Johnny Sins
JF-Expert Member
- Nov 4, 2019
- 2,536
- 3,883
SEHEMU YA 36
ILIPOKOMEA JANA
.“Sasa kama unajua hivyo, kwa nini unatuletea hadithi za kitoto hapa msh’kaji wetu?” kwa mara nyingine Kapamba alizuka tena. “Kwa vyovyote vile mwanamke yule hatanusurika. Huo nd’o ukweli wenyewe. Ni mawili; ama ahukumiwe kifungo cha maisha au atahukumiwa kifo! Unataka kumuoa mwanamke wa kifungwa? Unataka kumuoa mtu anayesubiri hukumu ya kifo?”
Ndonya aliachia tabasamu la mbali huku akitwaa chupa ya bia na kunywa funda moja na kuirudisha mezani. Kisha: Mbona unageuka kuwa jaji mapema hivi, Kapamba? Yaani tayari umemhukumu motto wa watu! Unasahau kuwa yeye sio mhalifu bali ni mtuhumiwa wa uhalifu?”
***SASA ENDELEA***
"Lakini si ameua?” Kapamba alikazia. “Alikamatwa na askari akiwa na chupa ya sumu kali ya PAK. Na hata marehemu Machemba alipopimwa ilithibitika kifo chake kilisababishwa na kuvuta hewa ya yenye sumu kali sana. Huoni mpaka hapo huyo mkeo mtarajiwa kesi imekalia vibaya? Atapona hapo?”
“Sijakataa kuwa alimuua kaka’angu,” Ndonya alijitetea. “Najua ni yeye aliyemuua. Lakini nilichotarajia kutoka kwenu siyo shutuma kwa uamuzi wangu wa kumuoa mtuhumiwa wa kesi nzito ya mauaji wakati siijui hatima ya kesi yenyewe.”
“Ok, tupe stori,” Kipini alisema.
Ndonya aliachia tabasamu huku akikimalizia kinywaji chake na kuisogeza chupa kando. Akatupa macho kwenye meza nyingine iliyokuwa imefikiwa na wateja wawili muda huo. Mhudumu alikuwa akiwasikiliza wateja hao na alipoanza kuondoka alitupa macho kwenye hii meza ya kina Ndonya na walipokutanisha macho, Ndonya akamwashiria kwa mkono aende.
“Ongeza,” Ndonya alimwambia alipowafikia.
“Moja tu?” mhudumu alimuuliza huku akiwa ameishika chupa tupu aliyokuwa Ndonya amemalizia kinywaji chake.
“Tatu kama mwanzo. Wenzangu wanamiksi.”
Mhudumu aliondoka kwa tembea ya kujitupatupa na kuyavuta macho ya Ndonya kwa muda mfupi. Kisha akawarudia wenzake. “Najua ni ka’vile ndoto ya mwendawazimu kutamka kuwa ninataka kumuoa mtuhumiwa wa kesi kubwa ya mauaji,” alisema. “Halafu hata sijaongea naye. Tena mtuhumiwa mwenyewe yuko rumande na dhamana imefungwa. Kwa kweli taswira halisi iliyopo hapo ni kwamba, hilo ni jambo lisilowezekana. Lakini nawaaambia, jambo hilo kwangu linawezekana.”
Kipini na Kapamba waliguna huku sasa kila mmoja akijimiminia kinywaji kile kikali na kunywa kwa mkupuo. Kisha Kapamba akamuuliza, “Litawezekana kivipi?”
“Kwa kumpata mtu atakayechukua nafasi ya Scolastica.”
“Mi’ sijakusoma, ujue,” Kipini alisema.
“Nina maana kuwa,” Ndonya alisisitiza, akiwatazama kwa makini, “italazimu kumpata mtu mwingine atakayechukua nafasi ya Scolastica badala ya huyu tunayemzungumzia.”
Lilikuwa ni tamko ambalo Kipini na Kapamba walilichukulia kama mzaha mwingine wa kitoto. Ukazuka ubishi, Kapamba akimtaka Ndonya aachane na wazo hilo ambalo yeye alilichukulia kuwa ni wazo la kipuuzi. Naye Kipini akadai kuwa hata kama Ndonya hakuwa na masihara katika hiyo hoja yake, hata hivyo utekelezaji wake ulikuwa ni jambo lisilowezekana.
Bado Ndonya alikuwa ngangari. Akasema, “Tatizo lenu nyie mko katika karne ya kumi na tisa. Hii ni karne ya ishirini na moja wash’kaji. Wanadamu wa sasa hawako kizani. Wanadamu wa leo akili zinachemka vilivyo. Kwa sasa hakuna jambo lisilowezekana. Si ajabu baada ya siku utasikia maghorofa yanajengwa huko kwenye sayari ya Mars. Tambueni hivyo.
“Ninaposema hilo ni jambo linalowezekana, mjue nimeshaliwazia na kulitafakari kwa kina kabla sijawashirikisha. Sijakurupuka. Mnachopaswa kujua ni kwamba kila jambo linawezekana kama tu pesa ipo. Mimi ninaamini hivyo. Mipango madhubuti na kutokuwapo kwa uhaba wa fedha ni nyenzo sahihi ya kufanikisha mpango mzito.”
Ukimya ukazuka baada ya mhudumu kuwaletea vinywaji. Alipoondoka, Ndonya akaendelea, “Nimelitoa wazo hilo nikitambua fika kuwa msipolitafakari kwa kina, lazima mtatoa pingamizi kubwa. Lakini tambueni kuwa sikuwa fala tu kuwaambia hivyo. Kama ni pesa, hilo siyo tatizo. Nimeshaweka bajeti ya kukamilisha ishu hiyo. Na mbele ya pesa kwa Tanzania ya leo, Tanzania hii ya karne ya ishirini na moja, lolote linawezekana. Hapa sasa ninachohitaji kwenu ni msaada usiowagharimu mifuko yenu. Hilo tu.”
Akatulia tena, akiwatazama kwa zamu na kubaini kuwa walitekwa na maneno yake. Macho ya Kapamba na Kipini yalikuwa katika mshangao na udadisi. Hilo likampa matumaini kuwa kila alilosema kwa wakati huo lilipenya kwa usahihi vichwani mwao.
“Kuna uwezekano wa kumpata Scolastica Temu bandia?” hatimaye aliwauliza.
Kimya kifupi kikapita, Kipini na Kapamba wakitupiana macho. Kisha Kipini akajibu, “Hilo linawezekana. Lakini ni lazima mtu huyo awe ameshayachoka maisha huru au awe ni mpenzi wa kuishi jela.”
Kapamba aliafiki kwa kutikisa kichwa. Kisha naye akachangia, “Na pia lazima kuwe na makubaliano halisi kati yake, sisi na watu wa gereza la Keko. Hapo ndipo pesa itakapotumika. Na siyo pesa ya kitoto.”
Ndonya hakuoneshwa kushangazwa na kauli ya Kapamba. Alionekana kujiamini kwa kiasi kikubwa. Akagongagonga kidole mezani huku akimtazama Kipini. “Kwa kauli yako unaweza kuifanya kazi hiyo na ukafanikisha?” hatimaye alimuuliza.
“Ipi kati ya hizo mbili?”
“Ya kumpata Scolastica bandia.”
“Inawezekana,” Kipini alijibu kwa kujiamini. “Lakini ni lazima ujipapase mifuko. Nakwenda kuonana naye na anipe hesabu yake kama tutaafikiana.”
“Najua,” Ndonya alikenua meno kidogo, akiachia tabasamu ambalo halikujiweka bayana. “Cha muhimu ni kumpata huyo atakayejitoa mhanga kuchukua nafasi ya Scolastica wangu tangu kukaa rumande hadi kusimama kizimbani. Na ni lazima atambue kuwa lolote linaweza kumkuta mwisho wa kesi hiyo. Huenda mahakama ikamwachia huru, huenda ikamhukumu miaka michache, huenda ikamhukumu kifungo cha maisha na huenda pia ikamhukumu kifo. Atapaswa kutambua hivyo. Huo ndio ukweli!”
“Tunajua hivyo,” Kipini alisema kwa utulivu. “Na ndiyo maana nasema itakupasa ujikamue mifuko kikamilifu. Ubahili weka kando.”
“Mimi sio bahili,” Ndonya alisema akikunja uso kwa mbali. “Ningekuwa bahili nisingewaita na kuwashirikisha ishu hii. Najua fika masuala ya aina hii, hufanikiwa kwa pesa kumwagwa. Kama nilivyowaambia awali, Tanzania ya leo siyo Tanzania ya karne ya kumi na tisa wala karne ya ishirini. Hii ni Tanzania yenye Watanzania wengi ambao wana mipango ya maendeleo yao binafsi. Hao hawajui kutoa huduma kwa wananchi bali kila kitu ni kwa pesa.”
Ukimya mfupi ukatawala mezani hapo. Ni wazi Kipini na Kapamba walikuwa wakimsikiliza zaidi aliyewaalika.
Ndonya akaendelea, “Nimewaita nyie rafiki zangiu wa karibu ili nipate uhakika wa kufanikisha au kutofanikisha suala hilo. Vinginevyo…”
“Ni suala dogo, Ndonya,” Kipini alimkata kauli. “Ni suala ambalo haliwezi kutuchukua hata siku mbili kulikamilisha.”
“Nakuuliza tena, nikikupa kazi hiyo utaiweza?” kwa mara nyingine Ndonya alimuuliza Kipini.
“Kwa nini inishinde? Pesa yako tu.”
“Pesa siyo tatizo,” Ndonya alitamba.
Baada kimya kingine kifupi, Ndonya alimgeukia Kapamba. “Kwa maoni yako una hakika tukiwasiliana na watu wa magereza mambo yatakwenda vizuri?”
Kapamba aliachia kicheko dhaifu, kicheko cha kujiamini. “Kama unavyojua, mimi ni mtoto wa town, kaka,” hatimaye alisema. “Siwezi kushindwa na jambo dogo kama hilo. Lakini kaa ukijua kuwa kuonana na wahusika wa gereza la Keko kwa suala hilo, siyo jambo la kulichukulia kwa uzito mdogo….”
“Hilo pia nalijua,” Ndonya alimkata kauli. “Nauchukulia uzito wa jukumu lako sawa na uzito wa jukumu la Kipini. Kwa kifupi naomba mnifanyie kazi hiyo huku mkijua haki yenu ipo.”
Akayagandisha macho kwa Kipini na kumwambia kwa sauti yenye msisitizo kiasi, “Kipini, fanya kazi ya kumpoata mtu ninayemhitaji. Mtu atakayekuwa Scolastica Temu halisi mbele ya askari polisi na hata jaji. Asiwe na dosari yoyote itakayowafanya watu wa dola wamshtukie na kushuku kuwa wana mtuhumiwa bandia.”
Akatulia kidogo na kumgeukia Kapamba. “Wewe itakubidi usubiri matokeo ya jukumu la Kipini. Sawa?”
“Poa, tu,” Kapamba alijibu.
***ITAENDELEA***
Sent using Jamii Forums mobile app