Riwaya: Afisa usalama

Riwaya: Afisa usalama

RIWAYA: AFISA USALAMA
MTUNZI: EMMANUEL PHIRI
NAMBA: 0758 195 890
INSTAGRAM: immaphiri

SEHEMU: 11
ILIPOISHIA

Mrembo aliyekuwa katikati ya warembo wenzake aliruka teke kali lililompeleka afande yule chini kama mzigo, polisi mwenzake akahamaki kwa jazba akataka apulize filimbi yenye kuashiria hatari lakini kabla hajatimiza lengo akapigwa buti la kifua na mrembo yule machachari, akapepesuka mpaka chini. Muda wa kama sekunde kumi polisi wote wawili walikuwa wamedhibitiwa ipasavyo. Hakuna aliyekuwa kidume mbele ya warembo wale. Wakafungwa kamba kwenye mikono na miguu yao kisha wakalazwa chini kama magunia ya mbolea. Binti mmoja akachukua silaha zao za moto kisha akawaamuru wasijigeuze wala kutoa sauti yoyote inayoweza kuwapa taarifa polisi walio ndani. Binti aliyeruka mateke dakika tano zilizopita akachungulia ndani kupitia sehemu ya kutazamia katika geti lile, akaona jinsi polisi wawili walivyo bize kuwashurutisha wafungwa wafanye kazi bila kupumzika. Akawatazama vizuri wale wafungwa ndipo akagundua hawajafanya kosa lolote bali wapo sahihi kama walivyopewa taarifa, akageuka kisha akawaambia wenzake

“Godfrey yupo…Hatuna muda wa kupoteza hapa”

ENDELEA

Wenzake wote wakatabasamu kuonesha kufurahishwa na taarifa hiyo. Hakika hawakuwa na muda wa kupoteza

“Royce kamata vizuri silaha, sisi tunaingia ndani ya jengo kutimiliza kazi iliyotuleta. Ndani ya dakika mbili mpaka nane kazi itakuwa imekwisha…Kuwa makini na hawa wa nje”

Binti aliyeonekana kuwa kiongozi wao akampa amri mwenzake aliyeshika silaha za wale polisi kisha akamgeukia mwingine, akamwambia

“Kuwa makini, kazi bado hajaisha”

Mabinti wale wakachomoa bastola zao wakazifunga kizuia sauti (silencer) tayari kwa kazi iliyo mbele yao kisha kiongozi wao akachungulia tena ndani ya geti lile, akawageukiwa wenzake akasema

“kazi ya pili inaanza”.

Akachungulia mara nyingine ndani ya geti kisha akagonga mara tatu. Polisi mmoja kati ya wale wawili waliokuwa ndani akaja haraka bila silaha yoyote mkononi akifikiri aliyegonga geti alikuwa ni polisi mwenzetu.

KOSA

Alipofungua geti alikutana na midomo miwili ya bastola huku sura nzuri za warembo waliojiremba wakarembeka zikitabasamu kwa bashasha na furaha

“Piga magoti chini na weka mikono yako kichwani”

Kiongozi wa warembo wale akaamuru, polisi hakuamini alichokiona. Mwili ukamtetemeka baada ya kusikia harufu ya kifo ipo mbele yake, akashindwa afanye nini dhidi ya mabinti wale akaishia kupiga magoti na kuweka mikono kichwani kama alivyoamuriwa. Polisi mwenzake hakujua nini kilikuwa kikiendelea kwa sababu alikuwa bize na wafungwa akiwashurutisha kufanya kazi nguvu pasipo kuwapa muda wa kupumzika, akashitushwa na kauli kali.

“Hapo hapo ulipo tulia! Ukijaribu hata kujitigisha namwaga ubongo wako”

Kauli ile ikapenya ipasavyo katika masikio ya polisi lakini akashindwa kuielewa ilikuwa ikitoka kwa nani, akageuka huku bunduki yake ikiwa mkononi lakini alichokiona akaishiwa nguvu kabisa, mdomo wa bastola ulikuwa ukitazama paji lake la uso.

“Weka bunduki yako chini na uweke mikono kichwani kama mwenzako…Hatukuja kufanya mauaji hapa lakini mkihitaji mauaji tutafanya mara moja, tutawateketeza pasipo kujiuliza mara mbili"

Kauli nyororo lakini kali ikamshurutisha polisi, pasipo kubisha wala kugoma akapiga magoti na kuweka mikono kichwani kama alivyoamuriwa na mrembo yule. Polisi wa ndani wakakusanywa pamoja na kuwekwa chini ya ulinzi. Hali ya hofu na uwoga wa kifo ikawasumbua wafungwa wote waliokuwa wakifanya kazi eneo hilo, hawakujuwa wafanye nini ili kuepukana na kinachoendelea. Wachache walilala chini lakini wengine walikuwa mara wakae mara wainuke, wote walichanganyikiwa hawakujuwa nini kitachofuata dhidi yao baada ya kushuhudia polisi wakidhibitiwa na watoto wazuri. Kiongozi wa mabinti wale akavunjwa ukimya kwa sauti kali huku bastola ikiwa imemuelekea Godfrey

“Tumekuja kukuchukua wewe, haraka kuja hapa”

Ilikuwa ni kauli ya amiri sio ombi iliyosababisha hofu kutawala moyo wa Godfrey, akashindwa kupiga hatua ili atimize alichoambiwa akahisi kifo sasa kimemfika. Jasho likamtiririka kama maji yanayomwagika bondeni, mwili ukamwishia nguvu kabisa kwa wasiwasi na hofu, akajikuta akianguka chini kama mzigo. Akapoteza fahamu. Kiongozi wa mabinti wale akawaamuru wafungwa wambebe Godfrey mpaka kwenye gari lao. Wafungwa walitekeleza amri ya mabinti wale kwa uharaka sana. Mabinti wale walipoona kazi iliyowapeleka imekamilika wakawaingiza ndani ya geti wafungwa wote pamoja na wale polisi wa nje kisha wakazitelekeza silaha za polisi nje ya geti, wakawafungia geti kwa nje kisha wakaondoka eneo lile kwa mwendo wa madaha huku wimbo maarufu wa Simi uitwao Angelina ukiwaburudisha mioyo yao pasipo hofu yoyote.

Baada ya dakika kumi hali ya hewa eneo lile ilikuwa imechafuka, polisi walitapakaa kama siafu kila kona huku silaha za moto zikiwa mikononi mwao. Raia walikuwa majumbani mwao wakifatilia tukio hilo kupitia madirishani. Waandishi wa habari wa redio, televisheni na magazeti walikuwa bize wakijaribu kutafuta habari zaidi juu ya tukio lile lakini ushirikiano wa polisi kwao ulikuwa mdogo sana. Polisi hawakuwa tayari kuzungumza zaidi juu ya taarifa hizo kwa sababu walihisi sio wakati maalumu na sahihi kuongelea tukio hilo. Walikuwa wamevurugwa na kitendo kilichofanyika katika nyumba ya mkubwa wao wa kazi, walihisi ni dharau iliyopitiliza mpaka au kikomo. Kipindi purukushani za hapa na pale zikiendelea katika eneo hilo, gari la RPC, Mr Phidelis Edward mmiliki wa nyumba hiyo likapiga breki hatua chache toka usawa wa geti la jumba hilo. Akashuka akiwa kaongozana na polisi wanne lakini kabla hajapiga hatua hata nne waandishi wa habari wakamvamia wakitaka kufanya nae mahojiano, Mkuu yule akawatazama kisha akaongea.

“Sina mengi ya kuongea lakini nimepewa taarifa na polisi wangu kuwa kuna uharifu na uvunjwaji wa amani umefanyika nyumbani kwangu”

Akacheka kidogo kwa dharau kisha akaendelea

“Sijui wamejiamini nini? Lakini siku zao za kuwa uraiani zinahesabika…Uchunguzi ukikamilika mtapewa taarifa kamili”

Baada ya maelezo hayo mafupi akaondoka taratibu kuelekea ndani ya jumba lake la kifahari, kama ilivyo kawaida waandishi wa habari waliendelea kumsumbua kwa maswali yao ya kiudadisi lakini hakufumbua mdomo wake tena. Haukupita muda marefu tangu tukio lile lilipotokea, vyombo vya habari vikatangaza tukio la kuvamiwa kwa nyumba ya RPC na kuchukuliwa kwa mfungwa mmoja, wafungwa wengine pamoja na polisi waliokuawa wakisimamia kazi na kudumisha ulinzi wakifungiwa ndani ya jengo hilo bila kushambuliwa. Masaa matatu baada ya tukio lile kupita RPC akatangaza kuwa kutokana na uchunguzi mdogo uliofanywa na jeshi la polisi kuhusu tukio hilo wamegundua kuwa waliokuja kumchukua Godfrey ni majambazi wenzake wanaofanya mauaji kila siku na kuacha ujumbe wa kikatili mwenye kuandikwa kwa damu, mwenye kusomeka

“Very sorry marehemu”.

Katika taarifa hiyo RPC akasema kulingana na taarifa kutoka kwa mashuhuda wa tukio pamoja na polisi waliovamiwa walidai majambazi walikuja na gari la kifahari kitu kinachodhibitisha ni walewale wauaji wa watu matajiri na maarufu nchini, wakasema haiwezekani achukuliwe Godfrey peke yake alafu wengine waachwe. Akaahidi polisi watafatilia mkasa huo bega kwa bega mpaka wawatie nguvuni kila waliohusika na matukio hayo. Picha ya Godfery ikabandika kila kona ya mtaa, juu ya picha hiyo maandishi yakasomeka

“WANTED”

Yakaongezewa naksi na urembo kwa kila aliyeiona. Chini ya picha maandishi mengine yakaongeza msisitizo wa ujumbe wa juu ya picha hiyo, maelezo ambayo alikua fursa kwa jamii nzima, yakasomeka

“ZAWADI NONO ITATOLEWA KWA ATAKAE FANIKISHA ZOEZI LA KUMKAMATA”

## ## ##
Giza la jioni lilifanikiwa kuufukuza mwanga ulioshinda kutwa nzima katika sura ya uso wa dunia, kila baada ya dakika moja giza likaongezeka mara dufu huku mwanga ukiishiwa nguvu polepole na kuanza kukimbia kusiko julikana. Giza lilisisitiza ile maana ya kutesa kwa zamu. Watu waliwasha mataa yao kwa lengo la kulidhibiti giza na kuendelea na shughuli zao za kila siku. Godfrey Mdemu akashtuka toka usingizini akajikuta yupo juu ya kitanda kizuri chenye taa hafifu nyekundu kila kona ya kitanda. Akili yake ikazunguka haraka kwa lengo la kujua yupo wapi na kwanini lakini jibu alilolipata likashababisha aishiwe nguvu

“Oooh! My God”

Akakumbuka mara ya mwisho yeye na wafungwa wenzake pamoja na polisi walivamiwa na majambazi katika nyumba ya RPC, Phidelis Edward, akakumbuka jinsi jambazi yule alivyomwamuru amfuate lakini baada ya tamko hilo hakuna kingine alichokumbuka. Akajipiga piga kichwani kwa lengo la kulazimisha kichwa chake kikumbuke lakini hakupata jawabu jipya zaidi ya kutengeneza maumivu kichwani kwake. Swali likamjia kichwani

“Hapa nipo wapi?...Au wale majambazi walinichukua? Kwanini lakini?"

Akajiuliza maswali mfululizo lakini akawa kama anatwanga maji kwenye kinu, akainuka taratibu na kushuka juu ya kitanda kisha akakitazama kitanda kile kilivyokua kimepambwa na vitu vya gharama kila kona, akapitisha macho yake katika chumba kile kilichokua kikichorwa kwa mwanga hafifu mwekundu uliozalishwa kwenye mataa madogo yaliyo kwenye kila nguzo ya kitanda. Hakika akadhibitisha kuwa yupo kwenye chumba ghari ambacho hajawai kukiona katika maisha yake ya kawaida, vyumba kama hivyo amezoea kuviona kwenye filamu za mataifa ya magharibi. Pembeni ya mlango wa kuingilia ndani ya chumba hicho akaona kitufe cha kuwashia taa, akasogea mpaka kilipo akawasha taa. Akastajabu kuona uzuri wa chumba kile kwa mapana. Swali la awali likajirudia ndani ya akili yake

“Nipo wapi hapa?”

Kipindi akiendelea kukikagua kwa macho chumba kile akagundua kuna kamera ndogo imetegeshwa ukutani katika kona ya upande wa kushoto wa chumba hicho, kamera ilikua kazini kama ilivyokusudiwa na waliyoiweka. Moyo wa Godfrey ukapiga

Paaah!!!

Akaamini wahusika wa chumba hicho wanamshudia kila akifanyacho. Moyo ukamwenda mbio akajihisi kama yupo uchi baada ya kuiona kamera ile ikimtazama kwa umakini wa hali ya juu, akaamua kuzima taa na kuacha ule mwanga mwekundu utawale kama ilivyokuwa awali kisha akarudi kitandani kusubiria hukumu yake. Mawazo yakaendelea kukipiga kichwa chake pasipo kukipumzisha hata dakika moja, akahisi kichwa kizito kama mtu aliyebeba gunia la unga wa sembe. Kipindi akiendelea kupambana na kichwa chake ghafla akaona mlango ukifunguliwa kisha wakaingia wasichana wanne wakiwa wamevaa kofia aina ya kepu zilizoficha sehemu kubwa ya sura zao, mmoja kati yao alikua ameshika Diary ndogo mkononi. Kwakuwa walikuwa wamevaa kofia hakuweza kuwatambua hata mmoja. Hofu ikaongezeka akajua wakati wa kifo chake sasa umefika akajiandaa kwa lolote linaloweza kujitokeza, akasali kimoyo moyo sala ya mwisho, akajikuta anakumbuka dhambi alizowahi kutenda, akamuungamia Mungu wake haraka haraka. Hakuwa na uhakika kama Mungu amesikia na kumsamehe dhambi zake lakini alikuwa na uhakika kama ameungama kwa Mungu. Taswira ya mdogo wake ikamjia kichwani mpaka akahisi kuchanganyikiwa. Kipindi akaendelea kupambana na akili yake, mabinti wote wakavua kofia zao kitu kilichosababisha Godfrey awaone vizuri sura zao nyororo.

“Mungu wangu!”

Godfrey akahamaki baada ya kuwaona wasichana wale, mmoja wao ilikuwa ni sura ngeni lakini waliobaki hazikuwa sura ngeni hata kidogo, aliwatambua vizuri. Wawili kati yao ndio waliohusika kumkamata, na mmoja wa mwisho ndio chanzo cha yeye kuwekwa gerezani. Akauliza kwa ghadhabu

“Colotlida hujalizika na hukumu niliyopewa? Why unataka kuniua kinyama!...mpaka umetuma watu waje kuniteka?”

Colotlida akatabasamu kicheko hafifu kama mtu aliyelazimishwa kucheka kisha akaongea maneno machache

“Jeshi la polisi linakutafuta kila kona ya nchi hii na endapo ukikamatwa tena sijui itakuwaje...picha yako imesambazwa kila kona ya nchi hii ikihusishwa na kundi la The Devil"

Akapumzika kidogo kisha akaendelea

“Sina ugomvi na wewe hata kidogo lakini nataka kujua kwanini ulikubali kubeba msalaba usiokuhusu?”

Godfrey akashangaa kauli ya Colotilda, akabaki kamkodolea macho asijue ajibu nini, Akajikaza kiume kisha akaongea

“I`m involved with everything that happened, that is real reality”
(Nilihusika kwenye kila kitu kilichotokea, huu ndio ukweli halisi)

Colotilda hakuongeza neno lolote, akapokea diary toka kwa binti aliye pembeni yake kisha akamtazama Godfrey, akamwambia

“Soma diary hii kisha nitarudi baadae kusikiliza msimamo wako”

Akaitupa juu ya kitanda diary ile kisha akawatazama wasichana wenzake wakapeana ishara kwa kichwa, wakageuka nyuma wakaondoka hata bila kuaga. Godfrey aliwashuhudia warembo wale wakiondoka mmoja baada mwingine, akapuuza. Akaichukua ile diary akaifungua, akakutana na kichwa cha habari kilichosomeka.

MTOTO WA KWANZA WA MZEE MDEMU

Taratibu akaanza kuisoma.

“Kama kichwa cha habari kinavyoeleza. Godfrey ni mtoto wa kwanza katika familia ya watoto wawili, mtoto aliyekuwa akipendwa sana kipindi mama yetu mzazi aliokuwa hai (kabla hajafariki) mpaka ndugu wa wazazi wetu wakawa wakisema

kwanini mtoto wa kiume anadekezwa kiasi hicho?.

Nakumbuka jibu la baba lilikua ni moja tu, aliwajibu

‘anampenda sana Godfrey kwa sababu ni mtoto wake wa kwanza katika maisha yake’.

Upendo wa baba kwa kaka haukuathiri maisha yangu hata kidogo kwa sababu nilitimiziwa mahitaji yangu kama ilivyotakiwa japokuwa mara nyingi mama ndiye aliyekuwa kipaumbele kutimiza kila nilichohitaji. Hakika tuliishi maisha bora na yenye furaha. Mama alifariki nikiwa kidato cha tatu katika shule ya sekondari ya wasichana iliyo chini ya masista wa Kikatoliki “Carmel girls” inayopatikana Ujiji jirani kabisa na ziwa Tanganyika. Kaka alikuwa kidato cha sita katika shule ya sekondari ya wavulana ‘Minaki’ inayopatikana Pwani, hapo ndipo hali tuliyokuwa hatujaizoea ilipoanza. Baba aliishi maisha ya upweke kipindi watoto wake tulipokuwa shuleni, aliishi na wasaidizi wa kazi kama watoto wake (msaidizi anayeangalia mifugo na bustani ya maua, na msaidizi wa kazi za ndani pamoja na mlinzi wa geti).

Alitamani mtu wa karibu zaidi ndipo alipoamua kuoa mwanamke mwingine ili aweze kupata faraja ya mke. Mama yetu mpya hana utofauti mkubwa wa kiumri na kaka Godfrey, nahisi anamzidi kaka miaka mitatu au minne kitu kilichopelekea wazoeane sana pindi kaka alipokuwa nyumbani. Upendo wa mama huyo ukawa maradufu kwa kaka mpaka nikaanza kusahaulika kama kuna mtoto mwingine tofauti na kaka ndani ya familia yetu, baba aliliona lile na alipomuuliza mke wake alijibiwa kuwa

Godfrey ni mtoto wa kwanza tena wa kiume anastahili kupewa mapenzi ya wazazi ili aweze kurisisha upendo huo kwa mdogo wake.

Kaka aligundua hofu ya baba juu ya ukaribu wake na mama huyo. Akaona suluhisho la jambo hilo ni kujiweka mbali na mama. Mara nyingi alipopata likizo alikataa kurudi nyumbani kwa kizingizio kuwa yupo bize anajiandaa na masomo ya muhula unaofuata. Alifanikiwa kujiunga na chuo kikuu Mzumbe kinachopatika Morogoro katika wilaya ya Mvomero, nakumbuka alinambia alichaguliwa kozi inayoitwa Shahada ya Menejimenti ya Mifumo ya Afya (Bachelor of Health Systems Management) inayopatikana kwenye chuo hicho hicho kimoja Tanzania nzima, bara na visiwani.

Kwenye maisha yake ya chuo tabia yake ilikuwa ni ileile hakupenda kurudi nyumbani kitu kilichomkasirisha sana baba, mara kwa mara baba alikuwa akimfokea sana akimlazimisha arudi nyumbani pindi apatapo likizo lakini kaka hakutimiza maagizo ya baba. Nilimbembeleza sana kwa njia ya simu ili afikirie suala la kurudi nyumbani lakini ilikuwa ni sawa na kumpigia mbuzi gitaa au kudeki bahari ya hindi kwa kanga nyepesi zinazotokea India, alikataa katakata. Nilipomuuliza kwanini anagoma kurudi, alidai kuna anapambana ili baadae nije kuishi maisha mema na yenye furaha tele. Sikuwa na mashaka na kauli ya kaka yangu kwa sababu najua upendo wake kwangu. Nakumbuka alipomaliza chuo hakurudi nyumbani alitimkia Dar es salaam kwa siri, aliniambia mimi tu kua ameenda Dar es salaam na kunitaka nisimwambie yeyote kuhusu taarifa zake. Nilipomuuliza ameenda Dar es salaam kufanya nini?, bado jibu lake lilikua ni lile lile

“Kukutafutia maisha baadae uje kuishi maisha mema na yenye furaha tele”.

ITAENDELEA
 
Mzee unaijua Mzumbe University ndani nje
Hongera BHSM itabaki kileleni tupe madini
Najivunia kuwa mwanamzumbe
 
Back
Top Bottom