipo ulipe na kuingia chumbani au unaambiwa hakuna chumba na hapo hutakuwa na la kukukalisha pale. Kwani watu mmekwenda kupiga stori?”
“Mzoefu wa gesti,” Rahma alimchomekea.
Wote wakacheka.
“Kwa hiyo?” Materu aliwauliza huku akiwatazama kwa zamu. Kisha akaimalizia bia yake kwa kuvuta funda mbili za mkupuo.
“Hatuna cha kutukalisha hapa,” Rahma alisema. “Tuwape dakika kama tano tena halafu tutie timu. Tutakuta nd’o kwanza wamenogewa.”
Kwa mara nyingine wote wakaangua vicheko kama vile hawakuwa hapo kwa madhumuni maalum, kikazi.
“Tutawaharibia starehe yao,” Materu alisema.
“Haijalishi,” Geranija alichangia.
Dakika kumi baadaye, wakanyanyuka vitini na kuliacha eneo hilo taratibu wakiufuata uchochoro uleule walikopita Scolastica na Machemba.
*****
PUPA ya Machemba bado ilikuwa dhahiri. Mara tu chumba kilipowalaki, alimvuta Scolastica na kumkumbatia kwa nguvu, mikono yake ikiendelea kutalii kifujofujo mwilini mwa Scolastica.
“Subiri bwana,” Scolastica alisema kwa sauti ya deko huko akimsukuma taratibu na kuketi kitandani.
Kilikuwa chumba cha kawaida tu. Hakikuwa na mvuto lakini kitanda cha futi nne kwa sita kilichokuwa kikiwasubiri, kilitandikwa shuka safi nyeupe huku mito miwili, nayo mieupe ikiwa imeegemezwa upande wa ukutani.
Scolastica aliketi kitandani. Akaangaza pande zote, akitararija kuona hata stuli lakini hakukuwa na chochote kingine. Wakati Machemba alipoweka mfuko wenye bia mbili chini papohapo Scolastica akamwahi, “Tuimalizie kabisa mibia hii. Tukianza mambo mengine sitaweza kurudia kunywa. Huo nd’o utamaduni wangu.”
“S’o mbaya,” Machemba alijibu. “Lakini dah! ‘opena’ sina…”
“Nenda nazo hata dukani nje ukafungulie huko. ”
Machemba alitikisa kichwa akiafiki. Akaubeba mfuko huo na kuanza kutoka lakini mara tena Scolastica akamzuia. Akasema, “Lakini unajua si vizuri kuingia gesti na kutokatoka ovyovyo. Haileti picha nzuri au wewe unaona ni kawaida tu?”
“Ni kweli si fresh. Lakini tutafanyaje? Tufungulie nini bia zetu?”
“Meno yako yameshachoka?”
“Yako fresh kishenzi!” Machemba alisema kwa kujidai. “Umri bado unadai wewe. Hakuna tatizo lolote kwenye meno. Vipi wewe?”
Scolastica hakujibu, alitwaa chupa moja na kuifungua kwa meno. Kisha akanywa funda moja kubwa na kuitua chupa chini. Akamwangalia Machermba na kumuuliza, “Unasubiri nini? Opena? Si unasema una meno yasiyokuwa na tatizo? Mbona unashangaa?”
Machemba akaachia cheko la mbali la kibwegebwege. Kisha naye akatwaa chupa na kuifungua kwa meno. Akanywa kidogo na kuiweka chini chupa yake.
Ni hatua hiyo ambayo Scolastica aliihitaji. Akajitia kubofya bofya simu yake ile kubwa huku kakunja uso, kisha ghafla akaguna na kuangalia ukutani huku katoa macho. Kitendo hicho kikamshangaza Machemba.
“Vipi tena?”
“Aisee, kama unaweza tafadhali kanichukulie vocha,” Scolastica alimjibu huku akionekana kukosa furaha. Alimwangalia Machemba kwa namna ya kusihi. Akaongeza: “Kuna jambo muhimu nataka nimwagize msichana wangu wa kazi nyumbani. Ni munihmu sana, please. Najua tulikubaliana tusitoke-toke nje, lakini kwa mwanaume kuonekana akiingia au kutoka gesti haiwashangazi wenye mimacho ya kuwachunguza wengine. Mwanamke ndiyo noma.”
Hakusubiri kukubaliwa na Machemba. Akawa ameshatoa noti ya shilingi elfu moja na kumnyooshea mkono akimpatia. Machemba hakuichukua noti hiyo. “Hapana usijali, ngoja nikakuchukulie.”
“Nashukuru sana,” Scolastica alisema huku akimcheka kimoyomoyo. Aliwajua wanaume wanavyopenda kujikweza. Eti anapewa pesa ya kununulia vocha, na vocha hiyo siyo kwamba ataitumia yeye bali ni ya anayemtuma. Halafu eti anajitia kukataa kupokea pesa ili tu atumie pesa yake, ajisikie mwanamume aliyekamilika kwa kumnunulia mwanamke kitu.
Wakati Machemba alipoufungua mlango ili atoke, naye Scolastica papohapo akanyanyuka na kumfuata. “Hivi toilet ni wapi?” alimuuliza akiwa nyuma yake.
“Tukamuulize mtu wa mapokezi,” Machemba alijibu kama vile naye ni mgeni hapo. Hii ilikuwa ni mara ya sita kwake kuingia humo lakini hakupenda Scolastica ajue hivyo. Wakafuatana hadi mapokezi.
Mhudumu akampa maelekezo Scolastica. Hata hivyo si kwamba Scolastica alikuwa na haja ya kwenda msalani, alihitaji tu kujua umbali wa kutoka hapo hadi katika duka lolote huko nje. Badala ya kuelekea msalani alimfuata tena Machemba aliyekuwa akikanyaga ngazi za kushuka nje.
“Niletee na maji…” alisema na kusita.
Machemba akamgeukia na kumuuliza aina ya maji.
Scolastica hakujibu. Badala yake akawa akiangaza macho kwenye maeneo ya hapo nje. Akagunduya kuwa duka pekee lililo umbali mfupi ni kiasi cha mita hamsini kutoka hapo. Aliufurahia umbali huo. Hata hivyo, akajitia kushangaa na kusema, “Kha! Kwani duka lenyewe nd’o lile kule?”
“Ndiyo,” Machemba alijibu kwa upole. “Us’jali ngoja nikakuchukulie. Unakunywa bia na kunywa tena maji? Duh!”
Wakaachia vicheko vya chini kisha Scolastica akasema, “Unajua nimekunywa bia sana. Ngoja nipunguze makali.”
Machemba akaitika kwa kutikisa kichwa kisha akaondoka.
Papohapo Scolastica akarudi ndani na wala hakuwa na shida ya kwenda msalani. Alipitiliza chumbani ambako mara tu alipoingia, haraka akaufungua mkoba wake na kuitoa tembe ya Olanzapin. Harakaharaka tena akatwaa kifuniko cha bia na kuelekea dirishani.
Huko akaiweka ile tembe kwenye ukingo wa dirisha,
akaikandamiza juu ya ubao wa ukingo huo na kuanza kuisaga taratibu. Haikuzidi dakika moja akawa amekamilisha kazi. Unga wa tembe hiyo akaumimina ndani ya kifuniko na kurejea kitandani.
Taratibu na kwa umakini, akahakikisha unga wote wa tembe hiyo unamiminika ndani ya bia ya Machemba. Kisha akakirejesha kifuniko kama kilivyokuwa kimeifunika bia hiyo.
Akashusha pumzi ndefu huku akinyanyuka na kuelekea msalani. Alichukua takriban dakika mbili huko, akinawa mikono na kuvisugua vidole kwa umakini ili tu ahakikishe hakuna dosari inayoweza kumwathiri na yeye kutokana na ile tembe ya Olanzapin.
Alipohakikisha kuwa yuko timilifu, akajifuta mikono na kurudi chumbani. Sasa akajihisi mwepesi kimwili, utulivu akilini. Akaitwaa chupa ya bia na kunywa funda tatu za nguvu. Wakati alipokuwa akiirejesha sakafuni mlango ukafunguliwa.
Alikuwa ni Machemba aliyerejea huku tabasamu likimtoka, mkono wa kushoto kashika vocha na wa kulia kabeba chupa ya maji ya bkunywa.
“Hukuniambia kama ni ya baridi au moto. Mimi nimebeba ya baridi.”
“Maji ya moto kwa joto hili la Dar nani anywe?” Scolastica alisema huku akiipokea chupa na kuiweka chini. Ile vocha wala hakuhangaika nayo. Akaiweka mkobani.
“Si ulisema unataka kuwasiliana na msichana wako wa kazi nyumbani?” Machemba alimuuliza huku akimshangaa wakati alipomwona akiiweka vocha mkobani.
“Nimeghairi,” Scolastica alijibu. “Unaweza mtu kujikuta unapata ujumbe mwingine unaoweza kukuondolea stimu bure! Nisitake hata kuendelea kuwa humu.”
Machemba akaachia tabasamu fupi la majidai. Akaitwaa chupa na kukitoa kile kifuniko. Akakitupa kando na kuipeleka chupa kinywani. Akashusha funda kubwa la bia. Hakutulia, funda la pili likafuata!
***ITAENDELEA ***

Sent using Jamii Forums mobile app
 
SEHEMU YA 33



TULIPOKOMEA....
“Nimeghairi,” Scolastica alijibu. “Unaweza mtu kujikuta unapata ujumbe mwingine unaoweza kukuondolea stimu bure! Nisitake hata kuendelea kuwa humu.”
Machemba akaachia tabasamu fupi la majidai. Akaitwaa chupa na kukitoa kile kifuniko. Akakitupa kando na kuipeleka chupa kinywani. Akashusha funda kubwa la bia. Hakutulia, funda la pili likafuata!
***SASA ENDELEA***
KWA chati Scolastica alimtupia jicho huku naye akiipeleka chupa yake kinywani na kunywa funda dogo la bia. Machemba aliiweka chupa chini na kuupeleka mkono kiunoni mwa Scolastica. Akamtekenya kidogo na kujilaza chali kitandani huku miguu ikiwa chini.
Akavuta pumzi ndefu huku mkono ukitalii mgongoni kwa Scolastica. Mara akamvuta ili amlalie kifuani. Scolastica akakubali kuvutika. Akamlalia kifuani. Wakatazamana huku macho ya Scolastica yakiwa makini usoni kwaMachemba.
Mikono yao haikutulia. Walipapasana hapa na pale, Scolastica akiwa kinara zaidi, ilhali akili yake ikiwa ikifuatilia kila hatua. Hakujali pale Machemba alipolivuta gauni juu na kuanza kumpapasa mapaja na makalio.
Hata hivyo, dakika ya tatu hakuwa yule Machemba mwenye uchu mkubwa. Alikuwa ameugandisha mkono mmoja kwenye paja la kulia la Scolastica huku mwingine ukiwa umetulia mgongoni, lakini hakuwa akiendelea kumpapasa. Macho yake yalianza kulegea na kuonekana kujishangaa.
Scolastica akajing’atua taratibu kifuani pale na kuketi tena kitandani, akiendelea kumtazama. Machemba alikunja uso na kuhema kwa nguvu, ulegevu wa macho ukizidi ilhali akilazimisha kukodoa. Na hakukubaliana na hali hiyo iliyomzulia sintofahamu. Akakusanya nguvu na kunyanyuka. Akaketi kama Scolastica.
Sasa akamtazama kwa namna ya kukodoa zaidi, akikunja uso na kuukunjua. Akajilazimisha kusimama. Akaweza, lakini kitendo hicho kikawa kosa alilolijutia. Alipitiliza na kwenda kujibamiza uso ukutani jirani na mlango.
Papohapo akageuka na kutaka kurudi kitandani. Kitendo hicho nacho kikamgharimu! Alikwenda mzima sakafuni kifudifudi na kuanguka kwa kishindo! Akatoa mguno mzito huku akikoroma.
Scolastica aliachia tabasamu la mbali huku akiufungua mkoba wake . Akaitoa chupa ya PAK na kuiweka chini. Kisha akatwaa kitambaa na kujifunga eneo la mdomo na pua kwa ustadi.
Aliporidhika, akaitwaa tena ile chupa na kunyanyuka. Akamfuata Machemba pale sakafuni. Akamsukumia teke dhaifu la kumgeuza alale chali.
Machemba alikuwa ameshatepeta. Japo aliweza kumwona Scolastica kwa usahihi, huku akilazimisha kukodoa macho na kuukunja uso na kuukunjua mfululizo, hata hivyo hakuwa na uwezo wa kutamka chochote. Alionekana akijitahidi kuufumbua mdomo na kutaka kutamke neno lakini hakufanikiwa.
Alikuwa akihema kwa nguvu na hata pale Scolastica alipomjaribu kuona uwezo wa nguvu alizosaliwa nazo, akagundua kuwa hajiwezi kabisa! Akaupiga teke mkono wa kulia na kugundua kuwa hauna hata nguvu ya kujimudu kwa lolote.
Taratibu, huku akizingatia usalama wake, Scolastica aliiifungua ile chupa ya PAK na kuisogeza puani kwa Machemba. Ule uhemaji wa Machemba ulimrahisishia jukumu Scolastica. Mwanamume alihema mara mbili kwa nguvu wakati chupa ya PAK ikiwa kwenye tundu moja la pua.
Ilitosha!
Wakati akiirudisha chupa mkobani huku akiwa hajafungua kitambaa alichojifunga usoni, akasikia mlango ukigongwa. Akakumbuka kuwa alikuwa hajaweka umakini wa kuhakikisha amefunga kwa funguo. Hata pale Machemba alipoingia kutoka dukani, aliusukuma tu kwa mguu ukajifunga. Hakujishughulisha na funguo au komeo.
Mlango uligongwa mara ya pili, safari kwa nguvu zaidi. Na mara kitasa kikazungushwa, mlango ukafunguliwa!
*****
INSPEKTA Materu na wenzake walipokwishaingia eneo la mapokezi ndani ya Matemende Lodge, hawakutaka kuchelewa. Ni Materu aliyemvaa mhudumu wa mapokezi huku akimwonesha kitambulisho kwa mbali na kutamka kwa sauti thabiti, lakini ya chini,“Askari polisi!”
Mhudumu aligwaya. Akatoa macho pima asijue ni kipi kimewaleta askari hao.
“Kuna wateja wako wameingia hapa muda si mrefu,” Materu alimwambia huku kamkazia macho. “Mwanamume ni mfupi, kavaa fulana nyeupe na suruali ya jeans. Mwanamke ni mrefu, kavaa gauni jekundu lililomtaiti, kofia ya kapelo kichwani na miwani usoni. Ana hipsi. Nywele ndefu zilizomwagikia mgongoni. Wako chumba gani?”
Macho ya askari hawa ambayo yalionekana kuwa mbali sana na mzaha au kuchelewesha kutekelezewas agizo hilo, yalimfanya mhudumu huyo aharakishe kuwaonesha chumba walichoingia Machemba na Scolastica. Dakika iliyofuata walikuwa wakiutazama mlango wa chumba walichooneshwa.
Inspekta Materu akagonga mara mbili kisha akatulia. Sekunde chache baadaye akagonga tena, safari hii kwa nguvu zaidi. Akawageukia wenzake. Wakatazamana, kisha akaurudia mlango na kukishika kitasa. Akakizungusha, kikatii. Haukuwa umefungwa kwa funguo!
Akausukuma na kuingia ndani kiaskari zaidi, wenzake wakimfuata. Macho yao yalivutwa na mwili uliokuwa sakafuni ukionesha kutokuwa na uhai! Kisha wakamgeukia mwanamke mrembo aliyekuwa kasimama huku kajifunga kitambaa eneo la mdomo na pua.
“Uko chini ya ulinzi!” Materu alimwambia Scolastica huku kamkazia macho.
Sajini Geranija aliuinamia mwili wa Machemba na kuugusa kifuani na sehemu nyingine, kisha akasogeza sikio eneo la usoni, akitaka kunasa kama mtu huyo anapumua au la. Alipowageukia wenzake, alisema, “Hayuko hai, afande!”
Bastola ikiwa mkononi kwa Inspekta Materu, ikimtazama Scolastica usoni, Sajini Rahma aliutwaa ule mkoba na kuufanyia upekuzi. Chupa ya PAK ikaonekana! Kitambulisho cha kazi nacho kikakutwa humo mkobani, kikitaja moja kwa moja jina la SCOLASTICA TEMU akiwa ni mfanyakazi wa Kampuni ya Uwakili ya ED Advocates. Sintofahamu iliyowasumbua kwa muda ikawatoka.
“Scolastica Temu!” Sajini Rahma alimaka huku akimtazama Scolastica kwa macho makali. Kofi kali likamtoka na kutua shavuni mwa Scolastica kwa usahihi. Likamyumbisha kidogo. “Mwanamke mrembo kumbe muuaji mkubwa! Kha! Una matatizo gani wewe?”
“Ni vigumu kuamini,” Geranija alisema kwa sauti tulivu huku naye akimtazama Scolastica kwa makini. “Siamini. Naona kama ndoto vile!”
“Unaona kama ndoto lakini siyo ndoto, ni tukio halisi!” Inspekta Materu alisema. Kisha akamgeukia Rahma na kumwambia, “Haya mtu wako huyo. Si ulisema unataka awe shoga’ako? Ni juu yako sasa kujua utakachomfanyia. Mtangulize nje.”
Wakati Rahma akimsukuma kutoka humo chumbani, huku akiwa ameubeba mkoba wake mwenyewe, Scolastica alikuwa akiona kama hiyo ni moja ya tamthiliya isiyopendeza. Aliongoza kutoka huku akifuatwa na Rahma.
*****
BAADA YA SIKU TATU…
KARANDINGA la Polisi lilisimama nje ya lango kuu la gereza la Keko, Dar es Salaam, saa tisa alasiri. Watuhumiwa kadhaa waliotoka katika mahakama mbalimbali jijini, waliteremka na kuongozwa na askari kuelekea rumande.
Watuhumiwa hao walikuwa ishirini na mmoja wa jinsi tofauti, wake kwa waume. Walipewa maelekezo kwa sauti za kibabe kutoka kwa askari wawili, mmoja wa kiume, mwingine wa kike.
Hakuna aliyekaidi amri zilizotolewa. Walitii kama kondoo walionyeshewa mvua. Ni nani angekaidi ilhali hizo sura za askari hazikuwa hata na chembe ya urafiki? Bunduki zikiwa mikononi mwao, askari hao walikuwa makini, wakihakikisha hakuna kosa litakalofanyika na kusababisha mtuhumiwa hata mmoja atoroke.
Aghalabu, linapokuja suala la ulinzi madhubuti dhidi ya mtuhumiwa wa kesi yoyote kubwa, ni wanaume ndio huongoza. Baadhi ya tafiti zinaonesha kuwa rekodi za uhalifu wa kutisha nchini Tanzania, zinawaangukia zaidi wanaume, ambao hukumbwa na tuhuma za ujambazi wa kutumia silaha, mauaji ya kikatili, unyang’anyi na kadhalika.
Tuhuma nyingi zinazowakabili wanawake huwa ni zile zisizohitaji ulinzi mkali. Tuhuma za kujeruhi mtu kwenye ugomvi, kudhalilisha kwa maneno machafu, kutukanana, kupigana hadharani, udokozi, madai na nyinginezo ambazo masikoni mwa wengi huzichukulia kuwa ni tuhuma za kawaida.
Hata hivyo, tafiti hizo haziwezi kuwafanya wanawake waonekane kuwa ni viumbe bora, wenye vijikosa visivyostahili kuunda tuhuma. La. Kila mtu ameumbwa na moyo wake na akili yake. Ndivyo ilivyo pia katika maumbile. Kuna wafupi na warefu, wembamba na wanene. Vivyohivyo katika tabia; kuna wastaarabu na wakorofi, wapole na wakali.
Katika watuhumiwa hawa walioshuka kwenye karandinga, mtuhumiwa mmoja wa kike, hakuonekana kuwa katika mwonekano wa kustahili kuingia katika gereza lolote, iwe ndani ya nchi au hata nje ya nchi kwa tuhuma yoyote ile. Tazama yake, vaa yake, umbo lake na hata tabasamu lake, vilikuwa vikitoa taswira ya mwakilishi wa Malaika Mkuu wa Mungu aliyetumwa duniani kwa kazi maalum, akiwa katika sura na mwili wa binadamu.
“Wewe nd’o nani vile?” baada ya nusu saa askari wa kike alimjia na kumuuliza.
Hakujibiwa. Mrembo huyo aliachia tu tabasamu dogo na kuuinamisha uso.
“Pole sana, dada,” askari huyo alimwambia huku akimtazama kwa makini, akiingiwa na wivu dhidi yake. Akajiuliza, kwa nini na yeye asiwe na umbo kama la huyu mwanamke na sura kama yake? Alikiri kimoyomoyo kuwa anamtazama mwanamke mzuri kupindukia.
“Naitwa Maisara,” askari huyo alijitambulisha. “Ni tatizo gani lililokukumba hadi ukaletwa humu dada yangu?”
“Sijui,” kauli ya kwanza kutoka kwa mtuhumiwa huyo.
Maisara hakuridhishwa na jibu hilo. Akaendelea kumtazama kwa makini na kuigundua simanzi iliyojikita usoni japo alikuwa akitabasamu kwa mbali.
“Hujui?”
“Ndiyo, sijui.”
Maisara hakuridhishwa na jibu hilo la mara ya pili, jibu ambalo sasa lilitolewa kwa msisitizo fulani. Akanyanyuka na kutoka, kichwani mwake akiwa ameshajenga imani kuwa mtuhumiwa huyo anaringa. Akasonya huku akijisemea moyoni, ‘hapa ni Keko. Akileta mauzuri-zuri yake, cha moto atakiona.’
***SCOLASTICA TEMU AMESHAKAMATWA NA KUFUNGULIWA KESI YA MAUAJI.. NI KIPI KITAKACHOENDELEA?

Sent using Jamii Forums mobile app
 
SEHEMU YA 34




ILIPOKOMEA JANA...
Maisara hakuridhishwa na jibu hilo. Akaendelea kumtazama kwa makini na kuigundua simanzi iliyojikita usoni japo alikuwa akitabasamu kwa mbali.
“Hujui?”
“Ndiyo, sijui.”
Maisara hakuridhishwa na jibu hilo la mara ya pili, jibu ambalo sasa lilitolewa kwa msisitizo fulani. Akanyanyuka na kutoka, kichwani mwake akiwa ameshajenga imani kuwa mtuhumiwa huyo anaringa. Akasonya huku akijisemea moyoni, ‘hapa ni Keko. Akileta mauzuri-zuri yake, cha moto atakiona.’
***SASA ENDELEA***
Usiku ulipoingia, mtuhumiwa mwingine, mwanamke mwenye umri wa kukaribia miaka sitini, alimuuliza kwa mnong’ono, “Mwanangu, pole sana. Unatuhumiwa kwa kosa lipi mwanangu?”
Scolastica alimtazama kidogo mwanamke huyo. Sauti yake haikuwa na dalili za dhihaka, tazama yake haikuwa ya dharau. Aliuliza mithili ya mama amuulizaye mwanae wa kuzaa. Hata hivyo, yeye alikuwa mbali kimawazo. Aliwaza kama hatua ya Mwenyezi Mungu kumleta duniani katika umbo la mwanamke ni upendeleo au uonevu. Kwa upande wake, hadi dakika hizi, akiwa rumande, alijiona kama kiumbe dhaifu ambaye amezaliwa ili adhalilike.
Kiumbe wa kike, asiyestahili heshima wala utu. Kwa nini nilizaliwa mwanamke? Alijuliza kimoyomoyo, hasira zikiwa zimejikita kichwani. Kumbukumbu ikazidi kuelea kichwani mwake, kumbukumbu ya tukio la kuogofya, tukio la kumdhalilisha, lililomkuta kiasi cha mwezi mmoja uliopita! Hakupenda kulikumbuka tukio hilo lakini katu halikufutika akilini mwake!
*****
KUKIRI kosa mahakamani na hasa kosa lenyewe likiwa ni la kuua, ni jambo ambalo hutokea kwa nadra sana. Baadhi ya tafiti huonesha kuwa katika kila watuhumiwa kumi wa kesi za mauaji, ni wawili tu ambao huwa wako tayari kukiri kosa moja kwa moja mara tu wasomewapo shtaka.
Pia, katika idadi hiyohiyo ya watuhumiwa kumi, ambao aghalabu huwa ni wanaume, ni watatu au wanne tu kati yao, ambao nyuso na siha zao zitaonekana kuwa katika mwonekano wa kawaida, labda hata wakitabasamu kama vile wako kwenye sherehe fulani au jukwaani kama vile wakijinadi kwa wananchi, labda wachaguliwe katika uchaguzi fulani.
Mtuhumiwa wa kesi ya mauaji, ambaye ni mwanamke, aghalabu hutiririkwa machozi siku yake ya kwanza tu kusimama kizimbani na kusomewa shtaka, awe ametenda kweli kosa au hajatenda. Yasemekana machozi ya mwanamke yako karibu sana, hivyo, hata yule mwanamke aliyeua kwa kudhamiria na akakamatwa, hulia kwa uchungu pale atakaposimamishwa mbele ya hakimu au jaji.
Labda hulia kwa kulikumbuka kosa alilotendewa na marehemu, lililosababisha amuue. Labda hulia kwa kuwafikiria wanae, kama anao, ambao huhisi kuwa wataishi maisha magumu katika kipindi ambacho atakuwa rumande, dhamana ikiwa imefungwa. Na pia, huenda akalia kwa kuamini kuwa, pamoja na kusota kwa muda mrefu rumande, bado atahukumiwa kifungo cha maisha au akahukumiwa kifo kabisa!
Hiyo ni tathmini inayomhusu mwanamke anayekabiliwa na kesi ya mauaji. Lakini hivyo sivyo ilivyotokea siku ambayo mwanamke mrembo, Scolastica Temu alisimama kizimbani. Ni mwanamke, lakini kizimbani hakuwa kama wanawake wengine wanaopanda pale.
Huyu alikuwa ni mwanamke mwingine kabisa, asiyeonesha kuwa na hofu yoyote wala kubabaishwa na lolote. Na aliposomewa shtaka kwa mara ya kwanza, shtaka ambalo hakupaswa kukiri wala kukana, yeye aliachia tabasamu kubwa, akiwatazama kwa zamu, bila woga wala masikitiko, hakimu, mwendesha mashtaka na umati mkubwa wa watu uliofurika mahakamani hapo.
Mwanamke mwenye tuhuma ya mauaji, kutabasamu kizimbani, bila ya kuwa na hofu, lilikuwa ni tukio lililowashangaza wengi, baadhi wakiwa ni marafiki zake, wapangaji wenzake, wafanyakzi wenzake na hata majirani zake.
Ndiyo, wengi walishangaa. Ni wengi, siyo wote. Mtu mmoja aliyekuja kushuhudia kesi hiyo, hakushangaa japo alijiuliza ni kipi kilichomfurahis
ha huyo mwanamke huyo mzuri kiasi cha kujawa na tabasamu muda wote. Mtu huyo alikuwa ni ndugu wa ‘toka-nitoke’ wa marehemu Machemba. Alikuwa ni mdogo wa marehemu Machemba.
Aliitwa Ndonya. Alikuwa kasimama tuli, mikono mifukoni, utanashati ukijidhihirisha kutokana na kuvaa shati la mikono mirefu, jeupe lililomkaa vyema, tai nyeusi, fupi shingoni, suruali nyeusi, viatu vyeusi vilivyong’ara, huku kichwani akiwa na nywele fupi sana, zilizochongwa vyema na kinyozi.
Aliendelea kumwangalia tu Scolastica na kwa kiasi fulani aliamini kuwa huenda matukio aliyoyafanya ndiyo yaliyomwathiri kisaikolojia, kiasi cha kuwa nusu mwendawazimu, akitabasamu ovyo.
Kabla ya kuja huku mahakamani alikwishasikia tetesi kuwa mwanamke huyo ndiye aliyehusika kwa kuua watu watatu; na yeye kama yeye, Ndonya, alikuwa na kumbukumbu ya siku moja alipozungumza na kaka yake, kiasi cha mwezi mzima uliopita.
Alikumbuka kuwa siku moja, wakiwa katika baa moja wakipata vinywaji, pale Kinondoni, walimwona Scolastica akipita, na kaka yake akamdokeza kuwa anajisikia kumpenda sana lakini si kwa lolote la ziada, bali ni kuhitaji kupata siku ambayo watafanya ngono.
Aidha, almdokeza kuwa rafiki yake, Kibutu alikuwa akimfukuzia sana mwanamke huyo lakini amekuwa ‘akimtolea nje,’ hivyo kulikuwa na mpango wa kumbaka kwa pamoja wote watatu. Baada ya tukio hilo, kaka yake hakuficha, alimwambia kuwa tayari wamefanikiwa, akichukulia kama vile ni tukio la kawaida tu.
Aliendelea kumtazama na kuzidi kukiri kuwa ni mwanamke mzuri. Kwa mbali naye aliachia tabasamu la mbali huku akiinamisha uso na kuikunja mikono kifuani. Kesi hiyo ilitajwa kuwa itasikilizwa mahakama kuu, hivyo ikaahirishwa muda huohuo. Umati wa watu ukaanza kuondoka.
Ndonya naye alikuwa miongoni mwa walioondoka, akiwa muda mwingi uso umeinamishwa, mikono ikiwa mifukoni mwa suruali. Alikuwa amejiwa na wazo ambalo kabla hajalifanyia utekelezaji, alihitaji kuliweka bayana kwa marafiki zake wawili aliowaamini kwa asilimia mia moja.
*****
BARABARA ya Mwinjuma inayotoka eneo la Studio ikiwa imekutana na Barabara ya Kawawa, Kinondoni, inakwenda moja kwa moja mpaka Mwananyamala. Kando ya barabara hiyo, miaka kadhaa iliyopita kulikuwa kumeshamiri kumbi kadhaa za starehe na baa ambazo zilikuwa na mvuto kwa wateja wake.
Baada ya mamlaka za serikali kuzivunja kumbi kongwe za Vijana na Mango Garden, bado kulibaki baa kadhaa hususan upande wa kulia kuelekea Mwananyamala. Miongoni mwa sehemu hizo za starehe ni Uhuru Peack ambayo kuna miti mikubwa iliyounda kivuli kizito kwa muda wote.
Siku ya yatu baada ya Scolastica kusomewa shtaka mahakamani, Ndonya na marafiki zake, Kapamba na Kipini, waliingia hapo Uhuru Peack, jioni kati ya saa kumi na saa kumi na moja, kila mmoja kwa wakati wake na kwa usafiri wake.
Walikubaliana kukutana hapo jioni hiyo kwa mwaliko wa Ndonya.
Kwa wakati huo, eneo hilo lilikuwa tulivu, wateja wakiwa ni wachache sana, na labda huenda ni kutokana na kuwa siku hiyo ni katikati ya juma, ambayo watu huwa bado makazini. Zaidi ya utulivu wa hapo chini ya miti, upepo wa wastani ukiwa ni burudani halisi kwa yeyote akaaye hapo, kelele za mabasi ya dalaldala hususan yale makubwa ndiyo ilikuwa kero pekee.
Mabasi ya safari ndefu za Mbagala, Makumbusho yalipita kwa kasi na kupiga honi zake kali zilizowashtua baadhi ya watu wenye midadi, pia kuwakera wanaohitaji utulivu halisi.
Ndonya na marafiki zake walikuwa katika meza moja, vinywaji mbele yao huku meza za jirani zikiwa tupu. Wateja wengine walikuwa katika meza za mbali kidogo, na Ndonya aliipenda hali hiyo ili tu mazungumzo yao yasiweze kuyafikia masikio yasiyohusika.
Wakati bia mbili, mbili za awali zikipotelea matumboni mwao, huku karanga za kukaangwa zikitafunwa, walikuwa wakiongea hoja hii na ile, hoja za kawaida tu. Ni pale mzunguko wa tatu ulipoingia, ndipo Ndonya alipoikita hoja yake.
“Kuna suala moja, muhimu ambalo nimependa kuwashirikisha,” alisema huku akiipapasa glasi iliyojaa kinywaji chake. Akawatazama kwa zamu, uso ukiwa unaonesha umakini wa hilo analotaka kulisema. Akaongeza, “Nitahitaji mawazo yenu na ushauti wenu vilevile. Nahisi tutakuwa na mjadala kwa kuwa hamkulitarajia hili ninalotaka kuwaambia.”
*****KIKAO HICHO KINA AJENDA GANI? TUKUTANE TENA KESHO MCHANA***

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Divine... glory to yhwh Nifah BansenBurner Alisen
Papushikashi Magazine Fire miss chagga succinate coA hydrogenase SANCTUS ANACLETUS mngony
Excel Mussolin5 Jimena Inferiority Complex
gwijimimi wambura marwa Hoshea Shareef Conscious wambeke The Boss deejay Nasmile
gkileo JUMA Chief mangi flani hivi Ngongo
makaveli10 KENZY kadada wa pili Root
aretasludovick jonnie_vincy Clkey KAFA.cOm
mbewe makedonia Afande Nyati peterchoka
Leonard Robert Nchi Kavu STUNTER
Chrizo jully van persie Khalidoun Tetramelyz punje haradari Mazigazi Alybaba babu na mjukuu
platozoom jimmyfoxxgongo Nicodemas Tambo Mwikozi Ls man Heaven Sent sifongo Infantry Soldier haa mym 20acres MTS MarkHilary compos
Tembo2 Erick the future nancy1983 Bulah binsaad
Fazzaly The Wolf Firegironsa everhurt Melvine
Mgibeon kijana wa leo samsun Coolant Jagood
pacesetter apologize payton George Betram
kisengeli
Kiranga Jiwe Linaloishi Madame B jay john Guasa Amboni Dinazarde Juma chief Analyse Diva Beyonce snowhite Mmanu Expected Value
onechromosome Missy rose Innocenthezron
Immortal_MH Ficus sunola Robot la Matope

Sent using Jamii Forums mobile app
 
SEHEMU YA 35




Wakati bia mbili, mbili za awali zikipotelea matumboni mwao, huku karanga za kukaangwa zikitafunwa, walikuwa wakiongea hoja hii na ile, hoja za kawaida tu. Ni pale mzunguko wa tatu ulipoingia, ndipo Ndonya alipoikita hoja yake.
Nina suala moja, muhimu ambalo nimependa kuwashirikisha,” alisema huku akiipapasa glasi iliyojaa kinywaji chake. Akawatazama kwa zamu, uso ukiwa unaonesha umakini wa hilo analotaka kulisema. Akaongeza, “Nitahitaji mawazo yenu na ushauti wenu vilevile. Nahisi tutakuwa na mjadala kwa kuwa hamkulitarajia hili ninalotaka kuwaambia.”
***SASA ENDELEA***
Ukimya wa muda mfupi ukatawala, wakitazamana. Kisha Ndonya akaitwaa chupa ya kinywaji na kuipeleka mdomoni. Akanywa funda kubwa na kuirudisha chupa hiyo mezani. Akilini mwake alikuwa akiliwazia hilo analotaka kuwaambia hao wenzake. Aliamini kuwa hataeleweka wala kuaminika. Zaidi, watamchukulia kuwa anawaletea masihara au amechanganyikiwa kutokana na kifo cha kaka yake.
Lakini aliamua kuwa iwe, isiwe, alishapanga kuwa hilo analowashirikisha, kamwe hatalitengua. Wakimhisi kuwa anaanza kuwa chizi ni juu yao. Hajali. Akakohoa kidogo na kujiweka sawa kitini.
“”Kama mnavyojua, msh’kaji wenu sina mke, japo ajira yangu inaniingizia posho ya maana. Tuko pamoja?”
“Tuko pamoja,” Kipini alijibu kwa sauti ilhali Kapamba alitikisa tu kichwa akionesha ishara.
“Wewe Kipini una mtoto, ingawa huna demu mmoja,” Ndonya aliendelea. “Kapamba unaishi na demu, ingawa ni kwa siku moja, moja kama unavyoniambiaga. Mimi sina demu wa kudumu wala sina mtoto. Napaswa kuondokana na hali hii, nijijengee heshima. Tumeelewana hapo?”
“Hiyo ni kweli,” Kapamb aliafiki.
“Huo nd’o ukubwa, kaka,” Kipini naye alisema.
Ndonya alishusha pumzi ndefu na kuwatazama wenzake kwa zamu. Wakati huo alikuwa akipanga namna ya kuiweka hoja yake hadharani. Alitambua fika kuwa wenzake wangehitaji kumjua huyo mke mtarajiwa. Ni hapo ndipo aliamini kungezuka mjadala. Mjadala mkubwa. Wangetaka kujua ni kwa nini kamchagua huyo mke mtarajiwa. Angewatajia bayana sababu ya kumchagua huyo mke mtarajiwa. Ndiyo, angewatajia, lakini ikiwa ni sababu ya kinywani tu, si ya kutoka moyoni.
“Nimewaambia hivyo kwa sababau tayari nimeshayasumbua sana macho na nimeihangaisha akili kumsaka yule ambaye moyo utaridhia kumuoa,” alisema huku akiendelea kuwaangalia kwa zamu, akionesha umakini. Akaendelea, “Nimempata, lakini sijaongea naye chochote. Kama akinikubali, basi sitachukua siku nyingi kabla ya kuwaambia kuwa siku fulani, tarehe fulani, mwezi fulani, mwaka huu, nitakuwa na sherehe ndogo nyumbani kwangu, sherehe ya kumpata mwenza.”
Kipini na Kapamba walitazamana kidogo kisha wote wakamrudia Ndonya.
“Nadhani ni vizuri ukitutajia walao jina na wasifu wake huyo mke mtarajiwa,” Kipini alisema.
“Hilo halina shida,” Ndonyab alisema huku akiitwaa tena chupa ya bia na kuipeleka kinywani. Funda lingine kubwa likapenya kooni. Akasema, “Mtu mwenyewe mnamfahamu sana tu na huenda mkashangaa kusikia nimemchagua yeye.”
“Tunamfahamu?” Kipini alimuuliza huku akimtazama kwa makini.
“Nd’o maana’ake. Mnamfahamu vizuri.”
“Ni nani?” Kapamba alidakia.
“Ni Scola.”
“Scola?” Kipini na Kapamba kwa pamoja wakalitaja jina hilo, macho yao yakiwa yamemganda Ndonya.
“Ndiyo, ni Scolastica Temu,” macho ya Ndonya ni kama yalikuwa yakitoa nuru fulani isiyoelezeka kwa urahisi, akiwatazama wenzake kwa zamu kama anayeyasoma mawazo yao.
Kimya kifupi kikatawala huku Kipini na Kapamba wakimtumbulia macho, wasiiamini kauli yake.
Hatimaye Kipini alikivunja kimya hicho. “Tufafanulie, please. Ni Scolastica Temu gani unayemzungumzia?”
“Wewe unamfahamu yupi au unawafahamu wangapi?”
“Yule malaya,” Kipini alijibu papohapo.
“Malaya?” Ndonya alimkzia macho. “Malaya gani unayemsema wewe?”
“Yule malaya aliyewaua ndugu zetu.”
Ndonya alishusha pumzi ndefu. “Nimekuelewa,” alisema kwa utulivu, macho akiwa ameyagandisha mezani. Kisha akayainua tena na kumwangalia Kipini sawia. “Sikulaumu. Labda una haki ya kumwita hivyo na kumpa sifa hiyo ya umalaya. Lakini pia huenda hastahili kupewa sifa hiyo…”
“Ni malaya tu!” Kapamba naye alidakia. “Kamuua kaka’ako, Machemba. Kawaua na wanaume wengine wawili. Yote hiyo kwa nguvu ya umalaya wake tu!”
“Lakini…” Ndonya alisema.
“Hakuna cha lakini, Ndonya!” Kipini alimkata kauli huku akimtazama sawia, uso kaukunja. “Yule ni malaya tu! Tena malaya mbwa! Yaani kwa hilo mi’ sikuelewi kabisa!”
“Hata mimi sikuelewi msh’kaji!” Kapamba naye alidakia.
Kwa mbali tabasamu likachanua usoni pa Ndonya. “Nilitarajia hoja hii ingegota hapo,” hatimaye alisema huku bado akiachia tabasamu lake dhaifu. “Ninachopenda kuwaambia tu ni kwamba, najisikia kumpenda sana mwanamke yule.”
Ukimya mwingine ulitawala katika meza hiyo. Kisha Kapamba akamwita mhudumu aliyekuwa akitoa huduma kwenye meza nyingine. Mhudumu huyo alipofika aliagizwa pakiti ya sigara na alipoletwa, kitu cha kwanza alichofanya Kapamba ni kuchoma moja na kuiwasha. Pakiti akaiweka mezani.
Kipini naye alikuwa mshirika. Akatwaa moja na kuwasha. Ndonya alikuwa akiperuzi kwenye simu yake. Ukimya huu ulichukua muda mrefu kuliko wakati mwingine tangu wafike hapo.
Mara Kapamba akajitoa kitini. “Mniwie radhi, ngoja nipate akili kidogo,” alisema huku akisogea pembeni na kuvuta sigara kwa mikupuo ya mfululizo, akihakikisha moshi haurejei upande wenye wateja wengine akiwamo Ndonya. Kipini naye alikuwa amejitoa na kwenda upande mwingine.
Dakika kama tatu hivi walirejea mezani huku kila mmoja akimalizia kwa kuupuliza moshi angani.
“Nadhani akili yangu haiko sawa, siamini ninachokisikia toka
kwako,” hatimaye Kapamba alisema huku akiimalizia bia na kusogeza chupa pembeni.
“Ongeza,” Ndonya alimwambia.
“Hapana, labda nipate kitu kikali, kinichangamshe akili,” Kapamba alisema.
“Agiza tu,” aliambiwa.
Muda mfupi baadaye chupa ndogo ya pombe kali ilikuwa imelala mezani hapo baada ya kufunguliwa. Kapamaba alikuwa ameshapiga kiwango kikubwa kidogo cha kinywaji hicho. Akashusha pumzi kwa nguvu. Vitone vya jasho vikajitokeza kwa mbali katik paji lake. Akatwaa leso na kujifuta. Kisha kwa mara nyingine akamimina kinywaji hicho, safari kiwango kidogo tu.
Akairejesha glasi mezani bila ya kunywa tena. Akakiegemea kiti. Akamtazama Ndonya kwa macho makali. Kisha: “ Hivi uko serious, Ndonya?”
“Sina masihara, mjue,” sauti ya Ndonya ilimtoka kwa utulivu na kujiamini.
“Inakuwaje unampenda mtu aliyemuua kaka’ako,” Kapamba sasa alikuwa alikuwa na ujasiri wa kuhoji.
“Unataka kuniambia nilipaswa kumchukia?” uso wa Ndonya, uso ulionawiri kiukwasi, ulikuwa katika mtazamo wa utulivu vilevile, macho yakiendelea kuwatazama rafiki zake kwa zamu.
Kapamba alimtazama Ndonya na kumwona akiwa kawaida, akionekana kutoichukulia taarifa yake kama mzaha. “Sijakuelewa,” alisema huku akiendelea kumtazama.
“Sina sababu ya kumchukia,” Ndonya alisema. “Lakini kama ni wewe ndiye ungekuwa umefanyiwa vile alivyofanyiwa Scola, ungelichukulia poa tu?”
Si Kipini wala Kapamba aliyejibu. Zaidi, waliendelea kumtazama kwa macho yasiyoamini akisemacho.
Ndonya akaendelea, “Uamuzi aliouchukua Scola, unatokana na uchungu wa ukatili aliotendewa. Amedhalilishwa utu wake! Yeyote anayefanyiwa kitendo kile, anaweza kuchukua uamuzi wowote bila ya kujali madhara yake. Na kwa upande mwingine, msinichukulie kuwa nafurahia kuuawa kwa kaka yangu, Machemba. Hapana. Kifo chake kinaniuma sana. Machemba kanilipia karo ya masomo yangu ya uhasibu. Leo napata pesa
kutokana na mkono wake….”
“Huna uchungu wowote, Ndonya!” Kapamba alisema kwa msisitizo, japo sauti yake ilikuwa ya chini. “Nakwambia Ndonya, huna majonzi ya kufiwa na kaka’ako! Labda useme tu unalingine la kutuambia! Zungumza kitu halisi ulichotuitia hapa!”
“Sina lingine la kuwaambia,” Ndonya alijibu haraka kwa msisitizo. “Lingine litoke tena wapi wash’kaji?”
“Una maana umetuita hapa kwa mzaha huo usio na maana?” Kipini alimuuliza.
“Unaweza kuuita mzaha au vyovyote vile,” Ndonya alijibu kwa upole. Hakuonekana kubabaishwa kwa maneno ya wenzake. “Na ninajua itakuwa ni vigumu kwenu kuniamini. Lakini ukweli wangu nd’o huo. Nahitaji kuoa, na mtu pekee ambaye moyo wangu u radhi kwake s’o mwingine zaidi ya Scolastica! Ni huyo tu! Ni yeye pekee!”
Kipini na Kapamba waliguna, wakatazamana kidogo kisha wakamrudia Ndonya.
“Na mimi nakuuliza, uko serious?” Kipini naye akauliza.
“Nd’o maana’ke.”
Kwa mara nyingine Kipini aliguna. Kisha: “Lakini si unajua kuwa Scolastica ana kesi ngumu sana? Na si unajua kuwa huenda mwisho wa kesi ya ukawa mbaya?”
“Hilo pia nalijua vizuri sana.”
“Sasa kama unajua hivyo, kwa nini unatuletea hadithi za kitoto hapa msh’kaji wetu?” kwa mara nyingine Kapamba alizuka tena. “Kwa vyovyote vile mwanamke yule hatanusurika. Huo nd’o ukweli wenyewe. Ni mawili; ama ahukumiwe kifungo cha maisha au atahukumiwa kifo! Unataka kumuoa mwanamke wa kifungwa? Unataka kumuoa mtu anayesubiri hukumu ya kifo?”
Ndonya aliachia tabasamu la mbali huku akitwaa chupa ya bia na kunywa funda moja na kuirudisha mezani. Kisha: Mbona unageuka kuwa jaji mapema hivi, Kapamba? Yaani tayari umemhukumu motto wa watu! Unasahau kuwa yeye sio mhalifu bali ni mtuhumiwa wa uhalifu?”
***ITAENDELEA ***

Sent using Jamii Forums mobile app
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom