SoC01 Mitandao ya kijamii kichocheo kipya cha Demokrasia

Stories of Change - 2021 Competition

Magobe T

JF-Expert Member
Mar 19, 2008
4,621
2,567
Kwenye dunia ambayo demokrasia imeshuka sana katika asilimia 70 ya nchi 167 zilizofanyiwa utafiti duniani, kwa mujibu wa The Economist Intelligence’s Unit Democracy Index 2020 tangu kushuka huko kuanze kuonekana mwaka 2006, tunategemea sana mitandao ya kijamii kuhuisha demokrasia kwa sababu ni muhimu kwa maendeleo endelevu.

Watu wengi duniani wanatumia mitandao ya kijamii kupokea na kutoa habari mbalimbali ambazo ni mpya na hazijavifikia vyombo vya habari vya magazeti, redio na televisheni. Baadhi ya watu wameacha kusoma magazeti, kusikiliza taarifa ya habari inayosomwa kwenye vituo vya redio na televisheni kwa sababu wanaamini watakachokisikia ni kile ambacho tayari wanakifahamu kupitia mitandao ya kijamii.

Kichocheo kipya cha demokrasia

Mwelekeo mpya wa kuhabarishana unaibeba mitandao ya kijamii, hasa kwa kuzingatia kwamba karibu katika kila familia kuna mtu mmoja au zaidi wenye simu za kigangani hata kama hawana redio au televisheni na wanazitegemea sana kwa mawasiliano yao na katika shughuli zao za kila siku.

Kadiri mitandao ya kijamii inavyoendelea kutumiwa zaidi ndivyo pia inavyowapa watumiaji fursa ya kupokea na kutoa habari kwa wakati. Kutokana na kutokuwa na urasimu wa kutengeneza na kutoa habari, ni dhahiri kwamba mitandao ya kijamii ni huru zaidi katika kujenga na kuendeleza demokrasia.

Kwa nchi kama Tanzania demokrasia ni takwa la kikatiba na ina maana ya mfumo wa uongozi wa serikali na nchi na utendaji unaoheshimu haki ya uhuru wa kusema, kukusanyika, kuabudu, kutoa maoni na kushiriki uchaguzi huru na wa haki, kusisitiza utawala wa sheria na wa haki, utawala wa walio wengi, pamoja na kuheshimu haki za wachache, yakiwemo makundi mbalimbali ya watu.

Demokrasia ni pamoja na haki ya vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara na kuuza sera zao kwa wananchi, kupata na kuwajenga wanachama wapya, kujenga chama na kudai na kulinda haki zao kwa njia ya amani katika sehemu yoyote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ibara 9(k) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema mamlaka ya nchi na vyombo vyake vyote vinawajibika kuelekeza sera na shughuli zake zote katika lengo la kuhakikisha - kwamba nchi, pamoja na mambo mengine, inatawaliwa kwa kufuata misingi ya demokrasia.

Kuwa na taasisi na mifumo imara ya siasa ya demokraisia ni kichocheo pia cha maendeleo kwa sababu ya kuwa na mazingira wezeshi ambapo uchaguzi wa sera unategemea wananchi wanaoweza kuifanya serikali na vyombo vyake iwajibike kwa utekelezaji wake. Hivyo, mitandao ya kijamii ni afya ya demokrasia.

Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa haki ya uhuru wa maoni. Inasema kila mtu ana uhuru wa kuwa na maoni yake na kutoa nje mawazo yake na, au kutafuta, kupokea na kutoa habari bila ya kujali mipaka ya nchi. Inasema pia kwamba kila mtu ana uhuru wa kuwasiliana na kulinda mawasiliano yake yasiingiliwe kati na ana haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi, na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii.

Kupokea na kutoa habari
Kwa vile baadhi ya watu mara nyingi wanakuwa hawako nyumbani wakati wa taarifa ya habari ya redio au televisheni na pia kulingana na shughuli zao za kila siku au kwa kipato chao hawawezi kununua magazeti kila siku, hawa wote hutegemea zaidi mitandao ya kijamii kufahamu kinachoendelea nchini na sehemu mbalimbali duniani.

Kuendana na mwelekeo huu mpya wa kuhabarishana, kila chombo cha habari kimeanzisha kitengo cha habari za mtandaoni ili wasomaji wa magazeti au wasikilizaji wa redio na watazamaji wa televisheni waweze pia kupata habari mpya kupitia simu zao za kiganjani.

Taasisi na wizara mbalimbali za serikali na asasi za kiraia, pamoja na mashirika ya dini, zinatumia mitandao ya kijamii kupokea na kutoa habari. Baadhi ya viongozi wa serikali wanatumia mitandao ya kijamii kupokea na kutoa habari zao. Hivyo, mitandao ya kijamii ni muhimu sana kwa mawasiliano katika dunia ya leo.

Chanzo muhimu cha habari mpya
Kukua kwa kasi kwa mitandao ya kijamii kunatokana na kukua kwa teknolojia ya mawasiliano. Baadhi ya habari ambazo zimeisaidia serikali, vyama vya siasa, asasi za kiraia, mashirika ya dini na makundi mbalimbali ya jamii kuchukua hatua ni habari zilizoanzia kwenye mitandao ya kijamii. Hii inaonyesha umuhimu wa wamiliki wa mitandao ya kijamii kuwekeza kwenye kuboresha mitandao yao ili itole habari ambazo zinaisaidia jamii na hasa zinakuza uhuru wa kujieleza na kutoa maoni kwa namna ambayo inajenga taifa huru.

Uzuri wa mitandao ya kijamii ni kwamba habari zake zinatoka muda huohuo zinapopatikana bila kusubiri muda maalumu wa taarifa ya habari au kusoma magazeti asubuhi kesho yake. Kuna pia ushiriki wa moja kwa moja wa wananchi katika kupokea au kutoa habari bila urasimu ulio kwenye vyombo vingine vya habari. Habari zinatoka kama zilivyo bila kubadilishwa kutokana na kuhaririwa.

Habari zilizohaririwa wakati mwingine zinabadilishwa maudhui kulingana na masilahi ya chombo cha habari husika, wakati siyo hivyo kwa mitandao mingi ya kijamii, labda ile inayomilikiwa na taasisi, kampuni, vyombo vya habari au wanasiasa ambao wana masilahi na habari zinazotolewa.

Kutoa habari bila upendeleo
Mitandao ya kijamii inatoa habari kwa jamii bila upendeleo. Kwa sababu hii, inasaidia kutoa fursa hata kwa watu wengine ambao habari zao zisingeweza kutoka katika vyombo vingine vya habari kwa sababu za kisiasa au kiimani.

Idadi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii na wageni (mfano jamiiforums yenye wanachama waliosajiliwa zaidi ya 580,590) ukiingia mtandaoni unakuta kwa muda huo wanaotumia mtandao ni zaidi ya 4,400 (wanachama waliosajiliwa: zaidi ya 1,460 na wageni: zaidi ya 2,940). Fikiria kwa siku nzima, juma, mwezi au mwaka mzima wanakuwa wamefika wangapi. Na huu ni mtandao mmoja tu wa kijamii, wakati bado kuna mingine mingi.

Mitandao ya kijamii inatoa habari zinazosambaa kwa watu mbalimbali duniani kote kwa wakati mmoja – Afrika, Ulaya, Marekani, Amerika Kusini na Asia, isipokuwa kwenye nchi ambazo zina udhibiti mkubwa wa habari zinazoingia au kutoka.

Mitandao ya kijamii ni kiungo muhimu kati ya serikali na wananchi kwa maana ya kuhabarisha wananchi juu ya miradi ya maendeleo, uwekezaji, kuvutia watalii, kulinda ushirikiano na wadau na washirika wa maendeleo na mataifa rafiki. Kuna kuuhabarisha wananchi pia juu ya mipango ya muda mfupi na mrefu ya serikali, kuibua vitendo vya rushwa au uhalifu, utoaji haki, usimamizi wa rasilimali za taifa na usalama wa raia na mali zao na pia kuihabarisha serikali juu ya matarajio ya wananchi kwa serikali na viongozi wao.

Mitandao ya kijamii ina wajibu pia wa kuibua habari za mambo ambayo hayaendi vizuri ili serikali iyafanyie kazi habari hizo kwa kuchukua hatua stahiki. Hii inatokana na uhuru mkubwa wa wachangiaji na watumiaji kuliko ilivyo katika vyombo vingine vya habari.

Mitandao ya kijamii ina mchango mkubwa pia katika kuhakikisha tunakuwa na mchakato wa uchaguzi huru, wa haki na wa amani na kujenga vyama vya siasa shindani na asasi za kiraia kwa kutoa habari zao kwa usawa ili wananchi wazifahamu na wafahamu viongozi wa vyama hivyo vya siasa na asasi za kiraia wanafanya nini na wapi. Pamoja na hayo, kwa vile mashirika ya dini yanasaidia kutoa huduma muhimu za kijamii, za kiroho na kujenga maadali, haya pia habari zao inabidi zitangazwe kutokana na mchango yanayotoa kwa serikali na kwa jamii.

Kuna pia makundi maalumu katika jamii – wazee, wanawake, watoto, vijana, wajasiliamali, wakulima, wafugaji, walemavu, watoto wa vitaani au wanaoishi katika mazingira magumu – hawa nao habari zao ziandikwe mtandaoni.

Kufanya hivi ni kufanya sauti ya serikali na viongozi wake na wananchi na makundi mbalimbali katika jamii isikike. Hapa ndipo serikali itakapopata taarifa sahihi za wananchi wake na wananchi pia na makundi mbalimbali watapata pia taarifa sahihi za serikali na kuzifanyia kazi kwa kujiletea maendeleo.

Changamoto za mitandao ya kijamii
Hata hivyo, changamoto kubwa ya mitandao ya kijamii ni kujua ukweli wa habari mpya zinazoripotiwa. Vyanzo vingi vya habari za mtandaoni vinatumia majina bandia na hata kwenye habari husika mara nyingi hakuna watu walioulizwa wanaoweza kuthibitisha ukweli wa habari iliyoripotiwa.

Hii ni kwa sababu kila mtumiaji wa mitandao ya kijamii (aliyesajiliwa) anaweza kuripoti tukio aliloliona au kusikia bila kufuata utaratibu unaotumiwa na vyombo vingine vya habari, wa kutafuta kwanza ukweli wa habari husika, ingawa baadhi ya vyombo hivyo pia huripoti baadhi ya habari bila kuzingatia taaluma au maadili ya uandishi wa habari. Mfano, kudhalilisha baadhi ya watu au kusema uwongo juu yao kwa lengo la kuwachafua kwa masilahi binafsi.

Changamoto ingine ya mitandao ya kijamii ni kuibuka kwa habari za uwongo kuhusu baadhi ya watu kama vile viongozi wa serikali,viongozi wa dini, wanasiasa, wasanii na watu wengine mashuhuri au kuripoti tukio lolote kwa lengo la kuhamisha mjadala unaoendelea.

Nini kifanyike?
● Kuendelea kutumia vizuri mitandao ya kijamii katika kupokea na kupata habari maana ndio mwelekeo mpya wa kupashana habari na kuendeleza tasnia ya habari.
● Kuboresha uwasilishaji wa habari za mtandanoni ili ziaminike na kuwafikia walengwa.
● Kuachana na habari zinazolenga kuwachafua watu wengine au kuwavunjia heshima machoni pa jamii kwa masilahi binafsi.
● Kuendelea kupokea na kutoa habari ambazo zina masilahi ya umma/taifa maana ni muhimu kwa ujenzi wa taifa.
● Kuwekeza kwenye kuboresha mitandao ya kijamii ili kuwafikia watu wengi zaidi maana mitandao hii ndicho kichocheo kipya cha kujenga na kukuza demokrasia.
● Mitandao ya kijamii iwe kichocheo pia cha kujenga maadili na utamaduni wa kuchukia kupokea au kutoa rushwa maana rushwa ni adui wa haki.

Growing democracy gap for 15 years.png
 
Back
Top Bottom