SoC03 Ofisi za kazi mkoa tatueni kero hizi wanazopitia wafanyakazi wa viwandani

Stories of Change - 2023 Competition

Lidafo

JF-Expert Member
Sep 26, 2019
551
747
Viwanda ni katika sekta zinazotoa ajira nyingi sana kwa wananchi, Sekta hii ni ya muhimu katika ukuaji wa uchumi , Nikiwa kama mdau ambaye nimefanya kazi viwandani nathibitisha hilo kuwa viwanda vinatoa ajira kwa watanzania wengi.

Pamoja na umuhimu huo, Kwa muda ambao nimefanya kazi viwandani nimebaini ya kuwa viwanda ni katika sekta ambazo zina malalamiko mengi yasiyo fanyiwa kazi, Nitaeleza baadhi ya mambo yanayoendelea huko ili wahusika waweze kuyafanyia kazi.

Ofisi za kazi mkoa fanyieni kazi mambo haya ambayo sio tu nimeyashuhudia yakifanyika viwandani lakini pia mimi binafsi yamenitokea na hivyo naeleza mambo ambayo na uhakika nayo.

Matusi na udhalilishaji.

Imekuwa ni tabia ya kawaida kwa viongozi wa viwandani kutukana na kudhalilisha wafanyakazi hasa hawa raia wa kigeni kutoka nchini india wengi wao wanadhalilisha sana watanzania kwa matusi, Dharau na kejeli. Ifahamike kuwa kazi za viwandani ni kazi kama kazi nyingine hivyo basi misingi na maadili ya kazi ni muhimu kuzingatiwa muda wote.

Uachishwaji kazi usiofuata utaratibu.

Sio jambo la kushangaza kwa viwanda vingi mfanyakazi kuachishwa kazi pale ambapo mwajiri atajisikia pasina kutoa sababu za msingi, Hii inatokana na wafanyakazi wengi wa viwandani kufanya kazi bila kuwa na mikataba jambo ambalo linampa mwajiri nafasi ya kuamua anavyotaka.

Usalama mdogo makazini.

Usalama wa kiafya kwa wafanyakazi wengi ni tatizo, viwanda vingi vianatumia kemikali ambazo ni hatari kwa afya, Matumizi ya kemikali hayaepukiki viwandani. Hivyo ni wajibu wa kiwanda kujali afya za wafanyakazi kwa kuwa na vifaa kinga vitakavyosaidia kuzuia madhara ya kiafya jambo ambalo ni muhali na kama linafanyika ni kwa kiwango kidogo sana au kwa kutumia vifaa kinga visivyokuwa na viwango. Mfano unakuta mfanyakazi anafanyakazi katika ghala la kuhifadhia vitambaa katika viwanda vya nguo lakini barakoa aliyenayo ni ya kitambaa tena inayoruhusu vumbi kuingia.

Katika Viwanda vinavyotumia kemikali Mfano kiwanda cha A to Z Arusha – Kisongo kimekuwa kikilalamikiwa sana juu ya uchafuzi wa mazingira kwa kutiririsha maji machafu maeneo ya makazi ya watu, Hali hii inaleta wasiwasi mkubwa juu ya usalama wa wafanyakazi waliopo ndani.

Utitiri mkubwa wa Raia wa kigeni viwandani.

Ni ukweli kuwa wamiliki wengi wa hivi viwanda vikubwa ni raia wa kigeni hasa wahindi, Nimejaribu kufuatilia suala hili na kubaini ya kuwa wengi wa raia wakihindi wanakuja Kufanya kazi Tanzania kwa kibali cha kuja kufundisha kazi watanzania kisha watanzania wakijua wao hutakiwa kurudi kwao na kuacha nafasi ile kwa wazawa, Jambo ambalo sio kweli kwani wengi huja kufanya kazi moja kwa moja na hufanya kazi ambazo Mtanzania wa kawaida anaweza kuzifanya jambo hili linaondoa dhana nzima ya kutoa ajira kwa wazawa, Kwani kazi nyepesi za kufanywa na watanzania wanapewa raia wakigeni, Ofisi za kazi na idara ya uhamiaji jaribuni kufuatialia jambo hili la utitiri wa raia wa kigeni ili muweze kuzilinda kazi za wazawa.

Je Wafanyakazi wa viwandani wanachukuliaje kero hizi?

Katika muda niliofanya kazi viwandani nimegundua kuna shida kubwa ya wafanyakazi wengi wa viwandani kutokujua haki zao hivyo madhila yanapo wafika hawajui wapi waanzie na wapi wakalalamikie shida zao.

Wengi huwa wanajua sehemu ya kwenda kutoa taarifa ni kituo cha polisi pale wanapofikwa na shida tajwa hapo juu, Hata hivyo sio wafanyakazi wote wanaothubutu kutoa taarifa polisi kwani wengi huogopa watakapoenda kutoa taarifa polisi huishia kufukuzwa kazi na uongozi wa kiwanda kumalizana na askari polisi hapa rushwa hutumika kuzima kesi.

Hali hii hupelekea wafanyakazi wengi kuogopa kupaza sauti ukizingatia hata maafisa kazi wanapokuja viwandani huishia kuongea na uongozi pasina kukutanana na wafanyakazi ili waweze kueleza kero zao hii inawafanya wafanyakazi wengi kukosa pa kukimbilia na wenye kushidwa kuvumilia kabisa kero hizo huamua kuacha kazi huku wakiacha tatizo likimea na kukita mizizi.

Hivyo basi kwa ujumla ninaweza kusema kuwa, Wafanyakazi wengi wa viwandani wanachukulia kero hizi kama kero sugu na zisizoweza kutatuliwa.

Kipi Kifanyike kukabiliana na matatizo hayo?
  • Elimu iwafikie wafanyakazi huko viwandani.
Ofisi ya waziri mkuu Wizara ya kazi, Ofisi za kazi mikoa wasiishie tu kukaa maofisini kusubiri malalamiko yawafanyakazi bali waandae mipango kazi wezeshi ya kuwafikia wafanyakazi huko katika viwanda na kuwapa elimu kuwa, Wana haki ya kuwa na mikataba, Haki ya kuthaminiwa na kusikilizwa kama wafanyazi.

Njia hii itawafungua macho na kuongeza hari kwa wafanyakazi na hivyo kuwa na mazingira rafiki kati ya mwajiri na mwajiriwa, Elimu ambayo wanatakiwa kupewa wafanyakazi ni pamoja na wapi wafikishe malalamiko yao na hatua zipi wanapaswa kuchukua katika kukabiliana na manyanyaso kazini.

  • Kuwachukulia hatua wote wenye kufanya vitendo vya uvunjaji haki viwandani.
Taarifa zinaweza fikishwa mahala husika lakini zisifanyiwe kazi hii pia ni kasumba ambayo mamlaka zetu zinazo , Hapa ni suala la maafisa kazi kuamua kwa dhati kukomesha udhalimu unaofanywa kwa wafanyakazi wa kitanzania. Kuwachukulia hatua ni pamoja na kuwafutia vibali vya kazi wafanyakazi wote wa kigeni wanaonyanyasa wazawa, Lakini kuwafikisha katika vyombo vya sheria watanzania wanao nyanyasa watanzania wenzao maeneo ya kazi.

Hitimisho

Suala la kukomesha manyanyaso kazini sio suala la Kuachia ofisi za kazi tu bali ni suala la uongozi wa serikali kwa ujumla kuanzia mawaziri wenye dhamana, Wakuu wa mikoa, Wakuu wa wilaya, Mamlaka za mazingira na usalama kazini kama NEMC na OSHA pamoja na asasi za haki za binadamu kwa pamoja kudhamiria kuwepo kwa mazingira rafiki ya ufanyaji kazi viwandani.

Mwisho nitoe rai kwa wafanyakazi wote wa viwandani kutokaa kimya dhidi ya vitendo vya unyanyasaji, Ubaguzi na udhalilishaji viwandani wapaze sauti na kufuata taratibu za kisheria katika kudai haki zao ili kuwa na ajira zenye tija na zenye kujali utu.
 
Kwa mwenye kusoma bandiko hili tafadhali usiache kunipigia kura natanguliza shukrani
 
interesting.. nimepost bandiko lenye maudhui kama haya kabla sijaingia na kukuta tayari umepost ila utofauti upo kwenye uwasilishaji, asante kwa kuliona hilo pia
 
interesting.. nimepost bandiko lenye maudhui kama haya kabla sijaingia na kukuta tayari umepost ila utofauti upo kwenye uwasilishaji, asante kwa kuliona hilo pia
Ooh! Shukrani na hongera kwa kupaza sauti pia. That's great.
 
Back
Top Bottom