Amani iwe Nanyi, nawapeni mkono wa Krismas!
Mkandara nashukuru sana kwa kuongezea uhai kwenye hii mada, pamoja na wachangiaji wengine wote.
Nafikiri kinachowashina wengi kuelewa ni kwa nini Mkapa aonekane ni Rais mbovu pamoja na kujitutumua kwake kulipa madeni (ambayo tuliishia kusamehewa wala si kuyalipa), kuongezeka wa wawekezaji(walianza nyakati za Mwinyi, Mkapa akafanya urahisi kwa kulegeza kodi na ushuru ulioruhusu utapeli na uhujumu) kujenga shule na barabara( ambazo hazikuwa na msingi imara) na uafanisi serikalini.
Ukiangalia kosa la kwanza la uhujumu BOT, jiulize je huoni kuwa uhujumu wote uliotokea BOT huku Mramba, Yona, Ballali na Mgonja wakiwa vinara unatokana na uzembe wake ikiwa yeye kama Rais hakukagua mahesabu ya mwaka ya BOT?
Ikiwa ni yeye aliidhinisha Jeshi lianzishe mradi wa Meremeta, na kuruhusu usiri wa kukopa nje ya nchi na wala si ndani ya nchi kutumia mabenki yetu na kisha kushurtisha BOT na serikali ilipe deni hamuoni kuwa kuna kasoro na matumizi mabaya ya uongozi na dhamana ya madaraka? je uaminifu alioapia katika katiba ulikwenda wapi kwa kuhakikisha kuwa JWTZ linafungua kampuni na kuisajili nje ya nchi kisha ije kufanya kazi nchini?
Je nia hii ilikuwa ni kuhakikisha Meremeta inapata huduma kama Barrick, misamaha ya kodi na ushuru, upendeleo kutoka Serikaini na usiri kusema hii ni kampuni ya kigeni tuwape zulia jekundu?
BOT walipoendelea kutumbua kujenga majengo yao huku kwa kutumia pesa zaidi ya mtaji mzima wa kuendesha BOT, je ni nani aliidhinisha hizo pesa bila kuwa mwangalifu kujua kuwa gharama ya ujenzi wa majengo ni zaidi ya mtaji wa BOT?Jek ama BOT ndio wadhibiti wa sarafu yetu ikiwa ni pamoja na kutuliza mfumuko wa bei, kupanda na kushuka kwa thamani ya shilingi, iweje walitumia pesa nyingi zaidi ya mtaji wao kwa matumizi ambayo hayakuwa ya ulazima?
Mimi si mchumi, lakini kama wale wafanyabiashara wa Tandale au mtu mwingine, inapofika hatua kuwa gunia la mchele kutoka Shinyanga linapata tabu kuja Dar kuuzwa lakini gunia kutoka Kampuchea linafika kwa uharaka na hata kupunguziwa kodi, hiyo ni dalili tosha kuwa uchumi si mzuri na kuna udhaifu ndani ya uongozi na mipango. Leo bidhaa tunazozalisha hakuna Mtanzania anayeweza kununua na mzalishaji huishia kuingia hasara. Waulizeni watu wa Kilimanjaro na Arusha kuhusu kahawa yao na kwa nini wanakimbilia kulima maharage au ulezi.
Sasa kama BOT walitumia pesa ambazo zinazidi mtaji na hivyo kushusha thamani ya fedha yetu, je Mkapa alikuwa wapi kudhibiti matumizi haya holela na si kujenga barabara kutoka Shinyanga au kuboresha kilimo cha kahawa na hata usindikaji ili pato letu kama Taifa lisitegemee kodi na wawekezaji pekee bali lishamiri kutokana na uuzaji wa mali asili nje ya nchi?
Leo hii nimesoma kuwa vita vya Kagera vilitugarimu dola za Marekani $500 milioni, hivyo ni wazi kuwa Mwinyi alipokuja kazi yake ilikuwa ni kusisimua uchumi.
Lakini Mwinyi, hata kama alikuwa ndiyo Mzee Ruksa au mkewe alikamatwa na dhahabu (je tuna ushahidi kuwa alikuwa ameiba hiyo dhahabu?) hakufanya maamuzi mabaya ama binafsi au kwa uzembe. Cha kumlaumu Mwinyi si kinachojadiliwa hapa, bali ni alichofanya Mkapa kuruhusu mianya ya kuhuju uchumi.
Ningetegemea kuwa Mwinyi na Mkapa wangeleta mapinduzi ya uzalishaji mali kutumia mfumo wa Kibepari na miundo mbinu yake na si kukimbilia soko huria kama mfumo wa uzalishaji ambao umeendeleza utegemezi.
Nyerere ana makosa yake ya kiutendaji. Azimio la Arusha halikuwa kosa lake binafsi wala hakuamua pekee,vijiji vya ujamaa, elimu ya UPe na mengineyo yalikuwa ni maamuzi ya Chama na Serikali na si Nyerere pekee.
Ndiyo maana hata Azimio la Zanzibar, simnyooshei Mwinyi au Malecela kidole kwa kuwa yalikuwa maamuzi ya jumla na si mtu mmoja au wawili.
Lakini maamuzi mengi ya Mkapa ambayo ndiyo chimbuko la kesi hii yalikuwa ni yake binafsi bila hata kuhusisha Chama au Serikali.
Jee hii inatokana na kiburi cha kuwa Rais wa nchi na kuamini ana madaraka ya kufanya kila anachotaka kwa kuwa yeye ni Rais?
Ikiwa Katiba yetu inasema hivi katika kifungu cha 27
27
.-(1) Kila mtu ana wajibu wa kulinda mali asilia ya Jamhuri
ya Muungano, mali ya Mamlaka ya Nchi na mali yote
inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi, na pia kuiheshimu mali
ya mtu mwingine.
(2) Watu wote watatakiwa na sheria kutunza vizuri mali ya
mamlaka ya nchi na ya pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu
na ubadhilifu, na kuendesha uchumi wa taifa kwa makini kama
watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadaye ya taifa lao.
iweje leo tutetee kinga kwa Mkapa kwa kushindwa kulinda mali asili ya jamhuri au kutunza mali za jamhuri kwa kudai ana kinga?