Kufuatia amri ya waziri mkuu Mizengo Pinda kusitisha hadharani agizo la waziri wa Ujenzi na barabara, John Magufuri kuhusu tafsiri na adhabu kwa uzito unaozidi wa magari ya mizigo, watu wengi tunadhani huu ni wakati muafaka sasa kwa Magufuri kujiuzuru nafasi ya uwaziri kwa kuwa agizo la Waziri Mkuu Pinda linaingilia utendaji wa moja kwa moja wa Magufuri na wizara yake lakini pia linakiuka 'sheria' ambayo John Magufuri aliapa kuisimamia.
Ikumbukwe kuwa hii ni mara ya pili kwa Magufuri kuingiliwa utendaji wake na Waziri mkuu Pinda. Mara ya kwanza ilikuwa kwenye zoezi la bomoa bomoa ambapo baadaye Magufuri alitishia kujiuzuru lakini mwisho wa siku aligwaya na kunywea kimya kimya.
Ili kudhihirisha kuwa John Magufuri ni mtu imara na jasiri(kama watu wengi wanavyoamini), huu ni wakati wake sasa kujiuzuru ili kulinda 'heshima' yake kisiasa na kijamii kuhusu dhana ya uwajibikaji.