Riwaya: Afisa usalama

Riwaya: Afisa usalama

RIWAYA: AFISA USALAMA
MTUNZI: EMMANUEL PHIRI
NAMBA: 0758 195 890
INSTAGRAM: immaphiri

SEHEMU: 09
ILIPOISHIA

Colotilda akafungua mkoba wake akachomoa kioo kidogo kisha akarekebisha nywele zake zilizosambaa baada ya kupamiana na wanafunzi wale, akajiweka vizuri mavazi yake pia. Lakini alipogeuza kichwa mbele ili aingie ndani ya jengo la mahakama akaiona picha ikimtazama, picha iliyobeba watu wawili. Akainama taratibu na kuiokota picha ile kisha akaitazama kwa jicho la udadisi. Maswali yakaongezeka kwenye akili ya Colotilda. Sasa aliamini kuna kitu asichokijua kati ya mwanafunzi yule na mtuhumiwa wake

ENDELEA

“Huyu binti ni nani haswa? Ana uhusiano gani na Godfrey?”

Kauli hiyo ikamtoka Colotilda baada ya kuitazama vizuri picha ile. Pichani alimuona Godfrey akiwa kamkumbatiana msichana yule wa shule huku sura zao zikiwa zimeandamwa na furaha isiyoweza kupimwa na mzani wa aina yoyote.

“Au ni girlfriend wake?”

“Mbona katolewa mahakamani kwa fujo kuna nini kinachoendelea?”

Alijiuliza maswali mengi pasipo majibu yake kisha akatoa tabasamu hafifu lililoshindwa kuruhusu meno yake yaonekane, akajisemea ndani ya moyo wake

“Hii ni kazi yangu na huu ni mwanzo mzuri”

Akaiweka ile picha ndani ya mkoba wake wa gharama na kutokomea ndani ya mahakama. Colotilda alikua amevaa miwani kubwa nyeusi iliyoficha muonekano wa sura yake hivyo basi haikua rahisi kwa watu asiye wa karibu kwake kumfahamu haraka. Muda huo Godfrey alikua ndani ya kizimba akisubiri hukumu yake isome. Waendesha mashitaka waliendesha kesi kwa utaratibu na umakini wa haki na misingi ya mahakama kama ilivyotakiwa. Hakimu Mr Stephen Mashimba alikua makini na maelezo ya pande zote mbili. Godfrey hakupata wakili wa kumtetea hivyo basi alikua chini ya mawakili wa mahakama (serikali) kujaribu bahati yake. Baada ya muda mfupi kupita kesi ilikua imeshasikilizwa vizuri, kesi haikua ngumu hata kidogo kwasababu mtuhumiwa alishadhibitisha kuhusika na mauaji hivyo basi alitakiwa kuhidhibitishia mahakama kwa mara ya pili, na ndivyo alivyofanya. Umati mkubwa ulishangazwa na jibu la Godfrey ukashindwa kuamini jinsi alivyoishi maisha ya shida, walishindwa kuelewa uhusiano wake na lile kundi la kigaidi, kundi linaloaminika lina utajiri na mali za kutosha.

Sasa kwanini Godfrey ni masikini wa kupitiliza?

Au alijifanya masikini kwenye macho ya watu ili atimize kazi yake?.

Ikawa gumzo ndani ya mahakama.
Hakimu, Mr Stephen Mashimba akautazama umati uliofurika mahakamani kisha akarudisha macho kwa Godfrey, akaongea

“Kutokana na mwenendo na kesi hii tangu siku ya kwanza mpaka leo naona kila kitu kipo bayana kabisa kama mtuhumiwa alivyoelezea”

Akakohoa kidogo kisha akaendelea

“Vile vile kama mlivyomsikiliza Colotlida alivyoelezea kuwa waliowateka walikua wawili, mmoja aliweza kumfahamu sura yake lakini wa pili hakuweza kuiona sura yake kabisa kwa sababu kofia aliyovaa ilifanikiwa kuificha”

Akatazama saa yake ya mkononi, akamkazia macho Godfrey kisha akamwambia

“Una chochote cha kuongea kabla sijapitisha hukumu?”

Godfrey akamtazama hakimu kisha akarudisha macho yake katika umati uliofurika mahakamani hapo, akawatazama kwa muda wa kama sekunde tano, akajikuna kichwani kinyonge kisha akarudisha macho yake kwa hakimu akaongea

“Nilitaka kuongea na mdogo wangu kipenzi baada ya kumuona nilipokua naingia ndani ya mahakama yako tukufu lakini siwezi kuongea nae tena, Polisi wamemfukuza mahakamani…Sina la kuongea nipo tayari kwa lolote”

Godfrey akainamisha kichwa chini akisubiria hukumu yake. Maneno ya mwisho ya Godfrey yakajibu swali moja alilojiuliza Colotilda baada ya kugongana na kuokota picha ya mwanafunzi aliyetolewa ndani ya mahakama kwa nguvu ya polisi.

“Kumbe yule binti ni mdogo wake!”

Colotilda akakumbuka siku aliyokwenda kuonana na Godfrey ndani ya ofisi ya Inspekta Emmanuel Ngogo, akakumbuka jinsi Godfrey alivyouliza kuhusu mdogo wake kipenzi akiamini yeye pekee ndiye anayeweza kuja kumuona.

“Huyu jamaa hana ndugu nini? Aaah! Wapi hapa kuna kitu…Haiwezekani amtegemee mdogo wake katika mambo mazito kama haya!...wazazi wako wapi?”
Colotilda akajiuliza moyoni.

Hakimu akamtazama Godfrey kisha akamuuliza

“Hakuna mtu anayekutegemea?”

“Sina wa kunitegemea zaidi ya mdogo wangu, wengine wote mimi ni mchafu mbele yao”.

Godfrey akamjibu hakimu kwa sauti ya upole kama mtu anayeomba msaada na msamaha. Hakimu akamtazama kijana yule aliyebebeshwa mzigo mzito wa dhambi mabegani kwake, akamsomea vifungu vya sheria vinavyomtia hatiani kisha akatoa hukumu iliyowaacha midomo wazi kila aliyeuzuria mahala pale.

“Kutokana na mauaji ya watu mbalimbali yanayofanywa na wewe au kundi lako ulilokataa kutoa maelezo na ushirikiano wa kulipata na kulidhibiti, mahakama hii tukufu inakuhukumu kifungo cha maisha jela kinachoambana na kazi ngumu ili iwe fundisho kwako na kwa vijana wote wenye tabia kama yako”

Hakimu Stephen Mashimba akagonga nyundo na kuondoka zake eneo la tukio, mahakama yote ikazizima kwa minong`ono, wapo walioafikiana na hukumu hiyo lakini wapo ambao hawakuafikiana hata kidogo na hukumu hiyo akiwemo msichana mrembo, Colotlida. Godfrey hakuamini alichokisikia akajikuta akiishiwa nguvu na kukaa ndani ya kizimba, taswira ya mdogo wake ikamjia kichwani akakumbuka ahadi zote alizompatia ila leo hii ahadi zote zimebaki stori, akawakumbuka rafiki zake wa aliosoma nao chuo kisha picha ya msichana mrembo wa kichaga Janeth Kimaro ikamjia kichwani. Akajikuta akiongea sauti ya chini peke yake, sauti iliyoambatana na majuto mazito

“Oooh! My Lord kwanini ulinikutanisha na Janeth? Kwanini lakini…Yasinge nikuta haya”

Akapiga ngumi chini kwenye sakafu kwa hasira kisha akajaribu kuinuka lakini miguu ikakataa. Kupitia uwazi wa mbao za kizimba alichomo ndani yake akamuona msichana mrembo akipiga hatua kuelekea alipo, akamkazia macho na kuamini msichana huyo ndio chanzo cha yeye kuhusishwa na kesi hiyo. Kushoto na kulia mwa msichana huyo walikuepo polisi vijana wenye hali ya kufanya kazi kwa umakini, akawatazama watatu wale mpaka wakafika alipo. Colotilda akamtazama Godfrey kisha akaongea sauti hafifu yenye ujumbe mzito ulioshindwa kueleweka kwenye masikio ya Godfrey na wale polisi walioongozana pamoja nae kwa lengo la kumchukua Godfrey kumpeleka katika makazi yake ya milele, binti yule alisema.

“Upo kwenye mikono salama na ipo siku utajua mimi ndie Colotlida Kamanzi, haki ya mtu huwa haipotei bali inachelewa tu”

Akawatazama wale polisi kisha akaongea

“Mdogo wako anaitwa nani?”

“Dada hatukukuruhusu uje kufanya maongezi hapa! Naona maongezi yameanza”

Polisi mmoja akaingilia kati

“Anatakiwa kupelekwa gerezani kama mahakama ilivyotangaza hukumu yake”

Polisi wa pili akaongezea. Colotilda akawatazama wale polisi kwa jicho la dharau kisha akawaambia

“Huyu ni wa kwenu maisha yake yote, Sihitaji kuwapotezea muda ila nachotaka kujua ni jina la mdogo wake tu na sio vinginevyo”

Polisi wale hawakuwa na muda tena wa kumsikiliza mrembo yule, wakamtoa Godfery ndani ya kizimba na kuondoka nae, dakika chache mbele zikasikika gari za polisi zikiondoka mahakamani hapo

“Maisha mema Godfrey, najua huhusiki na chochote dhidi yangu lakini kwanini umekubali? Ipo siku nitajua”

Mawazo yakapita katika kichwa cha Colotilda.

“Mdogo wako anaitwa nani?”

Ndani ya gari la polisi tena chini ya ulinzi mkali wa polisi wasiopungua nane Godfrey akakumbuka alivyoulizwa jina la mdogo wake. Akajisemea moyoni

“Anataka jina la nini?, Hukumu niliyopata bado hawajalizika tu!”

Mwanzo alimuona Colotilda kama ni mwema lakini baada ya hukumu na kumuuliza jina la mdogo wake hofu ikamwingia, akahisi maisha ya mdogo wake nayo yapo matatani, akainua macho juu kutazama mbingu kisha akaongea na moyo wake

“Mungu mpe ulinzi mdogo wangu”

Haikuchukua muda mrefu wakafika katika gereza la mkoa wa Kigoma mjini maarufu kwa jina la Bangwe, wengine huliita Sentro. Godfrey akashushwa na kuingizwa katika chumba maalumu cha mavazi akakabiziwa jezi yake ya kifungo yenye namba 890 moja kwa moja akaswekwa ndani ya gereza kuanza maisha mapya.
## ## ##

Wanafunzi wa shule ya sekondari Newman walikua wamezagaa katika viwanja vyao vya michezo wakiendelea kuboresha afya zao kupitia mazoezi ya viungo, wapo waliocheza mpira wa miguu katika uwanja wao unaopatikana chini kidogo ya mabweni ya wanaume (Bweni la Saint Albert, Mwalimu Nyerere na Mkwawa). Wasichana wachache walikua wakicheza mpira wa mikono (Netball) katika uwanja wao unaopatikana pia jirani na mabweni ya wanaume, pembeni ya uwanja wa mpira wa miguu. Michezo iliyowaunganisha wasichana na wavulana ilikua Volleyball na Basketball katika viwanja vinavyopatikana jirani na geti la kuingilia katika shule hiyo maarufu mkoani Kigoma, shule iliyo chini ya kanisa katoliki jimbo la Kigoma inayoongozwa na Watawa wa ‘Brothers of Charity’.

Gari aina ya Noa lilipiga honi mara mbili katika geti la kuingilia ndani ya shule hiyo, baada ya sekunde chache mlinzi alilifuata gari lilipo na kufanya mahojiano ya awali kabda hajaliruhusu gari hilo liingie ndani. Kioo cha mbele cha gari lile kikashushwa ili kuweza kuonana vizuri na mlinzi aliyekua zamu.

“Habari yako kaka”

Msichana mwenye kila vigezo vya kuitwa mrembo akamsalimia mlinzi aliyesimama pembeni ya gari lake

“Salama dada yangu, Sijui nikusaidie nini?”

Mlinzi akauliza baada ya kujibu salamu ya mrembo yule

“Mimi ni mwakilishi toka haki za binadamu, nimekuja kuonana na uongozi wa shule”

Mrembo yule akajibu

“Nioneshe kitambulisho chako tafadhari”

Msichana yule akafungua pochi yake dogo na kuchomoa kitambulisho kilichomtambulisha kama mfanyakazi wa shirika la haki za binadamu Tanzania. Bila kipingamizi mlinzi akafungua mlango wa geti na kumruhusu binti yule aingie ndani kisha akamuelekeza ofisi zilipo. Gari aina ya Nona likapiga breki nje ya ofisi yenye kibao kilichoandikwa
‘MKUU WA SHULE’
kisha mrembo akashuka na kuingia ndani ya ofisi hiyo. Akapokelewa na sekretari.

“Za asubuhi dada yangu”

Akasalimia

“Salama…Karibu sana”

Sekretari akajibu

“Naitwa Colotlida Kamanzi kutoka shirika la Haki za Binadamu nimekuja kuonana na uongozi wa shule kuna mambo nahitaji kujua kutoka kwao”

“Mkuu ana taarifa zako?”

“Hapana”

Sekretari akainuka kisha akaingia katika ofisi ya mkuu wa shule ili kuomba ruhusa ya mgeni kuingia, baada ya sekunde ishirini akatoka na kumwambia Colotlida

“Unaweza kuingia”

Bila kupoteza muda Colotlida akaingia katika ofisi ya mkuu wa shule.
Baada ya salamu na utambulisho wa awali Colotlida akamwambia mkuu wa shule

“Kama nilivyojitambulisha na kitambulisho changu kinavyoonesha…nina shida na mwanafunzi wako mmoja kwa mahojiano zaidi kuhusu masuala ya haki zake”

akapumzika kidogo kisha akaendelea

“Nasikia alifanyiwa fujo alipoenda kufatilia kesi ya kaka yake, nataka kumsaidia ajue nini cha kufanya ili aweze pata haki zake za msingi”

“Unamzungumzia Walterblanca Mdemu?”

Mkuu wa shule, Brother Faraja James Almas akamkatisha kwa kumuuliza swali

“Nafikiri atakua ni huyo huyo”

Colotlida akamjibu huku akirekebisha nywele zake zinazofika mpaka mgongoni

“Sizani kama mtaweza kuelewana vizuri”

Brother Faraja James Almas akakohoa kidogo kisha akarekebisha tai yake, akaendelea

“Tangu juzi alipoletwa na polisi kutoka mahakamani hali yake haipo vizuri, anaweweseka sana mpaka tunashindwa kuelewa nini tatizo lake”

Mshangao ukateka sura ya Colotilda baada ya kusikia taarifa za mdogo wake Godfrey, akamkazia macho mkuu wa shule na kumwambia

“Naweza kuonana nae?”

Mkuu wa shule hakujibu swali lile akachukua simu yake ya mkononi na kutafuta namba katika simu yake kisha akapiga

“Hallo Matron”

Akakaa kimya kidogo kumpa nafasi aliyempigia aitikie kisha akaendelea

“Nakuhitaji ofisini kwangu, kuna mgeni anayehitaji huduma yako”.

Baada ya dakika tano kupita akaingia sister Raheli Manase Mtinangi aliyekua akifanya kazi katika shule hiyo kama matron, akasalimia aliowakuta kisha akakaa kimya kusikiliza alichoitiwa.

“Unayemuona mbele yako ni mwakilishi toka haki za binadamu, amekuja hapa ili afanye mahojiano mafupi na Walterblanca kuhusu tatizo lake”

Akavuta pumzi ndefu ndani kisha akaitoa taratibu, akaendelea

“Najua hali ya Walterblanca sio nzuri sana lakini mpeleke akaonane nae kwasababu anaweza kuwa msaada wa saikolojia kwa mwanafunzi wetu”.

Sister Raheli Mtinangi hakua na pingamizi lolote juu ya suala aliloambiwa na mkuu wake wa kazi, akamwamuru mgeni yule amfuate ili akaonane na Walterblanca.
Wakatoka ndani ya ofisi ya mkuu wa shule, mwendo wa kwenda chumba maalum cha kupumzikia wagonjwa maarufu kama ‘Sick Bay’ ukaanza. Baada ya kufika ‘Sick Bay’ wakakaribishwa na nesi aliyekua akitoa huduma kwa wanafunzi wagonjwa. Sister Raheli Mtinangi akamueleza nesi dhumuni la ugeni huo katika chumba kile maalum cha kulaza wagonjwa. Nesi akamtazama Colotlida kisha akamuuliza

“Kuna ulazima wowote wa kuongea nae leo? Maana hali yake sio nzuri”

Colotilda akarekebisha miwani yake vizuri kisha akajibu swali aliloulizwa

“Ofisi inahitaji taarifa zake mapema inavyowezekana ili jambo lake lipate ufumbuzi yakinifu…naomba ruhusa yako please”

Nesi akamtazama Colotilda kwa macho ya udadisi kisha akarudisha macho kwa matroni, Matroni akampa ishara ya dole gumba akimaanisha amruhusu mgeni huyo afanye mahojiano yake

“Nakupa dakika kumi tu utimize shida yako”

Kauli ya nesi ikaleta tabasamu hafifu katika mashavu ya Colotilda kisha akatingisha kichwa chake juu chini akimaanisha ameafiki maelekezo ya nesi. Wakaingia katika chumba alicholala Walterblanca, msichana aliyegubikwa na mawazo toka kwenye unyayo wa miguu yake mpaka utosi mwa kichwa chake. Wakawakuta rafiki zake wakimlazimisha kula matunda pasipo mafanikio yoyote. Baada ya salamu kupita nesi akaanzisha mazungumzo

“Walterblanca”

Nesi akaita lakini kabla hajaitikiwa chochote akaendelea

“Hii sura ngeni unayoiona mbele yako ni ugeni wako, jitahidi unavyoweza kumpa ushirikiano wa kutosha”

Nesi akaweka kituo kisha akawaamuru rafiki zake Walterblanca waondoke kidogo ili mgeni apate nafasi ya kuongea na rafiki yao. Walterblanca akamkazia macho Colotilda, akafikiria kama kashawahi kumuona wapi lakini ubongo wake ukakataa kumpa taarifa hizo, hakika ilikua sura ngeni kwake.

“Eti mgeni wangu, mgeni?”

Swali fupi likapita katika akili ya Walterblanca pasipo jawabu lolote. Akafungua mdomo wake akasema

“Ni nani? Mbona simfahamu!”

ITAENDELEA

  • Mbona simuelewi Colotilda?
  • Yupo wapi God Mother?
  • Nini hatima ya Godfrey?
shukran mkuu
 
Back
Top Bottom