Basil Msongo
Daily News; Sunday,June 01, 2008 @00:01
Spika wa Bunge, Samuel Sitta amesema yeye si fisadi na hana hata senti moja nje ya nchi. Mbali na hilo, Sitta amesema ni vema sasa suala la mgombea binafsi likaamuriwa.
Pia alizungumzia serikali kuwasilisha mapendekezo ya Richmond pamoja na ya uchunguzi wa kashfa ya Akaunti ya Madeni ya Nje katika Benki Kuu (BoT) bungeni katika kikao kitakachoanza wiki moja ijayo.
Sitta aliyasema hayo Dar es Salaam jana alipozungumza na watendaji wakuu wa vyombo vya habari, wahariri, waandishi waandamizi, na waandishi wa habari za Bunge ikiwa ni mwanzo wa utaratibu wake wa kuzungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari kila mwezi.
Kiongozi huyo wa Bunge amesema Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali atatoa taarifa kuhusu tuhuma zinazomhusu yakiwamo matumizi mabaya ya fedha za umma. Alisema wabaya wake wamekosa hoja hivyo wameamua kumgonga kwa kutoa tuhuma za kipuuzi za kijamii ikiwa ni pamoja na kuihusisha familia yake.
Hainipi shida sana alisema Sitta na kueleza kuwa mambo hayo ni sehemu ya maisha yake. Alisema kasi ya wabaya kumtuhumu imepungua baada ya kugundua kuwa yeye si fisadi na kwamba tuhuma kuwa anatumia Sh milioni mbili kwa ajili ya tiba yake kila mwezi ni upuuzi usio na kifani.
Sitta alisema anaamini yupo katika mstari mzuri katika kuliongoza Bunge na kwamba wabunge na wananchi katika jimbo lake la uchaguzi wanamuunga mkono. Mimi sibadiliki hata kidogo
..kama tunavyoelewa katika siasa ukiwa unapika kwa kuni usiogope moshi, alisema na kuongeza kuwa katika umri wake, amepita katika changamoto nyingi.
Naamini hata wabunge wananiunga mkono, alisema Spika wa Bunge na akatoa msimamo wake pia kuhusu masuala yanayogusa maslahi ya taifa ukiwamo uamuzi kuhusu kuwapo au kutokuwapo kwa mgombea binafsi, uchunguzi kuhusu wizi wa fedha za EPA na utekelezaji wa mapendekeo ya Bunge katika mkataba wa kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond.
Sitta ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki, alisema kuna haja ya kufikiwa kwa uamuzi wa mwisho kuhusu suala la mgombea binafsi kwa kuwa limeshajadiliwa kwa muda mrefu. Tufike mwisho, tukubaliane au tusema haiwezekani, alisema katika mkutano huo wa kwanza na vyombo vya habari ulioonyeshwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha serikali, TBC 1.
Kama jambo limeamuriwa na majaji watatu, na bado hujaridhika, unaweza kukata rufaa likaamuriwa na majaji saba, alisema Sitta akizungumzia suala hilo ambalo serikali imekata rufani Mahakama ya Rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu kuruhusu mgombea binafsi katika uchaguzi.
Kuhusu Richmond, alisema atashangaa kama serikali haitawasilisha taarifa ya utekelezaji wa mapendekezo ya Bunge kuhusu mkataba huo uliozua utata na kusababisha kujiuzulu kwa mawaziri mawili pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, Februari mwaka huu.
Alisema pia anatarajia kuwa katika Mkutano wa 12 wa Bunge utakaoanza Juni 8, mwaka huu, serikali itawasilisha taarifa kuhusu maendeleo ya uchunguzi wa wizi wa fedha za umma kupitia EPA.
Spika Sitta alisema katika mkutano huo wa bajeti, atatoa uamuzi kuhusu kauli ya Mbunge Nazir Karamagi, kuwa uamuzi wa kuongeza mkataba wa Kitengo cha Makontena katika Bandari ya Dar es Salaam (TICTS) ulifanywa na Baraza la Mawaziri.
Alisema Karamagi amewasilisha ushahidi kwake, lakini isingekuwa busara kutoa maelezo ya suala hilo nje ya Bunge kwa kuwa suala hilo lilizungumzwa bungeni. Sitta alisema katika mkutano huo unaotarajiwa kumalizika Agosti 25, mwaka huu, Ofisi ya Bunge itaanza kuwadhibiti wabunge watoro wakiwamo wanaoingia kusaini asubuhi na kuondoka kisha wanarudi baadaye kuchukua posho.
Kwa mujibu wa Spika, miongoni mwa mipango yake hivi sasa ni kubadilisha jina la Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma kwa kuwa kwa sasa inahusika na mashirika yenye hisa zaidi ya asilimia 50 za serikali, lakini kuna mashirika mengine serikali ina hisa chini ya hizo.
Alisema atakapofanya mabadiliko hayo, kamati hiyo itaitwa Kamati ya Bunge ya Mitaji ya Umma. Spika pia alitetea azma ya wabunge kuongezewa mishahara akisema kuwa kiwango wanacholipwa kinajumuisha mahitaji yao yote zikiwamo gharama za usafiri na mishahara ya madereva.