Mkapa above the law?: Allegations

Mkapa above the law?: Allegations

...soma kwanza thread ya tetesi ya chadema na maaskofu, hii ni cha mtoto, utaielewa tu!
Una maanisha nini hasa? ile thread naona mode ameitoa kwakuwa ina ukweli kiasi fulani wenye forum "inawaboa" wanahitaji kusifiwa kwamba chadema ni nzuri "lakini hizo hila hazitowafikisha popote" wengine tunawasaidia wawe wa Kitaifa zaidi" kuliko ku-biased
 
Una maanisha nini hasa? ile thread naona mode ameitoa kwakuwa ina ukweli kiasi fulani wenye forum "inawaboa" wanahitaji kusifiwa kwamba chadema ni nzuri "lakini hizo hila hazitowafikisha popote" wengine tunawasaidia wawe wa Kitaifa zaidi" kuliko ku-biased

...Mkuu, sina uhakika na madai yako kwa kweli, maana nimefanya search iliyo basic tu nikatuna na post zako kwenye thread yenye mada hizo: https://www.jamiiforums.com/jukwaa-...ma-mbadala-kwa-ccm-post509628.html#post509628
 
Kubenea kweli kaishiwa sasa anaunga unga habari kwa super glue tu...

Na Saed Kubenea
MPANGO wa kumtetea rais mstaafu Benjamin Mkapa umelenga mbali. Umeandaliwa mahsusi kubeba wote wanaolalamika kuwa Rais Jakaya Kikwete amewatelekekeza, MwanaHALISI limeelezwa.
Taarifa za ndani ya serikali zinasema mpango wa kumsafisha Mkapa, uliozinduliwa bungeni na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Ijumaa iliyopita, umelenga orodha ndefu.
“Ndugu yangu, Mkapa naye ana ndugu na marafiki. Lakini pia anajua mengi juu ya kila aliyeko madarakani sasa. Akiamua kubwatuka asubuhi moja, nchi inaweza kutikisika,” ameeleza.
Pinda alilieleza bunge kuwa Mkapa ni mcha Mungu, mwadilifu, siyo fisadi na hana fedha nje ya nchi, katika kile ambacho wafuatiliaji wamesema ni “kupoza hasira za Mkapa na kuogopa ulipizaji kisasi wakati ukiwadia.”
Alikuwa akijibu baadhi ya hoja za wabunge ambao wamekuwa wakisisitiza kuwa Mkapa ahojiwe na hata kufikishwa mahakamani kutokana na kukiuka maadili ya utawala bora.
Kilio kikubwa cha wabunge kimekuwa juu ya miliki ya mgodi wa mkaa wa mawe wa Kiwira, mkoani Mbeya ambao inadaiwa kampuni ya Mkapa na familia yake, ilijibinafsishia tena kwa bei ya “bure.”
MwanaHALISI limeelezwa kuwa hatua ya Pinda ya kumtetea Mkapa hadharani imekuja baada ya kukwama kwa mpango wa awali wa kumfanya rais huyo wa zamani kuwa Kamanda wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UV-CCM), ambao wangepewa jukumu la kumlinda.
“Kwanza angetangazwa kuwa Kamanda wa Vijana. Akasimikwa na Rais Jakaya Kikwete, na kwa kofia hiyo, angejitokeza kwa nguvu zote na kuvunjilia mbali tuhuma zote huku akibebwa na vijana,” kimeeleza chanzo cha habari hizi.
Imefahamika kuwa kiongozi wa vijana ambaye angebeba bango la Mkapa angekuwa yule anayeheshimika kwa vijana wengi; mwenye hoja nzito na ambaye hatiliwi mashaka na wengi katika umoja huo.
Hata kama kijana wa aina hiyo angepatikana, na taarifa zinasema alikwishatonywa, tatizo jingine lingekuwa jinsi ya kushawishi vijana kuwa kamanda wao siyo tena Mzee Rashid Mfaume Kawawa, na bila sababu yoyote nzito.
Hata hivyo, kutopatikana kwa kijana mwenye uwezo wa kuunganisha wenzake kumbeba Mkapa, kulifanya hata pendekezo jingine kukwama.
Hili ni lile lililohusu makamu mwenyekiti mstaafu wa CCM, John Samwel Malecela. Kumekuwa na ushawishi wa chini kwa chini, tangu mwaka jana kwa kuhusisha baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu (CC) kumfanya kamanda wa vijana.
Mkakati wa ukamanda wa vijana umekuwa ukienda sambamba na kauli za wabunge za kumtetea Mkapa; na hivi karibuni Chrysant Mzindakaya (Kwale-CCM) alilazimika kunukuu maandiko matakatifu kumtetea.
Kwa hiyo kuibuka kwa Pinda na utetezi ambao haukutarajiwa, kumechukuliwa na wachunguzi wa siasa za sasa kuwa Mkapa bado ana nguvu “nyuma ya pazia.”
Taarifa zinasema kinachofanyika hivi sasa ni mshikamano miongoni mwa wote ambao wanalalamika kuwa wametupwa nje ya duara la madaraka tangu Rais Kikwete aingie madarakani.
“Sasa hakuna sababu ya kuangalia nani ametupwa nje na kwa sababu ipi. Kila mtu aweza kuwa na sababu zake. Hawa wakiungana wana uwezo mkubwa wa kurudi kwa kishindo hata kama ni kwa sanduku la kura,” ameeleza mmoja wa wabunge.
Miongoni mwa walio kwenye foleni na wenye shauku kubwa ya kurejea madarakani, ni aliyekuwa waziri mkuu Edward Lowassa.
Wengine ni waliokuwa mawaziri wa zamani wa nishati na madini, Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha waliojiuzulu kufuatia kashfa ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond ambayo ndiyo pia ilimng’oa Lowassa.
Mbunge wa Bariadi Magharibi Andrew Chenge, Katibu Mkuu wa zamani wa CCM Philip Mangula, mweka hazina wa zamani wa CCM, Rostam Aziz, ni miongoni mwa wanaoweza kuungana na yeyote ili kuhakikisha hadhi yao inarejea.
Kauli ya waziri mkuu Pinda sasa itatumika kama wito wa kuunganisha wote wenye malalamiko kuwa serikali ya Rais Kikwete imeshindwa kuwalinda na kuwatetea na wote ambao kwa muda sasa wamevikwa tuhuma za ufisadi.
Wachunguzi wanasema kinachotendeka ni maandalizi ya kutafuta muwafaka kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.​
 
Mkapa hali mbaya


Na Luqman Maloto

Wakati sakata la ufisadi, likiendelea kuchukua nafasi pana ndani ya nchi hii, wachambuzi mbalimbali wa mambo ya kisiasa wamesema kuwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa yupo kwenye hali mbaya kisiasa.

Wamesema kwamba kama hali iliyopo itaendelea bila jitihada za kumkinga rais huyo mstaafu kufanyika, si ajabu akapoteza umaarufu wake wa kisiasa ndani ya kipindi kifupi kijacho....

Wakiongea na mwandishi wetu kwa nyakati tofauti, jijini Dar es Salaam, wikiendi iliyopita, wachambuzi hao walifafanua kwamba ‘ishu’ ambazo zinaelekea kumkaanga Mkapa ni ile ya Akaunti ya malipo ya madeni ya nje (EPA) na mikataba yote ambayo ilisainiwa wakati wa utawala wake.

Katika mikataba, kipimo cha kwanza walikielezea kuwa ni kauli ya wafanyakazi wa Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (TANESCO) ambao walimshushia lawama nzito Mkapa kuwa utawala wake ndiyo umeifanya taasisi hiyo iwe hohe hahe.

“Waswahi wanasema mwehu mtoto akikuvua nguo usimkimbize, ni kweli Mzee Mkapa hataki kukimbizana na watoto, lakini ukimya wake unafanya hali yake izidi kuwa mbaya kisiasa,” alisema Dk. Zaid Kamsa wa Dar es Salaam.

Dk. Kamsa ambaye ni mhitimu wa Shahada ya Uzamivu, Chuo Kikuu cha Arizona Marekani katika masomo ya Sayansi ya Siasa (Political Science), aliongeza: “Kikwete ameshatangaza Mzee Mkapa asibughudhiwe, lakini ni jambo gumu kwa sasa.

“Ni jambo gumu kwakuwa kuna uwezekano watu wakaendelea kumrushia madongo na kwasababu hali ya sasa ni mbaya, itakuwa ngumu kumsafisha kutokana na hili wimbi la ufisadi.”

Ijumaa iliyopita, wafanyakazi wa TANESCO walifanya kikao kujadili mikataba mibovu ya shirika hilo ambapo moja kwa moja walimrushia lawama Rais Mkapa enzi ya utawala wake kwa kuingia mikataba mibovu kama ule wa IPTL na Songas.

Wakati akiwashiwa moto TANESCO, tayari kumekuwa na msukumo kutoka kwa watu wengi, wakitaka rais huyo mstaafu awajibishwe kwenye sakata la EPA ambalo lililomfukuzisha kazi, aliyekuwa gavana wa Benki Kuu, Daud Ballali.

Pointi iliyo nyuma ya shinikizo hilo ni kuwa Mkapa awajibishwe kwakuwa upotevu wa shilingi bilioni 133 katika mfuko wa EPA, ulifanyika enzi ya utawala wake.


Source: Global Publishers
 
Mkuu kilicho andikwa kinaweza kuwa na ukweli lakini hiyo source mh. Global publishers is not a credibale source. Japo siku hizi magazeti yetu mengi yamekaa kiudaku udaku lakini magazeti ya global ni openly udaku & know one serious would take them seriously.
 
Hakuna kitu, mbona anaafya njema kabisa ...mwisho wa kelele 2010
 
Arudishe mali zote na awajibishwe kwa mikataba yake mibovu netgroup na mingine yote......IPTL,Mchuchuma,Songas etc
 
Mkapa anatakiwa kufunguliwa mashtaka mahakamani. Mkapa ni FISADI mkubwa sana, aliingiza nchi matatizoni kwa kusaini mikataba mibovu ambayo imelisababishia hasara kubwa taifa hili. Ndiye aliye sababisa Tanzania kuendelea kuwa among the 10 poorest countries in the world.
 
Mkapa anatakiwa kufunguliwa mashtaka mahakamani. Mkapa ni FISADI mkubwa sana, aliingiza nchi matatizoni kwa kusaini mikataba mibovu ambayo imelisababishia hasara kubwa taifa hili. Ndiye aliye sababisa Tanzania kuendelea kuwa among the 10 poorest countries in the world.

Ni kweli Mkapa alituingiza mkenge, lakini tuwe makini pia, hii isije kuwa ni juhudi maalumu ya kutufanya tuelkeze mashambulizi kwa Mkapa ili JK na timu yake wafanye mambo yao kwa raha zao!

Kwa sasa nadhani ni muhimu kuelekeza juhudi zetu kumdhibiti JK asituletee ya Mkapa.

Kwa mfano huu ujanja ujanja wa :
-Kilimo kwanza
-Pesa zilizo rudishwa za epa? ziko wapi? na ningapi?zinafanya nini?
-Mabilioni ya Jk yanatoka wapi? na huwa yanawanufaisha kina nani? kwa
vigezo gani?
-Haya mabilioni yaliyo tengwa eti kufidia makampuni ya mazao? ni yapi hayo? na yalipata hasara kiasi gani? na kwanini makampuni si wakulima husika?

Yaani kuna mambo mengi yanaendelea tusipotoa macho kuhoji, baada ya muda wake tutaishia kumshambulia kama Mkapa tukimruhusu atakaye kuwepo madarakani aendeleee kujichotea na hivyo muendelezo wa TZ kuwa shamba la bibi kuendelea kama kawa
 
Ni kweli Mkapa alituingiza mkenge, lakini tuwe makini pia, hii isije kuwa ni juhudi maalumu ya kutufanya tuelkeze mashambulizi kwa Mkapa ili JK na timu yake wafanye mambo yao kwa raha zao!

Kwa sasa nadhani ni muhimu kuelekeza juhudi zetu kumdhibiti JK asituletee ya Mkapa.

Kwa mfano huu ujanja ujanja wa :
-Kilimo kwanza
-Pesa zilizo rudishwa za epa? ziko wapi? na ningapi?zinafanya nini?
-Mabilioni ya Jk yanatoka wapi? na huwa yanawanufaisha kina nani? kwa
vigezo gani?
-Haya mabilioni yaliyo tengwa eti kufidia makampuni ya mazao? ni yapi hayo? na yalipata hasara kiasi gani? na kwanini makampuni si wakulima husika?

Yaani kuna mambo mengi yanaendelea tusipotoa macho kuhoji, baada ya muda wake tutaishia kumshambulia kama Mkapa tukimruhusu atakaye kuwepo madarakani aendeleee kujichotea na hivyo muendelezo wa TZ kuwa shamba la bibi kuendelea kama kawa
Hata iweje, kama ni jitihada za JK kutufanya tusimjadili yeye tumjadili BWM bado itafika zamu yake akitoka madarakani tutabanana naye tu...

Sidhani kama ni janja ya JK... Mkapa has to come out clean! Ikifika zamu ya JK atahukumiwa na historia
 
Mkisoma between the line hotuba nzima ya Pinda inasherehesha jambo moja tu.. ufunguzi wake.. hasa maneno haya:- "Ndugu yangu, Mkapa naye ana ndugu na marafiki. Lakini pia anajua mengi juu ya kila aliyeko madarakani sasa. Akiamua kubwatuka asubuhi moja, nchi inaweza kutikisika,"

Ukiweza kuelewa undani wa maneno haya basi tumefunga mjadala.
 

Mkapa na Bulyanhulu, Kikwete na North Mara!

Julai 23, 2009
rC.jpg

NAPENDA kuliendeleza kidogo suala lile nililolijadili toleo lililopita la vifo vilivyotokea katika mgodi wa Barrick wa North Mara, na pia vifo tunavyovitarajia kutokea vya wafanyakazi wa kampuni ya TanzaniteOne kutokana na ukaguzi wa kupitishwa, kila siku, kwenye mashine za mionzi kinyume cha matakwa ya Kamisheni ya Mionzi Tanzania (TAEC).
Hata hivyo, napenda kuanza kwa kukumbusha kidogo ya Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa. Alikuwa ni mtawala asiyetetereka wala kuyumba kimsimamo katika jambo aliloliamini (au mwenye maslahi nalo); hata kama jambo hilo linapingwa na wengi.
Kwa mfano, aliamini kwa dhati kwamba jibu la matatizo ya uchumi wa nchi yetu ni wawekezaji wa kigeni. Kwamba tatizo litapungua kama wawekezaji wengi wa kigeni watakuja nchini kuvinunua viwanda na pia kuwekeza katika migodi na kwenye sekta ya utalii.
Kwa sababu ya kuamini hivyo, ingawa wapinzani wa sera ya uwekezaji ya Serikali ya CCM walipiga kelele sana, ilikuwa sawa na kumpigia mbuzi gitaa ukitarajia acheze.
Kwa kumbukumbu zangu, mahali pekee alikopata kushindwa na akanyoosha mikono, ni kwenye mradi wa kamba kwenye Delta ya Rufiji.
Mkapa alitaka mwekezaji wa Ireland, John Nolan awekeze huko; hata kama mradi huo ungesambaratisha maisha ya mamia ya wavuvi wadogo wadogo katika delta hiyo. Lakini kishindo cha kuupinga mradi huo cha wanamazingira, mabalozi na wahisani wa nje kilikuwa kikubwa kiasi kwamba, hatimaye, Mkapa alinyoosha juu mikono!
Hata hivyo, kusambaratika kwa mradi wa kamba katika Delta ya Rufiji hakukumkatisha tamaa Mkapa; kwani aliendelea kuwakaribisha wawekezaji wa kigeni katika sekta nyingine kwa nguvu zake zote.
Kwa hakika, kila alipopata jukwaa la kuzungumzia suala hilo, Mkapa hakusita kulitumia kuwahakikishia wawekezaji wa nje kwamba anawaamini (yawezekanaje umuamini mwekezaji wa nje?), atawalinda na anawakaribisha nchini.
Kwa mfano, pamoja na kelele nyingi zilizopigwa na wananchi kuhusu jinsi machimbo ya Mererani na Geita yanavyowanufaisha wageni (makaburu) badala ya wazawa, bado Mkapa alikwenda Afrika Kusini kuwakaribisha wawekezaji zaidi wa sekta ya madini kutoka nchi hiyo.
Kama vile hiyo haikutosha, Mkapa aliamua kuwapa majaji na mahakimu nchini changamoto ya ‘kuwalinda’ wawekezaji wa kigeni (badala ya wazawa) alipokwenda Arusha kufungua mkutano wao.
Kwa hiyo; tunapolalamika, leo hii, suala la mikataba mibovu katika sekta ya madini – mikataba isiyozingatia maslahi ya nchi, asili yake ni Mkapa; kwani aliweka mazingira ya wawekezaji wa kigeni katika sekta hiyo kulindwa iwezekanavyo; hata pale maslahi ya taifa yanapokuwa hatarini!
Kwa hakika, uumini wake kwa sera za uwekezaji wa kigeni katika sekta ya madini unaweza kupimwa vizuri na kauli aliyopata kuitoa wakati akifungua mgodi wa Bulyanhulu uliopo Kahama, Shinyanga. Mkapa alisema hivi: “Wanaopinga sera za uwekezaji katika migodi ni wenye uchovu wa akili lakini waliojificha katika mwavuli wa wanataaluma.”
Mapenzi hayo ya kupindukia kwa wawekezaji wa kigeni katika sekta ya madini ndiyo yaliyomfanya Mkapa kukataa katakata kuundwa tume huru kuchunguza madai mazito ya mwaka 1996 kwamba watu 30 walikufa kwa kufunikwa na matingatinga wakati zilipochukuliwa hatua za kuwahamisha kwa nguvu wachimbaji wadogo wadogo katika eneo hilo ili mwekezaji wa kigeni (Barrick) apate kuingia.
Japo wanaharakati wa haki za binadamu wa ndani na nje ya nchi waliwasha moto hadi Benki ya Dunia (WB) na kwa serikali ya Canada kutaka wafute udhamini kwa Barrick kwa sababu ya kuhusika na mauaji hayo, Mkapa aliendelea kuikingia kifua mwanzo hadi mwisho, na hakutaka kamwe tume huru kuundwa kuchunguza.
Kwa sababu ya hulka yake hiyo ya kuibeba Barrick na kukataa tume huru kuundwa; ukweli kuhusu madai yale kwamba kuna watu 30 waliofukiwa katika eneo la mradi huo, haukuweza kuthibitishwa hadi Mkapa anaondoka Ikulu.
Mkapa na wasaidizi wake walikanusha kwa nguvu zote madai ya kufukiwa watu hao, lakini hapo hapo hawakutaka kabisa tume huru iundwe na ufukuaji mpya ufanyike ili ukweli ufahamike! Kwa nini walikataa? Jibu ni dhahiri; nalo ni kwamba hatua hiyo isingekuwa na maslahi kwa Barrick; hata kama ni maiti moja tu ingepatikana!
Hayo ndiyo ya Mkapa. Alimaliza muda wake wa urais na kuondoka Ikulu mwaka 2005 bila kukitegua kitendawili hicho cha Bulyanhulu. Na ukweli ni kwamba hakutaka kukitegua.
Sasa tunaye katika Ikulu yetu Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete. Naye huyu, hivi karibuni, ametwishwa kitendawili kingine kinachowahusu pia wawekezaji wa kigeni katika sekta ya madini.
Kitendawili hicho ni kile kinachouhusu Mgodi wa North Mara unaomilikiwa na kampuni ya Barrick. Mgodi huo umekuwa ukiachia sumu kuingia katika mto Tingithe, na hivyo kusababisha vifo vya zaidi ya watu 25; huku wengine wakiwa wamechubuka na kuvimba miili.
Idadi ya waliokufa (ikiwemo mifugo) inatarajiwa kuongezeka kwa sababu sumu hiyo aina ya cyanide huutafuna mwili kidogo kidogo, na hivyo athari zake ni za muda mrefu.
Hiyo ina maana kwamba waathirika wataendelea kufariki kidogo kidogo miaka mingi tu baada ya Barrick kuondoka North Mara wakati dhahabu katika mgodi huo itakapomalizika. Kwa ufupi; makovu na machozi yanayotokana na uwekezaji wao tutabakinayo miaka mingi tu baada ya wao (Barrick) kufungasha virago!
Hata hivyo, wakuu wa mgodi huo wamekuwa wakikanusha kuhusika na uingiaji wa sumu hiyo katika mto Tingithe ambao maji yake hutumiwa na wananchi kwa ajili ya mifugo na matumizi ya nyumbani. Na si tu wanakanusha kuhusika, lakini pia wanailaumu serikali kwa kuruhusu wanavijiji kulikaribia eneo la mgodi kinyume cha sheria.
Suala hili nyeti la mgodi wa North Mara linalohusu maisha ya Watanzania wenzetu limeibua mjadala mkubwa sehemu mbalimbali nchini; kama lilivyokuwa suala lile la mwaka 1996 la madai ya kufukiwa wachimbaji wadogo weadogo katika mgodi wa Bulyanhulu.
Kwa sababu ya kishindo cha kelele za wanavijiji wa North Mara, wanaharakati wa haki za binadamu, wabunge na vyombo vya habari, timu ya Bunge ilikwenda huko kufanya utafiti, na tayari imeshawasilisha ripoti yake kwa Spika. Ripoti hiyo bado haijawekwa wazi bungeni na kujadiliwa.
Aidha, Serikali mpaka sasa imepeleka watendaji wake wawili waandamizi (mawaziri wawili) kwenda North Mara kutafuta ukweli na kuuwasilisha kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Lakini mpaka sasa bado hatujui kilichomo kwenye ripoti zao. Hata hivyo, tunachofahamu (kupitia kwa mmojawao - Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Khamis Kagasheki), ni kwamba Barrick walimficha ukweli kwa kutompeleka kwenye maeneo yaliyoathirika hadi raia mwema mmoja alipoamua kumpeleka kwenye maeneo hayo!
Ukizingatia mienendo ya nyuma ya kampuni hiyo katika mgodi wake mwingine wa Buzwagi ambako fidia kwa wanavijiji, mpaka sasa, hazijalipwa; huku baadhi yao wakiwa ndani, hupaswi kuishangaa hila hiyo ya Barrick ya kutompeleka Waziri Kagasheki kwenye maeneo yaliyoathirika.
Ukizingatia yote hayo; swali kuu la kujiuliza ni hili: Je, Serikali ya Rais Kikwete itasimamia haki ya wananchi wake na kuhakikisha Barrick inaadhibiwa kwa unyama iliyoutenda North Mara? Je, Kikwete atahakikisha waathirika na familia za wafiwa wanalipwa fidia na Barrick?
Sina hakika na majibu ya maswali hayo; lakini nina hakika kwamba utakuwa mtihani mgumu kwa Rais Kikwete kuiadhibu Barrick; hata kama ripoti za uchunguzi mbalimbali wa kashfa hiyo ya North Mara zitainyooshea kidole kampuni hiyo ya Barrick.
Nasema hivyo kwa sababu Kikwete naye, kama alivyokuwa Mkapa, amejenga mapenzi makubwa mno na wawekezaji wa kigeni katika sekta ya madini nchini; kiasi kwamba hapendi kabisa kuwaudhi; hata pale maslahi ya wananchi (wanavijiji) au ya taifa yanapoumizwa.
Hii inaeleza ni kwa nini mpaka sasa serikali yake haijaifanyia kazi ripoti ya timu ya Jaji Bomani kuhusu sekta ya madini – ripoti ambayo baadhi ya mapendekezo yake yamewaudhi ‘kina Barrick’.
Itakuwa pia vigumu kwa Rais Kikwete kuiadhibu “ipasavyo” Barrick kutokana na unyama huo wa North Mara, kwa kuwa kigogo mkuu wa kampuni hiyo ni swahiba wake wa muda mrefu.
Si siri kwamba Rais Kikwete ni rafiki wa muda mrefu (zaidi ya miaka 14) wa bosi mkuu wa kampuni ya Barrick Gold Corporation ya Canada, James Sinclair. Kampuni hiyo ya Canada ndiyo inayomiliki mgodi huo wa North Mara na mingine kadhaa nchini.
Inaaminika kwamba uhusiano kati ya Rais Kikwete na Sinclair ulianza wakati Kikwete akiwa Waziri wa Nishati na umeendelea hadi sasa ambapo ni rais.
Kwenye toleo la Raia Mwema la Desemba 19, 2007, Lula wa Ndali Mwananzela (mwandishi wa safu), aliyaita mahusiano kati ya Rais Kikwete, Sinclair na Barrick kuwa ni “mahusiano ya pembetatu ya machozi”.
Kama hivyo ndivyo, hatutashangaa kama unyama huo wa Barrick huko North Mara utafumbiwa macho na Rais Kikwete kwa suala hilo kupigwa danadana hadi mwishowe life kifo cha asili!
Akizungumza bungeni, wiki iliyopita, mbunge wa Kahama, James Lembeli (CCM) alisema kwamba Barrick ni kampuni yenye kiburi cha ajabu na yenye jeuri. Labda kiburi hicho kinatokana na mahusiano ya Rais Kikwete, Sinclair na Barrick katika hiyo “pembetatu ya machozi”.
Lakini nihitimishe kwa kusisitiza tena kwamba makovu na machozi ya North Mara tutabakinayo Tanzania miaka mingi tu baada ya Barrick kufungasha virago kutokana na kumalizika kwa dhahabu katika mgodi huo!
Tafakari.
 
Msimammo wa Mkapa ndio SIFA YA UONGOZI...alieleweka na kutambulika alikuwa na visheni gani katika uongozi wake..

Nampongeza BWM kwa uwezo wake wa kusimamia yale anayoyaamini hasa unapokuwa kiongozi kuanzia ngazi ya familia mpaka Taifa.

Ametufundisha tunu ya Uongozi ni kusimamia kwa dhati yale unayoyaaminii ili kufikia lengo ulilonaloo.

Kwa North Mara ni vichekeshoo tuu kwani Viongozi wote waliofika hawana kinachowaelekeza wasimamie lipi zaidi ya kulalama tuu kama kundi lisilokuwa na kiongozi..

Uko wapi msimamo wa Mkuu wa kaya katika hili zaidi ya maagizoo ya kisiasa ili muda uende..

Mkapa aliamini katika kujenga uchumi mpana kupitia wawekezaji wa nje kwa muda wake wotee..Leo hii dira ni ipi????????????????????????????
 
Ingekuwa ni katika nchi zenye mwamko Mkapa angefikishwa kizimbani kwa high treason. Alichowafanyia Watanzania ni worse than high treason.
 
Mali za Muluzi zakamatwa Malawi


Mwandishi Wetu, BLANTYRE,Malawi
Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo
Agosti 5, 2009
rC.jpg

bul2.gif
Ni magari 44, jumba la biashara

TAASISI ya Kuzuia Rushwa nchini Malawi (ACB) imekamata mali za rais wa zamani wa nchi hiyo, Bakili Muluzi, kama dhamana katika kesi ya rushwa inayomkabili.
Hatua hiyo ya ACB imechukuliwa wakati bado inaendelea na uchunguzi katika kesi hiyo ambayo Muluzi anadaiwa kuingiza kwenye akaunti yake fedha za wafadhili zinazofikia dola za Marekani milioni 11.
Taasisi hiyo imesema kwamba imekamata jumba analoishi lenye thamani ya mamilioni ya fedha lililoko katika mji wa biashara wa Blantyre. Imesema pia ya kuwa imekamata magari 44 kati ya magari 149 ambayo rais huyo wa zamani wa Malawi anamiliki.
Vingine vilivyokamatwa ni jumba lake la biashara la Keza Office Park ambalo lilizinduliwa kwa mbwembwe, mgeni mwalikwa wakati huo Rais wa Tanzania, Benjamin Mkapa, na akaunti zake zote za benki.
Habari zinasema wakati hayo yakiendelea, Muluzi mwenyewe yuko Uingereza kwa matibabu.
Ofisa Uhusiano wa ACB, Egrita Ndala, amekaririwa na gazeti la kila siku la Malawi- The Daily Times, akisema taasisi hiyo bado inaendelea na uchunguzi wake.
" Kikosi cha Kupambana na Rushwa (ACB) bado kinaendelea na uchunguzi wa mali nyingine ili kujiridhisha na umiliki wake. Ni vigumu kwa sasa kusema mali nyingine ambazo zimepangwa kuchukuliwa, " alisema Ndala.
Katika hatua nyingine, kabla ya tukio hili la wiki hii, hivi karibuni rais huyo wa zamani wa Malawi alizuiwa kusafiri kwenda Uingereza na pasi yake ya kusafiria ikanyang'anywa baada ya kuzuka uvumi kwamba angetorokea Uingereza.
Hata hivyo, aliruhusiwa kuondoka kabla ya ACB kuvamia mali zake kama dhamana endapo atashindwa kesi hiyo na hatarejea nchini humo.
Habari kutoka nchini humo zinasema ya kuwa mwanasheria wa Muluzi, Jai Banda, ameomba zoezi la kukamata mali za Rais huyo lisitishwe. Muluzi aliwahi kukamatwa huko nyuma kwa kwa kesi hiyo hiyo.
 
Njia ya Chiluba, Muluzi bado yamsubiri Mkapa

mkapa2.jpg


Na Mbasha Asenga
MwanaHALISI


KUPAMBANA katika kufunika kashfa za ufisadi au kujaribu kutosa wale ambao waweza kuonekana kondoo wa kafara kumeshamiri kipindi cha utawala wa awamu ya nne.
Serikali ya rais Jakaya Kikwete imeshadhihiri ni majeruhi wa kashfa hizi kwa sababu moja tu: kwa makusudi iliamuliwa tangu awali kuwepo watakaolindwa kwa nguvu zote hata wafisidi nchi namna gani.

Bila kutaja kesi zilizo mahakamani kwa kuchelea kuingilia uhuru wa mahakama, yatosha tu kusema utaratibu wa kushughulikia kashfa kwa nia tofauti – ya kusafishana na nyingine ya kutosana na kuangamizana – kamwe hautaisaidia serikali.

Ukitafakari kwamba serikali kwa miaka mitatu na ushei sasa imetumia kila aina ya nguvu na mbinu kufunika baadhi ya watuhumiwa wa kashfa ya ufisadi kama vile wamiliki wa kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd, huku ikijitahidi kuharakisha wengine kufikishwa mahakamani, unashindwa kujua nia ya vita dhidi ya ufisadi ni nini hasa.
Lakini ukiweka kando habari za ufisadi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), jaribu kufikiria kinachoendelea sasa kuhusu mgodi wa Kiwira. Je, nia ni kurekebisha kasoro zilizotokea katika uuzaji mgodi huu mali ya taifa au ni mbinu nyingine ya kumsafisha rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, dhidi ya tuhuma za ufisadi?
Vita na harakati za serikali katika kusafisha uoza ndani yake inakuwa ngumu si kwa sababu ushahidi haupo, ila ni kwa sababu tu ya undumilakuwili upande wa serikali.

Wakati kila Mtanzania akijua kwa hakika kwamba makundi ndani ya chama tawala yamekifikisha chama pagumu, bado serikali kwa kutofahamu nia ya kulinda kundi hili na kuangamiza lile, imeendeleza sera za kubaguana katika kushughulikia ufisadi.

Kwa mfano, inakuwa vigumu mno wananchi wengi kuamini vita dhidi ya ufisadi ni mkakati makini wakati kampuni iliyochukua karibu asilimia 30 ya fedha za EPA, haijaguswa.

Hatari kubwa zaidi ni pale unapoona mkuu wa chombo mahsusi cha kusimamia mkondo wa sheria kutekelezwa kama Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), analalama tu badala ya kuchukua hatua kubana wenye Kagoda. Eti anaogopa serikali itaishia tu kukamata waliosajili kampuni hii huku ikiwakosa wale waliowatuma.

Inawezekana vipi kwa mfano chama kinachopambana na ufisadi na serikali inayotumia vyombo vyake kuchunguza mafisadi ili kuwashitaki na kwa wakati, viongozi wake wawe wanakaa meza moja na watuhumiwa wakuu tena wakiwatazama kama malaika wasio na hata chembe ya tuhuma?
Wapi umesikia ujasiri wa namna hii? Lakini ndani ya serikali hiyohiyo watu wenye tuhuma za kuungaunga kwa mshumaa wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na kesi ambazo hata ofisi ya DPP imeyumba kuzitolea ushahidi.
Tarehe 18 Machi, mwaka huu, katika safu hii niliandika uchambuzi uliokuwa na kichwa cha habari: "Muluzi aonja korti, Mkapa presha juu."

Uchambuzi huo ulitokana na kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa rais wa zamani wa Malawi, Bakili Muluzi, ili kujibu mashitaka 80 ya rushwa na kujipatia mali ya umma kinyume cha taratibu.
Muluzi, aliyeingia madarakani kama mfanyabiashara, muda wake wa kukaa madarakani ulipita kwa kasi, lakini alijaribu kubadili katiba ili agombee muhula wa tatu, alikwama.

Baada ya kukwama kwa sababu alikuwa na siri moyoni, Muluzi alitafuta njia ya kujinusuru, alimtafuta Bingu wa Mutharika kwa njia ileile ya Frederick Chiluba wa Zambia ya kumtafuta Levy Mwanawasa, ili amlinde. Siri yao ilikuwa ni ya kufunika kombe mwanaharamu apite.
Kwa bahati nzuri, marais hawa majirani zetu, Muluzi na Chiluba, baada ya juhudi zao za kubadili katiba kukwama na kudhani kwamba eti salama yao itapatikana kwa kumtafuta mrithi wa kuwalinda, walikwama na wameendelea hawajakwamuka.
Kwa hiyo fomula ya Chiluba ambayo Muluzi aliikopi na kuitumia kavukavu, imekataa kufanya kazi; ila kwa bahati nzuri, kwetu Tanzania bado marais wastaafu wanaendelea kufurahia maisha yao ya kupumzika baada ya kutumikia umma, lakini kila mmoja kwa hisia tofauti moyoni mwake.

Nilipata kusema wapo waandishi mahiri, ninaowaheshimu ambao walisema wazi wanamuomba radhi rais mstaafu Mzee Ali Hassan Mwinyi. Kwa nini Mwinyi aombwe radhi?

Ni rais aliyezuliwa mengi mchana kweupe; alikejeliwa hata na watu wasioweza kupenga makamasi kwa kuwa tu aliruhusu uhuru wa kujieleza, alifungua minyororo ya uchumi, alifungua haki ya watu kujieleza kisiasa. Mwinyi aligeuzwa gunia ya kujifunzia kurusha ngumi kama ni kuazima lugha ya mabondia!
Wahenga walituasa kwamba ng'ombe hutambua thamani ya mkia wake siku ukikatika na nzi wanapoanza kumzonga. Hivyo ndivyo ilivyokuwa baada ya Mzee Mwinyi kuondoka madarakani na watu kuonja utawala wa mrithi wake.
Rais mbabe mwenye ubavu wa kufokea hata waliompigia kura, jasiri wa kutukana wananchi, mwenye kujiona mwelewa wa kila kitu hata utaalamu wa kugundua bomu la nyukilia.
Benjamin, mwanasiasa aliyeokwa ili umma uamini yu mtu safi, muadilifu na mbebaji mzuri wa dhamana ya uongozi kwa moyo wake wote. Ni kiongozi aliyejitoa katika muonekano wa ngozi ya kondoo, lakini baada ya kushika madaraka akaivua na kuonekana mbwa mwitu asilia.

Sasa baada ya kuacha madaraka, si tu hana tena ubavu wa kufoka, kutisha na kunyima magazeti pumzi ya matangazo; bali pia anakabiliwa na tuhuma kama za akina Muluzi na Chiluba.

Tawala zao zinashabihiana. Kila mmoja alijihusisha mno na harakati za kujinufaisha na familia yake. Mkapa na makampuni, Mkapa na Kiwira; Mkapa na ununuzi wa nyumba za serikali, Mkapa na ununuzi wa nyumba bila dhamana- urais ukiwa dhamana, Mkapa hapa Mkapa kule.
Kila uchao Watanzania wameelezwa mawaa ya Mr Clean wao! Hadi sasa Mkapa ana nafuu moja, kwamba katika vita dhidi ya ufisadi ameangukia kundi lile la kulindwa, kusafishwa na kufunika kombe mwanaharamu apite.

Bado nguvu za dola zinatumika asifikie hatua ya Chiluba au Muluzi – ya kushitakiwa – bado anapumua kwa rehema ya makundi ya CCM na ndani ya serikali.
Ni kwa muda gani Mkapa atabaki salama; hakuna ajuae. Ila itoshe tu kusema atabaki salama kadri hali hii ya sasa; ya mvutano wa makundi ya kimaslahi ndani ya CCM, itabakia.

Ikitokea mizania kubadilika kwa vyovyote vile, au kwa sababu kundi moja limezidi kete jingine kwa kiwango kikubwa zaidi; bado Mkapa hatakwepa njia waliyopita Chiluba na Muluzi.
 
• Ataka aunganishwe na Mramba, Yona

PAMOJA na jitihada za serikali kumsafisha Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, kuwa ni muadilifu, si fisadi, mchapakazi; Mbunge wa Karatu, Dk. Willbrod Slaa, ametaka kiongozi huyo afikishwe kwenye vyombo vya sheria kwa kuisababishia hasara serikali kupitia uwekezaji katika mgodi wa makaa ya mawe Kiwira.

Kauli hiyo ya Dk. Slaa, imekuja siku moja baada ya Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja akiwa mkoani Mbeya katika mgodi wa Kiwira, kutangaza kuanza kuwalipa wafanyakazi wa mgodi huo katika kipindi kifupi kijacho kuanzia jana.

Akizungumza na Tanzania Daima jana, Dk. Slaa alisema wananchi hawapaswi kushangilia hatua hiyo ya serikali, bali wanapaswa kwenda mbele zaidi kwa kutaka walioshiriki katika matumizi mabaya ya ofisi zao, akiwemo Mkapa wafikishwe kwenye vyombo vya sheria pasipo na kubagua.

Alisema kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imebainika mgodi huo kupata dola milioni saba (zaidi ya sh bilioni saba) kutoka katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa ajili ya kuuendeleza, lakini mwekezaji hakutimiza lengo hilo.

Dk. Slaa alisema pamoja na serikali kuwalipa wafanyakazi wa mgodi huo malipo yao, ni vema ikawawajibisha wale wote waliohusika na uwekezaji huo aliouita wa kitapeli, akiwemo Mkapa na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona.

“Nimefurahi kusikia wafanyakazi wa Kiwira watalipwa fedha za mishahara yao muda si mrefu kutoka sasa, lakini serikali inapaswa kumuwajibisha Mkapa na Yona, ambao ndio walikuwa wakiumiliki na kuchukua kiasi cha sh bil 7/- kutoka NSSF,” alisema Dk. Slaa.

Alisema makosa ya matumizi mabaya ya ofisi na kuisababishia hasara serikali, ndiyo yaliyowafikisha mahakamani waliokuwa mawaziri katika awamu ya tatu; Yona (Nishati na Madini), Basil Mramba (Fedha) na Gray Mgonja aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Uchumi, lakini anashangazwa na kutochukuliwa hatua kwa Mkapa na watendaji wengine.

“Kwa nini serikali isimfikishe mahakamani Mkapa na watendaji wengine kwa kuisababishia hasara kama ilivyofanya kwa Yona, Mramba na Mgonja? Kuna nini hapa?” alihoji Dk. Slaa.

Kwa muda mrefu sasa, mgodi wa Kiwira ambao ulijengwa na Serikali ya China kwa dola bilioni 4 na kukabidhiwa kwa Serikali ya Tanzania mwaka 1988, umekuwa ukihusishwa na kumilikiwa na familia ya Mkapa kupitia Kampuni ya ANBEN na Yona kupitia Kampuni ya DEVCONSULT Limited.

Mgodi huo unadaiwa uliuzwa kwa kampuni hizo kwa bei ndogo (sh mil 700/-), ambapo kiasi cha sh mil 70/- ndicho kilicholipwa serikalini, lakini pia mwekezaji alishindwa kuuendesha kwa sababu mbalimbali, ikiwemo kutokuwa na mtaji wa kutosha.

Kutokana na sakata hilo, baadhi ya wanasiasa kutoka ndani na nje ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamekuwa wakishinikiza kuondolewa kinga kwa Mkapa ili aweze kushtakiwa kwa kufanya biashara akiwa Ikulu.

Shinikizo hilo la wanasiasa na wanaharakati limekuwa likikumbana na vikwazo vingi, ikiwemo serikali kumtetea kiongozi huyo kwa kusema kuwa si fisadi na aachwe apumzike kwa kuwa aliifanyia nchi mambo mengi mazuri.

Serikali ilikwenda mbali zaidi pale Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alipotangaza kuzichukua hisa za mgodi huo na kumtafuta mwekezaji ambaye atakuwa na uwezo wa kuuendesha na hatimaye kuzalisha kile kilichotarajiwa na kutoa ajira zaidi.

Uamuzi huo ulionekana kupingwa na baadhi ya wanasiasa kwa madai kuwa, utaendelea kuzalisha na kufuga viongozi wabovu wasio na uchungu na rasilimali za taifa, hivyo jambo pekee la kukomesha ni kuanza kumuwajibisha Mkapa kwa mabaya aliyoyafanya bila kuangalia mazuri.

Katika hatua nyingine, Dk. Slaa, alimtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia, kujiuzulu wadhifa wake pamoja na watendaji wengine wa wizara hiyo kwa kushindwa kudhibiti tatizo la upotevu wa fedha za serikali kupitia wafanyakazi hewa wa sekta ya afya.

Alisema ni aibu na uzembe kwa serikali kupoteza zaidi ya sh bil 7/- kwa kuwalipa mishahara wafanyakazi hewa wa sekta ya afya na elimu katika kipindi cha miaka mitano.

Dk. Slaa, alisema ameshtushwa na idadi ya watumishi hewa 1,511 wa sekta ya afya waliolipwa kiasi cha sh bilioni 4.48 kuanzia mwaka 2005 hadi Machi 2009, ambao walikuwa wakipata fedha za mishahara kupitia akaunti za benki zao.

Alisema kitendo hicho kinadhihirisha uzembe mkubwa uliopo miongoni mwa watendaji wa serikali na kuzidisha ugumu wa maisha kwa wananchi, kwa kuwa fedha ambazo zingetumika katika shughuli za maendeleo zinaliwa na wajanja wachache wasio na uchungu na nchi yao.

Aidha, alibainisha kuwa anashangazwa na kutofikishwa mahakamani kwa wahusika kwa kuwa ushahidi wa kutenda wizi huo hauhitaji upelelezi mkubwa, kwani akaunti zao zinaweza zikatumika kuthibitisha wizi waliokuwa wakiufanya.

“Mimi nilitarajia juzi Waziri Ghasia angetueleza kuwa watu kadhaa wanashikiliwa na vyombo vya dola, badala ya kutueleza kuwa watakuwa wakali kwa watu wanaofanya wizi huo. Ghasia anapaswa aachie ngazi,” alisema Dk. Slaa.

Alisema kwa hali ilivyo, inaonekana serikali ilikuwa likizo katika kipindi chote ambacho watumishi hewa walikuwa wakijipatia mabilioni ya fedha za walalahoi bila kuyatolea jasho, hivyo ni vema watendaji wote waliohusika wakawajibishwa na ikiwezekana wafikishwe mahakamani.

Aliongeza kuwa, kama sekta mbili za elimu na afya zimetafuna bilioni saba, basi kuna uwezekano mkubwa wa kugundulika kwa ufisadi wa kutisha katika sekta nyingine ambazo bado hazijafikiwa na zoezi la uhakiki wa rasilimali watu.

“Tumekuwa tukipiga kelele nyingi kuwa nchi hii si masikini bali ufisadi unaofanywa na baadhi ya watendaji wa serikali ndiyo unaokwamisha maendeleo ya wananchi, sasa hebu tuangalie sekta mbili zimepoteza zaidi ya bilioni saba je, hizo nyingine?” alihoji Dk. Slaa.

Juzi, Waziri Ghasia, alitangaza serikali kupata hasara ya sh bil 4.48 kupitia ulipaji mishahara watumishi hewa wa sekta ya afya katika kipindi cha miaka minne (2005-2009).

Kubainika kwa hasara hiyo kunatokana na zoezi la uhakiki wa wafanyakazi hao katika sekta hiyo uliofanyika mwaka wa fedha 2008/2009, kwa lengo la kuangalia matumizi ya rasilimali watu na ubadhirifu katika eneo la malipo ya mishahara.

SOURCE: TANZANIA DAIMA
 
Back
Top Bottom