Shitambala: Nimetua mzigo mzito kwa kuhama Chadema
Imeandikwa na Na Gloria Tesha; Tarehe: 17th April 2011 @ 23: Gazeti la Habari leo
VUTA NIKUVUTE ya kunyang'anyana wanachama miongoni mwa vyama vya siasa ni msingi wa kuchochea umoja wa kweli na mapambano dhidi ya maovu ili kuleta maendeleo kwa jamii husika, ikiwa dhana nzima ya hatua hiyo, imejengwa katika misingi ya utulivu.
Tanzania ni nchi iliyoridhia marekebisho ya Katiba mwaka 1992 kuruhusu mfumo wa vyama vingi, vilivyo zaidi ya 18 hapa nchini kwa sasa, kujinoa pande zote kunakoonekana hivi sasa katika CCM ni njia moja wapo ya kujiimarisha kisiasa kuanzia ngazi za vijiji na mitaa hadi Taifa.
Wakati CCM ikijivua gamba na kufanikiwa kujipanga kwa safu mpya chini ya Katibu mpya Wilson Mukama, Chadema nayo inazidisha mashambulizi kwa kutoa kauli mbalimbali zinazoonesha wazi kuwa hatua hiyo si lolote si chochote mbele yao. Hata hivyo harakati za Chadema zinaonekana kuvunjwa nguvu kwa kiasi fulani na CCM, baada ya kiungo wake muhimu wa safu ya mashambulizi, Shambwee Shitambala, kuamua kujiunga na CCM hivi karibuni.
Shitambala alikuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mbeya. Amekihama chama hicho na kundi la wanachama zaidi ya 100, akiwemo aliyekuwa Katibu Mwenezi wa chama hicho wilayani Ileje, Henry Kayuni. Mwanasiasa huyo ambaye katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Mbeya Vijijini, alidai kuwa kura zake zilichakachuliwa, alitumia ipasavyo karama yake ya siasa, kuhakikisha kuwa ushindi unapatikana katika uchaguzi mkuu uliomalizika mwaka jana, ambapo Chadema kilifanikiwa kuibuka na wabunge wawili katika mkoa wa Mbeya pekee.
Mafanikio ya Shitambala akiwa Chadema, hayakuwa kitu kwake, hasa pale alipoamua kubwaga manyanga na kuondoka katika chama hicho. Anasema ameondoka ndani ya Chama hicho na kujiunga na CCM, kwa maelezo kuwa anaamini anaweza kufanya siasa vizuri akiwa CCM na sio Chadema. Alieleza zaidi katika mazungumzo yake na waandishi wa habari, mara baada ya kupokelewa rasmi katika chama na Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM, hivi karibuni.
Shitambala anasema, "Nimeamua mwenyewe kuja CCM, mahali ambapo nadhani ni salama na sahihi, ambako maoni yangu yanaweza kusikika na kufanyiwa kazi haraka zaidi kuliko kuwa katika chama kingine chochote hapa nchini". Katika kile alichodai anaelezea furaha yake, Shitambala anasema "Ni kama darasa, huwezi kulazimisha kusoma darasa moja miaka yote bila kumaliza au kupiga hatua nyingine, ndio maana unakuta mtu anapita madarasa mbalimbali ili kuiva na kuwa mjuzi wa jambo fulani, na mimi ndicho nilichofanya".
Anasema ameamua kujiunga na CCM bila kulazimishwa na mtu yeyote, kwa ridhaa yake mwenyewe, kwa akili zake timamu bila kushinikizwa, kupewa chochote au hata kuahidiwa jambo lolote. Anasema baada ya kukitumikia Chadema kwa miaka 13, amebaini kuwa mambo mengi yanayofanywa na hata viongozi wa chama, hufanywa kwa makusudi kwa maslahi ya wachache au ya mtu binafsi badala ya maslahi ya taifa.
"Naona Chadema wanatekeleza sera ambazo hazikuandikwa katika vitabu vya chama, wanachofanya ni kukaa katika vikao vyao vya viongozi wachache katika Kamati Kuu na kutoa matamko yanayoweza kuliangamiza taifa na kuanza kuyatekeleza bila kushirikisha chama katika ngazi nyingine", anasema Shitambala. Shitambala aliyekuwa machachari katika Chadema, kwa kuongoza mashambulizi ya kila aina kwa CCM wilayani humo, anasema yeye siku zote amekuwa akiamini katika amani na utekelezaji wa maazimio ya pamoja na si vinginevyo.
"Hata siku moja siwezi kutekeleza itikadi zisizo na maana, zinazoweza kuhatarisha amani ya taifa langu", anasema. Anasema vongozi wa juu wa chama hicho, wanakaa kwa uchache wao na kufanya maamuzi na kukibebesha chama mzigo bila kuwashirikisha viongozi wengine. KAZI KWELI KWELI NDANI YA CDM!!!! Anasema jambo hilo linawapa wakati mgumu kulijibu wanapoulizwa na wanachama wao mikoani. "Uamuzi wa kufanya maandamano haukuwa wa Chama, kwa maana ya vikao vilivyoshirikisha viongozi kutoka mikoani, kilichofanyika ni Kamati Kuu kukaa na kuja na uamuzi huo wa maandamano, ambao wamejikuta wakitumia fedha nyingi lakini wakapoteza heshima kwa wananchi," anasema.
Hata ile tabia yao ya kutoka bungeni wakati rais anahutubia, nayo licha ya kuwa hawakuvunja sheria, lakini haikuwa na manufaa kwa chama kama ilivyokusudiwa na badala yake haiukuwa ustaarabu kumtukana baba yako hata kama amekosema". Anasema baadhi ya wabunge wa Chadema wamejipotezea heshima katika jamii kutokana na kujiweka kama taasisi inayoweza kufanya maamuzi yake bila kuhojiwa wala kuwashirikisha viongozi wengine wa chama.
Anaongeza kuwa tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu, Chadema inaongozwa na kutolewa maamuzi na kamati ya wabunge wake na kundi dogo la viongozi waliopo katika kamati kuu, huku wale viongozi wengine walioshiriki kukijenga chama wakiwekwa kando kana kwamba sio sehemu ya chama. Shitambala anasema licha ya kuonekana kufanikiwa katika maandamano waliyoyafanya, ukweli ni kuwa chama kimepoteza wanachama wengi, kwa kuhofia kujiingiza katika vurugu, kutokana na lugha za kichochezi, zilizokuwa zikitumiwa na viongozi katika mikutano hiyo.
"Mimi niliwaambia, tumetoa ahadi nyingi, na tumefanikiwa kupata wabunge wengi, hivyo tuanze na utekelezaji wa ahadi tulizotoa, ahadi za kuongeza madarasa katika baadhi ya shule, wanasema hawana pesa, lakini kiasi kilichotumika katika maandamano kinaweza kujenga shule nyingi na sio madarasa machache kama nilivyowashauri", anasema. Anasema maandamano yaliyofanywa na Chadema katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, yalikigharimu chama fedha nyingi, lakini yamekipotezea heshima na kujipunguzia wanachama wengi, hasa wale makini na wanaoelewa mambo.
"Binafsi sikupenda mpango ule wa maandamano, siamini harakati za namna ile katika nchi iliyotulia kama hii", anasema Shitambala. Anatoa mifano ya nchi zenye machafuko, kama Tunisia, Libya, Misri na Ivory Coast na kuhoji ni nani anayetaabika leo kwa faida ya nani, leo nchi ikiwa na vurugu nani atapona, ni siasa ambazo kweli sikuzipenda na sioni sababu ya kuendelea kuwa ndani ya chama ambacho sikubaliani na mikakati yake.
Akifafanua sababu za kujiunga na CCM badala ya vyama vingine, anasema "CCM ni chama sikivu, chenye sera nzuri, mfumo wake wa kiutendaji umejipanga vizuri zaidi, kwa utashi wangu nimeona ni chama kinachofaa na kitakachowavusha watanzania salama, kutokana misingi yake ya kusimamia amani, utulivu na kinachohimiza maelewano".
Jambo ambalo mwanasiasa huyo anasema hatalisahau katika maisha yake ya siasa alipokuwa Chadema ni kukosa wavumilivu. Shitambala anaamini katika uwajibikaji, kila mtu kutekeleza wajibu wake, ambapo ameitaka Chadema na Watanzania kuishi katika jamii kwa misingi ya uhuru, amani na mshikamano ili wengine wajifunze kutoka kwao, wawe na shukrani na wakubali mabadiliko.
MWENYE MACHO AAMBIWE ONA, UKWELI UNAUMA!!!!!!