Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi, amedai amezushiwa juu ya habari kwamba ameoa tena na akadai kuwa uongo unaenezwa na watu aliowaita ni mafisadi wenye lengo la kutaka kumjengea chuki katika jamii.
Mengi anadaiwa kumwoa Lilian Kimaro na ndoa yao ilifungwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Kanali Fabian Massawe. Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, Mengi alisema habari hiyo pamoja na nyingine kama vile ana kashfa ya ufisadi na ndoa baina yake na Chadema yabainika, ni za kutunga na zinasambazwa na magazeti aliyodai yameanzishwa na wale anaowaita mafisadi.
Magazeti haya yanayofadhiliwa na watuhumiwa wa ufisadi yamekuwa yakiandika mambo mengi yaliyojaa fitina na uongo dhidi yangu na familia yangu, alisema Mengi. Hata hivyo, hakuyataja magazeti hayo zaidi ya kueleza kuwa yapo 15. Hata hivyo, Mengi aligoma kuulizwa maswali kuhusu hoja yake hiyo ya ndoa ili aweze kutoa ufafanuzi zaidi.
Naomba msiniulize maswali, nyie wenyewe fanyeni utafiti ndio maana mnaitwa waandishi makini, alisema. Mengi alisema mafisadi hao wameanzisha magazeti hayo ambayo alidai yanasambaza fitina na uongo uliotungwa kwa madhumuni ya kuufanya umma uelekeze nguvu na mawazo yao katika fitina na uongo huo na kuacha kufikiria na kuzungumzia tatizo kubwa la ufisadi.
Alisema fitina na uongo wa mafisadi hao ni sumu inayosambazwa ndani ya jamii na inaweza kujenga chuki, kuwagawa wananchi na kuvuruga amani. Iwapo vurugu zitatokea, basi mafisadi hao wataanza hata biashara mpya ya kuuza silaha ili Watanzania wazitumie kuuana wenyewe kwa wenyewe. Mengi alisema wengi wa mafisadi wanaishi maisha machafu, lakini akagoma kuyaeleza kwa madai kuwa ni hadi pale Baraza la Habari Tanzania (MCT) litakapotoa msimamo wake juu ya uandishi wa mambo ya faragha
HabariLeo: Gwiji la habari Tanzania | Mengi azungumzia ndoa mpya