[h=2]29 MARCH 2012[/h][h=3]
[/h]
*Wapiga kura wapinga kauli za Lusinde jukwaani
*Wadai zinakiuka maadili, wamtaja ajirekebishe
*Serikali yarejesha ardhi kwa wananchi ekari 5,000
Na Queen Lema, Arumeru
WANAWAKE wauza nguo katika masoko ya Usa River na Tengeru yaliyopo kwenye Jimbo la Arumeru Mashariki, mkoani Arusha, wamekishukia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa madai baadhi ya makada wake hawana maadili wanapokuwa kwenye kampeni za kumnadi mgombea ubunge wa chama hicho Bw. Sioi Sumari.
Wakizungumza na waandishi wa habari jana, wanawake hao walikwenda mbali zaidi na kudai kuwa, Mbunge wa Mtera, mkoani Dodoma, Bw. Livingstone Lusinde, amekuwa akitoa lugha za matusi jukwaani bila kujali aina ya watu anaowahutubia.
Walisema Bw. Lusinde ambaye ni kiungo muhimu wa CCM, alitoa lugha ya matusi katika mkutano wa kampeni uliofanyika eneo la Ngarasero Usa River wakati akimnadi Bw. Sumari.
Hata kama Bw. Lusinde ana chuki na wapinzani hasa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), anapaswa kutumia lugha nyepesi inayoeleweka.
Mikutano hii ya kampeni inahudhuliwa na watu wa aina mbalimbali wakiwemo watoto ambao tunawaalibu kimaadili, jambo la msingi vyama vyote vione umuhimu wa kuepuka lugha za matusi ambazo hazisaidii kupata ushindi, walisema wanawake hao.
Wanawake hao walimtaka Bw. Lusinde kuhakikisha harudii kutumia lugha zisizofaa kwenye kampeni badala yake atumie burasa kumnadi mgombea wao.
Wakati huo huo, siku tatu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo, Serikali imerejesha zaidi ya ekari 5,000 za ardhi mikononi mwa wakazi wa Kata za Nduruma Mlangarini iliyopo Arumeru Magharibi na Mashono jijini Arusha.
Ardhi hiyo ilikuwa ikimilikiwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kwa zaidi ya miaka 20 na kusababisha wananchi washindwe kulitumia.
Mkuu wa Mkoa huo Bw. Magesa Mulongo, alisema Serikali imeamua kufikia uamuzi wa kurudisha ardhi hiyo kwa wananchi.
Kwa sasa ardhi hii imerudishwa kwa wananchi hivyo ni mali yao kwa mujibu wa sheria...uamuzi huu umefikiwa na Raisi Jakaya Kikwete baada kusikiliza malalamiko yao ya muda mrefu.
Viwanda hivi vitaongezwa thamani kwa mujibu wa sera ya matumizi ya ardhi, kila mmiliki atalazimika kupima kiwanja na faida ambayo atapata ni pamoja na kukitumia kama mtaji, alisema Bw. Mulongo na kuwataka wakazi wa maeneo hayo kuhakikisha hawauzi ardhi hiyo hadi itakapopimwa.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. Goodlucky Ole Medeye, alisema wananchi katika kata hizo wanatakiwa kuweka sera ya ardhi ili kuiboresha.
Katika hatua nyingine, Mwandishi Pamela Mollel, anaripoti kutoka Arumeru kuwa, Mbunge wa Sumbawanga Mjini, mkoani Rukwa, Bw. Aeshi Hilal (CCM), amesema kampeni za uchaguzi wa Arumeru Mashariki zina usalama mkubwa kuliko ilivyokuwa Igunga, mkoani Tabora.
Bw. Hilal aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na waandishi wa habari na kusisitiza atahakikisha CCM inapata ushindi wa kishindo katika uchaguzi huo.
Ujio wangu katika kampeni hizi ni kuhakikisha chama chetu kinatetea jimbo hili, hatumwogopi mtu wala wapinzani, awali nilichukulia Arumeru Mashariki kama sehemu ya vurugu na fujo lakini baada ya kutia mguu, nimegundua kuna utulivu wa kutosha, alisema Bw. Hilal.
Wakati huo huo, mgombea ubunge wa CCM katika uchaguzi huo Bw. Sioi Sumari, jana alipewa zawadi ya biblia na fimbo iliyotolewa na Kikundi cha Wazee waishio katika mazingira magumu cha 'Sikila Hope For Elderly' kilichopo Sakila wilayani hapa.
Wazee hao walisimamisha msafara wa Bw. Sumari na kumuomba awasaidia kwa sababu wanaishi katikia mazingira magumu.