Mfahamu 'Kamchape' mkamata wachawi na shughuli zake kwa ujumla kutokea hapa Mkoani Kigoma

Kigoma Region Tanzania

JF-Expert Member
May 25, 2021
229
593
Kamchape ni mganga wa jadi hupatikana Africa hasa nchini DRC Congo na wengine wao hupatikana hapa mkoani Kigoma.

Katika makala hii nitakujulisha kunako tasnia hii ya Uganga na nguvu za giza kutokea hapa Kigoma, nitakusafirisha na kukujuza kinagaubaga ili uweze kutambua Kamchape ni na nani? wapi anapata nguvu hiyo? na shughuli zake ni zipi.

Kwa lugha nyepesi 'Kamchape' ni Mkamata wachawi.

Ili mtu uwe na uwezo wa kua Kamchape ni lazima uwe na kiongozi mshauri 'Mentor' ambaye huyu ni 'Mganga-Mchawi' : Huyu ndiye ataanza kukupa mafunzo ya awali ambayo huchukua siku 7.

1689171022914.png


Mambo kadhaa utafundishwa na huyo 'Mentor' wako ikiwemo
-'Kusambira' (kuwanga kwa kuzunguka moto),
-Kukutambulisha kwa washirika wenzake ambao ni wachawi kwamba wewe ndiye unakwenda kuwa mrithi wake katika upande huo',
-Kisha atakufundisha uganga wa 'Kuchapa' kushika wachawi.
-Kisha atakufundisha miti aina mbalimbali kwa ajili ya dawa kwasababu kamchape mara nyingine huwa anatibu.

Mkishamaliza hiyo awamu ya kwanza ya masomo ambayo ilijumuisha na vitendo vya kusambira (kuwanga):
Awamu inayofuatia huwa ni ngumu, ambapo yeye 'mentor' wako atalazimika kukupeleka chuo ambapo huko kuna wajuzi zaidi.

Na lengo la kukupeleka chuo ni ili upate ujuzi wa ziada katika mitishamba na vizimba ambapo yeye atakuja kumalizia maelekezo ya mwisho ukishatoka mafunzoni.

Vyuo vinavyotoa mafunzo hayo ni katika Vilinge vikubwa vya 'Uchawi na Uganga' kwa ukanda wetu huu wa Magharibi kilinge kikuu kipo eneo la Buzelwa katika mji wa Manono nchini DRC.

Mara nyingi kamchape wengi wanaopatikana Kigoma wanakwenda kupata mafunzo huko, baada ya kumaliza elimu ya awali kwa 'Mentor' wake.

Mji wa Manono nchini DRC
-Ili kufika katika mji huu, utakuja kwa njia ya kawaida kama binaadamu wa kawaida, ukishafika katika mji huu unatakiwa kwenda kwenye kijiji maarufu kiitwacho 'Kibelo Cha Banabake' ambapo hutafsiriwa kwa kiswahili kama 'Kijiji cha Wanawake' kwasababu wengi wa Waganga wanaopatikana hapo ni Wanawake.

1689172311238.png

Manono-DRC

Ili kufika katika kijiji hicho utakutana na mitihani ya kila namna kulingana na mahitaji yako yaliyo kupeleka huko.
Kwa hivyo 'Mentor' wako lazima akutahadharishe kwamba huko Kibelo hujafuata pesa, wala mwanamke, wala utajiri wala kitu chochote ispokua Uganga tu. Kwasababu watu wengi hukwenda huko kwa mahitaji tofauti tofauti, ila la kwako ni Uganga tu.

Ukishafika eneo la Buzwela ili kuelekea huko 'Kibelo Cha Banabake' tayari utaanza kupambana na mambo yasiyo ya kawaida, zoezi la kwanza utaona hapafikiki, japo unapaona ni karibu kwa macho kama kilometa 1 lakini kufika hutaweza kwasababu utatembea sana umbali mrefu kwa muda mrefu. Hapo tayari unakua umeshaingia katika ulimwengu wa giza na miuzauza.

Usipokata tamaa ukazidi kusonga mbele unaweza tokewa na mnyama yoyote mara nyingi huwa ni 'paka', huyu atakutishia kukuparua kisha atakunyanganya kila kitu ulichopewa na 'Mentor' wako.

1689177783702.png


Kisha utazidi kusonga mbele kuelekea kwenye hicho kijiji kinacho-onekana kwa ukaribu lakini hakifikiki, mtihani mwingine huwa ni kukutana na shimo kubwa ambalo unatakiwa kulivuka, hapo utasimama kwasababu hutaweza kulivuka shimo hilo lenye upana sawa na uwanja wa mpira, hapo sasa utakiona kijiji kipo ng'ambo tu ya shimo hilo.

Wakati unajitafakari ndipo utajikuta umefunikwa shuka kuanzia kichwani mfano wa mtu anapojifukiza, na hapo utapofunuliwa shuka ghafla utajikuta tayari upo ndani ya kijiji cha 'Kibelo Cha Banabake'

Hizi sio hadithi za kusadikika bali ni kila Kamchape hupitia hatua hizi kabla ya kuanza kazi zake. Ispokua vilinge vya 'Uchawi-Uganga' vipo vingi na vyenye nguvu tofauti tofauti, lakini walio wengi hupitia 'Kibelo Cha Banabake'

Utapofika hapo watakushangilia kwa vigeregere huku wanakukaribisha kwamba umefika. Utaandaliwa sehemu ya kulala, na kisha utaanza kupewa mitihani kukupima ambapo ukionekana kufeli mitihani hiyo basi hutaweza kurudi ulikotoka.

Mitihani hiyo hujumuisha kupatiwa mwanamke mzuri ulale nae, kupatiwa vito vya thamani na madini ya thamani, na mambo mengine kadha wa kadha ya kukuvutia lakini ukisahau kilichokupeleka na ukavutika na mambo hayo mengine basi hautaweza kurudi.

Mara nyingi Kamchape hawana umri mkubwa, wengi wao huwa ni vijana tu kati ya miaka 17 hadi 25.

Katika chuo hichi cha 'Kibelo Cha Banabake' kozi maalumu ya awamu ya pili huchukua siku 7, mambo kadha utafundishwa hapa ikiwemo
-Njia mbalimbali za Kusambira (kuwanga) kwa siku 3 mfululizo kwa vitendo
-Kusambira ni kuwanga au kuruka kwa kutumia Ungo au Mwichi wa kinu.

Hapa utajiuliza inakuaje mtu anatafuta uganga wa kukamata wachawi halafu yeye anajifunza tena uchawi?

Jibu ni kwamba huwezi kufanya kazi ya kuchapa na kua kamchape bila kujua uchawi upoje, ni lazima na wewe uingie humo kwanza tena kwa vitendo.

1689171725597.png

Kilinge cha Uganga-uchawi

Sasa humo 'Kibelo Cha Banabake' utafundishwa mbinu na njia mbalimbali za kusambira (kuwanga) ikiwemo
-Upigaji wa filimbi ya kukutana na washirika wenzako, filimbi ya dharura na filimbi ya furaha.
-Uvaaji wa mavazi maalumu kaniki za kuwangia
-Utafundishwa Dawa mbalimbali za kujipaka wakati wa kuwanga
-Utafundishwa namna ya kusafiri masafa ya mbali na masafa mafupi
-Nyenzo mbalimbali za kurukia ikiwemo ungo na mtwangio wa kinu
-Utafundishwa matumizi ya fimbo katika kufufua watu (mizimu) makaburini
-Utafundishwa namna fimbo inavyofungua milango na kuchana kuta za majumba ya watu ili kuingia.
-Utafundishwa nyimbo mbalimbali za kichawi (Kamchape mara nyingi wanapofanya kazi yao huwa kuna nyimbo wanaimba)

1689173523674.png


Baada ya kupokea mafunzo hayo kwa siku 3 sasa zinabakia siku 4 za kukupa kinga, yaani kuutengeneza mwili wako na namna utavyoweza kuwasiliana na viumbe vingine vya kichawi.

Baada ya hapo utakwenda Kaburini mwenyewe na kupiga fimbo ya uchawi kwenye kaburi na hapo mtu aina ya mzimu huinuka na atakukabidhi mkoba, kisha hapo ndio utakua umefuzu, ambapo utapatiwa vitu vingine ikiwemo 'Mukana'' ni mfano wa Bangili (hirizi ya kuvaa mkono wa juu pamoja na sindano,

Kisha utafundishwa kuruka kwa kutumia ungo mmoja mkiwa watu wengi, ambapo kila mtu hukanyaga mguu wake hapo kisha mnashikana, ungo ule unakichupa cha mafuta ya mtoto mfu, kisha mnafumba macho kisha mmoja wenu anataja mnakwenda sehemu fulani.

Pia utafundishwa kuruka kwa kutumia Mtwangio wa kinu, mitwangio miwili unaiweka parallel kisha mnaondoka. Ukishapatiwa hayo mafunzo yatakurahisishia kazi yako ya Kuchapa wachawi.

Uchawi ni kazi ngumu sana, ndio maana watu hawaachi kwasababu michakato yake ni mirefu, kuna mambo mengi huko.

Sasa utarudi kwa Mentor wako baada ya kupewa hivyo vitu, ambapo yeye atakuja kumalizia namna ya kuvitumia hivyo vitu ulivyopewa.

1689176891255.png


.......................................

Tunaendelea.

Baada ya kutoka huko na kurejea kwa Mentor wako, sasa mtaingia kozi ya 3 kwa msaada wa vitu ulivyopatiwa huko mafunzoni.

Kozi hii ya awamu ya tatu huchukua siku tatu, hii inaitwa 'Kozi ya kupotea'

Yaani baada ya kurudi kwa Mentor wako, yeye atakuruhusu kurudi kwenu uraiani, siku hiyo unaporudi utapatwa na jambo ambalo watu watakua wanakushangaa lakini wewe hutajitambua, unaweza kujitupa kwenye maji kwa siku tatu au ukapotea kwenye mazingira tatanishi lakin nduguzo wakawa wanakutafuta bila mafanikio.

Wakati huo umepotea sasa, ndio inakuja hiyo kozi ya tatu, ambapo wewe utakutana tena na Mentor wako, atakuelekeza kazi mbalimbali ya vitu ulivyopatiwa kule mafunzoni.

-Mentor wako atakupatia hirizi ya kuweka kwenye suruali
-Atakupatia 'usinge' (mkia)
-Atakupatia makopo ya Vizimba mbalimbali
-Mentor wako atakufundisha jinsi ya kuchanganya vizimba

1689177615815.png


Vizimba huwa ni zana/Nyenzo mbalimbali za kufanyia kazi zilizo sagwa na kuhifadhiwa pahala au kuchanganywa, hujumuisha Nywele za Albino, Kucha za mapacha, Kamba ya mtu aliyojinyongea, Fimbo ya kipofu, Ubongo wa fisi, mafuta ya binaadamu, maji ya kuoshea maiti, vitovu vya watoto vilivyo katika n.k (Ni vitu vingi vilivyochanganywa kwa pamoja). Mchanganyiko huo ndio huitwa Kizimba na huo ndio uganga wako unapewa.

1689173277115.png


Mganga wako ambaye ndio Mentor wako atakufundisha jinsi ya kupandisha mapepo (mashetani) kwa kujipaka unga wa pemba, kupiga mnyanga, kukaa kwenye kinu, atakufunza nyimbo za ziada kisha wakati unapandisha atakuingizia mapepo aina tatu, ambao ni Pepo aina ya Kongolo' pepo aina ya Kizinga' na pepo aina ya Nyunzu' haya mapepo yatakuingia mwilini kisha mapepo haya ndio yatakua yanafanya kazi kwa niaba yako, ikiwemo kutibu watu na kuchapa au kukamata wachawi.

Kamchape pia huwa wana uwezo wa kutafuta vitu vilivyopotea au vilivyoibiwa kwa msaada wa mapepo hayo yakishapanda.

Sasa, baada ya kozi hiyo ya kupotea kwa siku 3 utarejea na kujikuta umezungukwa na watu wakikushangaa, lakini vitu ulivyo navyo hawavioni, utarudi kwenu na kuendelea na majukumu yako.

SASA, UNAINGIA ZOEZI LENYEWE LA KUCHAPA, NAMNA YA KUKAMATA WACHAWI

Kamchape huwa hachapi hadi aitwe na watu au mtu, wanajamii huchanga pesa na kumleta kamchape eneo husika kuja kusafisha na kutoa wachawi.

Sababu zinazopelekea wanajamii kuleta kamchape ni pamoja na

-Kukithiri kwa vifo vyenye utata katika sehemu husika
-Kukithiri kwa majanga mbalimbali ikiwemo maradhi au ajali za mara kwa mara katika mji husika
-Vitisho vya mara kwa mara kutoka kwa baadhi ya watu wanaokisiwa ni wachawi
-Kutokua na maendeleo ya kiuchumi katika mji husika
-Kutokunyesha kwa mvua wakati wa msimu wanaamini kwamba mvua inazuiliwa na wachawi katika mji.
-Kuharibika kwa mazao shambani, biashara za watu kuyumba na kufirisika katika mji husika.

Sasa vitendo hivyo hupelekea wanajamii kuchoka na kuanza kuchanga pesa na kumleta kamchape ili aje asafishe mazingira.

KAMCHAPE ANAPOFIKA SASA

-Kwanza hujitenga mbali na watu wa mji huo, kisha huko huanza kusambira (kuwanga), halafu hupata majina kamili ya wachawi wote waliopo hapo kupitia kioo chake cha kawaida, majina yote ya wahusika huandikwa hapo kwenye kioo chake bila kuambiwa wala kudokezwa na mwanakijiji yoyote yule.

-Kamchape baada ya kuwafahamu kwa majina kupitia kioo chake, sasa hutaka kujithibitishia kwa kuwaona wakiwanga, Kamchape humtuma msaidizi wake aitwae 'Kungwe' ambaye huyu anakwenda moja kwa moja kwenye kilinge cha wachawi mara tu filimbi ya kukusanyika inapopigwa kwenye mji huo, hapo sasa Kungwe hujifanya kuwa mwenzao katika kuwanga, na kuthibitisha yale majina husika.

-Panapokucha sasa, kamchape hutumia njia ya Diplomasia huwafuata wale wahusika mmoja baada ya mmoja, bila mwanakijiji yeyote kufahamu, wanakijiji hudhania kamchape yupo milimani anajiandaa kumbe tayari ameshafika katika mji kuja kuwapa habari kwa wale watu aliowaona kwamba wamkabidhi huo uchawi autupe na awape kiapo cha kutorudia tena.

Wachache sana miongoni mwa wachawi ndio hukubali kujisalimisha katika njia hii ya kidiplomasia, walio wengi hukataa na kudharau kwasababu kamchape wengi huwa ni vijana wadogo kiumru, hivyo wachawi huleta jeuri na kusema tutapimana nguvu na mabavu.

-Baaada ya hatua hiyo sasa kamchape huwapa taarifa wanakijiji kwamba zoezi litaanza siku fulani, na hapo ndipo kamchape hutumia muda mrefu kujiandaa na kisha hupandisha yale mapepo makuu matatu ambayo hufanya kazi kwa niaba yake,

Na hapo ndipo huruhusu wanakijiji kumfuata nyuma huku wakiimba nyimbo, na huanza kuwatembelea wale wahusika nyumba baada ya nyumba.

-Wanapofika hapo huingia ndani na kuutoa uchawi kwa mkono wake, na kuutupa nje na watu wote wanauwona, na kisha kumnyoa nywele muhusika, na kumchanja sehemu ya utosi na kisha damu yake huchanganywa na dawa kisha muhusika hupatiwa ili anywe kama kiapo cha kutorudia tena mambo hayo.

-Kamchape huwa haelekezwi nyumba wala kudokezwa nyumba yenye uchawi kwasababu watu wote huwa anawafahamu na watu wote tayari ameshazungumza nao kabla ila wakakaidi.

........
Siku ya jana Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Mh Salum Hamisi Kalli amepiga marufuku watu wote wanaojihusisha na shughuli za ramli chonganishi zinazofanywa na rambaramba maarufu kama KAMCHAPE.
Hii ni Kigoma Region Tanzania
 
Kamchape wako hadi mkoa wa Rukwa. Huko Sumbawanga kuna mzee akivuna mahindi yake anayahifadhi kwenye kijumba chake cha shambani ambacho hata kofuli hakina. IBA UONE. BFF wa huyo dingi nae mchawi promax ila ka-specialize kwenye kutoa adhabu. Kwa mfano kuna mtu kakutendea ubaya kama wale mademu wala nauli halafu hawaji unaenda kumwona huyo mzee... pale utachagua mbaya wako awe kichaa au auwawe. Ukichagua kuua basi sharti ni ukisikia msiba hakuna kuhudhuria.. ikitokea dili za kuadhibu watu basi waganga wa eneo lile wanakuandikia rufaa ya kwenda kumwona huyo specialist.
 
Kamchape wako hadi mkoa wa Rukwa. Huko Sumbawanga kuna mzee akivuna mahindi yake anayahifadhi kwenye kijumba chake cha shambani ambacho hata kofuli hakina. IBA UONE. BFF wa huyo dingi nae mchawi promax ila ka-specialize kwenye kutoa adhabu. Kwa mfano kuna mtu kakutendea ubaya kama wale mademu wala nauli halafu hawaji unaenda kumwona huyo mzee... pale utachagua mbaya wako awe kichaa au auwawe. Ukichagua kuua basi sharti ni ukisikia msiba hakuna kuhudhuria.. ikitokea dili za kuadhibu watu basi waganga wa eneo lile wanakuandikia rufaa ya kwenda kumwona huyo specialist.
Hatari tupu
 
Back
Top Bottom