NITAKUPATA TU
SEHEMU YA 076
Alikuwa akitambaa akiuendea mfuniko tayari kwa kutoka nje. Kelele za Teddy bado zilikuwa zikipenya masikioni na hata moyoni. Chuki na hasira zikapanda kwa pamoja. Hata alipoufikia mfuniko na kuufungua, hakuna hata mmoja ambaye alimuona. Hata alipotua katikati ya watu hawa. Kila mmoja akainekana kuduwaa. Kila mmoja hakulitegemea na hata kutarajia. Masimba akauwahi mlango na kuufunga kwa ndani. Kisha akageuka na kumtizama Teddy wake pale kitandani alipofungwa mikono yake kwa nyuma. Macho yake yakapokewa na damu iliyokuwa ikivuja kutoka kwenye mwili wa huyu malaika wake. Damu iliyokuwa ikishuka kutoka kwenye kinywa cha huyu mrembo. Kinywa cha mwanamke wa maisha yake. Kinywa cha mpenzi wake. Baada ya hilo akageuza macho kwa watu hawa ambao Bunduki bado zilikuwa mikononi. Bado hawakuweza kuzitumia. Bado hawakuruhusu mikono yao kufanya hivyo. Waliganda mfano wa barafu, waliganda mfano wa masanamu. Carlos hakuwa Carlos na Hata Derick alikuwa kimya. Kimya kama hakuwa yule. Aligwaya na pia alikuwa ameelemewa na mduwaa. Hakuuona umuhimu wa bunduki zaidi ya kumuangalia Masimba. Macho yake yakakutana na macho ya Masimba yaliokuwa yakiwaka. "Carlos mfungue huyo mwanamke hapo. Kisha hayo maswali mliokuwa mnahitaji huyu ajibu, mtaniuliza mimi na nitawajibu mimi." Aliongea masimba kwa sauti ya utulivu. Bado macho yake yalikuwa kwa Kipenzi Chake. Carlos akasogea kitandani na kufanya kama kile alichotakiwa kukitenda. Akaifungua kamba mikononi kwa Teddy. Baada ya kufunguliwa kamba kikatokea ambacho hakuna aliyekitarajia. Hata masimba hakutegemea kitu kile kutokea pale tena kutendwa na Teddy. Lakini wasichokitegemea ndicho kilitendeka. Carlos alikuwa chini kichwa kikiwa kimepasuka. Risasi kutoka kwenye Semi Automatic pistol zilitosha kukipasua kichwa cha Carlos. Derick akapagawa huku wengine wakichachawa. Sasa mdomo wa Semi automatic ulikuwa ukikitizama kichwa cha Derick, kichwa ambacho hakikuimaliza hata Sekunde moja. Tayari ubongo na damu ulikuwa hewani ukisambaratika na kutapakaa ndani ya chumba kile. Harufu ya Damu na Mauti ikasikika kwenye pua za watu wake. Huyu hakuwa Teddy wa muda mfupi uliopita, huyu hakuwa Teddy wa kipindi chote. Alikuwa teddy mtamu na mwenye kuvutia katika medani hiyo. Alikuwa mtamu na mwenye kuleta hamu. Bado bastola mkononi na Bado macho yakiwatizama watu hawa waliobaki. Watu hawa walioshtushwa na kilichotokea. Hapakuwa na utani wala masihara. Hapakuwa na utani katika macho na hata uso. Macho yalikuwa yakieleza kifo. Ni wakati wakiendelea kushangaa wakauona mlango ukisukumwa. Licha ya kusukumwa haukufunguka. Haukufunguka kwa kuwa Masimba aliufunga kwa ndani. Bado hawakujali kusukumwa kwa mlang0, lakini haikuchukua hata nusu dakika. Kitasa kilikuwa kikishambuliwa kwa Risasi kisha mlango kusukumwa huku watu wengine watatu wenye silaha mikononi wakiingia. Hawakujua kilichokuwa ndani, hawakujua kile ambacho kimewapata wenzao. Wakaingia wakiamini wanaweza. Waliingia wakiamini wanauwezo wa kupambana. Lakini kitendo cha kuingia ndani ya chumba kile. Wakapokewa na Risasi kutoka kwenye Bastola iliyoshikilia na Teddy aliyekuwa Akivuja Damu. Wote wakaanguka chini wakirusha miguu huku na huko. Teddy alikuwa kama amechanganyikiwa, teddy alikuwa kama mwenda wazimu. Chumba kilitapakaa damu huku harufu ya kifo akitamalaki chumba chote. Maiti za watu nane zilikuwa chini. Watu ambao walikuwa wana Usalama waliotumwa Bahasha. Bahasha ambayo ilikuwa na vitu vingi ndani yake. "Jifute damu hiyo tuondoke upesi, hii sehemu sio salama." Aliongea Masimba huku akichukua kitambaa ili kumsaidia Teddy kuifuta damu. Wakati anakichukua kitambaa simu yake ikaita tena. Macho yake yakaenda moja kwa moja kwenye kioo cha Simu. "Chief" ndio maneno yaliyosomeka Juu ya kioo. Masimba hakuipokea kwa muda ule. Akaiacha iendelee kuita mpaka ilipokata yenyewe. Alikuwa na maana yake kutokuipokea Simu ya Chief. Alitaka kujua kama watu hawa wametumwa na Idara au la. Kutokupokea simu kungemuwezesha Chief kujua kile ambacho kimetokea. Baada ya simu kukata, haikupita Hata Dakika moja, simu ya mmoja kati ya maiti zilizotambarajika Chini ikaita. Teddy na Masimba wakaangaliana. Kabla hajasema chochote Masimba akaichukua simu kutoka Mfukoni kwa maiti yule. "General Chomboko" ndio Jina lililosomeka juu ya kioo cha simu ile. "Mmh" masimba aliguna, aliguna kwa mshangao mkubwa. Kuliona Jina la Jenerali Chomboko kwenye simu ya mkora yule kulimshangaza. Kulimshangaza kwa kuwa ni huyu huyu mzee aliyepiga simu muda mfupi na kumwambia kuhusu kuitwa kwake Ikulu. Lakini muda huu jina lake lilikuwa likionekana Juu ya simu ya watu waliotumwa kuja kuichukua Bahasha. Akanyamaza na kutulia, hakuongea zaidi ya kuushika mkono wa Teddy na kuanzA kupiga hatua wakitoka ndani ya Hotel.
*******
Simu yake ya mezani ilikuwa ikiita katika usiku huo. Ilikuwa sio kawaida kupigiwa simu usiku mwingi kama ilivyoleo. Alijiinua Taaratibu na kuunyoosha mkono wake mpaka iliposimu. Akaisogeza karibu kisha moja kwa moja akaipeleka sikioni. "Hellow General Chomboko.!! Ilikuwa ni sauti kutoka upande wa pili. Sauti ambayo ilikuwa ikitoka kwa mkurugenzi wa Usalama wa Taifa. "Kimaro mbona usiku, kuna tatizo?" Aliuliza General Chomboko bila hata kusalimia. "Chomboko Hutakiwi kuruhusu uzee uchukue uwezo wako wa kiugunduzi. Chomboko yule wa kipindi kile asingeniuliza hili bali kutaka ufumbuzi." Akajibu Mr kimaro.
"Nimezeeka kwa sasa, nimewaachia nyie ambao bado mnadai. Tuyaache hayo, mpaka kunipigia simu usiku huu nahisi kuna jambo ambalo halikajakaa sawa." Akajibu jenerali Chomboko. Chief akatulia kwa Muda. Ukimya ukachukua mahala pake. "Kuna Bahasha imepotea mikononi mwa Askofu Ibrahim Lexandre Rengima. Bahasha hiyo inasemekana ipo mikononi mwa Masimba na Mwandani wake. Inasemekana Bahasha hiyo ina mambo mengi ya Siri na ya Hatari sana kwa Nchi. Sasa Mheshimiwa Rais Ameagiza kesho Masimba aitwe Ikulu apeleke bahasha hiyo walioichukua mikononi mwa Baba Askofu Rengima. Sasa nimekupigia kukuomba ushauri katika suala hili. Nimejaribu kuongea na Teddy lakini majibu aliyonipa ndio yaliyonifanya niinue mkonga wa simu nikupigie." Akaeleza Chief kwa kirefu. Jenerali chomboko akatulia kwa muda huku akitafakari maelezo hayo kutoka kwa Mkurugenzi wa Idara ya ujasusi. Baada ya kutafakari sana, akauliza. "Teddy amekujibu nini?"....
"Teddy amesema kama tuna uwezo wa kurudisha Roho ya Mdogo wake, roho ya Dee plus na Roho ya mama mzazi wa masimba, wataisalimisha Bahasha Hiyo. Lakini kama hatuna uwezo huo, basi hawataisalimisha Bahasha hiyo." Akajibu Chief.
"Kwa nini Mheshimiwa Rais Anaitaka Hiyo Bahasha? Akauliza generali Chomboko.
"Hata mimi bado sijajua kile kinachosababisha yeye kuihitaji hiyo bahasha na ni vipi ameijua kwamba ipo kwa askafu. Na kingine kinachonishangaza ni kuonekana kwa gari yenye Nembo ya Ikulu, ikitoka sehemu zote ambazo waliuawa Viongozi wa dini ambao wote wana Uhusiano na Hiyo Bahasha. Hapa ndipo ambapo pana nishangaza na kunipa wasiwasi." Akajibu Chief. Jibu la chief likaibua ukimya mwingine kutoka kwa General Chomboko. Kichwa chake kilikuwa kikifikiria mengi katika hili linaloendelea. Hili suala kukingiwa kifua na mheshimiwa Rais ni kuonyesha uhalisia kuwa kuna kitu anakijua na hata kukifahamu. Ameijuaje bahasha iliyochukuliwa nyumbani kwa Askofu. Ni nani aliyekwenda huko na gari ambayo ilikuwa na Nembo ya ikulu? Hayo yalikuwa maswali machache kati ya mengi aliokuwa nayo. Ilishaanza kuiona hatari, alishaanza kuuona msuguano katika idara. Idara ya usalama wa nchi. Lakini haya yote ni kwa sababu gani na zipi? Baada ya kujiuliza Maswali hayo yasio na majibu, akakumbuka kuwa bado Mkurugenzi wa Idara ya Usalama Yupo Kwenye laini. "Mr Kimaro vijana wako wapo nyuma ya suala hili. Ikiwa wewe mkuu wao hujui gari ile ilikwenda kufanya nini huko, ina maana kuna vitu vinafanyika pasipo wewe kushirikishwa. Sasa swali la kujiuliza Je Hili lililoibuka kwa sasa lina baraka ya kiti cha rais?" Akamaliza jenerali kwa kuuliza swali. "Nahisi lina baraka ndio maana anaihitaji hiyo bahasha. Unachotakiwa kufanya naomba umuarifu masimba kuhusu hili na pia hakikisha hiyo bahasha haifiki mikononi kwa rais wala Haipotei. Hiyo bahasha kuwepo kwake ndio uhai wa vijana hawa. Ikipotea ama kufika mikononi kwa Rais, basi tutakuwa tumepoteza watu sahihi." Aliongea Chomboko akionyesha kukijua kitu fulani. "Sawa nimekuelewa na nimekupata. Nakupongeza mwenzangu kwa kupata mwanga katika hili." Alijibu Jenerali. "Nadhani Asubuhi nitaongea na Masimba mimi mwenye ili kumpa Tahadhali katika hili." Akajibu kisha simu zikakatwa.
*****
Alimshika Teddy mkono na kuongozana naye kutoka katika viunga vya hoteli ile. Muda wote wakati wakitembea walikuwa wakihakikisha hawaingii mikononi kwa macho ya maadui zao.kichwani kwa masimba kulipishana mambo mengi sana. Vitu ambayo vilizidi kuisumbua akili ba hata kukivuruga kichwa chake. Kwa nini anahitajika Ikulu? Kwa nini Rais anaitaka Bahasha walioichukua kwa Baba askofu? Kwanza Rais amejuaje kuhusu hili? Kwa nini General chomboko awapigie simu watu hawa, wakati jana na hata Leo alinitahadhalisha? Ina maana hii vita iliyoanza kama utani leo hii imekuwa kubwa mpaka kumgusa Rais? Ni maswali hayo yaliomfanya amgeukie teddy. Akamwangalia kwa macho yake yenye kutia moyo. Kisha kwa Sauti ya utulivu akasema. "Teddy mke wangu, wakati huu lilipofikia hili ni wakati hatari kuliko huko tulipotoka. Naanza kuhisi kitukutoka ndani ya Taasisi kubwa hapa nchini. Naanza kuhisi kuwa tumegusa maslahi ya wahisani katika biashara hii. Niwakati wetu wa kusimama katika kupambana na hili. Meja jenerali chomboko ana kitu anachokijua kuhusu hili kinachoendelea. Teddy Nakupenda na sitaki kukupoteza katika hili. Wakati huu mimi nikielekea Ikulu, nakuomba wewe uwe ndani ya gari binafsi ukielekea Tanga kupanga mikakati ukiwa na hiyo bahasha. Bahasha ambayo imeonyesha kuleta sintofahamu kwa Nchi yangu. Natambua ni kiasi gani Chief Anasumbuliwa kwa sababu yetu. Nakuomba nenda Tanga ukajifiche huko hata kama huku wataniua utajua wapi pakuanzia." Alioongea masimba kwa mara ya kwnza machozi yakichungulia machoni. Hata Teddy alikuwa akilia sana. "Hapana Dady, siwezi kukuacha katika hili, siwezi kukuacha katika mapambano haya. Ufe mbele yangu au Nife mbele Yako." Aliongea Teddy akimaanisha kile anachokisema. "Fanya nilichokwambia Teddy, bahasha tulionayo hatupaswi kuwa nayo mikononi mwetu. Ondoka hapa jijini Upesi." Baada ya kuongea hilo akisubiri Teddy ajibu simu yake ikaita. Kuitizama namba ya mpangaji akagundua ilikuwa ni Namba ya Ikulu. Akamuonyesha Teddy kisha akaipoke.. "Tuna kusubiri wewe." Ilikuwa ni sauti iliyotoka upande wa pili, kisha simu ikakatwa. Masimba akaduwaa kwa muda akimuangalia Teddy. 'Kwaheri Teddy... fanya nilichokwambia." Akaaga masimba huku akiondoka akimuacha Teddy AMEDUWAA