Riwaya: Afisa usalama

Riwaya: Afisa usalama

RIWAYA: AFISA USALAMA
MTUNZI: EMMANUEL PHIRI
NAMBA: 0758 195 890
INSTAGRAM: immaphiri

SEHEMU: 08

ILIPOISHIA

Inspekta Emmanuel Ngogo akamuitikia polisi wake kisha akampa ruhusa ya kuondoka zake, kipindi mambo hayo yakiendelea Godfrey alikua akimuangaza mdogo wake ndani ya ofisi ile bila mafanikio. Macho yake yaliwaona watu wawili tu mle ofisini ambao ni Inspekta Emmanuel Ngogo na msichana aliyevaa wigi lililofanikiwa kuficha sehemu kubwa ya sura yake, kichwani akiwa kavaa kofia aina ya kepu iliyoongeza kipingamizi cha kumfahamu. Godfrey hakujali muonekano wa yule binti kwa sababu sio kilichompeleka ofisini pale.

ENDELEA

“Godfrey waweza kukaa hapo, usiwe na wasiwasi nipo na mgeni wako”

Afande Emmanuel Ngogo akaongea huku akimuonesha Godfrey mahala pa kukaa, Godfrey akakaa mahali alipooneshwa huku kichwa chake kikiwa kinaendelea kupambana na mawazo na maswali yaliyojitengeneza. Godfrey akamuuliza afande Emmanuel Ngogo

“Mdogo wangu yupo wapi?”

Swali la Godfrey liliibua swali kwa afande Emmanuel Ngogo, akauliza kwa mshangao

“Mdogo wako! Nani amekwambia mdogo wako yupo hapa?”

Godfrey alikosa cha kuongea, akabaki kamtumbulia macho afande Emmanuel Ngogo, afande alifahamu hali hiyo, akamwambia

“Hapana Godfrey, mgeni wako ni huyo binti pembeni yako.Sina taarifa za mdogo wako …Nitawaacha na mgeni wako muongee vizuri, nafikiri mtaelewana”

Inspekta Emmanuel Ngogo akakazia. Godfrey akarudisha macho yake na kumtazama msichana yule aliyeficha muonekano wake, kisha akauliza

“Nini kinachoendelea?”

“Hata mimi sielewi pia, nahitaji msaada wako kuelewa vizuri”

Inspekta Emmanuel Ngogo akamjibu Godfrey akiwa kamtazama moja kwa moja usoni kisha akarudisha macho kwa msichana aliyeficha muonekano wake.

“Nilitaka niwapishe muongee kwa uhuru lakini sitawapisha, nataka niwe sehemu ya mazungumzo hayo ili nipate maelezo ya moja kwa moja ili tuweze kulisaidia jeshi la polisi kikamilifu”

Binti aliyeficha muonekano wake akamtazama Inspekta Emmanuel Ngogo kisha akamuonesha ishara ya dole gumba akimaanisha kuwa ameafikiana na maneno yake. Godfrey akawatazama kwa jicho la udadisi mmoja baada ya mwingine kisha akahamaki kwa sauti iliyoteka ofisi yote

“Bora mnirudishe mahabusu nikaendelee na maisha yangu niliyoyazoea kuliko hapa mnapo niigizia movie, siwaelewi kabisa”

Binti aliyevaa kofia ya kepu pamoja na wigi lililoficha taswira yake akamtazama Godfrey kisha akamuuliza swali bila hata kutoa salamu

“Unaelewa nini kuhusu Colotlida Kamanzi? Binti aliyetekwa pamoja akiwa na Mr Hamisi Ernest, mfanyabiashara mkubwa nchini”

Sauti nzuri iliyoathiriwa na mafua ilikua kama kisu cha moto katika masikio ya Godfrey

“Colo…Aaaah! Wewe ni nani unayeniuliza maswali?”

Godfrey akauliza kwa sauti ya mshangao iliyojaa mashaka. Afande Emmanuel Ngogo alikua kimya akifatilia mazungumzo yaliyoanzishwa na msichana yule

“Sikiliza kijana, mimi najua mambo mengi kuhusu wewe na nimekuja hapa kwa ajili ya suala lako hivyo basi nahitaji ushirikiano wako”

Godfrey akamjibu binti yule, hakika hakuona umuhimu wa kuhojia

“Kama unajua mambo mengi kuhusu mimi sasa umekuja ili ujue nini zaidi?”

Godfrey hakua na mpango wa kutoa ushirikiano kwa mtu yeyote, aliamini alichokiandika kwenye makaratasi aliyompa afande Hassani Mgao yakitosha kabisa na sio vinginevyo. Msichana yule aliyeficha taswira yake akavua kofia na wigi vilivyokua vikimweka mbali na sura yake, sasa akabaki sura wazi. Mdomo wa Godfrey ukabaki wazi asiamini alichokiona, kila alipotaka kutamka neno ulimi ukawa mzito, akabaki akibabaika kama mtoto, mapigo ya moyo yakaongezeka maradufu kama maji yanayoporoka bondeni. Akajitahidi kuongea lakini wapi ulimi ukakataa

“Nahi…”

Kipindi Godfrey akipambana na ulimi wake, binti yule akamkatisha kwa kumuuliza swali lingine

“Mbona ulichelewa kuandika maelezo kuhusu tukio lililokufikisha hapa? Kuna nini kilichojificha ndani yako au ndani ya maelezo hayo?”

Akili ya Godfrey bado ilikua ikitafakari kuhusu binti huyo, swali aliloulizwa lilikua kama kelele tu katika masikio yake, alishindwa kuamini kama aliyemuona ni yeye kweli au alikua akiota ndoto za mchana kweupe. Hakika alichanganyikiwa.

“Colotilda!”

Godfrey akaita kwa mshangao

“Yes, ndio mimi wala hujakosea”

Msichana mrembo akajibu

“Leo hii nipo mahala hapa kwa sababu yako na marehemu Mr Hamisi Ernest…Uhai wako ni nuru ndogo katika maisha yangu”

“Kitendo ulichokifanya ulifikiri umefanikiwa kuwaua wote? La hasha, Mungu mkubwa ameokoa maisha ya Colotlida”

Afande Emmanuel Ngogo akaingilia kati mazungumzo yale. Colotlida akamtazama Godfrey kisha akarudisha macho kwa afande Emmanuel Ngogo, akatamka maneno yaliyomchanganya Godfrey pamoja na afande Ngogo

“Sina hakika kama Godfrey anahusika kwenye kesi hii, nahisi kuna jambo lililojificha hapa. Kesi hii itakua imezungukwa na watu wakubwa”

Inspekta Emmanuel Ngogo akaropoka kwa sauti

“Why!”

Kabla hajajibiwa swali la awali akauliza swali lingine

“Godfrey na akili zake timamu kama unavyomuona amelidhibitishia jeshi la polisi kuwa amehusika na mauaji hayo alafu wewe unasema huna uhakika, unataka uhakika gani sasa?”

Emmanuel Ngogo akameza mate kisha akaendelea

“Colotilda, umekuja hapa ukidai unataka kuonana na jambazi aliyekusudia kuondoa maisha yako, uliniomba uonane nae ndani ya ofisi yangu ili upate utulivu wa mahojiano yenu…sasa unaropoka nini?”

Macho ya afande Emmanuel Ngogo yakabadilika yakawa mekundu ndani ya muda mfupi, akahisi kuchanganyikiwa asiamini alichosikia kutoka kwa Colotilda. Upande wa Colotilda hakuogopeshwa hata kidogo na hali hiyo, hakika alikua mwanamke mkakamavu zaidi ya walivyokua wakimjua. Ndani yake kuna kitu kilikua kimejificha ipasavyo, kitu kilichomtenganisha yeye na wanawake au wasichana wengine. Akajibu malalamiko ya Inspekta wa Polisi

“Inspekta, ndio maana nimesema sina uhakika kwa sababu sioni uhusiano wa tukio langu na maisha ya Godfrey, hata kama alikua ananisumbua na upuuzi wake wa mapenzi…Labda kama alikua na chuki dhidi ya Mr Hamisi Ernest, sielewi”

Colotilda akavuta pumzi ndefu ndani kisha akaitoa taratibu, akaendelea

“Ila kwakuwa ameidhibitishia polisi kuwa yeye ndiye muhusika hapo hakuna neno la ziada. Anastahili hukumu”

Akakohoa kurekebisha sauti yake kisha akaendelea

“Alama za vidole katika kisu kilichotumika kufanyia mauaji zinaonesha wazi kuwa ni Godfrey…acha akalitumikie gereza”

Godfrey akamtazama Colotilda kisha akamwambia

“I have learned more in the streets and prison than in any classroom, acha niendelee kujifunza zaidi kwa sababu hakuna mzani wa haki unaoweza kuniondoa katika janga hili linaloniandama na kuniondolea furaha ya maisha yangu”.

Akakohoa tena kisha akaendelea

“Nilifundishwa na mwalimu wangu wa darasa la nne kuwa aliyeshikwa na ngozi ndiye aliyekula nyama. Nipo tayari kuidhibitishia mahakama kuwa niliua”

Baada ya kumaliza kuongea Godfrey akainamisha kichwa chini

“Vipi kuhusu wenzako? Maana inaonesha mna mtandao mkubwa wa mauaji”

Colotilda akauliza haraka baada ya Godfrey kukaa kimya

“Nachojua mimi nimeua, sijui chochote kuhusu swali lako”

Kisha akainamisha tena kchwa chake kilichonyolewa nywele zote.

“Itawezekanaje sasa usielewe kuhusu ujumbe ule wakati wewe ni mmoja wao? Au ndio kiburi au viapo ulivvyoapa vya kutokutoa siri?”

Colotilda akaongea kwa jazba na hasira

“Colotlida punguza jazba, hili ni jambazi sugu tunashukuru Mungu ametoa taarifa baadhi kuhusu tukio zima, atahukumiwa kwa makosa yake, wewe acha awafiche wenzake”

Inspekta Emmanuel Ngogo akapumzika kama sekunde tatu kisha akaendelea

“Serikali ina mkono mpana na mrefu, hao waliobaki watapatikana tu kama alivyopatikana yeye”

Afande Emmanuel Ngogo akamtuliza Colotlida aliyejawa na hasira kisha akachukua simu yake ya mkononi akatafuta namba katika sehemu ya kuhifazia majina akafanikiwa kuipata namba anayoitaka, akapiga na kumuamuru anayempigia aje ofisini kwake. Baada ya kama dakika tatu afande Isaac Nyiti akaingia na kumchukua Godfrey, safari ya kurudi ndani ya chumba cha mahabusu ikaanza.
## ## ##

‘Hakuna marefu yasiyo na mwisho’
Huo ni msemo uliozoeleka kutumika kila ifikapo mwisho wa jambo lenye uzito au utata wa namna fulani. Hakika mwisho wa maswali waliyokua wakijiuliza raia juu ya hatima ya Godfrey Mdemu ulikua umefika. Umati mkubwa wa watu ulifurika katika mahakama tukufu ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, kila mmoja akitaka kutambua nini kitakachoamuriwa katika kesi ile.

Wapo walioamini Godfrey atafungwa kifungo cha maisha ila wapo wachache sana walioamini hastahili hukumu kubwa kiasi hicho. Ndani ya mahakama umati wote ulikua kimya ukimsubiri mtuhumiwa na waendesha kesi waingie ndani ili mjadala uendelee. Wapo waliokua wakinong`onezana mambo mbalimbali, wapo waliokuwa wameandamwa na chuki usoni mwao dhidi ya Godfrey lakini katika kona ya kulia ya mahakama hiyo alikuwepo msichana mdogo wa miaka kumi na tisa akiwa ndani ya jezi ya shule maarufu mkoani Kigoma, shule inayoitwa ‘Newman secondary school’, mkononi alikua ameshika picha ndogo iliyosababisha atoe machozi kila alipokua akiitazama.

Msichana yule hakuweza kutulia mahala alipokaa, alikua mara ainuke mara akae wakati mwingine alichuchumaa kitu ambacho kilishindwa kueleweka kwa watu waliokua karibu nae, wakahisi labda alikua kachanganyikiwa. Binti huyo aliongozana na wanafunzi mwenzake wawili, wanafunzi wale muda wote walikua makini sana wakijitahidi kumtuliza lakini haikuwezekana hata kidogo, walivyoona hazuiliki wakaamua kumuacha ajitulize mwenyewe. Raia wachache waliomfahamu binti yule walinong`onezana chini chini maneno ambayo hayakusikika kabisa kwa mtu asiyehusika.

Kelele za magari ya polisi zikasikika nje ya jengo la mahakama, baada ya kama dakika tatu jengo zima la mahakama likageuka nyuma kutazama mlango wa kuingilia baada ya kuona polisi wanne wakiwa na silaha zao za moto wakimshindikiza Godfrey aliyefungwa pingu mkononi. Macho ya Godfrey yalikua yakitazama chini baada ya kukutana na macho ya umati mkubwa yakimtazama. Mashavu yake yaliacha michirizi ya machozi kitu kilichotafsiriwa alikua akilia muda mfupi uliopita. Msichana aliyeongozana na wanafunzi wenzake akaongeza sauti ya kilio na kelele zisizo eleweka baada ya kumuona mtuhumiwa akiingizwa mahakamani, kelele za kilio za binti yule zikawa kama kero katika masikio ya watu pamoja na polisi. Umati wote ukamgeukia mwanafunzi yule. Sauti ya kilio kile haikua ngeni katika masikio ya Godfrey, akajikuta akiinua shingo lake na kumtazama aliyekua akilia kwa sauti mpaka anawakera wengine. Moyo ukamuuma Godfrey alipodhibitisha sauti ile ya kilio hajaifananisha bali ni yenyewe, kitu kilichopelekea kuangusha chozi kwa mara ya pili mbele ya halaiki ya watu waliojitokeza kushuhudia hukumu yake.

“Samahani afande! Naweza kuongea kidogo na binti yule”

Godfrey akamwambia mmoja wa wale polisi waliokua wakimuongoza

“Songa mbele! Huu sio muda wa maongezi ya kipuuzi”

Sauti kali toka kwa afande Hassan Mgao ikamkaripia Godfrey. Godfrey akajaribu kusimama bila ruhusa kwa lengo la kuonana na kumtuliza mwanafunzi yule lakini zoezi lake likashindikana baada ya kusukumwa mbele na afande aliyemjibu awali. Kitendo kile kikaongeza kilio kwa mwanafunzi yule aliyeona umuhimu wa kuja kushuhudia hukumu ya mtuhumiwa huyo, kelele zake zikawa kero zaidi.

“Muondoeni ndani ya mahakama yule mwanafunzi…Tena mpelekeni mpaka shuleni kwake asije vunja shughuli na utaratibu wa mahakama”

Sauti toka kwa afande Hassan Mgao ikaamuru binti yule atolewa. Hazikupita hata dakika mbili, polisi wawili wakaenda kutimiza amri hiyo kwa nguvu. Wanafunzi wenzake wakamfuata nyuma, walipofika katika mlango wa kutokea ndani ya mahakama kwa bahati mbaya wakagongana na binti mrembo aliyekua akiingia mahakamani hapo. Bahati mbaya zaidi pasipo kufahamu mwanafunzi yule akaangusha picha aliyokua ameishika mkononi, picha iliyokua ikimkumbusha mambo mengi kati yake na mtuhumiwa. Colotlida alishuhudia wanafunzi wale wakipakiwa ndani ya gari la polisi na safari ya kwenda shule ya sekondari Newman ikaanza.

“Wameshindwa kutofautisha kati ya shule na mahakama? Au kuna nini?”

Swali lisilokua na majibu likapita katika kichwa cha Colotilda kama tiara iliyokatika kamba, akalishindikiza kwa macho gari la polisi lililowabeba wanafunzi wale mpaka lilipotoweka katika upeo wa macho yake. Colotilda akafungua mkoba wake akachomoa kioo kidogo kisha akarekebisha nywele zake zilizosambaa baada ya kupamiana na wanafunzi wale, akajiweka vizuri mavazi yake pia. Lakini alipogeuza kichwa mbele ili aingie ndani ya jengo la mahakama akaiona picha ikimtazama, picha iliyobeba watu wawili. Akainama taratibu na kuiokota picha ile kisha akaitazama kwa jicho la udadisi. Maswali yakaongezeka kwenye akili ya Colotilda. Sasa aliamini kuna kitu asichokijua kati ya mwanafunzi yule na mtuhumiwa wake

ITAENDELEA

NB: * Yupo wapi God Mother?
* Nini hatima ya Godfrey?View attachment 1837533
Ipo poa
 
Back
Top Bottom