Mke Wangu Alinifanya Niwe Mchawi - 29...
ILIPOISHIA;
SAA mbili asubuhi gari liliondoka Mlalo na kuelekea Dar es Salaam, Shedu alichukuliwa na usingizi na safari ilipoanza aliuchapa vya kutosha.
Miye niliendelea kuangalia mji wa Mlalo huku akili yangu ikiwa njiapanda nisipate majibu kuhusu mwanaume aliyemchukua mke wangu kama atakuwa amefariki dunia kwa ajali.
Akili yangu haikuamini, nilijua yule mzee aliamua kututoa kisiasa ili tusiondoke tukiwa hatuna imani naye.
Sifa alizonipa Shedu na mambo niliyoyakuta kule niliona kulikuwa na tofauti kubwa lakini sikutaka kuumiza kichwa zaidi, nilijua ukweli na uongo wa mganga nitaujua baada ya kufika nyumbani.
SASA ENDELEA...
KWA vile ilikuwa ni alfajiri nami usingizi ukaanza kuninyemelea lakini jambo hilo lilikuwa limechangiwa na mazingira ya sehemu tuliyofikia, siku zote sehemu usiyoizoea huwezi kulala vizuri, basi nami usingizi ukanichukua bila ya kujijua.
Shedu ndiye aliyenishtua kutoka usingizini, yeye aliamka muda ambao usingizi ulikuwa umeshanikolea.
Kazala amka tupate chakula cha mchana.
Wapi hapa? nilimuuliza baada ya kuona tumefika kwenye kituo cha basi.
Korogwe.
Sasa ni saa ngapi naona jua ni kali?
Saa saba.
He! Kumbe nimelala sana!
Tuliteremka Korogwe na kupata chakula cha mchana, kisha tukarudi kwenye basi na kuendelea na safari ya kurudi kwetu. Tulifika Chalinze saa tisa na nusu alasiri, tulipanda basi lililokuwa likitoka Dar saa kumi na nusu jioni tuliingia makwetu saa nne usiku.
Kwa vile muda ulikuwa bado Shedu alikwenda kwake na mimi nilirudi kwangu.
Nilishukuru kwa kuwa siku ya pili ilikuwa Jumamosi ambayo kwa kawaida huwa siendi kazini, hivyo niliamini ningekuwa na muda mrefu wa kupumzika.
Baada ya kula chakula nilichonunua, nilioga na kujitupa kitandani kutokana na kutawaliwa na uchovu usingizi haukuchelewa kunichukua.
Nilishtuka siku ya pili tena baada ya kugongewa na jirani yangu, nilifungua mlango na kutoka nje.
Vipi jirani za asubuhi, ulisafiri?
Nzuri, eeh nilitoka kidogo.
Mbona hukuaga?
Ilikuwa ni safari ya ghafla sana samahani kwa hilo.
Mkeo alirudi,
Eeh! nilishtuka kusikia vile.
Alikuja juzi pamoja na mwanao, walikusubiri mpaka usiku bila kutokea, ilipofika usiku ilibidi alale kwenye korido asubuhi ya jana ndiyo kaondoka.
Jana tena alikuja hapa bila mtoto alikaa mpaka saa tatu usiku akaamua kuondoka, aliendelea kunifahamisha jirani yangu.
Atakuwa amekwenda wapi?
Mmh! Kwa kweli siwezi kujua ila ameondoka na kuniomba nimuwekee mizigo yake vizuri na kusema atarudi kesho. Nia yake ilikuwa ni kuingia ndani, amesema anaweza kuja na fundi ili amfungulie mlango. Kwa nini hukuacha funguo?
Kama nilivyokwambia safari ilikuwa ya ghafla sana.
Basi kwangu kuna mizigo ya mkeo,
Sawa, nilichukua mizigo ya mke wangu na kuiingiza ndani.
Baada ya kuweka vitu vya mke wangu vizuri nilikaa kwenye kochi na kuanza kuwaza na kuwazua kama kauli ya mganga na niliyoyasikia muda mfupi kuhusu mke wangu kurudi nyumbani yalikuwa na uhusiano.
Nilijiuliza kama mke wangu amerudi ina maana ni kweli yule mwanaume amekufa kwa ajali kama alivyonieleza mganga au kuna lingine lililotokea.
Nikiwa katikati ya mawazo Simon alibisha hodi, nilimkaribisha ndani kwa vile mlango ulikuwa wazi. Simon aliingia akionekana kuwa na jambo alilotaka kuniambia, baada ya kuketi alisema:
Pole na safari.
Asante.
Mmh! mzee unatisha.
Kivipi?
Jamaa tumemzika jana.
Jamaa gani?
Si mgoni wako.
Muongo!
Kweli tumemzika jana, kwa kweli mimi na wote tuliosikia sababu ya kifo chake tulijua ni kifo cha kawaida lakini aliyonieleza Shedu nimeshtuka sana.
Unashtuka nini wakati hata mgoni wa Shedu naye alilamba udongo.
Ni kweli alilamba udongo, kifo chake wengi walijua kilitokana na kumchukua mke wa mtu, kulikuwa kama kuna miujiza fulani hivi, lakini kifo cha mbaya wako kilikuwa cha ajali, tena baada ya gari lake kugongana uso kwa uso na gari la mafuta. Waliofika kwenye tukio wanasema wala hakuomba maji, alikufa palepale.
He! Kumbe kweli? nilijikuta nikishtuka baada ya kusikia vile.
Unashangaa nini?
Unajua aliyosema yule mzee mimi nilijua anatudanganya, nilidhani alikuwa anatupa moyo baada ya kuona kazi imemshinda.
Kaniambia yote Shedu yaliyotokea huko, lakini ukweli unabaki palepale yule mzee ni tishio, hasa kwenye kazi za kulipa visasi.
Lakini naamini adhabu aliyopewa ni kubwa sana, nilisema.
Si ndiyo uliyochagua? Simon aliniuliza akinikazia macho.
Adhabu hii sikuichagua bali walinichagulia ili kumkomesha.
Basi tena ni kujipanga upya, shemeji amerudi?
Nasikia amerudi juzi jioni na kulala hapa, asubuhi ameondoka inaonekana labda ameenda kwao.
Sasa ndiyo mkeo atulie kama umemuua huyo, akiendelea na tabia yake utaua wangapi? Simon aliniuliza.
Kwanza Simon hebu ondoa hilo neno la kusema nimeua, kazi yote imefanywa na mganga, nilijitetea.
Kwa sababu ya nani?
Kwa sababu yangu, lakini kwa uamuzi wa wengine, mi nilikuwa namtaka mke wangu tu.
Basi ndiyo hivyo mkeo atarudi jipange kuhakikisha kosa la awali halijirudii tena.
Tukiwa katikati ya mazungumzo mara mlango wa mbele uligongwa, ilikuwa sauti ya mke wangu. Nilitamani ninyanyuke nikampokee lakini niliona aibu mbele ya ya rafiki yangu Simon.
Nilimkaribisha aingie ndani.
Mke wangu alipoingia alikuja moja kwa moja hadi nilipokuwa nimekaa na kupiga magoti kuomba msamaha.
Nini kitaendelea? Usikose baadae ....