SEHEMU YA 44
ILIPOKOMEA TOLEO LILILOPITA...
Mama yake alishtuka, akashangaa, kisha akapinga. Alimpenda sana Latifah, ingawa alikuwa na watoto wengine wanne wa kiume, waliokuwa wadogo zake Latifah. Huyu Latifah alikuwa tegemeo lake kuu. Alikuwa ni mtoto aliyewajali sana. Hazikuzidi siku tatu bila ya Latifah kufika na kuwapatia pesa za matumizi zisizo haba!
***SASA ENDELEA***
Kwa jumla maisha yao yalitegemea mfumo wa maisha ya Latifah. Wadogo zake Latifah kina Mkatamaji, Kiburugwa, Muumini na Lambalamba walikwishatekwa na maisha ya mitaani. Kiburugwa na Mkatamaji walijikita katika uporaji kwenye vichochoro vyenye giza totoro. Muumini na Lambalamba, wao walikuwa wasemaji wakuu katika vijiwe vya kahawa na kubobea katika sekta ya uvutaji bangi.
Hivyo, wazazi wake Latifah walijikuta hawapokei taarifa zozote nzuri kutoka vinywani mwa watu baki kuhusu watoto wao. Wengi waliwajia kwa malalamiko. Mtu mmoja alidai kuwa Lambalamba aliwakera kwa kuvuta bangi nyuma ya nyumba yake. Mwingine alisema kuwa Lambalamba huyohuyo aliapa kutolipa deni la pesa alizodaiwa baada ya kuchukua misokoto kadhaa ya bangi.
Muuza kahawa yeye alimshutumu Muumini kwa kutolipa deni la kahawa aliyowaagizia ‘washkaji’ zake kwa siku tano mfululizo; shilingi elfu tano na mia nane. Mwingine ambaye alikuwa ni Mwenyekiti wa Mtaa, alipeleka malalamiko kwa baba yake Muumini akidai kuwa Muumini kamkashifu kuwa hana ubavu wa kuwamiliki wake zake wawili wa ndoa.
Kulikuwa na idadi kubwa ya watu iliyomlalamikia kuwa wanawe, Kiburugwa na Mkatamaji, ama wamewapora pesa vichochoroni au wamekunywa pombe ya mnazi na kuondoka bila kulipa.
Tabia hizo ziliwafanya wazazi wakate tamaa kwa kiasi fulani. Hawakuwa na matumaini tena ya kusaidiwa na vijana hao. Walimtegemea Latifah pekee, ambaye aliwaletea pesa mara kwa mara.
Wazazi hao hawakujali kuwa binti yao alipata pesa kwa mfumo upi, wao walijali kupata pesa. Siyo kwamba walikuwa gizani kuhusu mfumo wa maisha ya Latifah. La. Walijua kila kitu, lakini hawakujali. Ndiyo maana mama yake hakukubaliana na taarifa hii ya Latifah.
“Tutaishije mwanangu?” aliuliza kwa masikitiko. “Huoni jinsi umri unavyotusogeza kaburini? Wewe ndiye Mungu wetu hapa duniani. Kama utakwenda huko Keko, nani atatulisha hadi mola atakapozitwaa roho zetu?”
Yalikuwa ni maneno yaliyomchoma sana Latifah. Lakini akapiga moyo konde na kusema, "Usihofu, mama. Sitafia huko na wala sitakaa zaidi ya miezi mitatu. Hata hivyo," akasita na kufungua mkoba aliokuja nao. Akatoa mafurushi kadhaa ya noti.
Akamkabidhi mama yake huku akisema, "Hizi zitawasaidia kwa kipindi ambacho sitakuwapo. Naomba mzitumie vizuri kwa sababu kiwango fulani katika hizo nitakitumia kwa kunitoa huko gerezani. Na itabidi mzifiche vizuri mama, hao kaka zangu wasijue kabisa!"
Mama yake aliyapokea mafurushi yale huku mikono ikimtetemeka. Hakuwahi kushika kiasi kikubwa vile cha pesa! Na kwa sauti ileile ya kutetemeka, akasema, "Mwanangu mbona sikuelewi? Hizi pesa zote za nini? Na ni shi’ngapi?"
"Ni shilingi milioni ishirini,"Latifah alijibu. "Hapa nina laki yangu ya kunilinda. Usihofu mama yangu kipenzi. Na hii iwe ni siri yako zaidi mama. Nakuamini zaidi wewe kuliko hata baba. Tunza siri hii. Nitatoka tu, ila hizo pesa zitunze sana. Nadhani hata ikiwezekana baba asijue kuwa unazo.
"Ukiweza zichimbie hata ardhini huko chumbani. Nina hofu baba akijua kuwa una pesa nyingi hivyo ataendekeza kunywa pombe. Nitakupa maagizo mengine ukija kuniona huko rumande. Ila kabla ya kuzichimbia , toa kiasi cha kutosha kwa ajili ya mahitaji yenu. Msishinde njaa eti mnanitunzia pesa zangu. Sawa mama?”
“Nimekusikia, mwanangu.”
*****
“SHEM Scola vipi, huamini kuwa sasa uko huru?” Kapamba alimuuliza Scolastica huku akimgusa begani. Wakati huo teksi ilikuwa katika mwendo wa wastani, zaidi ya mita mia tano kutoka Gereza la Keko. Walikuwa wameketi siti ya nyuma na wakati Kapamba akimuuliza hivyo, alitumia sauti ya chini sana, sauti ambayo haikuyafikia masikio ya dereva.
Scolastica aliguna, akamtazama kidogo kisha akayarejesha macho chini.
“Huamini?”
Sasa macho yao yakagongana. Kapamba akauona mrundikano wa maswali ndani mboni za macho ya Scolastica. Ndani ya maswali hayo yaliyojidhihiri
sha usoni, pia kulikuwa na taswira ya wasiwasi. Scolastica alionesha dhahiri kutoamini kilichotokea wala kumwamini huyu aliye kando yake.
“Usihofu kitu, shemeji,” Kapamba aliendelea. “Najua huelewi kitendawili hiki kilivyoteguliwa. Us’jali, tutakapoteremka nitakusimulia kwa kina.”
Alichokifanya Scolastica ni kukubali kwa kutikisa kichwa tu. Safari ikaendelea huku Kapmaba akiwa ameshazua mazungumzo mengine akimhusisha dereva moja kwa moja.
Safari yao ilikomea Kinondoni, Mtaa wa Kazima, hatua chache kutoka alipoishi Ndonya. Dakika chache baadaye walikuwa sebuleni, ndani ya eneo ambalo Ndonya aliishi kwa mkataba baina yake na mwenye nyumba.
Akiwa sofani, Scolastica Temu hakuchelewa kubaini kuwa
maisha ya mwenyeji wao siyo ya kubahatisha. Picha halisi ilijionesha. Ilikuwa ni sebuleni pana, iliyosheheni samani za kisasa. Wakati akiendelea kuangalia huku na kule, mara akawaona watu wawili wakiingia. Ni Ndonya na Kipini. Hawakuwa ni watu ambao Scolastica aliwafahamu, japo alihisi kuwa sura ya Ndonya haikuwa ngeni sana machoni pake. Ni wapi alipata kumwona? Au anamfananisha na nani? Alijiuliza na akakosa jibu.
Ndonya naye alipomtia machoni Scolastica, moyo ukapiga paa! Mshtuko ambao hata hivyo alijitahidi na akafanikiwa kuuhifadhi moyoni kiasi cha kutobainika kwa yeyote mwingine.
Baada ya kusalimiana, Ndonya akamtazama Kapamba na kisha akaserma, “Kapamba unastahili pongezi kaka. Safi sana.”
Kapamba aliona fahari kuambiwa hivyo. Naye kwa sauti ya majigambo, akasema, “Ni kweli haikuwa kazi ndogo. Lakini ni’shakwambia, kitakachonishin
da hapa Dar ni kuhamisha jengo la ghorofa thelathini na kulisogeza hata umbali wa mita mbili.
Lakini ukiniambia kesho unahitaji kuingia ikulu kuzungumza na rais, n’takuomba uahirishe hadi keshokutwa. Kesho hiyo mimi n’tatengeneza kila kitu na keshokutwa utapita lango kuu la ikulu huku walinzi wa pale wakikupa ‘shikamoo mzee’ kama vile wewe ni mfalme wa nchi moja tajiri duniani uliyekuja katika ziara kwa nchi changa.”
Kipini na Ndonya walicheka, lakini Scolastica hakucheka wala hata kuachia tabasamu la mbali; aliinamisha uso.
“Samahani shem,” Kapamba alisema huku akimgusa bega Scolastica. “Tunajua kuwa bado hujaelewa ni kipi kinachoendelea hadi sasa. Lakini ondoa hofu, ondoa mashaka moyoni mwako…”
Aliizungumza dhamira ya Ndonya. Akaweka bayana kuwa Ndonya katumia zaidi ya milioni sitini katika kuhakikisha suala hilo linakamilika bila ya shida yoyote. Ndiyo, alijitahidi kuzungumza katika namna ya kumtoa wasiwasi Scolastica na kwa kiasi fulani alifanikiwa, lakini hakufanikiwa kuuondoa udadisi uliokuwa moyoni mwake.
Scolastica alikuwa na kitu akilini mwake, kitu kilichomfanya ajikute akijiuliza maswali yalikosa majibu na udadisi aliosita kuuweka bayana kwa watu hao, kwa kile alichoamaini kuwa subira ilihitajika na umakini ulipaswa kuzingatiwa.
Alichofanya sasa baada ya kuyasikiliza haya ‘mashairi’ ya Kapamba, ni kuachia tabasamu la mbali, akiunyanyua uso na kuwatazama kwa zamu bila ya kuonesha woga wala chochote cha kutia taswira tata usoni pake. Kisha akasema, “Sijui niwashukuru vipi. Sidhani kama shukurani zangu zinaweza kutosha. Ningekuwa tajiri labda ningewapa pesa au magari. Lakini bahati mbaya mimi ni mwanamke hohehahe, nisiye na mbele wala nyuma…”
“Us’jali shem,” Kapamba alimdaka. “Ndugu yetu hahitaji chochote kutoka kwako. Anakuhitaji wewe. Anahitaji upendo kutoka kwako.” Kisha akamgeukia Ndonya. “Ndugu yetu nadhani sasa tumeutua mzigo. Nadhani ni muda mwafaka wa wewe na sisi tuwasiliane kisha tuachane kwa muda. Unaonaje?”
Ndonya alimwelewa. Hakupenda kupoteza muda. Akaingia chumbani ambako alichukua dakika kama kumi kisha akatoka na fungu la pesa kwenye mfuko. Akaketi na kuliweka mezani. “Hakuna siri baina yetu,” alisema. “Mzigo ni huo hapo. Fanyeni hesabu, mgawane.”
Zilikuwa ni shilingi milioni kumi.
Dakika kama ishirini baadaye, Kapamba na Kipini walikuwa wamenyanyuka vitini wakieleka mlangoni. Lakini kabla hawajatoka, Kapamba aligeuka na kumpungia mkono Scolastica huku akisema, “Shemeji, baadaye.”
*****
‘Shemeji!’ Scolastica aliwaza kwa hasira. Yamekuja vipi haya ya kuitwa ‘shemeji?’ Huyo Ndonya, hii ndiyo mara yake ya kwanza kumtia machoni. Alishangaa. Hata hivyo hakusema chochote. Akatulia aone kipi kitakachoendelea.
Sasa walikuwa wawili tu; yeye na Ndonya. Kimya kifupi kikatawala kati yao, kimya kilichovunjwa na Ndonya aliposema, “Pole sana Scola. Pole kwa matatizo yaliyokupata.”
“Asante,” Scolastica aliitika kwa sauti dhaifu akiyaepuka macho ya Ndonya.
Kilichofuata ni Ndonya kurejea yale yaliyosemwa na Kapamba, safari hii akiongezea viungo kadhaa katika kuhakikisha Scolastica anamwamini kwa asilimia mia moja. Lakini katika maneno yake, hakudiriki kumtamkia kuwa ana nia ya kufunga naye ndoa!
Kwa Scolastica yalikuwa ni maelezo yaliyomshangaza. Ni vipi mtu ahangaike kumtoa rumande mwanamke mwenye kesi kubwa kiasi hicho, eti kwa ajili ya mapenzi? Na kwa nini afanye hivyo pasi na hakika ya kupendwa na mwanamke huyo? Yawezekana mwanamume akahangaika, akitumia kiasi kikubwa cha pesa, lakini mwanamke akaja kumkana dakika ya mwisho, tena akiwa huru, uraiani! Atamfanya nini?
****ITAENDELEA****
Sent using
Jamii Forums mobile app