Riwaya: Afisa usalama

25phiri12

Senior Member
Jun 19, 2021
120
92

Attachments

  • received_597897344513294.jpg
    received_597897344513294.jpg
    62.1 KB · Views: 87
Karibu
RIWAYA: AFISA USALAMA
MTUNZI: EMMANUEL PHIRI
NAMBA: 0758 195 890
INSTAGRAM: immaphiri

SEHEMU 01

Manyunyu ya mvua yaliendelea kulowanisha ardhi taratibu bila papara wala haraka ya aina yoyote, japokuwa yalikuwa madogo lakini yalitosha kabisa kutoa maana ya haba na haba hujaza kibaba, kwa sababu muunganiko wa manyunyu hayo uliweza kutengeneza vimifereji vidogo vidogo vilivyoruhuru mkusanyiko wa maji upite hatua katika sura ya nchi. Manyunyu hayo hayakuwa kikwazo hata kidogo kwa msichana mrembo aliyekuwa mawindoni, hakujali wala hakutaka kufikiria kama nje ya gari kuna manyunyu yanayoendelea kushambulia sura ya nchi, yeye akili yake ilikuwa makini kufikiria na kufatilia kilichompeleka mahala pale, hakika alikuwa mawindoni na hakutaka kupoteza windo lake.

Sauti laini ya wimbo wa Asa uitwao 'Beautiful' uliteka sehemu yote ya ndani ya gari lake, wimbo huo ulikua ni sehemu ya maisha yake, hakuruhusu siku hata moja ipite pasipo kuusikiliza wimbo huo mara tano mpaka kumi au zaidi. Sio kwamba aliupenda sana wimbo huo wa Mfaransa mwenye asili ya Nigeria, la hasha bali ulimkumbusha umuhimu wa watu aliowapoteza miaka mingi iliyopita, watu waliomlea katika misingi ya utu na upendo na waliomuhimiza kutia juhudi katika kila jambo alilolihitaji. Mrembo huyo alikuwa ndani ya gari lililoegesha nje mita chache toka lilipo ghorofa lenye ofisi tofauti za Serikali pamoja na mashirika ya watu binafsi. Ndani ya jengo hilo kuna benki ya NMB, benki ya Exim, Mfuko wa Bima ya Afya wa Taifa (NHIF) pamoja na ofisi za mashirika mengine.

Kofia aina ya kepu yenye chapa ya adidas ilikua kichwani kwake huku macho yake mazuri yakiwa yamefichwa barabara kwa miwani kubwa nyeusi iliyoweza kuficha kabisa taswira yake halisi, hakika haikua rahisi kumfahamu. Macho ya msichana yule yalikua hayaishi kuutazama mlango wa kutokea ndani ya Benki ya NMB, alikua akipepesa macho sehemu nyingine kwa sekunde chache kisha macho yake yanarudi sehemu husika aliyoikusudia. Sehemu aliyoamini lazima lindo lake lipite. Hakika alikua kazini na hakuitaji kupoteza umakini kwa jambo alilolikusudia. Aliwatazama walinzi wa jengo hilo waliokua na silaha za moto mikononi aina ya SMG kisha akatabasamu, ilikua ni ishara ya kuwadharau. Aliamini hakuna mlinzi mwenye uwezo wa kuzuia au kukatisha misheni yake. Alirudisha macho katika mkoba wake uliokua juu ya mapaja yaliyokua wazi baada ya sketi futi aliyoivaa kushindwa kuyasitiri ipasavyo, akafungua zipu ya mkoba huo kisha akachomoa katiba ya nchi kisha akayasoma maandishi yaliyo juu kabisa ya katiba hiyo

“CONSTITUTION OF THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA OF 1977”
(KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA YA MWAKA 1977)

Baada ya kusoma maneno hayo akakumbua kiapo alichoapa akiwa ameshika katiba hiyo, kiapo alichoamini atakiishi mpaka siku Mungu atakapochukua maisha yake. Sasa yupo kazini, kazi inayokinzana na kiapo alichoapa cha kulitumikia na kulilinda Taifa teule la Tanzania. Hasira zikamvamia ghafla baada ya kukumbuka aliyemuongoza mpaka akawa mtu kamili ndani ya idara ya Usalama wa Taifa ndiye huyo huyo aliyesababisha leo hii yupo kwenye kazi ya kupambana dhidi ya wana idara hiyo na Serikali kwa ujumla. Akapiga kumi katika usukani wa gari. Aliichukia sana dunia na mara kadhaa alifikiria kujiua ili aweze kuwafuata wapendwa wake lakini moyo ulikataa, aliona atakua amefanya makosa makubwa kama hata pambana ipasavyo na maadui walio mbele yake.

Aliamini ndani ya dunia anapaswa kulinda maisha ya Finisher na Mtakatifu Makuta pekee, aliona hao ndio binadamu pekee asioweza kuwadhuru endapo kazi ikija mbele yake lakini waliosalia hawakumaanisha lolote wala chochote kwake na aliamini anaweza kumwaga damu zao muda wowote. Hakika alikua God Mother kama jina lake lilivyokua likichapishwa na kutangazwa kwenye vyombo vya habari ndani na nje ya mipaka ya Tanzania. Jina la God Mother lilikua maarufu sana katika masikio ya kila Mtanzania kwa uhalifu na mauaji ya kila siku aliyokua akiyafanya bila huruma yoyote lakini hakuna aliyekua akimfahamu God Mother halisi isipokuwa Finisher na Mtakatifu Makuta pekee, hata aliokua akifanya nao kazi za kigaidi walitamani kumfahamu God Mother lakini hawakufanikiwa. Katika kazi zake hakutaka kufahamika kwa watu asiotaka wamfahamu na waliobahatika kumfahamu bila ridhaa yake walikua wamenunua tiketi ya kifo pasipo wao kujua, walitangulizwa mbele ya haki hata kama alikua nao ndani ya kazi moja.

Muda wote alipokua kazini na magaidi wenzake alikua akivaa soksi usoni ili kuficha sura yake, hakua mtu wa kawaida hata kidogo. Alikua ni mtu mmoja mwenye sura tatu tofauti, wengi walimfahamu kama msichana mrembo na mkimya sana hasa watu wa mtaani kwake, wachache walimfahamu kama Afisa Usalama aliyeandaliwa kuja kulitetea Taifa, lakini watu wawili ndio waliofahamu sura yake ya tatu kuwa ni mwanachama halali wa kundi la kigaidi la The Golden Unit, kundi linalosumbua amani ya nchi pamoja na utajiri wake. God Mother akatazama saa yake ya mkononi ikamuonesha amekaa zaidi ya nusu saa akimsubiri mlengwa wake, mshangao ukashambulia sura yake kisha akajiuliza mwenyewe pasipo kujipa jawabu

“Mbona amechelewa kutoka au amefahamu kinachoendelea?”

Kipindi akiendelea kutafakari jibu sahihi la swali lake alimshuhudia mlengwa wake akitoka ndani ya benki hiyo. Akajisemea moyoni

“Very sorry Mr Amani Wilfred Mfunjo, Ujuaji wako ndio unakuponza…Utamsalimia Mr Hamisi Ernest ndani ya dakika chache zijazo”

God Mother akaibusu katiba ya nchi kisha akairudisha ndani ya mkoba wake uliokua juu ya mapaja yake awali, sasa ulikua katika kiti cha pembeni kisha akawasha gari na kuanza kuondoka eneo lile huku macho yakiendelea kumtazama Mr Amani Wilfred Mfunjo aliyekua akimsubiri muda wote. Mr Amani Wilfred Mfunjo alienda moja kwa moja mpaka alipoegesha gari lake lililokua jirani kabisa na eneo alilokua awali God Mother, sasa gari la God Mother lilikua limesimama katika barabara ya lami ya kuelekea Ujiji likisubiri tukio moja tu ili kazi iwe imekwisha. Hakika usilolijua ni kama usiku wa giza, Mr Amani Wilfred Mfunjo akiwa na begi lake mkononi aliingiza ufunguo katika mlango wa gari lake aina ya BMW kisha akauzungusha kuruhusu mlango kufunguka, akashika kitasa cha mlango kisha akafungua. Kilichofuata ni mlipuko mkubwa, bomu lililokua limetegwa katika gari lake liliripuka na kumsambaratisha viungo vyake. Hali ya sitofahamu ilivamia eneo hilo la benki lililo jirani zaidi na soko la Kigoma mjini, watu wakaanza kukimbia ovyo kwa lengo la kuokoa maisha yao pasipo kujua aliyekusudiwa ameshaingia ndani ya mtego.

Vilio vilisikika kila kona ya eneo hilo, wapo waliojeruhiwa sehemu za miili yao kama miguu, mikono na kadhalika lakini hakuna aliyetangulia mbele ya haki zaidi ya Mr Amani Wilfred Mfunjo. Baada ya dakika moja gari la God Mother lilikua limeshapotea eneo hilo. Muda mfupi baadae vyombo vya habari nchi nzima vilitangaza juu ya kifo cha wakili wa serikali aliyejizolea sifa kemkem kwa kupambana na wahalifu ndani ya mipaka ya nchi. Raia waliumia sana walipohakikishiwa kuwa aliyefariki ni wakili Amani Wilfred Mfunjo. Mawazo juu ya kundi la kigaidi la The Golden Unit yakaendelea kuhatarisha amani kati yao. Hakika hawakua salama hata kidogo. Hakika walikuwa kwenye mdomo wa kifo.

ITAENDELEA

*Nini kilichomsibu God Mother?
*Kesho muda kama huu

 
RIWAYA: AFISA USALAMA
MTUNZI: EMMANUEL PHIRI
NAMBA: 0758 195 890
INSTAGRAM: immaphiri

SEHEMU YA: 02

TULIPOISHIA

Hakika usilolijua ni kama usiku wa giza, Mr Amani Wilfred Mfunjo akiwa na begi lake mkononi aliingiza ufunguo katika mlango wa gari lake aina ya BMW kisha akauzungusha kuruhuru mlango kufunguka, akashika kitasa cha mlango kisha akafungua. Kilichofuata ni mlipuko mkubwa, bomu lililokua limetegwa katika gari lake liliripuka na kumsambaratisha viungo vyake. Hali ya sitofahamu ilivamia eneo hilo la benki lililo jirani zaidi ya soko la Kigoma mjini, watu wakaanza kukimbia ovyo kwa lengo la kuokoa maisha yao pasipo kujua aliyekusudiwa ameshaingia ndani ya mtego.

Vilio vilisikika kila kona ya eneo hilo, wapo waliojeruhiwa sehemu za miili yao kama miguu, mikono na kadhalika lakini hakuna aliyetangulia mbele ya haki zaidi ya Mr Amani Wilfred Mfunjo. Baada ya dakika moja gari la God Mother lilikua limeshapotea eneo hilo. Muda mfupi baadae vyombo vya habari nchi nzima vilitangaza juu ya kifo cha wakili wa serikali aliyejizolea sifa kemkem kwa kupambana na wahalifu ndani ya mipaka ya nchi. Raia waliumia sana walipohakikishiwa kuwa aliyefariki ni wakili Amani Wilfred Mfunjo. Mawazo juu ya kundi la kigaidi la The Golden Unit yakaendelea kuhatarisha amani kati yao. Hakika hawakua salama hata kidogo.
## ## ##

MWAKA MMOJA NA MIEZI KADHAA NYUMA.
Hali ya hewa ilionekana kuwa shwari huku upepo mwanana ukiibembeleza na kuipuliza sura ya nchi. Haukuishia hapo tu bali upepo uliendelea kufanya kazi nzito ya kuipeperusha bendera, tena sio bendera kama watu wasiojua thamani yake walivyozoea kuiita, bali bendera iliyokusanya rangi nne tofauti. Bendera ya Taifa teule la Tanzania ilionesha ushirikiano wa kutosha katika muhimili wake. Hakika bendera ile iliipendezesha shule ya msingi Airport, shule inayokusanya watoto wengi wa walala hoi wanaokaa mitaa ya Airport, Katubuka, Mwasenga, Mwanga, Nazareti, Vamia pamoja na mitaa mingine ya jirani. Godfrey Mdemu alikua sentimita chache toka ilipo bendera hiyo iliyobeba sifa kemkem hasa amani na utulivu duniani kote. Akaitazama bendera ile ilivyokua ikipepea kwa madaha kutoka kaskazini kwenda kusini mwa dunia, kisha akajisemea moyoni.

“Hakika nchi hii...nchi ya wachache sana, walala hoi tunazidi kuumia”

Akazitazama rangi zilivyoipendezesha bendera ile iliyokua ikikinzana na upepo kisha akayakumbuka maneno ya mwalimu wake wa maarifa ya jamii, mwalimu wake pendwa wa darasa la tatu.

“Rangi ya njano eti inamaanisha madini! kweli madini yapo ila….anajua Mola. Kijani eti inaelezea suala la kilimo ila mbona sisi walala hoi tunalia njaa kila siku….Maziwa, bahari, mito eti ni bluu, sasa sisi watu wa Kigoma hatuna hata kiwanda cha samaki!! Sijui inakuaje!…Hah hah hah!!! Rangi pekee inayotufaa walala hoi wengi ni nyeusi kwa sababu ndio rangi yetu sisi watu wa hali ya chini. Watu wenye pesa zao wanaikimbia rangi hii kupitia vipodozi”

Godfrey Mdemu akaitazama tena bendera ile kisha akatamka maneno hafifu yasiyo na nguvu yoyote mbele ya uso wa dunia ila yaliyobeba ujumbe mzito.

“Fumbua macho Tanzania”

Taratibu huku kichwa chake kikiandamwa na mawazo akaondoka eneo lile na kuelekea katika chumba kibovu alichopanga, jirani na Kanisa Katoriki la Mtakatifu Ritha – Airport. Akajitupa juu ya godoro lake chafu na chakavu lililojaa kunguni waliofanya maskani yake siku zote, akafikirisha kichwa chake nini anatakiwa kufanya kisha akapata wazo mpya, akainuka na kuchukua bahasha yake chakavu pembeni ya mlango uliomstili na aibu ya chumba chake, akafungua bahasha hiyo na kutoa karatasi tatu tofauti, akazitupa juu ya godoro lake kisha akakagua tena vizuri ndani ya bahasha ile, akatoa karatasi nyingine iliyojaa maandishi yaliyoandikwa kwa herufi kubwa tena kwa wino mwekundu. Akasogea na kukaa katika godoro lake lenye kunguni wenye chuki na hasira dhidi yake kwa njaa kali ya mchana huo, macho ya Godfrey yakatua katika yale makaratasi matatu aliyoyaweka kwenye godoro lake. Moyo ulimuuma sana alipoona vyeti vyake vya elimu havina faida katika maisha yake

“Niliambiwa nikimaliza chuo nitafanikiwa katika maisha yangu!...Nini maana ya ile kauli ya elimu ni ufunguo wa maisha! Maisha gani walikua wanamaanisha...Mungu wangu angalia maisha yangu”

Akatupa macho katika karatasi lenye maandishi makubwa yaliyoandikwa kwa wino mwekundu, akatabasamu na kujisemea moyoni

“One day nitafanikiwa tu”

Karatasi ile ilikua imejaa maneno yaliyompa moyo kila alipohisi anataka kukata tamaa, akaanza kuyasoma moja baada ya nyingine.

“No great mind has ever existed without a touch of madness (Hakuna mawazo mazuri yamekuwepo bila kuwepo wazimu)” - Aristotle

“Attempt the impossible in order to improve your work (Jaribu yasiyowezekana ili kuboresha kazi yako)” – Brain Tracy

“If you want to live a happy life, tie it to goal not to people or objects (Kama unataka kuishi maisha ya furaha, kazania malengo yako sio watu wala vitu)” – Albert Einstein

“The problem of the World is that, the intelligent people are full of doubts while the stupid ones are full of confidence (Tatizo la ulimwengu ni kwamba, watu wenye akili wamejaa shaka wakati wajinga wamejaa ujasiri)” – Charles Bukowski.

Akarudia kusoma mara ya pili kisha akatoa tabasamu hafifu lililopingana na moyo wake uliokunjamana kwa mawazo ya dhiki. Akarudisha karatasi zake zote katika bahasha yake mbovu na iliyochakaa kwa udongo mwekundu.
Akaingiza mkono wa kulia katika mfuko wa suruali yake isiyojulikana rangi yake halisi kwa ajili ya kupauka kisha akachomoa saa yake ya mkononi iliyokatika mkanda mmoja, hivyo basi humlazimu kuiweka mfukoni. Akatazama majira ikamuonesha ni saa nane na nusu mchana. Akaikumbuka familia yake lakini kauli ya baba yake dhidi yake ikamtoa machozi, kauli ambayo ilikua ikimtafuna kila aikumbukapo.

“Nisiione sura yako tena mbele yangu! na kuanzia leo wewe sio mwanangu….tafuta wa kumuita baba, sio mimi”

Maneno hayo yakajirudia akilini mwake taratibu, yalikua kama donda lililoacha kovu lisilofutika. Akajisemea moyoni

“Ipo siku baba utajua kilichotokea, leo hii sina thamani yoyote mbele yako na mbele ya jamii inayoamini kama wewe unavyoamini”

Akajilaza katika godoro lake ili atafute usingizi lakini mawazo tofauti yakakinzana kichwani mwake, wazo moja likafanikiwa kushinda. Akaona kuliko kujilaza bora aende kumuomba msamaha bosi wake, mzee Ramadhani Simba, aliyemnyang`anya bajaji siku mbili zilizopita kwasababu zisizo na kichwa wala miguu.

“Kisa kumuazima bajaji Godluck Semali ampeleke mke wake hospitali!...Bosi akanifukuza kazi, eti bajaji yake sio ya kuazimisha….Ngoja nikambembeleze tuu maana mimi ndio mwenye shida”

Kipindi akiendelea kusumbuliwa na mawazo mazito juu ya godoro lake lililokosa kitanda, akapitiwa na usingizi mzito kutokana na uchovu aliokua nao.
Hakupata muda wa kufaidi usingizi wake, kelele kali katika mlango wake mbovu zikamuamsha. Godfrey akaamka huku amekunja sura kwa hasira na kumlaani vikali aliyekua akigonga mlango wake kwa fujo bila ustaarabu wowote. Akainuka toka kwenye godoro na kuelekea usawa wa mlango wake unaogongwa kwa fujo ili kumfungulia mpuuzi anayemsumbua bila nidhamu. Moyo wa Godfrey ukasinyaa na sura ya hasira ikayeyuka kama seruji iliyotelekezwa juani baada ya kumuona mgongaji, akabaki akimtazama na asijue amwambie nini.

ITAENDELEA

  • Nini kilichomsibu Godfrey Mdemu?
  • Yupo wapi God Mother?
tupo pamoja mkuu,shukrani
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom