Uchaguzi 2020 Mgombea Urais kupitia CHADEMA, Tundu Lissu afanyiwa mahojiano kwenye kipindi cha ITV dakika 45

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,986
Turn and watch now.



Mgombea Urais wa Chadema Ndugu Tundu Lissu alipata fursa ya kuhojiwa na Mwandishi wa habari Bi. Farhia Middle katika kipindi cha dakika 45 kinachofanywa na kituo cha televisheni cha ITV ambapo aliongea mambo yafuatayo:

Mwandishi wa Habari: Kwanini unataka kuchguliwa kuwa Rais wa Tanzania?

Tundu Lissu: Ninataka kuchaguliwa kuwa rais wa Tanzania kwa sababu ninaamini nina uwezo na nina nia ya kuirudisha nchi yetu katika misingi yake ya mwanzo, misingi yake ya uhuru. Tulipopata uhuru kauli mbiu yetu ilikuwa Uhuru na Kazi, Uhuru na Umoja, Uhuru na Maendeleo. Uhuru lilikuwa ndio neno letu la kwanza, ulikuwa ndio msimamo wetu wa kwanza, mambo mengine yote yalifuata. Na tunahitaji maendeleo lakini tunahitaji maendeleo tukiwa watu huru, tunahitaji maendeleo ya haki. Sasa huo ndio msimamo wangu, hiyo ndio sababu ambayo imenifanya niombe ridhaa ya Watanzania ya kuwaongoza katika kipindi hiki muhimu.

Mwandishi wa Habari:
Hivyo ilikuwa ndoto yako siku moja kugombea urais wa JMT au kama ulivyoeleza kuwa suala la uhuru ndio maana unataka Urais wa JMT?

Tundu Lissu: Katika mazingira ya kawaida si jambo la ajabu kwa mtu yoyote yule ambaye ni Mwananchi na ni Mzalendo kutaka kuwa kiongozi wa hiki au kile, kuna nafasi nyingi sana za Uongozi, Urais ndio nafasi ya juu kabisa ya Uongozi na mimi kama Mwanasiasa, kama Mwanasheria, kama Mwananchi wa Tanzania nimekuwa nafikiria kwamba hivi nina uwezo kiasi gani wa kuwa rais wa nchi hii. Kwahiyo katika kujibu swali lako ni kwamba nilikuwa naifikiria. Lakini katika kipindi hiki cha Miaka mitano hicho nilichokuwa nakifikiria juu juu kimekuwa imara zaidi kwa sababu ya haya ambayo tumeona katika miaka mitano.

Mwandishi wa Habari: Kwa maana hiyo sasa ilani ya Chadema imejikita katika mambo hayo ya uhuru uliyoeleza?

Tundu Lissu: Ilani yetu inasema, Uhuru, Haki na Maendeleo ya watu. Afrika Kusini wakati wa ubaguzi wa rangi ilikuwa na maendeleo m,akubwa sana ya mabarabara, ya Miji, Ya miundo Mbinu, ya ndege ya kila kitu. Lakini ilikuwa sio nchi ya haki hata kidogo. Na watu walipigana, watu walikufa, watu walitoa zaka kubwa kabisa unayoweza kuitoa kwa nchi yako. Kujitolea kufa au kujitolea kuumia ili kupata uhuru na ili kupata haki. Kwahiyo tunapozungumzia maendleo ya watu, hayawezi yakawa maendeleo ya mabarabara tu, au ya ndege tu kama watu wenyewe hawatendewi haki. Uhuru, haki na maendeleo ya watu.

Nikutolee mfano, kuna kazi kubwa sana imefanyika ya kujenga miundo mbinu, ukipita barabara ya Morogoro mpaka Kibaha almost, eneo ambalo barabara inajengwa zamani ilikuwa makazi ya watu kwa maelfu ambao wamebomolewa nyumba zao, wamebomolewa biashara zao, sasa yes barabara ni nzuri lakini barabara hii ina maana gani kwa malefu na maelfu ya watu ambao unawavunja nyumba zao, vitegauchumi vyao unaharibu maisha yao kwa jina la maendeleo. Maendeleo hayawezi kuwa barabara, maendeleo yanapaswa kuwa jinsi hiyo barabara inavyowasaidia watu unaowabomolea.

Mwandishi wa Habari: Sasa kwa maana hiyo wewe unagombea nafasi ya Urais kupitia chama chako cha Chadema, utawafanyia nini Watanzania katika maswala hayo yote uliyoyazungumzia?

Tundu Lissu: Mimi nimesema,nkatiba yetu inasema jambo la kwanza tutarudisha uhuru kwa Wananchi ambao umepotea kipindi hiki, tutarudisha uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa Wananchi kutoa maoni yao kuisema serikali. Tendola kwanza kwa raia huru huwa ni kuwawajibisha wale wanaowaongoza, kuwasema vibaya ni tendo la kidemokrasia. Tunataka uhuru kwa taasisi za kiraia, kwa ujumla tunataka watu wawe huru, sasa baada ya hapo tukiwa huru. Tunataka uhuru wa watu kuendesha shughuli zao za kiuchumi. Tumefikia mahali ambapo leo hii watu wanaweza wasijue. Lakini ukiuliza Benki yoyote ya Tanzania leo hii mwezi huu mmeletewa Agency Notice ngapi za TRA Utashangaa. Tunataka watu waendeshe shughuli za kiuchumi wakiwa huru bila hofu kwamba nikipeleka hela Benki anagopa Agency Notice itachuku hela zao. Miaka ya 70 na 80 watu walikuwa wanahifadhi hela kweny magunia. Kwahiyo tunataka uhuru katika kila sehemu ya maisha yetu na hiyo ndiyo itakayotuletea maendeleo.

Mwandishi wa Habari: Uhru mnaouzungumzia Tundu Lissu, kuna baadhi ya watu watatafsiri kwamba Tanzania haiko huru. Mnamaanisha nini hasa?

Tundu Lissu: Uhuru ambao nauzungumzia ni Uhuru wa watu kutoa maoni yao, uhuru wa watu kujiunga katika makundi ya kiraia, kisiasa na kijamii, uhuru wa kuabudu, uhuru wa kufanya biashara, wa kufanya shughuli za kiuchumi. Sio uhuru ule wa wakoloni. Tunataka serikali isitukabe tunapofanya shughuli zetu za kawaida kabisa kama raia Wananchi wa nchi hii.

Mwandishi wa Habari: Mh. Tundu Lissu katika jambo la sera kuna baadhi ya watu ambao wanatafsiri ya kwamba mmekuwa walalamikaji ama mmekuwa wakosoaji zaidi. Labda sera ya Chadema ni nini hasa ili watu waweze kufahamu?

Tundu Lissu: Kwanza nianze kwenye hilo suala la ulalamikaji. Shida yake ni nini? Kama tunahitaji kulalamikia jambo ambalo halitendeki sawasawa, ukilalamika au ukikosoa tatizo lake ni nini? Mimi nafikiri kwa katiba na sheria zetu zilivyo tu. Uhuru wa kuzungumza ni pamoja na uhuru wa kulalamika pale unapoona mambo hayatendeki sawasawa na wale ambao wana wajibu wa kuyatenda sawasawa. Uhuru ni pamoja na kukosoa pale ambapo panahitaji kukosolewa. Sasa nirudi kwenye sera, kama kwa mfano kuna matumizi mabaya ya madaraka watu wanakufa, watu wanauawa unakuwa na lugha laini kiasi gani? katika maeneo ambayo kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaoharibu maisha yawatui, unaoharibu uhuru wa watu. Utakuwa na lugha laini kiasi gani.

Niache hilo turudi kwenye sera, tumetengeneza ilani ya uchaguzi ambayo mimi naiita ni agano letu la Watanzania. Hili ni agano la Chadema na Tanzania, na katika agano hili tumezungumza kila jambo linalowahusu katika maisha yao ya kila siku. Mfano katika elimu tumesema tunataka taifa la watu walioelimika wenye maarifa sio watu walioelimika kwa kupata vyeti vya makartasi. Tunataka kujenga nchi ya watu ambao wana maarifa, ukimpeleka Uingereza au Marekani ataweza kuajiriwa. Ukimpeleka Kenya, Afrika Kusini au Uganda ataajiriwa.

Tumezungumza habari ya afya, tumesema ili tuwe na taifa bora lazima tuwe kwanza na taifa lenye afya bora. Lazima tuwe na utaratibu wa kiafya ambao utahakikisha kila mtu anakuwa kwenye bima ya afya ili aweze kutibiwa pale panapohitajika. Kwahiyo tunataka tumuingize kila mtu katika bima ya afya na inawezekana. Nimekaa miaka mitatu karibu ulaya na mimi hapa ambaye nimetoka na majeraha makubwa hapa, nilipofika tu nikaambiwa kwa sababu umepata visa ya kukaa hapa kwa zaidi ya miezi sita lazima uwe kwenye bima ya afya. Tunafahamu huna kibali lakini unawekewa kiwango kidogo ambacho kinaendana na kipato chako. Mwenye kipato kikubwa sana analipa kikubwa zaidi lakini kila mtu yupo kwenye mfumo wa bima.

Matibabu anayoyapata Mfalme wa Ubelgiji ndio matibabu niliyoyapata mie ambaye sikuwa na kazi, sikuwa na kipato nilikuwa nachangiwa changiwa tu kwa sababu kila mtu yupo kwenye bima ya afya. Sasa lazima tuwe na utaratibu wa afya kila mtu atakayehitaji kutibiwa na jibu lake ni hili linaloitwa Universal Health Insurance ili kuwawezesha Wananchi kuwa na afya bora. Aidha Akiongelea usafiri Tundu Lissu amebainisha kuwa, wanafikiria kuwa na namna nyingine ya usafiri badala ya kujenga barabara kwa kuwabomolea watu nyumba. Pia Tundu Lissu amefafanua kuhusu chanzo mbadala cha kuzalisha nishati badala ya kutegemea mabwawa pekee hasa katika nchi yetu ya kitropiki.

Mwandishi wa Habari: Na vipi kuhusu suala la ukosefu wa ajira ambalo ndilo limekuwa tatizo kubwa hapa nchini na nchi nyingine barani Afrika. Katika sera yenu hili mmeligusia?

Tundu Lissu: Tumezungumza sana kuhusu ajira katika ilani yetu. Kimsingi ni hivi, suala la ajira ni suala la kiuchumi, Kama uchumi wako haukui matokeo yake utayaona kwenye watu wasioukuwa na ajira. Sasa sisi katika miaka hii mitano inayoisha na uchaguzi Mkuu, kiwango cha uwekezaji binafsi katika sekta za kiuchumi. Uwekezaji wa ndani na uwekezaji wa nje umepungua kwa zaidi ya nusu. Hizi ni takwimu za Benki ya Dunia na takwimu za wataalamu. Sekata binafsi imepungua ukuaji kwa zaidi ya nusu. Biashara za aina mbalimbali zimefungwa kwa kiasi kikubwa. Sekta ya utalii kwa mwaka huu kwa sababu ya Corona sekata ya utalii imeanguka kwa asilimia katibu ya 80. Sasa katika mazingira haya ajira zitatoka wapi? Serikali haiajili sana. Kuna maelfu ya wanafunzi wanatoka vyuo wanaranda mitaani kwa sababu uchumi haukui na serikali haina uwezo.

Kinachohitajika ni sera za uchumi za kuwezesha uchumi kukua. Tunataka kufungua milango huru ya kiuchumi ili kuwawezesha watu kufanya biashara, watu wajenge viwanda, watu wawekeze katika kilimo, wafanye mapinduzi ya kilimo ili kundi kubwa la vijana wanaoranda mitaani wakiuza bidhaa wamezishikilia mikononi. Tunafikia kila mji wenye vituo vya mabasi kuwa kituo cha biashara. Tunataka vijana wapate mahali pa kufanyia biashara badala ya kuzunguka mtaani. Hayo yote yanapunguza tatizo la ajira.

Mwandishi wa Habari: Umeongea kuhusu suala la mapinduzi ya kilimo pengine katika sera yenu hili mtalisimamia vipi hasa?

Tundu Lissu: Kwanza kabisa kama nilivyosema ajenda kubwa ni haki uhuru na maendeleo ya watu. sasa katika kilimo mkulima wetu leo anayelima mahindi au Shinyanga ina mpunga mwingi sana. Mkulima anajihangaika mwenyewe mwaka mzima. Analima, anapanda na akimaliza njiani anakutana na kila aina ya kizingiti, kila aina ya tozo kila aina ya kodi. Tunataka uhuru wa kufanya kazi. Tunataka mkulima soko lipo katika nchi mbalimbali mwezeshe mpatie uhuru wa kuuza mali zake mahali popote ambapo pana soko zuri. kwahiyo, kumsaidia mkulima unamsaidia kwa kuondoa hii mizigo ambayo haina ulazima ambayo amewekewa kila mahali.

Mwandishi wa Habari: Mh. Lissu tangu uhuru Tanzania inapambana na maadui watatu ambao ni ujinga, umaskini na maradhi, pengine chama chako kinakuja na silaha gani kuondoa hao maadui?

Tundu Lissu: Hiyo kauli mbiu ya Umaskini, ujinga na maradhi ni ya mwaka 1958 na wala si ya uhuru. Mwalimu Nyerere akiwa rais wa TANU alisema tunataka tuwe huru ili tuondoe umaskini, ujinga na maradhi. Umekuwa ni wimbo ambao kila mtu anajua ambapo baada ya miaka 60 ya uhuru bado mnaimba maadui walewale ni kwamba mmeshindwa kazi.

Habari ya kuondoa umasikini, ujinga na maradhi ni habari ya namna gani mnaendesha nchi. Shule nyingi zile ambazo zinajulikana katika nchi hii, shule bora kabisa, hizi hazikuwa za serikali, hospitali hizi sio hospitali za serikali kihistoria ni hospitali zilizojengwa na taasisi zisizokuwa za kiserikali.

Nachotaka kusema ni kwamba watu wakiruhusiwa kuwa huru, kufanya shughuli zao za uchumi kwa uhuru, kufanya shughuli zao za kijamii kwa uhuru, watajenga mashule, watajenga mahospitali, watafanya vitu ambavyo mtashangaa kama ambavyo ilishaanza kufanyika miaka kabla hatujapata uhuru. baada ya kupata uhuru ilipofika mwaka 1967 kila kitu kikawa chini ya serikali. waendeshaji wa masuala husika wakashindwa kuendelea kuyaendesha kwa uhuru. Sasa unawezaje kupambana na umasikini, ujinga na maradhi. Inapswa watu wawe huru kutawala na kufanya shughuli zao kuliko kutegemea kila kitu kutoka kwa serikali.

Mwandishi wa Habari: Je, suala la katiba ni kipaumbele katika chama chako kuelekea uchaguzi mkuu?

Tundu Lissu: Katika ilani yetu tumesema kwamba katika mambo ambayp tutayafanya katika siku 100 za kwanza za Urais wangu ni kurejesha mchakato wa katiba mpya. Yote haya ambayo tunayataka katika ilani yetu hayatowezekana kwa mfumo huu huu wa serikali, mfumo huu huu wa kikatiba ambao umekuwepo tangu mwaka 1962. Watu wengi hawaelewi wanafikiri shida ni katiba ya mwaka 1977. Katiba ya mwaka 1977 imejengwa katika misingi ya katiba ya mwaka 1962 na msingi ule ni kwamba Rais ni alfa na omega kwa Tanzania. Tunataka tukipata ridhaa ya Watanzania ilio tuweze kutatua matatizo yote hayo lazima tuweke kwanza utaratibu mpya wa kuongoza nchi. Leo hii watu wanazungumza sana kuhusu Wabunge lakini ukimuuliza hivi unajua kuwa Wabunge hawawezi kuleta mswaada wowote wa masuala ya fedha.

Mwandishi wa Habari: Ilani yenu inaongelea masuala ya uhuru na sasa hivi tupo mwaka wa 60 tangu tupate uhuru. Una neno gani kwa Watanzania ambao wanawapima kwa sasa.

Tundu Lissu: Baada ya miaka 60 ya kuondokana na Wakoloni wa Wazungu ni wajibu wetu sasa tutengeneze nchi ambayo watu watakuwa huru kuzungumza, kutoa maoni yao, kuchagua, kuchaguliwa, kuandika vitabu, kuchapisha magazeti. Tuwe na taifa ambalo watu wana uhuru wa kiuchumi na kuendesha maisha yao. Huo ndio ujumbe wangu katika mwaka ujao wa 60 wa uhuru wa taifa letu.

Mwandishi wa Habari: Katika mikutano yenu mmekuwa mkizungumza sana kuhusu mabadiliko, Chama Tawala pia wamekuwa wakizungumza kuhusu mabadiliko. Je, mabadiliko ganii ambayo pengine mnayazungumzia tofauti na yale ya Chama tawala?

Tundu Lissu: Tofauti ni kubwa sana, Chama Tawala wanazungumza kuhusu mabadiliko na kumekuwa na mabadiliko kweli ambayo yameturudisha nyuma badala ya kutupeleka mbele. Tumerudi kule ambako mwali nyerere alituasa akiwa Rais. Cheo ni dhamana, Mwalim Nyerere alikuwa anafahamu hatari ya madaraka makubwa aliyokuwa nayo na alisema hadharani. Ktaiba iliyopo ya Tanzania Rais ana mamlaka ya kuwa Dikteta, alisema hivyo mwaka 67 alihojiwa na gazeti la Uingereza la Obsever, akarudia tena mwaka 1978 alipohojiwa na BBC. unapojenga au kufanya mradi wowote lazima kandarasi ziwe wazi, umegharamia kiasi gani na kulipwa italipwaje. Uwazi uwazi uwazi, uhuru, uhuru, uhuru sasa huo ndio msimamo wetu.

Mwandishi wa Habari: Mh. Tundu Lissu umepita baadhi ya mikoa wakati unatafuta wadhamini na hapa mmeshafanya mikutano miwili na mnaendelea kwenda katika mikoa mingine kuzungumza na Watanzania na kueleza sera zenu. Kwa mtazamo huo kwa jinsi ambavyo umepita mikoani na kwa jinsi ambavyo umeona jijini Dar es Salaam, Watanzania wanaelewa ilani na sera ya CHADEMA?

Tundu Lissu: Swali zuri sana, tuna siku 60 za kuzungumza ilani na sera za Chadema kwa Watanzania katika mambo yote yanayohusu maisha yao. Kama ambavyo nimesema, hili ni agano letu na Watanzania, wakitukubalia hili ndilo litakuwa agano letu kwa miaka mitano na miaka mingi ijayo kwahiyo tutapata muda wa kuelezea. Lakini nirudi kwenye swali lako huko ambako tumepita.

Mimi sikuwepo nchini kwa miaka mitatu kwahiyo sikuwa na direct contact na wananchi ambayo nimeipata tangu mwezi uliopita na nimeshangaa sana jinsi ambavyo Watanzania hawa ambavyo wamebadilika, ambavyo wako tayari kufanya mabadiliko. Tumefanya mikutano katika mikoa 17 katika kipindi cha siku 12 na watu kwa maelfu wamejitokeza kutulaki pamoja na kwamba tulikuwa tunatafuta wadhamini tu. Watu wapo tayari kwa mabadiliko na hii inakwambia kwamba miaka mitano hii imekuwa ya adha kubwa sana kwao, ndio maana ya hiki ambacho tunakiona. Kwahiyo, mimi binafsi na chama changu, mimi na wenzangu tunaamini kwamba nchiyetu na watu wetu wapo tayari kufanya mabadiliko makubwa sana.

Mwandishi wa Habari: Mh. Tundu Lissu tulikuwa tukiskia katika mchakato wa kutia nia na kuwania Urais kuwa Wapinzani mngeungana. Nini kimetokea hasa? swali hili limekuwa likiullizwa na Watanzania wengi.

Tundu Lissu: Ni swali zuri sana, ni suala halali kabisa kuulizwa katika uchaguzi huu kwa sababu mwaka 2015 tuliunda Ukawa. Miimi binafsi naamini kwamba Ukawa ilituletea mafanikio makubwa sana. Pengine haikutupatia yale ambayo tuliyatarajia moja kwa moja lakini binafsi naamini kwamba mwaka 2015 ulikuwa ni mwaka muhimu sana kwa sababu kwa mara ya kwanza tulienda kwa pamoja kama vyama vinne vilivyoshirikiana. Sasa baada ya 2015 wale ambao hawatutakii mema nao walijua hatari ya Ukawa. Kwahiyo, walichokifanya mwaka jana wakabadilisha sheria. Yale marekebisho yanasema hivi:

"Chama cha Siasa kina uhuru wa kuungana na chama kingine cha siasa wakati wa uchaguzi ilimradi kila kitu unachokipanga lazima ukiwasilishe kwa msajili wa vyama vya siasa ambaye ana mamlaka ya kuwakubalia au kuwakatalia. Sasa masuala ya mtatumia fedha kiasi gani kwenye jimbo gani, mtatumia vyombo vya habari namna gani". Kila jambo linalohusu mkakati wenu wa ushindi lazima mumpelekee Jaji Fransis Mutungi ili aangalie amuulize yule aliyemteua kama inafaa au haifai.

Nachotaka kusema ni hivi, mazingira ya kisheria yaliyopo sasa hivi ya kuungana kwa vyama ni mitego mitupu na mitego ile haijatengenezwa na Chadema, wala ACT, wala Chauma ni mitego iliyotengenezwa na CCM ili tukinasa tu tumekwenda. Sasa tutakuwa watu wajinga sana kama vyama tukiingia katika mitego hii bila tahadhari. Kwahiyo tunachofanya tunazungumza na wenzetu wa ACT kwa sababu tunataka tuangalie hii kitego tun aweza kuiepuka kwa namna gani. Tushirikiane kwa namna ambayo itatuepusha na hizi hatari ambazo tumetegewa kila mahali.

Sasa Watanzania hawaoni hayo kwa sababu hawaambiwi na hao wanaowaambia mbona hamuungani. Hizi hatari mtadili nazo namna gani. Hatari ya msajili wa Vyama vya Siasa kuwakatalia dakika za mwisho na ana mamlaka hayo. Hatutakuwa watu wenye busara kama tutakimbilia muungano halafu tukajiingiza kwenye balaa kubwa zaidi ya ambavyo tungekuwa peke yetu. Kwahiyo tunazungumza na wenzetu kuangalia jambo ambalo linawezekana kushirikiana na wenzetu.

Mwandishi wa Habari: Mh. Tundu Lissu tafsiri iliyokuwepo ni kwamba upinzani ni watu wa shari na watu wa vurugu, wapinzani ni watu wa kuzua migogoro ya hapa na pale. Unazungumza na Watanzania kwa sasa tueleze ukweli wa hili.

Tundu Lissu: Sisi sio watu wa shari hata kidogo, katika mwezi huu tumefanya mikutano mikubwa mingi sana, tumefanya maandamano actual, tarehe 28 niliporudi kutoka Ulaya tulifanya maandamano kutoka Airport mpaka Kinondoni. Tumefanya mikutano kila mahali katika mchakato wa kutafuta maandamano mikubwa ambayo polisi hawakuwa na uwezo wa wa kufanya chochote. Wangefanya chochote wangesababisha maafa makubwa.

Lakini kwa sababu sisi ni watu wa amani watu wamekuja kwa maelfu, hakuna mtu ameibiwa simu. Kwa upande mwingine fikiria mambo ambayo sisi tumefanyiwa. Viongozi wetu wameuawa, wengine wamedakwa mchana wametekwa nyara na watu wasiojulikana. Niangalie mie, unaniuliza hapa hujambo hujambo kwa sababu unajua yaliyonitokea sio? Mnadhimu wa kambi rasmi ya upinzani bungeni kupigwa risasi kumi na sita ndani ya makazi ya viongozi wa serikali yanayolindwa masaa 24. Nafikiri tafsiri za hayo masuala tuanze kuzifikiria upya kama ni hivyo.

Mwandishi wa Habari: Na vipi kuhusu suala la kutumika na watu wa nje, kufadhiliwa harakati na watu kutoka nje ni kweli mnafadhiliwa na watu wa nje kwa manufaa yao binafsi?

Tundu Lissu: Hizi ni porojo tu, za watu ambao wamekosa la kusema. Hawana hoja ya kujibu. Mimi nimekuwa na msimamo huu tangu nilipokuwa kijana leo nna miaka 52. Msimamo wangu katika masuala haya haujawahi pindishwa. Nimeyazungumza haya miaka ya kikwete na nayazungumza haya wakati wa Magufuli. Wakiumwa hawa wanaenda kutibiwa huko. Hawa watu ni marafiki zetu tukipata shida tunawakimbilia halafu tunawatukana, tunawaita mabeberu huku tunawategemea. Tunategemea watupe hela za barabara, maji N.k. Mimi nitajenga mahusiano ya kimataifa, Tnzania inahitaji dunia, kuliko dunia inavyohitaji Tanzania. Lazima tuwe na utaratibu ambao utatufanya sisi sehemu ya familia ya kimataifa.
 
Back
Top Bottom