Mke Wangu Alinifanya Niwe Mchawi-9....
ILIPOISHIA:
Nilipotoka kazini nilikwenda sehemu aliyonielekeza na kushtuka kukuta amepanga kwenye nyumba ya gharama iliyokuwa ndani ya fensi, kitu kilichonipa wasiwasi na kujiuliza kama kodi aliyolipa mke wangu ikiisha nitaweza kuilipa. Mke wangu alinipokea kwa furaha.
SASA ENDELEA...
"Karibu mume wangu kwenye makazi mapya."
"Asante."
"Mbona kama unashangaa?"
"Nashangaa kwa mambo mawili, kwanza nyumba nzuri sana na pili na wasiwasi kodi yake ni kubwa."
"Ni kweli kodi ni kubwa lakini ni sehemu nzuri tutakayoishi bila bughuza za watu."
"Nyumba yote kwa mwezi shilingi ngapi?"
"Laki moja na nusu."
"Mke wangu laki moja na nusu kwa mwezi umelipa kwa muda gani?"
"Mwaka mzima."
"Ndiyo shilingi ngapi?"
"Hesabu unajua, zidisha laki na nusu mara kumi na mbili."
"Sasa mimi nitaweza kulipa fedha zote hizo?"
"Nitakusaidia, kuwa na amani moyoni mwako."
Sikutaka kuhoji sana fedha zote hizo kazipata wapi, kwani Waswahili wana msemo wao kuwa ukimchunguza sana bata huwezi kumla na ukimchunguza sana mkeo hutaweza kuishi naye. Tuliyaanza maisha ya Uzunguni, sehemu waliyokuwa wakiishi watu wenye uwezo. Kwa kweli maisha ya makazi mapya yalikuwa mazuri sana yenye furaha na amani.
Kwa muda mfupi, afya yangu ilirudi katika hali ya kawaida baada ya kuteseka kwa muda mrefu kutokana na vituko vya mke wangu. Kutokana na kuonesha mke wangu amejirekebisha tulimchukua mtoto wetu na kuishi naye. Heshima aliyoonesha ilimshtua hata mama yake mzazi.
Maisha yalisonga mbele, mke wangu akashika ujauzito wa pili, kitu kilichozidi kunipa faraja moyoni mwangu. Lakini ilikuwa tofauti kwa upande wa pili, mke wangu hakupenda kubeba ujauzito kwa vile mtoto wetu alikuwa bado mdogo.
"Mke wangu tatizo nini?"
"Huoni Zawadi bado mdogo."
"Miaka mitatu si michache na mpaka unajifungua atakuwa amesogea sana."
"Kwa upande wangu nilipanga kuzaa baada ya Zawadi kufikisha miaka mitano."
"Basi bahati mbaya, itabidi uzae hivyohivyo."
"Siwezi, lazima niitoe hii mimba."
"Usiitoe mke wangu, Zawadi tutampeleka kwa bibi yake ili asipate shida."
"Bado nina hamu ya kumlea mwanangu, kama mtoto utapata tu muda ukifika," mke wangu bado alishikilia msimamo wake.
"Nakuomba usiitoe hiyo mimba, nipo chini ya miguu yako mke wangu," nilimbembeleza mke wangu mpaka nikampigia magoti.
"Kwa hilo siwezi kukusikiliza, sihitaji senti tano yako, nitatoa kwa fedha zangu."
Kwa mara nyingine mke wangu alinizidi nguvu, nikamkubalia kwa shingo upande. Siku ya pili nikiwa kazini, majira ya saa tisa alasiri, mke wangu alinipigia simu kunijulisha kuwa amefanikiwa kuitoa mimba salama. Nilimkubalia lakini upande wa pili moyo uliniuma sana, hata kazi ilinishinda na kwenda sehemu ya peke yangu ambapo nililia sana kumpoteza mwanangu mtarajiwa.
Jioni niliporudi, nilimkuta mke wangu nyumbani, hali yangu ya unyonge ilimshtua mke wangu na kunifuata nilipokuwa nimekaa, akawa ananibembeleza.
"Mume wangu, najua kiasi gani nilivyokuumiza lakini sikuwa na jinsi, nilifanya vile kwa maana kubwa. Kwa sasa ni vigumu kunielewa lakini amini nilichokifanya si kukukomoa bali kumpa nafasi Zawadi. Kumbuka makosa yangu ya awali yalimtesa mwanangu hivyo sasa hivi nina deni la kumlea."
Kutokana na kumpenda sana mke wangu, nilikubaliana naye. Maisha yalisonga huku akionesha mapenzi mazito kwangu, kitu kilichofuta mawazo ya kutoa ujauzito.
Siku zote kimya kingi kina mshindo mkuu. Mwezi mmoja baada ya kutoa ujauzito, asubuhi moja nilidamka kwenda kazini huku hali yangu kiafya ikiwa si nzuri.
Nilijitahidi kwa kuamini mwanaume si mtu wa kujilegeza. Nilipofika kazini, nilijitahidi kufanya kazi lakini kutokana na kufanya kazi juani, hali yangu ilibadilika na kuwa mbaya hivyo niliruhusiwa kwenda hospitali kupata matibabu.
Nilikwenda hadi hospitali ya wilaya na kupata huduma japo dawa nilikwenda kununua duka la kuuza dawa. Nilibeba dawa zangu na kurudi nyumbani kupumzika. Nilipofika nyumbani, ndani ya geti nilikuta kuna gari ambalo kwangu halikuwa geni sana japo sikukumbuka nililiona wapi.
Baada ya kutafakari, niligundua lile gari ndilo lililomshusha mke wangu, nikashtuka kulikuta nyumbani kwangu na kujiuliza limefuata nini pale. Niliingia ndani na kukuta sebuleni kuna pombe kali juu ya meza na glasi mbili.
Sikujishughulisha navyo, nilielekea chumbani, nilipofika kwenye mlango wa chumbani, nilikuta umefungwa kwa ndani, nikasikia sauti mbili ya mwanamke na mwanaume. Sauti ya mwanamke ilikuwa ya mke wangu ya kiume sikujua ni ya nani. Kwa haraka nilitoka mpaka nje na kuzunguka dirishani na kuchungulia ndani.
Itaendelea baadae............