BARD AI
JF-Expert Member
- Jul 24, 2018
- 3,589
- 8,769
Mkurugenzi huyo Mkuu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo amesema Watu wenye uzito mkubwa wanapaswa kuchukua hatua za haraka kupunguza miili kabla hawajaingia kwenye hatari ya Magonjwa Yasiyoambukiza.
Amesema kasi ya ongezeko la Wagonjwa wa Figo inaonesha wazi Watu wengi wana mtindo wa Maisha usiofaa ikiwemo ulaji mbaya wa Vyakula, Matumizi makubwa ya Pombe na Dawa za Kutuliza Maumivu bila utaratibu mzuri pia kutofanya mazoezi.
Ameongeza kuwa tafiti zinaonesha 90% ya Watu hawajui kama Figo zao zina matatizo huku 40% wakifika Hospitali wakati Ugonjwa ukiwa hatua ngumu na za mwisho kutibika na hauwezi hata kusafisha Damu (Dialysis).
Kwa mujibu wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), ili kuepuka Magonjwa yanayotokana na Vyakula, Watu wanapasawa kutotumia Vyakula Vilivyopikwa kwa Mafuta Mengi, Vinywaji Venye Sukari Nyingi zikiwemo Soda aina zote na Juisi za Viwandani.
===========
Unachokula ndicho huamua afya yako ya figo, ndicho anachomaanisha Profesa Mohamed Janabi akisema sababu ya tatizo la figo ni vyakula anavyokula mtu.
“Kisukari ndio ugonjwa namba moja unaosababisha tatizo la figo, kisukari ni tatizo linalotokana na ulaji na ulaji unarekebishika,” anasema Profesa Janabi ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) wakati wa uzinduzi wa taasisi ya Profesa jay inayolenga kutoa misaada kwa wagonjwa wa figo.
Ili kukabiliana na unene wa kupitiliza, kwa siku 30, Profesa Janabi anashauri mtu akiamka asubuhi asinywe chai kama kawaida, bali asogeza muda hadi saa sita mchana.
Anasema baada ya hapo asitafune kitu chochote, bali atumie chai na maji hadi saa mbili usiku ndipo ale, hiyo itakuwezesha kufunga kwa saa 16 na kula kwa saa nane.
Baada ya kufanya hivyo kwa wiki mbili mfululizo, anasema mtu huyo anywe chai saa sita na kula chakula saa 12 jioni, hapo atakuwa amefunga saa 18 na kula kwa saa sita.
“Mbinu hiyo itaupa mwili kutafuta akiba ya nishati kwenye kitambi, misuli na maeneo mengine ya mwili. Watu wanakula mara nyingi sana na majibu yake hupatikana kupitia magonjwa yasiyo ya kuambukiza,” anasema.
Kinachoonekana Muhimbili
Profesa Janabi anasema kinachosababisha matatizo ya figo ni ugonjwa wa kisukari.
“Nikikusanya wagonjwa 150 wanaofanyiwa tiba ya kusafisha damu Hospitali ya Taifa Muhimbili, nitawagawa kwenye makundi matatu---kisukari, shinikizo la juu la damu na unene kupindukia.
“Tatizo lingine ni matumizi ya dawa za maumivu ambazo zinaathari kwa kiwango kikubwa figo,” anasema.
Tabia hatarishi kwa figo
Profesa Janabi anazitaja tabia hizo kuwa ni kutokunywa maji ya kutosha, yaani lita moja na nusu hadi mbili za maji kwa siku.
Pia ulaji wa chumvi nyingi, kutolala vya kutosha, unywaji wa dawa za kupunguza maumivu, uvutaji sigara na wenye kisukari kutofuata maelekezo ya daktari.
Akizungumzia tatizo la figo kwa wanawake na watoto, Profesa Janabi anasema katika kila wanawake watano mmoja ana shinikizo la damu na kwa kila wanaume wanne mmoja ana shida hiyo.
Unafahamu homoni ya insulini?
Anasema kabla ya mtu hajapata ugonjwa wa kisukari, hupitia hatua ya kupata ukinzani wa homoni ya insulini na pre diabates.
Anasema mtu akitaka kufahamu ameanza kupata ukinzani wa insulini, anapaswa kupimwa kiwango cha insulini na ikiwa zaidi ya sita, hiyo ni kiashiria kwamba yupo kwenye ukinzani wa homoni hiyo.
Anasema kiashiria kingine ni iwapo mwanaume anavaa suruali kiuno zaidi ya sentimita 40 na wanawake sentimeta 35 na kuendelea, hivyo wanatakiwa kuanza kuchukua hatua.
Dalili nyingine ni ikiwa unatibiwa shinikizo la damu kuanzia kiwango cha 140/90 au unatumia dawa za shinikizo la damu au kuwa na sukari zaidi ya 100, akisisitiza wote wachukue hatua.
“Kila mtu ana damu lita tano mwilini na yote inapita kwenye moyo kati ya asilimia 20 hadi 25 ya damu hiyo inapita kwenye figo, hivyo lita 1,400 hadi 1,800 kila dakika inapita kwenye figo. Hiyo ni sawa na kusema figo inachuja glasi 760 kila dakika za damu kazi ambayo ni kubwa zaidi,” anasema.
Pia anasema mtu akiona anna vidude vyeusi kwenye ngozi usidharau, aende kufanya uchunguzi. “Pia hivi sasa huko mjini kila mtu nguvu za kiume zimepungua, ni lazima zitapungua, ukiwa na ukinzani wa homoni za insulini nguvu za kiume zitapungua. Muulize mgonjwa yoyote wa sukari,” anasema Profesa Janabi.
Dalili ugonjwa wa figo
Profesa Janabi anasema mtu anapoona dalili zifuatazo si hatua za mwanzo za ugonjwa, bali ni hatua za mwisho.
Dalili hizo ni uchovu usioelezeka, kushindwa kulala usiku, kukosa hamu ya kula, mwili kuwasha, miguu kuvimba, uso kuwa duara kupumua kunakoambana na harufu, kukojoa mara kwa mara, haja ndogo kuwa na povu na kuanza kuona damu kwenye haja ndogo.
“Ukianza kuona damu kwenye mkojo maana yake figo lako limetoboka, kwanini haya yote unayaona ni kwa sababu kunakuwepo mkusanyiko wa sumu kwenye damu ndio maana tunawapeleka wagonjwa kusafisha damu,” anasema.
Hali ikoje…
Akitumia takwimu za nchi ya Marekani ambayo amefafanua kuonyesha uhalisia mataifa mengine kutokuwa salama, Profesa Janabi anasema hadi mtu anapata shida ya figo tatizo limekuwa kubwa.
Anaeleza zaidi ya asilimia 90 watu hawajui kama wana shida ya figo na karibu umri unavyoongezeka, tatizo sugu la figo litaongezeka kwa asilimia 40.
Anasema asilimia 40 ya wagonjwa wanaofika hospitali tayari ugonjwa upo hatua za mwisho ambao huitaji usafishaji damu.
Kulingana na takwimu za Marekani, katika kila wagonjwa watano wanaowekwa katika mashine ya kusafisha damu mgonjwa mmoja hufariki kwa mwaka.
“Hii ina maana asilimia 20 ya wagonjwa watakaoanza kufanyiwa usafishaji damu watapoteza maisha na kwa miaka mitano kwa wagonjwa waliokuwa wakipata huduma ya kusafishwa damu vifo vitakuwa nusu kwasababu figo inakuwa kwenye hatua ya mwisho wa kufeli,”anasema.
Profesa Janabi anasema hatari ya ugonjwa wa figo unaua zaidi ya saratani ya tezi dume.
“Ugonjwa wa figo unaua zaidi ya saratani ya tezi dume, ni muhimu tupeane elimu ili kila mmoja wetu ajue dalili,”anasema.
Lishe yako iwe hivi
Kulingana na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) ili kujikinga na kuzuia madhara yatokanayo na figo ni vema jamii ikachukua tahadhari kwa kufanya mazoezi mara kwa mara angalau kwa muda wa dakika 30 kila siku.
Zingatia ulaji wa vyakula mchanganyiko kwa kiasi kulingana na mahitaji ya mwili wako na kazi unazozifanya. Epuka vyakula vilivyopikwa kwenye mafuta mengi na vinywaji vilivyoongezwa sukari (soda aina zote, juisi za makopo).
MWANANCHI