Hotuba ya Rais Dkt. Hussein Mwinyi Katika Kutimiza Mwaka Mmoja wa Awamu ya Nane ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar | Novemba 6, 2021

The Sheriff

JF-Expert Member
Oct 10, 2019
610
1,770
Hotuba ya Rais Mwinyi

mheshimiwa Othman Masoud Othman; Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla; Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar,

Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid; Spika wa Baraza la Wawakilishi,

Mheshimiwa Jaji Khamis Ramadhan Abdalla, Kaimu Jaji Mkuu wa Zanzibar,

Waheshimiwa Viongozi Wakuu Wastaafu,

Mheshimiwa Dkt Jakaya Mrisho Kikwete Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mheshimiwa Dkt Amani Abeid Karume Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi

Mheshimiwa Dkt Ali Mohamed Shein Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi

Mheshimiwa Dkt Mohamed Gharib Bilal Makamu wa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais Mstaafu wa Zanzibar

Wajumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa,

Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa,

Waheshimiwa Mawaziri,

Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya, 3 Mhandisi Zena Ahmed Said;

Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi,

Makatibu Wakuu na Watendaji Mbali Mbali wa Serikali,

Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama wa SMT na SMZ,

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Magharibi Kichama. Viongozi wote wa vyama vya Siasa Mliopo,

Viongozi wa Dini, Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika mbali mbali ya Kimataifa,

Waheshimiwa Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi,

Wafanyabiashara, Wawekezaji na Wajasiriamali Mliopo,

Ndugu Wageni waalikwa na Wanahabari,

Mabibi na Mabwana, Assalamu Alaikum

UTANGULIZI
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, 4 Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa kutujaalia afya njema na kutuwezesha kukutana siku ya leo kuadhimisha kutimia kwa mwaka mmoja wa uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane tangu ilipoingia madarakani tarehe 2 Novemba, 2020. Mkutano huu una lengo la kuelezea changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali kwa kipindi cha mwaka mmoja. Nitazungumzia mwelekeo wa mipango ya Serikali katika kipindi hiki na kijacho kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya CCM, Ahadi tulizozitoa katika Kampeni za Uchaguzi mwaka 2020, MKUZA III, Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050 pamoja na mipango mingine ya maendeleo ya Kikanda na Kimataifa. Kaulimbiu ya maadhimisho haya ni: ‘Neema ya Amani na Umoja wetu, Safari ya Ujenzi wa Uchumi Mpya Inaendelea.’

KUMBUKUMBU YA VIFO VYA VIONGOZI
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Kabla sijaendelea, nachukua fursa hii kuwakumbuka Viongozi wetu wakuu waliotangulia mbele ya haki. Tunamkumbuka Dk. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyefariki tarehe 17 Machi, 2021. Kadhalika, tunamkumbuka Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar aliyefariki tarehe 17 Februari, 2021. Mwenyezi Mungu awape malazi mema Viongozi wetu hawa pamoja na Wazee wetu, ndugu, jamaa, marafiki na Watazania wote waliotangulia mbele ya haki. Amiin.

UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA SERIKALI
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, 5 Nakishukuru sana Chama changu cha Mapinduzi kwa kuniridhia na kunipa ushirikiano mkubwa katika kuitekeleza dhamira yangu ya kuongoza Serikali ya Awamu ya Nane yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa. Kadhalika, natoa pongezi na kukishukuru kwa dhati Chama cha ACT- Wazalendo kwa kukubali kushiriki katika uongozi wa Serikali kwa lengo la kuwatumikia wananchi na kuendeleza maridhiano na umoja wa Kitaifa. Aidha, Nampongeza kwa dhati Mheshimiwa Dkt Ali Mohamed Shein Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar kwa uongozi wake thabit wa Chama chetu na kuisimamia utekelezaji wa Ilani yetu ya CCM ya mwaka 2020 - 2025. Vile vile, navishukuru vyama vyote vya siasa vinavyoendelea kutuunga mkono katika kuyafikia malengo ya kuanzishwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar. Dhamira hii ya vyama vyote kuwa tayari kufanyakazi pamoja kwa maslahi ya wananchi wa Zanzibar, ndiko kulikopelekea katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Awamu ya Nane kufanikiwa sana katika kusimamia amani umoja na mshikamano.

TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA SHUGHULI ZA SERIKALI
Lazima nikiri kwamba Serikali ya Awamu ya Nane iliingia madarakani katika kipindi kigumu sana kiuchumi. Kipindi ambacho nchi yetu ilikumbwa na mdororo wa kiuchumi uliosababishwa na athari za maradhi ya UVIKO - 19. Hali hii si ya Zanzibar tu, bali ni ya dunia nzima, lakini Zanzibar iliathirika zaidi kutokana na utegemezi mkubwa wa uchumi wetu katika sekta ya utalii. 6

CHANGAMOTO ZA KIUCHUMI
Uchumi wa dunia ulianza kutetereka mara tu baada ya kutangazwa rasmi mripuko wa maradhi ya UVIKO - 19 mwezi Disemba 2019. Kama mnavyofahamu miongoni mwa sekta zilizoathirika sana ni sekta za utalii, usafiri wa anga na sekta nyengine za huduma ambazo ndizo nguzo kuu za uchumi wa visiwa, kama ilivyo Zanzibar. Katika kipindi cha mwaka 2020 kasi ya ukuaji wa uchumi wa Zanzibar iliporomoka hadi asilimia 1.3 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 7.7 ya mwaka 2019 kabla ya kuingia UVIKO -19. Kwa upande wa utalii, Idadi ya watalii waliongia nchini imepungua kwa asilimia 51.6 kufikia watalii 260,644 mwaka 2020 kutoka watalii 538,264 mwaka 2019 Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 95% ya hoteli zilizopo Zanzibar zenye nyota kuanzia moja hadi tano zilifungwa au kupunguza shughuli za uendeshaji kuanzia mwaka 2020 na kupelekea kupunguzwa wafanyakazi kwa zaidi ya asilimia 90.

Kama tunavyojua kuwa maendeleo ya sekta ya utalii yamefungamana sana na maendeleo ya ukuaji wa sekta nyengine hapa kwetu. Kwa hivyo, kuanguka kwa utalii na kufungwa hoteli kuliathiri sekta ya kilimo, uvuvi, ufugaji, usafiri wa anga na nchi kavu, biashara na maendeleo ya makundi mbali mbali ya wajasiriamali. Hali hii imeleta mdororo wa uchumi wa nchi yetu na kupungua kwa kiasi kikubwa mzunguko wa fedha katika uchumi wetu. 7 Kwa upande wa viwanda vya uzalishaji wa bidhaa za vinywaji laini (Maji, maziwa na juisi), na bidhaa asilia zinazotokana na mwani, na zile za kutunza afya ya ngozi na mwili, mauzo yake yaliporomoka kwa zaidi ya asilimia 90 kutokana na kupunguwa kwa mahitaji sokoni kulikosababishwa na kufungwa kwa mahoteli.

Aidha, takwimu zinaonesha kwamba, uingizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi ulipungua kwa asilimia 44.2 kufikia Dola za Kimarekani 11.1 milioni mwaka 2020, ikilinganishwa na Dola za Kimarekani 19.9 milioni katika kipindi kama hicho mwaka 2019. Kwa upande wa Usafiri wa Anga, idadi ya Ndege za Kimataifa ilishuka hadi kufikia 605 mwaka 2020 kutoka 1,834 mwaka 2019, wakati ndege za ndani zilishuka hadi kufikia 2,563.4 mwaka 2020 kutoka 4,632 mwaka 2019. Kwa hivyo, makusanyo ya mapato ya uwanja wa ndege yamepungua kwa zaidi ya asilimia 80 na kupelekea Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar kushindwa kumudu huduma zao za msingi. Mapato ya Mamlaka yalishuka katika mwaka 2020 hadi kufikia TZS bilioni 9.1 kutoka TZS bilioni 19.2, mwaka 2019 sawa na asilimia 47.4.

Hali hii ilipelekea Serikali kulazimika mpaka kulipa mishahara ya Mamlaka hiyo. Kutokana na athari hizo za kiuchumi, maisha na kipato cha wananchi kimeathirika, kutokana na ongezeko la bei za bidhaa, ambalo limechangiwa na upandaji wa bei za bidhaa hizo tunazoziagiza kutoka nje ya nchi, hasa bidhaa za vyakula na nishati ya mafuta. Kupanda kwa bei ya nishati ni changamoto kubwa kwetu kwa wananchi na uchumi wa 8 nchi kwa jumla. Hali hii ya upandaji wa bei za vyakula na nishati za mafuta inapelekea kupanda kwa mfumko wa bei katika nchi. Kwa ujumla changamoto za kiuchumi na kijamii zilizosabishwa na maradhi ya UVIKO - 19 ni nyingi. Hizi nilizozibainisha ni baadhi ya mifano tu. Hatuna muda wa kutosha wa kueleza changamoto zote hizo. Hivyo ieleweke kwamba hali hii ndio iliyosababisha kupanda kwa gharama za bidhaa, kupungua kwa mzunguko wa fedha katika uchumi na kuongezeka kwa mfumko wa bei. Mambo ambayo yanapekelekea kuwepo kwa ugumu wa maisha.

MAFANIKIO YALIYOPATIKANA KATIKA KIPINDI CHA MWAKA MMOJA WA SERIKALI KWA SEKTA MBALI MBALI AMANI, UMOJA NA MSHIKAMANO
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Katika kipindi cha mwaka mmoja wa Uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane, nchi yetu imefanikiwa sana katika kuisimamia, kuiendeleza na kuidumisha misingi ya Amani, Umoja na Mshikamano. Mambo hayo ndiyo msingi mkuu utakaotuwezesha kufanikisha azma yetu ya kukuza uchumi, kuimarisha huduma za jamii na kuhamasisha Uwekezaji. Nakupongezeni ndugu wananchi kwa kuendelea kuzilinda tunu hizi za amani, umoja na mshikamano na kuhakikisha zinadumu kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho. Kadhalika, navipongeza vyombo vyetu vya 9 Ulinzi na Usalama vya SMT na SMZ kwa kuhakikisha nchi yetu pamoja na mipaka yake iko salama. Serikali itaendelea kuchukua hatua katika kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa na amani na utulivu kwa kushirikiana na wananchi na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama.

SEKTA YA UCHUMI
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Pamoja na changamoto zilizojitokeza ukuaji wa uchumi wetu umeanza kuimarika. Hili limechangiwa na kuimarika kwa ukuaji wa kasi ya uchumi wa dunia. Takwimu zinaonesha kuwa katika robo mbili za mwanzo za mwaka huu 2021, uchumi wetu ulikua kwa kasi ya wastani wa asilimia 4.35. Ni matumaini yetu kwamba hali itaendelea kuimarika zaidi na Serikali imedhamiria kutekeleza mikakati mbali mbali ya kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi wetu, kama nitakavyoilezea.

UKUSANYAJI WA MAPATO
Kwa kipindi cha Novemba 2020 hadi Septemba 2021, makusanyo yamekuwa jumla ya TZS bilioni 710.84 sawa na asilimia 69 ya makadirio ya kukusanya TZS bilioni 1,023.56. Makusanyo hayo ni ongezeko la asilimia 24 ikilinganishwa na makusanyo ya TZS bilioni 572.61 kwa kipindi cha Novemba 2019 hadi Septemba 2020.

SEKTA YA UTALII NA MAMBO YA KALE. 10

Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Juhudi mbali mbali za kuifufua na kuiendeleza sekta ya utalii zimechukuliwa baada ya kuathirika kwa kiasi kikubwa na janga la maradhi ya UVIKO -19. Hivi sasa, tayari zipo Kampuni za ndege 34 zinazofanya safari za kuja Zanzibar, zikiwemo Kampuni mpya 7 zilizoongezeka mwaka huu. Juhudi zilizochukuliwa za kutafuta masoko mapya katika nchi za Ulaya Mashariki na Mashariki ya Mbali zimetusaidia sana. Tumeweza kupokea wageni wengi kutoka Urusi, Ukreini na nchi nyengine za maeneo hayo, na kuziwezesha hoteli nyingi kuwa wazi katika kipindi kigumu kwa sekta hiyo. Jumla ya watalii 330,659 wameingia nchini kwa kipindi cha Novemba, 2020 hadi Agosti, 2021, ikilinganishwa na watalii 273, 852 walioingia baina Novemba, 2019 hadi Agosti ,2020, ni sawa na ongezeko la asilimia 17. Katika maadhimisho haya ya kutimia Mwaka mmoja tumefungua na kuweka mawe ya Msingi ya miradi mitatu mikubwa ya Hoteli za Kitalii za daraja la juu zenye thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 3.15.

Kadhalika, kwa lengo la kukuza uwekezaji katika sekta ya utalii tumetangaza fursa ya kuwekeza katika visiwa vidogo vidogo, ambapo tayari jumla ya maombi 54 ya wawekezaji wenye nia ya uwekezaji katika visiwa vidogo yamepokelewa. Fursa hiyo imetolewa kwa visiwa 10 ambavyo ni Njau, Pamunda A, Pamunda B, Bawe, Kwale, Changuu, Mtumbini, Chumbe, Misali na Chapwani. 11 Kwa upande wa Mji Mkongwe, Serikali imefanya juhudi mbali mbali za utunzaji na uendelezaji wa Mji Mkongwe, ili uendelee kuwa na hadhi ya Urithi wa Kimataifa. Serikali inaendeleza kazi ya kulifanyia matengenezo jengo la Beit al Ajaib baada ya kuanguka pamoja na Makumbusho ya Kasri la Wananchi Forodhoni. Hivi sasa, kazi ya ujenzi wa kulizuwia jengo la Beit el Ajaib lisianguke inaendelea kwa kushirikiana na Serikali ya Oman ambayo imekubali kutoa jumla Dola za Kimarekani Milioni 5.93. Kazi ya matengenezo makubwa ya jengo lote inatarajiwa kuanza rasmi mwezi Februari 2022.

SEKTA ZA MIUNDO MBINU Bandari.

Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Jitihada zimefanyika katika kuimarisha mapato yanayokusanywa na Shirika la Bandari. Kabla ya Serikali ya Awamu ya Nane kuingia madarakani, makusanyo kwa mwezi yalikuwa wastani wa TZS bilioni 2.8 na faida ghafi ni wastani wa TZS Milioni 900. Hivi sasa, Shirika la Bandari linakusanya wastani wa TZS bilioni 3.3 kwa mwezi na faida ghafi ya wastani wa TZS bilioni 2. Kiwango hicho kimepanda zaidi katika mwezi wa Oktoba, 2021 na kufikia makusanyo ya TZS Bilioni 4.2 na faida ghafi ya wastani wa TZS bilioni 2.6 SEKTA YA MAFUTA NA GESI ASILIA Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Serikali imefanikiwa kutoa Zabuni ya Uchukuaji wa Taarifa za pamoja za Mafuta na Gesi Asilia kwa njia ya Mtetemo (Multi -Client Seismic Survey) kwa maeneo ya Mashariki ya bahari ya Zanzibar ambapo tayari Kampuni tatu (3) zimerejesha maombi ya Zabuni hiyo na Serikali inaendelea na 12 zoezi la kufanya tathmini kwa ajili ya kupata Kampuni itakayofanya kazi hiyo.

Hii ni hatua ya msingi ya upatikanaji wa taarifa katika maeneo hayo na kuelekea katika ugawaji wa vitalu vipya vya uwekezaji kwa ajili ya kutekeleza kwa vitendo dhana ya uchumi wa Buluu. Hatua inaendelea ya mazungumzo na Kampuni ya RAK GAS ili waendelee na hatua zilizositishwa baada ya kuzuka kwa maradhi ya UVIKO -19 Barabara Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Juhudi zimechukuliwa za kuimarisha miundo mbinu ya barabara. Serikali imeshafunga mkataba na Kampuni ya Mwananchi Engineering Construction Co. Ltd kwa ujenzi wa barabara ya Chake Chake – Wete (km 22.1) utakaogharimu TZS. Bilioni 23.5. Ujenzi wa barabara hiyo, utaanza wakati wowote kuanzia sasa. Vile vile, kazi ya upembuzi yakinifu imekamilika kwa ajili ya ujenzi wa barabara zifuatazo: Kitogani – Paje (km 11) Mahonda – Donge – Mkokotoni (km.13), Dunga -Kipilipilini – Pongwe na Chwaka Spur (km 30), Kinyasini – Kiwengwa (km.10), Kizimkazi- Makunduchi (km.13), Mshelishelini - Pwani Mchangani (km.7.5) na Muyuni – Nungwi (km12) Kadhalika, matayarisho ya ujenzi wa barabara za Wilaya na barabara za ndani zenye urefu wa km 300 yanaendelea. Hivi sasa Serikali iko hatua ya mwisho kufunga mkataba na mkandarasi wa barabara hizo, Jumla ya Dola za Kimarekani 80 bilioni zinatarajiwa kutumika katika mradi huu. Usafiri wa Barabara.

Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, 13 Usafiri wa barabarani umeimarishwa kwa kurahisisha huduma za ulipaji wa leseni za njia baada ya kuanzishwa kwa kituo cha huduma za pamoja (One stope centre) katika Ofisi za Mamlaka ya Usafiri Barabarani iliyopo Mwanakwerekwe. Awali huduma hizo zilitolewa Ofisi za Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) Mazizini na kusababisha usumbufu mkubwa. Vile vile, mapato yanayotokana na vibali vya udereva kwa wageni (Foreign driving permit) yameongezeka baada ya kuongezeka vibali kutoka 313 hadi 3,144 kwa mwezi na kupatikana kwa makusanyo TZS milioni 47.16 kutoka TZS Milioni 4.6. Aidha, katika kipindi hiki biashara ya usafiri wa Pikipiki na Bajaji umerasimishwa na kuanza kutambuliwa rasmi ili kurahisisha huduma za usafiri na kuifanya kazi hiyo ni rasmi inayochangia kodi kama usafiri mwengine. Viwanja vya Ndege na Usafiri wa Anga.

Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Jitihada zimechukuliwa katika kuimarisha viwanja vya ndege na usafiri wa anga kwa lengo la kukuza uchumi na kuimarisha sekta ya utalii. Kazi ya ukamilishaji wa ujenzi wa jengo la abiria la Uwanja wa ndege AAKIA imefikia asilimia 99, ikiwemo ujenzi wa barabara ya ndani (mita 210) inayoelekea jengo la “Terminal 3”. Aidha, kazi ya uwekaji wa taa za barabarani pamoja na uzio wenye urefu wa mita 887.5 inaendelea na inatarajiwa kukamilika hivi karibuni. Ujenzi wa uwanja wa ndege mdogo wa Kigunda Mkoa wa Kaskazini Unguja umeendelezwa kwa uwekaji wa lami nyepesi kwenye njia ya kurukia ndege (run way) urefu wa mita 1,200 na upana wa mita 40, kuweka alama za kuongozea ndege na kukamilisha ujenzi wa Ofisi katika uwanja huu. 14

SEKTA YA UWEKEZAJI
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Katika kipindi hiki cha mwaka mmoja, tumepiga hatua katika kuimarisha utendaji wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA). Tumeanzisha kituo kinachotoa huduma za uwekezaji kwa pamoja (one stop centre) zinazohusu ukaazi, vibali vya ujenzi, usajili wa kampuni, kodi na mazingira. Hivi sasa, ikiwa mwekezaji amekamilisha taratibu vizuri, anaweza kupata kibali cha uwekezaji Zanzibar ndani ya siku tatu (3). Dhamira yetu ni kuyafanya mambo hayo yote yawezekane ndani ya siku moja. Katika kutatua tatizo la upatikanaji wa Ardhi kwa uwekezaji, Serikali inaendelea na zoezi la kuandaa Benki ya Ardhi ambayo, pamoja na mambo mengine, itabainisha maeneo ya ardhi yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji. Serikali kupitia ZIPA, kati ya Novemba 2020 hadi Septemba 2021, imeidhinisha Miradi 73 ya Uwekezaji yenye mitaji ya makisio ya Dola za Kimarekani Milioni 4.17 ambayo inatarajiwa kutoa ajira 5,759 kwa wananchi. Tutaendelea kuchukua hatua zaidi za kuimarisha mazingira ya uwekezaji na vivutio ili kuhamasisha uwekezaji wa ndani na nje ili kukuza uchumi na kuongeza fursa za ajira nchini.

HUDUMA ZA JAMII SEKTA YA ELIMU
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Kwa lengo la kuimarisha ubora wa elimu ya Sekondari, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la misaada la Korea (KOICA) inatekeleza mradi wa ujenzi wa maabara katika skuli 11 Unguja na Pemba na kuwapatia mafunzo walimu. Mradi huo wa miaka mitano utagharimu Dola za Kimarekani milioni 10. Sekta ya elimu ina umuhimu mkubwa katika kuandaa nguvukazi ya Taifa. Jumla ya Dola za Kimarekani milioni 5.76 zimepangwa kutumika kwa awamu ya kwanza katika mradi wa kuimarisha ubora wa elimu ya maandalizi na msingi kupitia Washirika wa Maendeleo ya Elimu Duniani katika kuendeleza miundombinu ya elimu kwa kuzingatia mahitaji ya wanafunzi wote pamoja na wenye mahitaji maalum. Vile vile, Serikali imesaini makubaliano ya Mradi wa Shirika la Misaada la Sweden (SIDA) ili kuimarisha mazingira ya kujifunza katika Skuli za Maandalizi na Msingi. Mradi huo wa miaka mitano utagharimu USD milioni 5.4. Aidha, kwa ushirikiano na Shirika la UNICEF na Taasisi ya “Education Above All” ya Qatar, Serikali imesaini mkataba wa mradi unaogharimu Dola za Kimarekani milioni 3 wenye lengo la kuwarudisha Skuli watoto wote wenye umri kuanzia miaka 7 hadi 14 walio nje ya mfumo wa elimu rasmi. Katika kupunguza msongamano wa wanafunzi katika Skuli za Sekondari, Serikali imekamilisha mpango wa ujenzi wa Skuli tatu za ghorofa za Sekondari zenye dakhalia katika maeneo ya Gamba na Mfenesini kwa 16 Unguja na Kifundi huko Pemba. Aidha, Serikali imetiliana mkataba wa ujenzi wa dakhalia katika Skuli ya Mtule na Chwaka kwa Unguja na Tumbe Pemba kwa ushirikiano na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Korea (KOICA).

SEKTA YA AFYA
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Jitihada zimefanywa kuhakikisha huduma za afya zinazotolewa katika Hospitali na vituo vya afya vya Serikali zinakuwa bora. Katika kukabiliana na ugonjwa wa UVIKO – 19 ulioingia nchini, jumla ya watu 147,500 walioshukiwa, walipimwa virusi vya ugonjwa huu wakiwemo wasafiri 144,107. Kati ya waliopimwa, watu 3,598 waligundulika kuambukizwa na walipatiwa matibabu stahiki ambapo watu 3,299 walipona kabisa na vifo 69 viliripotiwa kwa Unguja na Pemba. Serikali imeanzisha vituo 36 vilivyoko Wilayani vyenye kutoa chanjo za UVIKO - 19 aina ya Sinovac, Johson Johson na Sputinik V. Hadi kufikia tarehe 1 Novemba, 2021 watu 68.142 tayari wameshapatiwa chanjo ya UVIKO – 19 hapa Zanzibar. Nasaha zangu kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari na kujihimu kwenda kupata chanjo kwani ni salama.

Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Jitihada zimefanywa katika uimarishaji wa miundombinu ya Hospitali ambapo Hospitali ya Abdalla Mzee inafanyiwa ukarabati wa baadhi ya maeneo ya huduma kwa ufadhili wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa 17 China ambao pia watajenga nyumba za wafanyakazi. Tayari vifaa kwa ajili ya ukarabati huo vimeshaagizwa. Aidha, Serikali imeshanunua CT Scan mpya kwa ajili ya Hospitali hiyo. Kazi ya ujenzi wa jengo la huduma za mama na mtoto katika Hospitali ya Chake Chake inaendelea na ipo katika hatua za mwisho kukamilika. Kwa upande wa Hospitali ya Makunduchi nayo imepatiwa mashine ya ‘Ultrasound’ ya kisasa na kuifanya hospitali hiyo sasa kuwa na mashine mbili (2), ujenzi wa maabara mbili zitakazotumiwa na Taasisi ya Utafiti wa Afya (microbiology na molecular) umekamilika na zitatumika kwa ajili ya kuimarisha udhibiti wa magonjwa ya binadamu.

MAJI SAFI NA SALAMA
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Sekta ya maji ni miongoni mwa sekta muhimu kwa maisha ya watu na maendeleo yao. Serikali inafanya jitihada kubwa sana za kuwaondolea wananchi adha ya ukosefu wa huduma ya maji safi na salama. Kwa kipindi cha mwaka uliopita, kwa kiasi fulani kuna baadhi ya maeneo yameanza kunufaika na juhudi hizo, jumla ya maeneo 25 yamerejeshewa huduma hiyo yakiwemo 6 Unguja na maeneo 19 kwa upande wa Pemba. Katika jitihada nyengine za kuimarisha Sekta hii, Serikali imenunua na kufunga pampu mpya katika visima vilivyokuwa vikikabiliwa na hitilafu ya pampu hizo na kusababisha kukosekana kwa huduma ya maji safi na salama katika maeneo ya visima hivyo. Jumla ya pampu na mota mpya 18 45 zimefungwa katika visima vilivyokuwa na hitilafu. Hatua hiyo imewawezesha baadhi ya wananchi kupata huduma hiyo na wanaendelea kufanya shughuli zao nyengine kwa utulivu. Serikali imeendelea kufanya upanuzi wa mtandao wa maji na kuondoa mabomba chakavu, ili huduma ya maji iweze kufika katika maeneo yote ya Unguja na Pemba.

Katika kipindi cha mwaka mmoja, jumla ya kilomita 10 za mabomba (7.3 Unguja na 2.7 Pemba) zimebadilishwa na kulazwa katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba. Serikali yenu imekuwa ikifanya juhudi kubwa za kuwapatia huduma bora na za uhakika wananchi wake ikiwemo kutafuta mikopo yenye masharti nafuu. Katika siku za hivi karibuni, Serikali imeanza utekelezaji wa Mradi wa Uhuishaji na Uimarishaji wa Mfumo wa Usambazaji Maji Zanzibar. Mradi huu unagharimu jumla ya Dola za Kimarekani Milioni 92.18 ambazo ni mkopo kutoka Benki ya Exim India. Mradi huo unatarajiwa kukamilika baada ya miezi 18 baada ya kuanza kazi rasmi.

SEKTA YA UMEME
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Katika kipindi cha mwaka mmoja, Serikali imepunguza gharama za uungaji umeme kwa asilimia 50%. Hatua hii imefanywa ikiwa ni kutekeleza dhamira njema ya Serikali ya awamu ya nane ya kuwapunguzia mzigo wananchi wa kupata huduma hii na inalenga kuwaongezea fursa wananchi wengi zaidi ya kuitumia nishati ya umeme katika kujiletea maendeleo. Kufuatia punguzo hilo, idadi ya wateja 19 imeongezeka kwa asilimia 175 ambapo kuanzia Januari hadi Septemba, 2021 wananchi wapatao 21,350 wameungiwa huduma ya umeme ambapo Unguja ni 16,932 na Pemba 4,418. Katika kipindi kama hicho mwaka 2020, wananchi walioungiwa umeme walikuwa ni 12,177. Kati ya hao Unguja ni 9,960 na Pemba 2,217. Katika hatua nyengine, Serikali imeongeza idadi ya vijiji vipya vilivyounganishwa na huduma ya umeme Unguja na Pemba. Katika kipindi hicho, jumla ya vijiji 67 vimeunganishiwa huduma hiyo ambapo kwa Unguja ni 43 na Pemba 24.

Katika hatua nyengine, Serikali inatekeleza mradi wa kujengea uwezo Shirika la umeme unaofadhiliwa na Serikali ya Norway. Miongoni mwa shughuli zitakazotekelezwa kupitia mradi huu ni pamoja na ujenzi wa laini za mkondo wa 11kV (Bambi, Dole, Kilimahewa na Maruhubi); upelekaji umeme visiwa vya Kokota na Njau (Gharama Dola za Kimarekani $456,128) na ubadilishaji wa mita zilizopitwa na wakati. Shughuli zilizotekelezwa hadi sasa ni ujenzi wa laini za usafirishaji umeme katika visiwa vya Kokota na Njau na ujenzi wa mkondo wa 11 kv.

SEKTA YA KILIMO
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Kwa kutambua umuhimu wa zao la karafuu kwa uchumi wa Zanzibar, Serikali ya Awamu ya Nane imechukua hatua za kuendelea kuwalipa wakulima bei nzuri ya zao. Kwa zao karafuu linalomaliza, serikali imelipa wakulim bei ya TZS 14,000 kwa kilo ya karafuu kavu za daraja la kwanza. Vile vile, tumefanya uamuzi wa kuwaruhusu wananchi 20 wanaoyatunza mashamba ya mikarafuu ya Serikali waendelee kunufaika nayo, badala ya Serikali kuyakodisha mashamba hayo kwa watu wengine wakati wa msimu wa karafuu. Nimefurahi kuona kwamba wakulima wakarafuu wamenufaika na hatua hizo za Serikali zenye lengo la kuliendeleza zao hilo. Kwa upande wa kilimo cha mpunga, Serikali imeendeleza mipango ya kuimarisha sekta ya kilimo ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara kwa kutumia mbinu za kisasa na kupunguza utegemezi wa mvua katika kilimo. Ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika hekta 1,524 za mabonde ya Unguja na Pemba kupitia Mradi wa Mkopo kutoka EXIM Bank ya Korea uliofikia asilimia 70. Ujenzi huo unatarajiwa kumalizika mwezi Machi, 2021 na Mradi kukamilika mwezi Aprili, 2022.

HABARI NA MICHEZO
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Serikali imeendelea kuchukua hatua za kuimarisha sekta ya habari. Idadi ya mawakala wa magazeti wa Shirika la Magazeti ya Serikali katika Mikoa imeongezeka kutoka Mikoa miwili hadi 12 ya Tanzania Bara. Hivi sasa Gazeti la Zanzibar leo linapatikana katika Mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Songea, Singida, Mwanza, Njombe, Mbeya, Iringa, Moshi, Arusha, Tanga na Morogoro. Katika uimarishaji wa sekta ya michezo, kwa mara ya kwanza Serikali imeweza kuendesha Mashindano ya Kombe la Mapinduzi bila ya kutegemea fedha kutoka Serikalini. Aidha, Timu ya Taifa ya Riadha ya 21 Zanzibar imefanikiwa kupata ushindi wa kwanza Kitaifa katika Mashindano ya Riadha ya Taifa Cup na kupata medali 30. Pia, tumeweza kuandaa Mashindano ya Judo ya Afrika Mashariki na Kati na kufanikiwa kupata medali 12. Nalipongeza Shirika la ZBC kwa kuendeleza Mashindano ya Yamle Yamle Cup. Mashindano haya yamekuwa na hamasa kubwa na chimbuko la wachezaji wazuri wanaoweza kuiwakilisha Zanzibar kutoka timu za mitaani. Aidha, natoa shukurani kwa wadhamini wote wa mashindano haya na nawapongeza washindi Timu ya Meli Nne City (Juve) kwa kuwa mabingwa wa mwaka huu.

UTUMISHI WA UMMA
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Utumishi bora wa Umma ni miongoni mwa vigezo vya Utawala bora. Serikali imekalimilisha mapitio ya Miundo ya Utumishi kwa kada mbalimbali zilizomo katika Wizara zote 16 za SMZ. Katika hili, jumla ya miundo 99 ya Maafisa, 75 ya Maafisa Wasaidizi, 33 ya Wasaidizi Maafisa na 13 ya Wahudumu imeandaliwa. Katika kurahisisha utekelezaji wa Miundo hiyo, Afisi Kuu ya Utumishi wa Umma imekamilisha zoezi la kuwapanga watumishi wa Umma katika madaraja kwa kuzingatia sifa za kielimu za kada husika na uzoefu, zoezi ambalo litapelekea kuimarika kwa maslahi ya watumishi na hivyo kulipwa mishahara kwa mujibu wa madaraja hayo. Katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wangu, nimekuwa nikiendelea kuchagua viongozi na wakuu wa Taasisi mbali mbali za Umma.

Aidha, katika uteuzi wangu nimekuwa nikiteua viongozi na wasimamizi wa Taasisi ambao awali walikuwa wakifanya kazi katika Utumishi wa Sekta binafsi. 22 Kifungu cha 12 cha Sheria ya Utumishi wa Umma namba 2 ya mwaka 2011, kimempa mamlaka Rais kuteua viongozi atawaona wanafaa kwa lengo la kuongeza ufanisi, kuimarisha utendaji na utoaji wa huduma kwa jamii. Katika uteuzi wangu nimekuwa nikizingatia zaidi taaluma na uzoefu wa viongozi. Aidha, nia na madhumuni yangu katika kuteua watendaji kutoka Sekta binafsi ni kuleta mabadiliko katika kuendesha na kusimamia shughuli za Serikali ni kuimarisha utoaji wa huduma kwa jamii.

MAPINDUZI NA MUUNGANO
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Kuyalinda Mapinduzi ya Zanzibar na kudumisha Muungano wa Tanzania ni miongoni mwa majukumu ya Serikali ninayoingoza. Tumefanikiwa kufanya hivyo kwa vitendo. Tumeendeleza Mapinduzi kwa kuyaimarisha na kuyaendeleza matunda yake kwa faida ya watu wote. Vile vile, tumedumisha Muungano na kuendeleza jitihada zilizoanza kuchukuliwa na Uongozi wa Awamu zilizopita kwa kuzitatua Changamoto za Muungano. Jumla ya kero za Muungano 11 zimeweza kupata ufumbuzi katika kipindi hiki zikiwemo suala la usimamizi wa ukokotoaji wa kodi kwenye huduma za simu, Sheria za uvuvi wa bahari kuu pamoja na ucheleweshaji wa mikataba ya miradi ya maendeleo ikiwemo ya ujenzi wa barabara ya Chake chake - Wete na Ujenzi wa Hospitali ya Rufaa Binguni. Masuala haya yameshapatiwa ufumbuzi.

UFUMBUZI WA CHANGAMOTO ZA KIJAMII
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Kutokana na changamoto za kijamii nilizozibainisha, Serikali imechukua hatua mbali mbali katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita .

VITENDO VYA UDHALILISHAJI
Kuhusu suala la matukio ya udhalilishaji, Serikali imeendelea kuchukua jitihada mbali mbali ili kupunguza na hatimae kuondosha kabisa matukio hayo. Miongoni mwa jitihada hizo ni pamoja na kufanyiwa marekebisho Sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai namba 7 ya mwaka 2018 ambayo pamoja na mambo mengine imefuta dhamana kwa watuhumiwa wa makosa ya udhalilishaji Vile vile, Serikali imeanzisha Mahkama Mpya Maalum ya udhalilishaji Zanzibar mwezi Februari, 2021 na kuongeza idadi ya Majaji na Mahakimu ambapo jumla ya Majaji wa Mahkama Kuu watatu (3) na Mahakimu kumi na tano (15) wa Mikoa wameongezwa katika kipindi cha Novemba 2020 hadi Oktoba 2021.

Kadhalika, Serikali kupitia Taasisi zake mbali mbali inaendelea kuelimisha jamii juu ya namna ya kukabiliana na suala la udhalilishaji ikiwemo kuongeza muamko wa kutoa taarifa na kufika Mahakamani kutoa ushahidi. Aidha Serikali imehimiza Taasisi zinazohusika kufanya vikao vya pamoja juu ya upatikanaji wa haki za kisheria. Taasisi hizo ni pamoja na Mahkama, Idara ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Polisi, Vituo vya mkono kwa mkono na Vyuo vya Mafunzo. 24 Kwa lengo la kuongeza kasi na ubora wa uendeshaji wa Kesi, Serikali imeimarisha na kuanza utekelezaji wa Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Kesi Mahkamani (Case Management System). Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Kutokana na juhudi zote hizo, taarifa kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka zinaonesha katika kipindi cha Januari hadi Septemba, 2021 kuna jumla ya kesi 630 zilizopokelewa ambapo kesi 446 sawa na asilimia 70 zimepelekwa Mahkamani. Aidha, taarifa kutoka Mahakamani zinaonesha kwamba katika kipindi cha Februari hadi Agosti, 2021 idadi ya kesi zilizofunguliwa ni 452. Kesi zilizotolewa hukumu ni 55 na Kesi zinazoendelea ni 397.

Hata hivyo, pamoja na jitihada zote zinazoendelea kuchukuliwa katika kutokomeza udhalilishaji wahusika mbali mbali, bado tatizo lipo kwa sababu baadhi ya wananchi hawataki kutoa ushirikiano kwa vyombo vya Sheria kutokana na muhali walio nao hususan mwamko mdogo wa kutoa ushahidi Mahkamani. Lazima tubadilike na tutoe ushirikiano katika mapambano haya.

MAPAMBANO DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Katika hotuba zangu mbali mbali nimekua nikisema kuwa miongoni mwa mambo yanayonikosesha usingizi ni changamoto za udhalilishaji na matumizi ya dawa za kulevya nchini. Sambamba na kuchukua hatua 25 dhidi ya vitendo vya udhalilishaji, vile vile Serikali imechukua hatua za kupambana na dawa za kulevya toka tulipoingia madarakani. Kwa lengo la kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya na kupata ufanisi zaidi, Serikali ipo hatua za mwisho za kuifanyia mabadiliko Sheria Namba 9 ya mwaka 2009 kuhusu dawa za kulevya ambayo ilihusu zaidi kuratibu na huduma za kinga. Tayari mswada wa Sheria mpya ya kudhibiti dawa za kulevya imeshaandaliwa na inatarajiwa kukamilika mwezi wa Disemba 2021. Miongoni mwa mambo ya msingi ambayo yamezingatiwa katika Sheria mpya ni kuanzishwa kwa Mamlaka kamili ya kupambana na dawa za kulevya badala ya Tume.

Vile vile, sheria hio inaipa nguvu taasisi hii za kukamata, kuchunguza na kupeleka Mahakamani washukiwa wa dawa za kulevya. Kufuatia mabadiliko yaliyofanywa yakiwemo ya uongozi katika taasisi hii, mafanikio yamepatikana ikiwemo jamii kuwa na mwamko mkubwa na uthubutu wa kutoa taarifa kuhusu dawa za kulevya hali ambayo imepelekea jambo hili kufanywa kwa uficho zaidi kuliko ilivyokuwa kabla. Kazi za uratibu wa kudhibiti dawa za kulevya imezidi kupata mafanikio kwa ushirikiano na taasisi mbali mbali. Kati ya Januari hadi Septemba, 2021, jumla ya kesi 393 za dawa za kulevya zimepelekwa Mahakamani ikilinganishwa na kesi 341 katika kipindi kama hicho mwaka 2020. Idadi hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 13.23. Ujenzi wa kituo cha marekebisho kwa waathirika wa dawa za kulevya Kidimni Unguja umefikia asilimia 60. Jumla ya vijana 50 wakiwemo 25 26 wanawake na 25 wanaume wanatarajiwa kukitumia kituo hicho na kupatiwa mafunzo ya amali. Eneo la kujenga kituo kama hicho lenye ukubwa wa ekari sita (6) limepatikana Kangagani huko Pemba mipango ya ujenzi wake inaendelea.

ATHARI ZA MABADILIKO YA TABIANCHI NA UHARIBIFU NA UCHAFUZI WA MAZINGIRA

Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,

Jitihada mbali mbali zimechukuliwa na Serikali katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Ukuta wenye urefu wa mita 350 umejengwa ikiwa ni sehemu ya ukuta na mita 500 uliokusudiwa kujengwa, katika ukanda na ufukwe wa pwani ya Msuka Magharibi kisiwani Pemba kwa lengo la kuzuia kuendelea kwa athari za mabadiliko ya tabianchi. Vile vile, katika kusimamia matumizi bora ya fukwe za bahari, maeneo 23 yamefuatiliwa, kusafishwa na baadhi yao yamepandwa mikoko. Katika kudhibiti uharibifu na uchafuzi wa mazingira katika maeneo yenye kuhusika na uchimbaji wa mchanga, mawe na kifusi, kaguzi za mara kwa mara zinafanyika kwa lengo la kuzuwia uchimbaji holela wa rasilimali hizo. Jumla ya maeneo matano ya mchanga na mawili ya kifusi yamekaguliwa na kuruhusika kuchimbwa rasilimali hizo yakiwemo Donge Kipange, Donge Mchangani, Panga tupu, Zingwezingwe na Matetema yameruhusiwa kuchimba mchanga. Maeneo ya kuchimbwa kifusi ni Jendele na Fumba. Mafanikio yameendelea kupatikana nchini katika juhudi za kudhibiti, uingizaji, biashara na matumizi ya mifuko ya plastiki. Licha ya juhudi zinazochukuliwa, bado kuna wafanya biashara wanaoingiza na kuuza 27 mifuko hiyo. Katika kipindi hiki jumla ya tani 2.8 za mifuko ya plastiki zimekamatwa na watu 104 kufikishwa katika vyombo vya sheria. Kiwango hicho ni kidogo kabisa ikilinganishwa na hali iliyokuwa nyuma. Vile vile, jumla ya kesi 32 zinazohusiana na uchafuzi wa mazingira zimeshughulikiwa. Kadhalika, katika kuhakikisha miradi ya kiuchumi na maendeleo inayoanzishwa nchini inazingatia hifadhi ya mazingira, jumla ya miradi 46 kati ya 60 iliyopangwa kutekelezwa imefuatiliwa ili kuhakikisha inazingatia sheria na masharti ya kimazingira.

Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,

UFUMBUZI WA CHANGAMOTO ZA KIUCHUMI MATAYARISHO YA SAFARI YA MWAKA WA PILI – MIPANGO YETU YA KUCHOCHEA UCHUMI NA MATUMIZI YA FEDHA ZA MKOPO WA KUPAMBANA ATHARI ZA UVIKO -19 KUTOKA SHIRIKA LA FEDHA DUNINIA (IMF)

Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Kama nilivyobainisha awali ni kuwa utekelezaji wa mipango yetu mikuu ya maendeleo pamoja na ahadi nilizotoa wakati wa uchanguzi mkuu lakini kwa bahati mbaya sana hatukuweza kuzitekeleza kama tuliyotayarajia kutoka na athari nyingi za kiuchumi na kijamii zilitokana na kuibuka kwa maradhi ya UVIKO – 19 au Korona kama ilivyozoeleka. Hali hii imezifanya Serikali zetu zote mbili kuumiza vichwa juu ya kutafuta hatua gani za kuchukua ili kuweza kujikwamua kutoka hapa tulipo kwani wananchi wametuchagua na wakakichagua Chama Cha Mapinduzi wakijuwa kwamba kina viongozi mahiri wenye uwezo na uweledi wa kuivusha nchi yetu hata kwenye safari yenye dharuba. 28 Kwa hivyo, pamoja na umahiri mkubwa tuliotumia katika kupambana na Korona kwa kuchukua tahadhari zenye kuzingatia miongozo ya afya, ustawi wa wananchi, na maendeleo ya uchumi wetu , sasa tunaendelea kupanga na kutekeleza mikakati itakayotuwezesha kuchochea na kuimarisha kasi ya ukuaji wa uchumi wetu na maisha ya wananchi. Dhamira yetu hivi sasa ni kuona kwamba kunakuwepo na mzunguuko wa kutosha wa fedha nchini, kuanzia mikononi mwa mwananchi wetu Serikalini na katika Taasisi za fedha kwa ajili ya kuendesha uchumi na kuimaarisha maslahi ya wananchi kwa kuwapatia huduma bora. Tunataka kuona kwamba uchumi wetu unakwenda vizuri ili kuwapa imani kubwa zaidi wawekezaji bila ya kuwa na hofu ya kutopatikana kwa mzunguko wa fedha madhubuti kwa ajili ya kuendesha shughuli zao.

Katika juhudi za kujenga uchumi wa nchi yetu, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeamua kuomba mkopo wa fedha kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) kwa ajili ya kufufua uchumi wetu, Zanzibar imetengewa jumla ya fedha za Dola za Kimarekani Milioni 100 sawa na TZS 230 bilioni. Miongoni masharti ya mkopo huo, ni kwamba zitumike zaidi katika kuimarisha sekta zilizoathiriwa na janga la Korona. Kwa hivyo, kuzingatia masharti ya mikopo, kiwango hicho cha fedha kitatumika kwa ajili ya kupunguza athari za Korona kwa uchumi na maisha ya wananchi. Hata hivyo, tumeamua kwamba Mungu akipenda mwaka huu wa pili tuuanze kwa kasi zaidi, kwa kutekeleza mambo yatayotuwezesha kuchochea kasi kubwa zaidi ya ukuaji wa uchumi wetu. 29 Katika mwaka huu wa pili, tumeamua kwamba tufanye kila linalowezekana ili tuongeze makusanyo ya mapato na vile vile tumedhamiria kukopa kiwango cha fedha sawa na mkopo huo wa IMF wa TZS Bilioni 230. Fedha hizo, zitokanazo na makusanyo, na mkopo na mwengine wa TZS 210 bilioni (Hapajakaa sawa hapa sijui umekusudia nini) kutoka taasisi nyengine za fedha zitumike katika maeneo ambayo hayako katika masharti ya mkopo wa IMF. Kwa hivyo, tukifanya hivyo tutaweza kuingiza TZS bilioni 460 katika uchumi wa Zanzibar, bila ya kujumuisha makusanyo tuliyodhamiria kuongeza. Kwa zile fedha za IMF, tutazitumia kwa kuimarisha sekta ya Afya, Elimu, Maji Safi na Salama, Umeme na Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi. Ni vyema wananchi wakaifahamu vyema mipango ya Serikali yao, kwa hivyo napenda nieleze mipango yetu kwa kila sekta. SEKTA YA AFYA Ndugu Viongozi na

Ndugu Wananchi, Ili kuweza kutatua changamoto nilizozibainisha awali katika sekta ya afya na kuweza kuimarisha vyema sekta hii, tumetenga jumla ya TZS bilioni 69, zinazotokana na TZS bilioni 230 za Mkopo wa IMF. Kwa kiwango hicho, tumepanga kutekeleza miradi ya kuimarisha miundombinu ya afya ikiwemo ujenzi wa hospitali mpya ya ngazi ya Mkoa katika Mkoa wa Mjini Magharibi katika eneo la Lumumba. Hospitali hiyo itakuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 200 kwa wakati mmoja na itakuwa ya ghorofa tano. 30 Hospitali hiyo itawekwa vifaa tiba vya kisasa, ikiwa ni pamoja, CT scan, MRi, Huduma za Uchunguzi wa Maabara za Kisasa na huduma za afya za dharura. Aidha, itakuwa na uwezo wa kutoa huduma mbali mbali za kibingwa pamoja na huduma za macho na meno. Itakuwa na kliniki na wodi za kulaza wagonjwa mbali mbali kwa nia ya kuongeza wigo wa kutoa huduma bora na kupunguza idadi ya watu wanaokwenda Hospitali ya Mnazi Mmoja ambayo nayo itaendelea kuboreshwa kupitia msaada wa Benki ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu – (BADEA) ili ikidhi hadhi yake ya kuwa Hospitali ya Rufaa.

Ujenzi wa hopitali mpya ya Lumumba utagharimu jumla ya TZS bilioni 14. Ujenzi huo utaanza mara moja. Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Sambamba na hilo, Serikali imeamua kwa makusudi kutumia fedha hizo za IMF kuiboresha kwa kuipatia vifaa vya kisasa na madaktari wataalamu wa kutosha Hospitali ya Abdalla Mzee iliopo Mkoani Pemba na kuipandisha hadhi kuwa ni Hospitali ya Mkoa ili iweze kutoa huduma bora kwa wananchi wa Mkoa wa Kusini na Kisiwa cha Pemba kwa ujumla. Sambamba na ujenzi huo, Serikali itajenga hospitali 10 katika ngazi ya Wilaya zenye uwezo wa kulaza wagonjwa 100 kwa wakati mmoja kila moja, pamoja na kujenga nyumba za wafanyakazi zitakazotosha kuhudumia familia 16 kwa gharama ya TZS bilioni 22.00. Hospitali hizo zitajengwa katika Wilaya zote Unguja na Pemba isipokuwa kwa Wilaya ya Mkoani ambapo itahudumiwa na Hospitali ya Mkoa. Michoro ya Hospitali zote imekamilika na taratibu za manunuzi ili kuwapata wakandarasi wa ujenzi zitatangazwa rasmi kwa kutumia njia ya haraka ili 31 kazi iliyokusudiwa ifanyike kwa muda uliopangwa. Kazi za ujenzi wa hospitali hizi itaanza mwezi wa Disemba, 2021. Hospitali hizi zitatoa huduma za uchunguzi kwa kutumia vifaa vya kisasa (X-ray ya kijiditali, Ultrasound, na maabara za kisasa). Huduma zitakazopatikana katika Hospitali hizi ni za ICU au wodi maalum kwa wagonjwa wanaohitajia uangalizi wa karibu, magojwa ya wanawake, upimaji wa mimba, uzazi wa kawaida na huduma za upasuaji.

Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Kadhalika, Serikali itanunua gari 12 za kubebea wagonjwa (ambulances). Gari hizo zitasambazwa katika hospitali zote za Wilaya na mbili za Mkoa. Vile vile, Serikali itanunua gari 5 za kusambazia dawa katika hospitali na vituo vya afya Unguja na Pemba kutoka Bohari ya Dawa. Huduma hii itaondosha gharama zinazotumika hivi sasa za kukodi gari za kampuni binafsi kwa kufanya kazi hiyo na pia kuhakikisha usalama wa dawa na vifaa tiba vinavyosafirishwa. Aidha, Serikali itanunua mitambo ya kuchomea taka za Hospitali (Incinerators) kwa hospitali zote za Wilaya na Mikoa. Aidha, kati ya mitambo hiyo, miwili itakuwa ni yenye uwezo mkubwa wa kuchoma taka hatarishi nyingi kwa wakati mmoja na itafungwa katika hospitali za Mikoa ili iweze kutoa huduma kwa hospitali za karibu za Serikali na pia Sekta binafsi. Huduma za Damu Salama zitaimarishwa kwa kupatiwa vitendea kazi muhimu vinavyoendana na mahitaji husika ili kuweza kutoa huduma 32 muda wote, hali ambayo kwa sasa, kitengo cha damu salama hakina vifaa hivyo. Uwepo wa vifaa hivyo utaongeza upatikanaji wa damu wa kuridhisha iliyopimwa na kuwa tayari kupewa wagonjwa wanaohitaji.

Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Serikali itanunua pia mitambo miwili katika Hopsitali za Pangatupu na Abdalla Mzee ya kuzalisha gesi tiba (oxygen), kila mmoja ukiwa na uwezo wa kuzalisha mitungi 400 kwa siku, itakayotumika kwenye hospitali nyengine Unguja na Pemba zitakazohitaji huduma hii. Matarajio yetu ni kwamba faida zitakazopatikana baada ya kukamilika miradi hii ni kuwa na huduma za Afya zilizo bora karibu na wananchi. Vile vile tutaweza kutekeleza dhamira yetu ya kupunguza idadi ya wagonjwa wanaosafirishwa nje ya Zanzibar kwa kufuata matibabu. Utekelezaji wa miradi hii mikubwa ya ujenzi wa miundombinu ya afya katika Wilaya zote za Unguja na Pemba, ni utekelezaji wa dhamira yetu ya tangu Mapinduzi Matukufu ya mwaka 1964 ya kuwapatia huduma bora na sahihi za afya wananchi wetu wa Zanzibar.

SEKTA YA ELIMU
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Kwa upande wa Sekta ya Elimu, tumeamua kuelekeza jumla ya TZS bilioni 69.0, sawa na ( USD bilioni 30) ya fedha za Mkopo wa IMF kwa ajili ya kuzifanyia kazi changamoto mbali mbali zilizopo katika sekta ya elimu na kuimarisha kiwango cha elimu inayotolewa hapa nchini. 33 Kwa kutumia fedha hizo, Serikali itakamilisha ujenzi wa madarasa 425 yaliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi, Shughuli hii itagharimu jumla ya TZS bilioni 7.656. Vile vile tumepanga kujenga madarasa mapya 706 katika Wilaya zote 11 Unguja na Pemba kwa ngazi ya Maandalizi, Msingi na Sekondari. Madarasa haya yanajumuisha ujenzi wa madarasa mapya na yale ambayo yatajengwa kupitia ujenzi wa skuli mpya 35 zikiwemo skuli 22 za maandalizi (skuli 2 kwa kila wilaya) na Skuli 13 za Msingi na Sekondari Unguja na Pemba. Skuli saba (7) kati ya hizi zitakuwa ni za ghorofa na zitajengwa katika maeneo ya Mwanakwerekwe, Mtopepo, Bweleo na Kwahani kwa Unguja na Mwambe, Kwale na Makangale kwa Pemba.

Aidha, Skuli mbili zitajengwa eneo la Jendele kwa Unguja na Chakechake kwa Pemba ambazo zitakuwa ni maalum kwa ajili ya elimu mjumuisho. Maeneo mengine ya ujenzi wa skuli hizi ni Mpendae, Kipapo, Pujini na Mgelema. Ujenzi huu utagharimu jumla ya TZS bilioni 43.973. Vile vile, tumeamua kuelekeza jumla TZS bilioni 6.871 kwa ajili ya ujenzi wa vyoo 1,693 vya wanafunzi katika ngazi zote za elimu. Kadhalika, jumla ya TZS bilioni 7.898 zitatumiwa kwa kufanya ukarabati wa skuli 22, kati ya skuli zitakazofanyiwa matengenezo makubwa ni skuli ya Haile Sellasie, Chaani, Mlimani, Matemwe na Uzini kwa Unguja na Konde, Chasasa na Kiwani Mauwani kwa upande wa Pemba. Vile vile, tutanunua vikalio 8,000 (madawati ya wanafunzi watatu) kwa Skuli za ngazi ya elimu ya msingi vitakavyogharimu jumla ya TZS bilioni 2. Tutajenga jumla ya nyumba 10 za walimu katika maeneo ya visiwa 34 vidogovidogo vikiwemo Tumbatu, Uzi, Njau, Kokota na Ng’ambwa. Ujenzi huo utaghaarimu jumla ya TZS milioni 600.

Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Serikali itatumia wakandarasi wakubwa wa daraja la I, II, na III kuhakikisha ujenzi huu unakuwa wenye ubora mzuri. Taratibu za kuwapata wakandarasi hao zinaendelea ambapo Serikali inatarajia kusaini mikataba na kuanza kwa utekelezaji wa mradi kuanzia mwezi Disemba mwaka huu. Aidha, gharama zote za ujenzi kwa kila shughuli pamoja na michoro ya majengo hasa skuli mpya imekamilika. Serikali ina mategemeo makubwa ya mafanikio ya utekelezaji wa miradi yote hii na hatimae kuweza kutoa elimu bora kwa watoto wetu ambao ndio warithi wa Taifa letu. Kama nilivyoeleza imani yangu ni kwamba miradi hii ya ujenzi wa miundombinu ya elimu na afya itachochea sana mzunguko wa fedha kwa kuwa itatoa ajira kwa mafundi waashi, seramala, wahunzi Mama lishe na makundi mbali mbali sambamba na kukuza biashara hasa ya vifaa vya ujenzi vikiwemo saruji, nondo na mchanga.

SEKTA YA MAJI
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi changamoto nilizozieleza katika Sekta ya Maji Safi na Salama, tumetenga jumla ya TZS bilioni 34.2 ambazo tutazitumia kwa ajili ya kazi kuu tatu. 35 Kwanza, kuongeza uzalishaji wa maji kwa kuchimba jumla ya visima ishirini na nane (28) Unguja na Pemba. Visima hivyo vinategemewa kuzalisha jumla lita za maji 14.1 milioni kwa siku. Shughuli hii inatarajiwa kutumia TZS. Bilioni 2.1. Aidha, Serikali imejipanga kununua vifaa vya aina mbali mbali ambavyo kwa namna moja au nyengine vitasaidia katika shughuli zenye mnasaba na uchimbaji wa visima. Tumepanga kutumia jumla ya TZS bilioni 2.1. Vile vile, tutatumia jumla ya TZS bilioni 1.5 kwa ajili ya kuviendeleza visima 36 Unguja na Pemba vilivyochimbwa kupitia mradi wa Ras Al Khaimah. Visima hivyo vinategemewa kuzalisha lita za maji 15.7 milioni kwa siku.

Sambamba na hatua hizo, tutavifanyia ukarabati visima vilivyowekewa pampu zilizo chini ya kiwango. Jumla visima 49 Unguja na Pemba vinategemewa kubadilishwa pampu na kutiwa pampu zenye uwezo unaostahiki kwa mujibu wa uzalishaji au uwezo wa visima. Visima hivyo vinategemewa kuzalisha lita za maji 23.4 milioni kwa siku. Jumla ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli hii ni TZS bilioni 6.9. Vile vile, kupitia fedha hizo, tumepanga kubadilisha bomba za maji chakavu na kusambaza bomba za maji mpya kwa maeneo ambayo huduma ya maji haijafika. Jumla ya kilomita 319 zinategemewa kubadilishwa na kuboresha mtandao wa maji. Jumla ya TZS bilioni 8.2 zimepangwa kutumika kwa kazi hiyo.

Kadhalika, tumetenga jumla ya TZS milioni 210 kwa ajili ya kukarabati Matangi ya Maji kwa Unguja na Pemba ili kuongeza kiwango cha uhifadhi wa maji. Unguja matangi mawili na Pemba tangi moja, yote kwa pamoja yakiwa na uwezo wa kuhifadhi jumla ya lita za maji 3.2 milioni. Vile vile, tumetenga jumla ya TZS bilioni 12.4 kwa ajili ya ujenzi wa matangi mapya (9) yenye ujazo wa lita milioni moja kwa kila moja. Unguja matangi matano (5) na Pemba Matangi manne (4). Jumla ya lita za maji 9.2 milioni zinategemewa kuhifadhiwa katika matangi hayo. Kwa kipindi kifupi kijacho tumedhamiria kuongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 131.8 kwa siku sawa na asilimia 55 hadi lita 170 milioni sawa na asilimia 71 ya mahitaji kwa siku ya wananchi. Aidha Serikali itawezesha Zawa kununua magari mawili ya kuchimba visima – moja Unguja na moja Pemba.

SEKTA YA NISHATI
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Kwa upande wa sekta ya umeme, Serikali imetenga jumla ya TZS bilioni 11.00 kati ya Fedha za Mkopo wa IMF kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi changamoto zilizojitokeza kwenye sekta ya umeme. . Fedha hizo zitatumika kwa ajili ya kuwapunguzia gharama za uvutaji umeme wananchi Unguja na Pemba. Wastani wa wateja elfu thelathini (30,000) wanatarajiwa kufikiwa. Hii itajumuisha ujengaji wa miundombinu ya umeme mkubwa pamoja na ununuzi wa vifaa mbali mbali vitakavyotumika katika kazi hizo. Katika mpango huu, Muombaji wa 37 umeme atachangia TZS 200,000 badala ya TZS 600,000 na gharama zilizobaki zitafidiwa na Serikali. Lengo la uamuzi huu wa Serikali juu ya kupunguza gharama za uungaji wa umeme kwa wananchi ni kuwapunguzia wananchi wetu gharama hizo na kuweza kumudu huduma hiyo muhimu kwa maisha ya kila siku.

SEKTA YA UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI \
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Wakati wa Kampeni na katika ziara zangu mbali mbali nilikutana na makundi ya wajasiriamali kwa ajili ya kujadili maendeleo na kufahamu changamoto zinazowakabili. Nilikutana na makundi ya vijana, waendesha boda boda, wavuvi, mafundi gereji, wauza mbao, wafanyabiashara wa masokoni, wakulima, wauza vinyago, mama lishe, wabanja kokoto, wajane, wabeba mizigo, wafua vyuma, vibarua wa ujenzi, viwanda, jumuiya za kinamama wajane na waendeshaji wa vyombo vya moto. Nilifurahishwa sana na juhudi zao za kujituma na michango yao katika ujenzi wa nchi yetu na kuendesha familia zao. Niliahidi kuzifanyia kazi changamoto zao ambapo kilio chao kikubwa ilikuwa kukosekana kwa mitaji, masoko ya bidhaa wanazozizalisha maeneo ya kufanyia biashara zaona vituo vya kutolea mafunzo. Vile vile, nafahamu kwamba makundi yote haya yameathiriwa sana, na kuzuka kwa maradhi ya UVIKO-19, na wengine kupoteza kabisa ajira walizokuwa wakizitegemea.

Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Nina furaha kuwajuilisha wajasiriamali wote wa Unguja na Pemba kwamba tumetenga TZS bilioni 85.4 kwa shughuli za Uwezeshaji 38 Wananchi Kiuchumi. Kwa kuendelea wajasiriamali katika sekta ya Uchumi wa Buluu na sekta nyengine za uwezashaji. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kuleta mageuzi ya kiuchumi kwa kutekeleza sera na mipango ya kuendeleza uchumi wa buluu. Nimeahidi na nimedhamiria kutekeleza ahadi nilizotoa wakati wa uchaguzi wa kuwawezesha wananchi na kutafuta fedha kwa ajili ya kuendeleza sekta hiyo. Kwa hivyo katika fedha hizi za Mkopo, nimeelekeza tutumie jumla ya TZS bilioni 36.5 kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali wa sekta ya Uvuvi na Mazao ya Baharini. Kati ya fedha hizo jumla ya TZS 20,368,100,000 zitatumika kwa kuwapatia wavuvi wadogo wadogo boti 577 za kisasa zenye vifaa vyote muhimu vya uvuvi ikiwemo mitego ya kisasa ya kuvulia na majokofu ya barafu. Mpango huu utawanufaisha wavuvi wasiopungua 5,770.

Aidha, juhudi kubwa zitaelekezwa kuwapatia wananchi na wajasiriamali wapatao 31,770 vifaa vya uvuvi na ufugaji wa mazao ya baharini pamoja na usarifu wa dagaa. Aidha tumetenga jumla ya TZS bilioni 2.5 kwa kuwaendeleza wakulima wa mwani. Jumla ya boti au vihori 500 vitanunuliwa. Matumaini yetu ni kwamba jumla ya wakulima wa mwani 5,000 watanufaika na mpango huu. Kadhalika jumla ya TZS bilioni 1.7 zitatumika kununulia vifaa kwa ajili ya kuendeleza zao hilo.

Vile vile, Serikali itakamilisha ujenzi wa kiwanda cha Mwani Pemba kwa thamani ya TZS 500,000,000 kwa lengo la kusaidia katika uongezaji wa thamani ya zao la mwani ili kuongeza tija ya zao hilo. 39 Pamoja na hayo, Serikali imetenga jumla ya TZS bilioni 1.1 za kuviwezesha vikundi 100 vya ufugaji wa majongoo ya bahari Unguja na Pemba. Pia, jumla ya TZS milioni 402, zitatumika katika kuendeleza vikundi 60 vya ufugaji wa kaa na TZS bilioni 1.2 zitatumika kuwawezesha wajasiriamali wanaojishughulisha na ufugaji ambapo jumla ya vikundi 40 vitanufaika na mpango huu. Kwa ujumla, fedha zote tulizozitenga kwa kuendeleza uchumi wa buluu tunatarajia kwamba zitawanufaisha wananchi 158,850 katika mnyororo wake mzima wa thamani. Hiyo ni hatua muhimu katika kutekeleza hadi yetu ya kukuza ajira nchini.

Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Kwa upande wa sekta nyengine za kiuchumi, Serikali imetenga kutumia jumla ya TZS milioni 5.6 zimetengwa kwa ajili ya uwezeshaji wa wajasiriamali wa sekta nyengine. Uwezeshaji huu unatarajiwa kuwanufaisha wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo wapatao 101,704 wa Unguja na Pemba. Uamuzi huu umelenga kuimarisha kasi ya mzunguko wa fedha kwa kuzifufua shughuli za ujasiriamali zilizokuwa zimedororoa au kufa kabisa pamoja na kutekeleza kwa vitendo sera na mikakati yetu ya kuendeleza sekta ya uchumi wa buluu. Jumla ya TZS bilioni 4.056 zitatumika kuwanufaisha wafanyabiashara wenye viwanda vidogo vidogo, na vya kati katika sekta ya useremala, ushoni, utengenezaji wa sabuni, usindikaji wa mazao, viwanda vya kusaga nafaka na viwanda vyengine. Vile vile, Jumuiya za waendesha 40 boda boda kila Mkoa watakopeshwa, kwa kuanzia boda boda 50, kwa ajili ya vijana wa mkoa husika. Mategemeo yetu ni kwamba jumla ya wajasiriamali 2,906 walio katika makundi nliyoyataja watanufaika katika mpango huo.

Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Sekta ya kilimo na ufugaji ni miongoni mwa sekta tulizozipa kipaumbele, ambapo eneo hili litakuwa na jumla ya miradi 413. Jumla ya TZS bilioni 6.7 zitatolewa na zitawanufaisha wakulima na wafugaji wapatao 8,444. Kwa upande wa wananchi wanaojishughulisha na kazi za mikono wakiwemo wahunzi, watu wenye ulemavu, wachoraji hina, watengenezaji wa mabango, mafundi gereji na ufinyanzi, wao tumewatengea jumla ya TZS bilioni 5.075 ambazo zitawanufaisha wananchi wapatao 22,600 Unguja na Pemba. Kwa ndugu zetu wafanyabiashara wa maduka ya reja reja, jumla na jumuiya za masokoni, makundi haya yametengewa jumla ya TZS bilioni 5.2 ambapo tunatarajia kwamba zitawanufaisha jumla ya watu 950 Unguja na Pemba.

Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Vile vile, tumezielekeza jumla ya TZS bilioni 2.5 kwa ajili ya Mama lishe, baba lishe, wamiliki wa mikahawa, vijana wanaotengeneza simu, na vifaa vya umeme kama mafriji na Komputa Unguja na Pemba. Idadi ya wanufaika tunaikadiria kufikia wajasiriamali 16,000. Sehemu za fedha hizi zitatumika kujenga mazingira mazuri ya uendeshaji wa Kituo cha Kulea na kukuza Wajasiriamali na kutoa mafunzo mengine, ikiwa ni 41 pamoja kuwapatia mafunzo ya ufugaji wa nyuki jumla ya wajasiriamali 5,834 Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Serikali inaandaa maeneo maalum ya kufanya biashara kwa wajasiriamali wanaojishughulisha na biashara za ‘Garage’, Uhunzi na Welding pamoja na Mbao na Uchongaji wa Samani ili kuwawekea mazingira mazuri ya kufanyabiashara Unguja na Pemba.

MIPANGO MENGINE YA KUCHOCHEA UCHUMI
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Kama nilivyosema awali, tumeamua kukopa jumla ya TZS bilioni 230 kwa ajili ya kuimarisha sekta na maeneo mengine ambayo hayapo kwenye mipango ya matumizi ya fedha za Korona kutoka IMF. Kuendelea kufufuka kwa uchumi wa dunia na kuimarika kwa uchumi wetu hasa sekta ya utalii kunanipa imani kwamba tuna uwezo wa kuhimili mkopo huu ili tuweze kufanya mambo mengi mengine makubwa kwa wananchi. Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Fedha hizi tutakazokopa tutazitumia kuongeza mzunguko wa fedha kwa wafanyabiashara na wananchi. Katika mwaka huu wa pili wa Uongozi wangu nataka kuhakikisha kwamba tunalipa madeni makubwa ambayo Serikali inadaiwa na wazabuni, malipo ya fidia za mali za wananchi malipo ya wastafu na wafanyakazi. Malipo ya ndani hivi sasa yamefikia jumla ya TZS bilioni 68.22 Nimeamua tufanye hiyo nikiamini kwamba Serikali inapochelewesha kulipa madeni kwa wazabuni na wafanyabiashara, kwa kiasi kikubwa tunaathiri mitaji ya 42 wafanyabiashara na wazabuni na hatimae kuathiri ukuaji wa biashara na mzunguko wa fedha. Tukiwa na mipango imara ya kuyalipa madeni hayo basi shughuli nyingi za kiuchumi na kijamii zitaimarika kwani kutakuwa na kiwango kikubwa zaidi cha fedha katika mzunguko.

Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Moja ya athari kubwa iliyosababisha mzunguko wa fedha kupungua katika uchumi ni sakata la kampuni ya Masterlife. Kampuni hii ilikusanya kiasi cha shilingi bilioni 38.7 kutoka kwa wananchi wapatao 10,317 Wengi wao wakiwa ni wananchi wanyonge. Idadi hii ya watu na kiwango hicho cha fedha ni kikubwa mno kwa watu masikini na kimepelekea kundi kubwa hili la wananchi kupata matatizo makubwa ya kiuchumi. Serikali imefanya uamuzi wa kuwalipa wananchi hawa Amana walizoweka baada ya kufanya uhakiki. Lengo ni kuwasaidia wahanga hawa ambao maisha yao yameathirika sana na tatizo la kitapeli. Serikali itaendelea kukamata mali za Kampuni na za Wakurugenzi wa Kampuni hii ili kufidia fedha zitakazotolewa na Serikali. Hadi sasa kiasi cha shilingi bilioni 6.7 kimepatikana kutoka kwenye akaunti zao.

SHUKURANI
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Natoa shukurani maalum kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kunipa ushirikiano mkubwa katika utekelezaji wa majukumu yangu. Shukurani za pekee kwake kwa jitihada zake zilizotuwezesha kupata mkopo wa kupambana 43 na athari za maradhi ya UVIKO- 19 kutoka Shirika la Fedha Duniani IMF utakatuwezesha kutekeleza miradi mbali mbali niliyoitaja. Kadhalika natoa shukurani kwa Shirika la IMF kwa kukubali ombi la mkopo huu. Nawashukuru Viongozi wote wakuu walioko madarakani na Wastaafu kwa michango yao katika kufanikisha shughuli za Serikali katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Natoa shukurani zangu za dhati na pongezi kwa Makamu wa Kwanza wa Rais, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla, Mawaziri wote, Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Viongozi wa CCM, Viongozi wa vyama vya siasa, Watendaji na Watumishi wote wa Serikali kwa namna wanavyonipa ushirikiano katika kutekeleza majukumu ya Serikali.

Nawashukuru Washirika wetu wa maendeleo na Taasisi zote za Kitaifa na Kimataifa zilizotupa ushirikiano katika sekta mbali mbali ndani ya mwaka mmoja uliopita. Nathamini sana ushirikiano wao na naahidi kuendelea kufanya kazi nao kwa kipindi kinachoendelea. Vile vile, shukurani zangu ziende kwa wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutekeleza majukumu ya ulinzi na usalama ipasavyo. Nawashukuru pia viongozi wa madhehebu yote ya dini kwa kuendelea kuiombea amani nchi yetu. Shukurani pia ziwaendee es wasanii 44 Natoa shukurani maalum kwa familia yangu hususan, mke wangu Mama Mariam Mwinyi kwa kunipa ushirikiano mkubwa katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu yangu. Katika kufanikisha maadhimisho ya mwaka mmoja, natoa shukurani kwa Kamati ya Maandalizi ya Maadhimisho haya, Viongozi na Watendaji wote wa ngazi mbali mbali kwa ushiriki wao katika kufanikisha shughuli hii. Shukurani maalum nazitoa kwa wananchi kwa kushiriki kwenu katika matukio mbali mbali yaliyoandaliwa kwa ajili ya maadhimisho haya. Pia nawashukuru waandishi wa habari kwa kuwapa taarifa ya matukio haya wananchi na leo tuko nao hapa wakiwatangazia shughuli hii moja kwa moja.

HITIMISHO
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi, Kwa jumla, mambo tunayoazimia kuyatekeleza ni mengi lakini itoshe tu kwa hayo machache niliyoweza kuyabainisha kwa muhtasari. Hata hivyo, nawaelekeza Waheshimiwa Mawaziri kila mmoja kuandaa taarifa maalum ya utekelezaji wa shughuli za Wizara yake kwa mwaka mmoja na kuiwasilisha kwa wananchi, sambamba na kuelezea mipango yao ya baadae. Tunamuomba Mwenyezi Mungu aizidishie nchi yetu Amani, Umoja, Mshikamano na atuwezeshe kuitekeleza mipango yetu ya maendeleo tuliyojipangia, kwa mafanikio zaidi.
 

Attachments

  • HOTUBA YA MH. RAIS.pdf
    883.1 KB · Views: 23
1. Utawala wa JPM ulikuwa hatarishi. Mwamba alikuwa na ndoto za kutengeneza matajiri wapya kwa kuwamaliza waliokuwepo. Alifanya hivyo kwa misingi, kanuni na taratibu haramu na ya kikatili! Ili kufanikiwa azma yake aliiondoa Tanzania kwenye mashirikiano ya kimataifa akaificha kule Chato!

2. Kwa kuwa utawala wa SSH umeirudisha Tanzania kwenye mifumo na amani ya dunia inabidi sasa tutumie akili za ziada kwenda na kasi na matakwa ya uchumi wa dunia!

3. Yawezekana kupitia utawala wa SSH fedha safi na haramu zitakuja kwa urahisi sana.

4. Sasa yatupasa tuamke tupambane. Wazungu wanasema "the world is not fair". Tusipopambana tutajikuta tunaongeza idadi ya watu wenye stress na wapenda chupa za soda za mirinda!!
 
Back
Top Bottom