Makame: Operesheni Sangara 'ruksa'
Jackson Odoyo
MWENYEKITI wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Lewis Makame amekiruhusu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuendelea na mikutano yake ya kampeni zake za Operesheni Sangara mkoani Mbeya ili zisiathiri harakati za uchaguzi wa ubunge unaoendelea katika mkoa huo.
Chadema haishiriki kwenye kinyang'anyiro cha uchaguzi mdogo wa kiti cha ubunge cha Mbeya Vijijini baada ya mgombea wake, Sambwee Shitambala kuenguliwa na tume ya uchaguzi kutokana na mapungufu yaliyogundulika kwenye kiapo chake.
Hata hivyo, chama hicho kilisema kuwa kitaendelea na mikutano ya Operesheni Sangara, ambayo lengo lake limekuwa likielezewa na chama hicho kuwa ni kufagia ufisadi na kurejesha maadili ya taifa ambayo yamepotezwa na baadhi ya watu wenye ubinafsi.
Akizungumza na Mwananchi jana jijini Dar es Salaam, mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Lewis Makame alisema operesheni Sangara haihusiani kabisa na uchaguzi kwa sababu chama hicho hakina mgombea katika uchaguzi huo.
Mikutano ya Chadema haiwezi kuathiri hali ya kampeni za uchaguzi kwa sababu Chadema haina mgombea na sheria za uchaguzi hazizungumzii chama ambacho hakihusiki katika uchaguzi, hivyo wao wako huru kuendelea na ratiba yao kama walivyoipanga, alisema Jaji Makame.
Moja ya kanuni za tume ya uchaguzi ni kusimamia vyama vinavyoshiriki katika kampeni hadi siku ya uchaguzi na moja ya mambo tunayoyatazama wakati huo, ni mahusiano baina ya vyama vinavyoshiriki uchaguzi. Endapo msuguano kati ya vyama hivyo utajitokeza, tume ya uchaguzi inaweza kuviita kwa ajili ya usuluhishi.
Mwenyekiti huyo alitoa kauli hiyo siku moja baada ya katibu mkuu wa Chadema, Dk Wilibrod Slaa kusema kuwa wataendelea na ratiba yao ya Operesheni Sangara kwa sababu walishaanza harakati hizo mapema hata kabla ya uchaguzi huo kuwepo.
Hata hivyo, kauli ya Dk Slaa ilionekana kuongeza wasiwasi kwa baadhi ya wanachama kwamba, mikutano yao ya kampeni ingekosa baraka za tume wakati huu ambao vyama vinavyoshiriki vinaendelea na kampeni za kunadi wagombea wao.
Kuhusu suala la vurugu kutokea wakati wa kampeni hizo ama kuwepo kwa malalamiko kuhusu kampeni za Operesheni Sangara, Jaji Makame alisema sheria na kanuni za tume yake haziwezi kutumika katika vurugu baina ya vyama visivyo shiriki katika uchaguzi na vile vinavyoshiriki bali watakaohusika katika vurugu hizo hushughulikiwa na Jeshi la Polisi.
Sisi tunasimamia kampeni za uchaguzi, hatusimamii vurugu wala kampeni za Operesheni Sangara. Hiyo ni kazi ya polisi; ndio wenye jukumu la kuhakikisha kwamba, vurugu hizo hazitokei na endapo zitatokea wataamua sheria ichukue mkondo wake au la, aliongeza mwenyekiti huyo.
Alifafanua kuwa kutokana na maandalizi mazuri waliyofanya katika uchaguzi huo wa Mbeya Vijijini, ana hakika shughuli za kampeni zitafanyika vizuri na hatimaye uchaguzi utafanyika katika tarehe iliyopangwa.
Hata hivyo, Jaji Makame alipoulizwa kwamba maamuzi ya tume yake kuiondoa Chadema katika uchaguzi huo yanafanana na maamuzi ya aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Kenya, Samuel Kivuitu alingaka na kusema:
Sitaki uniulize maswali ya kipuuzi na wala sitaki unifananishe na Kivuitu kwa sababu Kivuitu ni wa Kenya na mimi ni Jaji Makame wa Tanzania na Tanzania si Kenya, hivyo naomba usitishe maswali ya aina hiyo.
Nina kuomba uniulize maswali yanayohusiana na uchaguzi wa Mbeya na si vinginevyo ama ulitaka tuipendelee Chadema ndipo ujue tumetenda haki."
Source:
Mwananchi Read News