Mke Wangu Alinifanya Niwe Mchawi - 31....
ILIPOISHIA;
NAKUMBUKA siku moja usiku nikiwa kitandani nilishtuka na kujikuta nimelala peke yangu.
Sikuwa na wasiwasi kwa kuwa niliamini kuwa huenda mke wangu alikuwa amekwenda msalani.
Kwa vile choo na bafu vilikuwa nje nilijua amekwenda kujisaidia tu, nilijilaza, sikuchelewa sana nikapitiwa na usingizi. Niliposhtuka nilishangaa kumuona mke wangu akiwa pembeni yangu amezidiwa na usingizi.
SASA ENDELEA...
Siku hiyo kabla ya kulala nilijaribu kumgusa mke wangu lakini aliniomba radhi kwa kuniambia kuwa tumbo lake lilikuwa limeshtuka ghafla.
Kwa vile ile hali haikuwahi kumtokea, nilimuacha na kuendelea kuuchapa usingizi,
siku ya pili tena nilipomgusa alinieleza bado alikuwa akisumbuliwa na tumbo.
Sasa mke wangu umetumia dawa gani?
Si...sijatumia dawa yoyote mume wangu.
Sasa utaendelea kuilea hali hii mpaka lini? Kumbuka mumeo lazima nipate haki yangu kutoka kwako!
Najua mume wangu, samahani kwa hilo, kesho nitakwenda hospitali.
Mmh! sawa.
Nisamehe mume wangu, alisema huku akinibusu na kunifanya mwanaume nilegee kabla ya usingizi haujatuchukua, kama kawaida yetu tulilala tukiwa tumekumbatiana ili kupeana joto, mpaka pale kila mmoja wetu alipopitiwa na usingizi na kugeukia upande wake kwa kupeana migongo.
Nilishtuka katikati ya usiku, usingizi ulikuwa umenipaa na kujikuta nikiwa peke yangu kitandani, hata hivyo sikuwa na wasiwasi kwa kuwa nilihisi mke wangu atakuwa amekwenda msalani, niliendelea kujilaza huku macho yangu nikiyaelekeza darini.
Muda mrefu ulipita bila mke wangu kurejea kitu ambacho kilinitia wasiwasi labda tumbo lilikuwa limemzidia kule msalani. Nilinyanyuka kitandani na kutoka nje kwenda kumuangalia.
Nilifika hadi msalani, sikuona dalili ya kuwepo kwa mke wangu, nilijaribu kuliita jina lake lakini hakukuwa na jibu lolote.
Niliingia hadi msalani lakini sikumuona, nilitoka nje na kujiuliza atakuwa amekwenda wapi, nilizunguka nyumba nzima sikumuona, niliamua kurudi ndani nikiwa na mawazo tele kwa kutomuona usiku wa manane kama ule.
Nilikaa kitandani nikijiuliza maswali mengi, nilishangaa usiku kama ule atakuwa amekwenda wapi, nilihisi labda atakuwa amezidiwa na kuamua kwenda nyumbani kwao, lakini nilipingana na wazo hilo kwa kujua kuwa kama ingekuwa hivyo ni lazima angenijulisha, asingeweza kuondoka peke yake tena kimyakimya.
Nikiwa nimekaa kitandani niliona mlango ukifunguliwa kwa uangalifu mkubwa, mtu aliyekuwa akiufungua alitulia kwa muda, nikataka kumuona aliyekuwa akiingia kwa kunyata kwa kudhani labda alikuwa ni mwizi.
Baada ya mlango kufunguliwa mtu aliyekuwa akiingia ulitanguliza mguu wake wa kulia, kisha mwili wake ukaonekana.
Alikuwa ni mke wangu akiwa katika vazi la khanga moja,aliponiona alipatwa na mshtuko mpaka khanga aliyokuwa ameivaa ikamdondoka na akabakia mtupu kama alivyozaliwa, hakuiokota bali aliendelea kusimama kama mwanga aliyekamatwa wakati akijiandaa kuwanga.
Nilimuangalia na kushindwa kumuelewa kwa nini alikuwa katika hali ile ya kutahayari.
Vipi mke wangu? nilivunja ukimya baada ya kumtazama kwa muda mrefu.
Sa...sa... alishindwa kusema alichokuwa amekikusudia.
Unatoka wapi?
Msalani, tumbo lilinizidia nikachelewa kurudi.
Ulienda choo kipi?
Cha nje.
Kweli?
Ndiyo mume wangu.
Na sasa hivi ndiko unakotoka huko au...?
Ndiyo mume wangu, alijibu huku vidole vyake vya mkono mmoja akiwa ameviweka mdomoni.
Wakati mimi nilipokuwa nikiingia msalani wewe ulikuwa wapi?
Kwani wewe umekwenda msalani saa ngapi?
Hebu kwanza vaa nguo yako, niliposema hivyo aliinama na kuiokota khanga yake na kujifunga, kisha akasimama palepale na kuendelea kuweka vidole vyake mdomoni kama mwanamke aliyekuwa akitongozwa kwa mara ya kwanza.
Mke wangu ulikuwa wapi?
Msalani mume wangu, alingangania jibu lake.
Si kweli, nimeshtuka kutoka usingizini muda mrefu na kukaa macho, nikawa na wasiwasi labda umezidiwa na tumbo, nikatoka hadi msalani sikukuona, nikazunguka nyumba nzima, sikukuona sasa huo msala ni msala gani uliokwenda wewe? nilimuuliza huku nikimsogelea hadi karibu yake na niliweza kuhisi mapigo yake ya moyo yalivyokuwa yakimuenda kwa kasi.
Mke wangu alishindwa kunijibu, kitu ambacho kilinipandisha hasira na kunifanya nitambue kuwa kulikuwa na mchezo mchafu aliokuwa akinichezea.
Nilimkazia macho na kumuuliza kwa mara nyingine tena kwa hasira huku nikiivuta khanga aliyokuwa amejifunga na kumfanya abakie mtupu.
Hebu niambie ukweli, ulikwenda wapi? kama utanidanganya, nitakachokufanyia hutakuja kukisahau mpaka utakapoingia kaburini. Ni mwaka wa tatu na nusu tangu moyo wangu upone majeraha. Hujaridhika unauchubua tena, niambie ulikuwa wapi?
Samahani mume wangu nilipokuwa nikirudi kutoka msalani, nilipofika kwenye mlango wa God, aliniita kwake lakini sijafanya naye kitu chochote kile.
Leo hukufanya naye kitu, sawa siku zote ulizokuwa ukienda kwake ulikuwa ukifanya naye nini?
Swali langu lilimpa wakati mgumu kulijibu, akabakia akiumauma meno, nikapata nafasi ya kuongeza maneno mengine.
Mke wangu wewe ni kiumbe gani, umenifanya nimechuma dhambi kwa ajili yako, tumetulia umeanza tena, kibaya zaidi ndani ya nyumba tunayoishi. Wewe ni kiumbe gani? umerogwa na nani mpaka kuwa katika hali hii?
Nisamehe mume wangu ni shetani tu, mi nipo chini ya miguu yako, sitarudia tena, mke wangu alinisogelea na kupiga magoti.
Haya nieleze ukweli tangu umerudi hapa nyumbani umeshaisaliti ndoa yetu mara ngapi?
Kwa haki ya Mungu ni mara nne tu.
Na wanaume wangapi?
Mmoja tu mume wangu, ni God tu, ukweli wa Mungu tangu nimkubalie ni wiki ya pili sasa, hata hivyo nilijitahidi kumkatalia lakini nimeshindwa kwa kuwa amekuwa akinisumbua sana.
Amekuwa akinipa ofa na fedha
za pombe, siku zote shetani ana nguvu, nimejikuta nikimkubalia na kukusaliti kwa mara nyingine mume wangu.
Najua ni kwa jinsi gani ninavyokuumiza lakini nakuomba usiniache, pombe ndiyo sababu mume wangu nitaiacha, siku aliyonipa ofa ya pombe ndiyo ilikuwa mwanzo wa kunisumbua kimapenzi, kwa kweli nilijitahidi lakini nilijikuta nimemkubalia bila kujua, naomba usiniache mume wangu.
Mama alishaniambia siku nikifanya ujinga kwako kisha ukanifukuza, basi nitafute mahali pengine pa kwenda, nisirudi kwake.
Unataka kujua kilichotokea? Usikose kusoma baadae...