Serikali irejeshe nyumba zilizouzwa
Na Dismas Lyassa
Tanzania ni mojawapo ya nchi duni sana duniani ingawa tunao wajanja wachache wanaoishi maisha bora na ya kifahari kama waishivyo wakazi wengi wa nchi za Ulaya.
Kulingana na ripoti za mashirika tofauti ikiwemo Benki ya Dunia, umaskini Tanzania ni wa hali ya juu, huku thamani ya fedha nayo ikiendelea kuporomoka.
Wastani wa pato la Mtanzania ni chini ya sh1000 kwa siku, wakati thamani ya fedha ya Tanzania ni zaidi ya Sh1,269 kwa dola moja ya Marekani.
Huenda Tanzania ikawa ni mojawapo ya nchi inayoongozwa kwa kupewa ahadi nzuri za kuboreshewa maisha, lakini ukweli ni tofauti, hali ya uchumi inaendelea kuwa mbaya, watu wengi wanaonekana kukata tamaa.
Wanaoongea ukweli kama huu ninaoueleza hapa wanaonekana wabaya machoni mwa watu wanaoishi kifahari katika nchi hii iliyo na utitiri wa maskini.
Katika hali duni ya maisha iliyopo nchini, uko umuhimu wa Serikali kuangalia njia tofauti za kuimarisha uchumi ikiwa ni pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji wa shughuli zake.
Sehemu mojawapo muhimu ya kupunguza matumizi ni kuhakikisha nchi inakuwa na nyumba za kutosha kwa ajili ya watumishi wake.
Inashangaza na kutia kichefuchefu kuona nchi inahitaji nyumba zaidi ya 300,000 kwa ajili ya watumishi, lakini zilizopo chache zinauzwa.
Tayari nyumba 7700 zimeuzwa na 1800 zimesalia baada ya zoezi hilo kusitishwa. Ni lini nyumba 300,000 zitajengwa ili kukidhi mahitaji ya nyumba za watumishi nchini? Ni swali lisilo na jibu.
Tunauza nyumba ili watumishi waishi wapi? Hilo nalo ni swali ambalo naamini hakuna mwenye uwezo wa kulijibu kwa ufasaha.
Ninachokiona mimi mpango wa kuuza nyumba za Serikali umeanzishwa sio tu kwamba pengine haukufanyiwa uchambuzi wa kina, lakini inawezekana ni wajanja wachache wametamani kupora nyumba hizo.
Naamini hivyo kwa sababu kama kweli lengo lilikuwa kusaidia maisha bora ya mtumishi, kungekuwa na mradi maalum wa kujenga nyumba za kuziuza, lakini sio kuuza zilizopo ambazo ni chache.
Ni suala linalowezekana kwa Serikali kuanzisha mradi wa namna hiyo, kwa mfano inaweza kuingia katika mji fulani na kujenga nyumba kisha wakawa wanalipa kidogo kidogo.
Athari za kuuza nyumba hizi zimeshaonekana, kwani baadhi ya viongozi hadi sasa inadaiwa wanaishi hotelini kutokana na kukosa nyumba.
Pia kuna baadhi ya watumishi kwa sababu ya uzito wa nyadhifa zao inakuwa vigumu kuwapangishia nyumba katika mazingira ya ajabu-ajabu, matokeo yake wanalazimika kukaa hotelini kwa muda mrefu huku wakitafutiwa sehemu nzuri za kuishi.
Matokeo ya hali hii, ni kwa nchi kutumia fedha nyingi kuendesha Serikali badala ya shughuli za maendeleo.
Hivi karibuni Serikali ilitoa kauli ya kusitishwa zoezi zima la kuuza nyumba, taarifa hii ni nzuri, lakini ni vema ikafikiria kuzirejesha nyumba zote zilizouzwa.
Wale waliozinunua nyumba hizo warudishiwe fedha zao.Suala hili halihitaji mjadala, bali linapaswa kutekelezwa mara moja.
Nifahamu waliozinunua nyumba hizi wanajua wamefanya dhambi, sio tu kwa sababu wamezinunua, lakini kwa sababu wamenunua kwa bei ndogo ukilinganisha na thamani halisi ya majengo.
Kwa mfano taarifa za vyombo vya habari zinasema katika Halmashauri ya Rungwe, mkoani Mbeya, zipo nyumba za Serikali ambazo zimeuzwa hadi Sh1.6milioni.
Hata Jijini Dar es Salaam ambako thamani ya nyumba inaongezeka kadri miaka inavyokwenda mbele, zipo nyumba zilizouzwa hadi Sh10milioni, bei ambayo ni ndogo.
Inakuwaje nyumba yenye nyumba vitatu au zaidi iuzwe bei ndogo kama hiyo wakati gharama za ujenzi ni za juu sana, kiasi kwamba ujenzi wa chumba kimoja pekee hadi kinakamilika unaweza kugharimu Sh2milioni.
Kwanini zinauzwa bei chee kiasi hiki kama njugu? Mimi sina jibu.Nina hakika ukichukua fedha ya mauzo ya nyumba iliyouzwa na kwenda kutafuta nyumba kama hiyo ya kununua huwezi kupata.
Nina imani kuuzwa kwa nyumba hizo ni mipango michafu ya wachache kutaka kujichukulia mali za umma, wakitumia kigezo kuwa inaziuza kwa watumishi ili kuboresha maisha yao.
Wengi wa watumishi walionunua nyumba hizo ambao nao hawajamalizia malipo kwa sababu wanahojia watanyanganywa, ni wale wenye uwezo wa kujenga kutoka na mishahara mikubwa wanayopata.
Je kuna Polisi gani wa kawaida anayelipwa mshahara wa Sh100,000 au chini ya hapo, aliyeuziwa nyumba hizo kama sio vigogo wanaolipwa mishahara minono na ambao wana uwezo wa kujenga majumba kibao kwa mwezi mmoja tu? Je, ni walimu wangapi wa shule ya msingi waliouziwa nyumba hizo? Wafagizi na wapika chai wangapi wanaofanya kazi ofisi za Serikali waliouziwa nyumba hizo?
Nina maswali mengi ya kuuliza ambayo naamini nikiorodhesha yote ukurasa huu pengine ukawa hautoshi.
Ushauri wangu ni kwa Serikali kuachana na mipango ya kuuza nyumba, na pia kuzirudisha nyumba zote zilizouzwa.
Kutokana na ukweli kuwa wengi wa wale waliouziwa nyumba hizi ni watumishi wenye uwezo kifedha, ni vema wakaziacha nyumba hizi na kujenga zao waishi kwa amani.
Nina hakika hata kama sasa Serikali haitazirudisha nyumba hizi, lakini ipo siku Mungu atatupatia Rais ambaye atazirudisha, iwe kwa fidia au bila fidia.
Kama ambavyo chama kilichotawala Kenya kwa muda mrefu Kenya (KANU) kiliweza kuondolewa madarakani bila ulimwengu kuamini kilichokuwa kikitokea, inawezekana pia kwa chama fulani ndani ya Tanzania kikawa imara au kudhoofika. Yote yanawezekana!!!
Waulize machinga leo ukitokea uchaguzi mkuu utampigia kura nani, nina hakika jibu halitafanana na lile ambalo angekupa wakati wa kampeni za kunadi sera za maisha bora kwa kila Mtanzania.
Ninachotaka kusisitiza hapa ni kuwa Serikali irejeshe majumba yaliyouzwa, badala yake ianzishe mradi wa kujenga nyumba na kuziuza kwa mkopo kama kweli lengo ni kuboresha maisha kwa jamii Tanzania, sio kuuza zilizopo.
Dismas Lyassa ni mwandishi wa makala gazeti Mwananchi, 0754 498972