Miaka 45 ya CCM ni tumaini na imani ya umoja wa kitaifa kwa Watanzania

Deogratias Mutungi

Senior Member
Oct 1, 2019
137
179
Miaka 45 ya CCM ni tumaini na imani ya umoja wa kitaifa kwa Watanzania

Deogratias Mutungi


Hii ni tafakuri fupi inayomulika kipindi cha miaka 45 ya Chama cha mapinduzi CCM katika uongozi wa kisiasa ndani ya taifa letu katika nadharia ya siasa, itikadi sambamba na kusimamia na kuenzi falsafa ya kiafrika, “mila na tamaduni za waafrika” nianze na usemi wa Kiswahili usemao “Mnyonge Mnyongeni lakini haki yake mpeni” Chama Cha Mapinduzi CCM kimekuwa na wakati mgumu wakati mwingine kwa kunyoshewa vidole na baadhi ya watanzania kuwa ni chama kilichoshindwa kuendesha dola ipasavyo lawama na mashambulizi ya udhaifu wa CCM yalishika hatamu wakati wa awamu ya kwanza, ya pili, tatu na awamu ya nne zaidi mwaka 2008 ambapo chama kiliamua kuja na kauli mbiu ya “kujivua gamba,

Aidha lawama zimeendelea kuwepo hadi sasa dhidi ya CCM, hata hivyo kisiasa ulimwenguni kote hakuna chama kilichopo madarakani kilicho salama katika kukwepa mashambulizi ya kutoridhishwa na utawala, sera na falsafa za kiuongozi, na katika ulingo wa siasa zenye mfumo aidha wa chama kimoja au vyama vingi kamwe huwezi kumridhisha kila raia, hivyo ni vigumu kukwepa lawama kwa namna yoyote ile pindi hatamu ya usukani wa dola inapokuwa mikononi mwa chama chochote kile cha kisiasa.

Kwa kutumia uhuru wetu kikatiba na demokrasia tuliyo nayo tunaweza kuishambulia CCM kadri tuwezavyo lakini linapokuja suala la kuipa sifa CCM na serikali yake kwa kutuvusha kama taifa katika dhana ya umoja wa kitaifa, sharti tusifu na kupongeza bila kupepesa hata ukope wa macho, Inawezekana kabisa yapo mapungufu ndani ya mfumo wa chama katika kusimamia na kuendesha dola kwa mantiki kuwa viongozi wa CCM ni binadamu na wala sio malaika kutoka mbinguni hivyo makosa ni jambo lisilo kwepeka hata kidogo, hulka za kukosoa ni za kila binadamu aliye hai Japo uwa vigumu kwa binadamu huyo kujikosoa mwenyewe kabla ya kukosoa maasimu wake kisiasa na kijamii.

Chama Cha Mapinduzi CCM kimefanikiwa sana katika ujenzi wa falsafa ya “Umoja wa Kitaifa na kuimiza uzalendo kwa watanzania” ndipo usemi wa mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni unapochukua nafasi yake kwa CCM, Ishambulieni CCM kwa vyovyote vile lakini ipeni sifa yake katika ufanisi huu wa Amani, utu na uzalendo ulio tamalaki miongoni mwa jamii ya Watanzania, tafakuri hii fupi inadriki kukiri wazi kuwa amani tuliyo nayo kama taifa ni kwa sababu ya chama cha mapinduzi kuwa nguzo ya kuilinda na kuisimamia kupitia dola, kwa mantiki kuwa ndicho chama dola chenye wajibu wa kulinda amani na haki kwa watanzania wote bila kujali utofauti wa itikadi zao.

Aidha katika ukanda wetu huu wa Afrika Mashariki na kati Tanzania imekuwa ni kioo cha dhahabu katika dhana ya amani, utu na uzalendo, hata hivyo si kwa ukanda huu tu bali kwa Afrika nzima Tanzania ni taifa lenye heshima ya pekee katika taswira ya amani ulimwenguni, Katibu Mkuu wa zamani wa umoja wa mataifa na mshindi wa tuzo ya nobel Kofi Annan aliwahi kuisifia Tanzania chini ya serikali ya CCM kuwa taifa lenye upekee wa amani ndani ya mataifa ya Afrika, unaposimulia pongezi kutoka kwa viongozi wa kidunia uwezi kusita kuipa sifa CCM kama chama dola.

Hapa Afrika vyama vingi vya kisiasa vimekosa dira ya kuifadhi amani na utulivu ndani ya mataifa yao na hivyo kupelekea chuki na ukiukwaji wa haki za binadamu kwa wananchi wao vitendo ambavyo upelekea wananchi kuwa wakimbizi nje ya mipaka ya nchi zao, tunayo mifano ya wazi kwa mataifa kama Rwanda, Burundi, Liberia, Sierra leone, Sudan, Somalia na kwingineko lakini kwa Tanzania chini ya CCM imekuwa ni tofauti kabisa na mataifa hayo.

Aidha Amani ndio tunu ya maisha ya mwanadamu yaliposimama, bila amani dunia haiko sawa, Mwandishi wa kitabu cha “Ufilosofi wa amani na uzima wa umma” aitwaye David Swanson anaelezea kwa kina umuhimu wa amani katika ulimwengu huu ambao binadamu tunaishi, Muktadha wa mwandishi Swanson katika kitabu chake cha amani naulinganisha na mantiki ya Chama Cha Mapinduzi CCM kutambua thamani ya amani kwa raia wake na hivyo kutuvusha hadi sasa kama nchi tunapojivunia kuwa taifa la mfano kwa Afrika na ulimwenguni kote.

Kwa nukta hiyo tafakuri hii inahitimisha kwa kutoa pongezi kwa Chama Cha Mapinduzi CCM kwa jitihada zake za kuendelea kuisimamia na kuilinda amani ya taifa letu ndani ya uhai wake wa miaka 45, Rai ya tafakuri hii ni kuomba falsafa hii ya kuitetea na kuilinda amani iendelee kwa wivu wote bila kukengeuka kwa namna yoyote ile kwa tija ya kizazi cha sasa na hapo badae.

dmutungid@yahoo.com

 
Back
Top Bottom