Ndugu wana JF,
Nimeingia leo kwenye forum yenu. Mara chache nimekuwa nikifungua kusoma baadhi ya mijadala inayochapishwa hapa. Nimekuwa nikisoma na kuondoka. Pole pole, nimegundua kwamba baadhi ya mijadala ina umuhimu, ila inajadiliwa bila mpangilio, na kuna watu wanaingia kati kuvuruga wenzao kwa lugha ambazo hazishahabiani na usomi unaotajwa tajwa katika forum hii.
Nimegundua pia kuna mijadala ya kijiweni kabisa, ambayo inashusha hadi ya forum na wanaojadili. Kwa sababu hii, nimepata kuwaza kwamba inawezekana hili linapaliliwa sana na ukweli kwamba wanaoandika hapa wanadhani hawajulikani. Hivyo wanaandika lolote wanalojua hawawezi kuwa 'responsible' nalo.
Huko nyuma, niliwahi kusoma baadhi ya wachangiaji wakitaka watu wajiandikishe kwa majina yao ili kuufanya mjadala uwe wa maana. Baadhi yao walijibu kwamba wengine humu wasingependa kujulikana kwa sababu wanafanya kazi "usalama wa taifa"!
Katika kufuatilia hoja za wachangiaji hapa, sijaona kitu chochote kinachofanana na hoja zao na kazi yao, kitu ambacho mtu anaogopa kusema na kuhusishwa nacho. Nilifika mahali nikadhani kwamba kama baadhi ya kauli hizi zinatoka kwa watu wanaojiita watu wa "usalama wa taifa," basi ndiyo maana taifa letu haliko salama! Ni wazi kabisa kwamba tafsiri yangu ya dhana za "taifa" na "usalama" ni ile inayohusu usalama wa watanzania, si viongozi au watawala; ni ile inayolinda raslimali za taifa kwa ajili ya vizazi hivi na vijavyo; ni ile inayojali maslahi ya taifa, ya wanyonge... ambao mara nyingi maisha yao ya kila siku yapo hatarini! Huu ni mjadala mpana.
Kwa sababu hiyo, kabla ya kuingia hapa nimefanya jitihada binafsi kujua wanaoandika hapa. Nimefanikiwa kuwajua baadhi yenu kwa majina halisi. Nilifanya hivi kwa sababu kwa 'nature' ya kazi yangu, napaswa kuwa curious.
Sikutaka kujadiliana na watu waliovaa mask, wanaoficha utambulisho wao bila sababu ya msingi katika nia njema waliyo nayo. Naamini kwamba mtu msomi, mkakamavu na jasiri, mwenye kusema ukweli huusema ukweli huo na kukubali matokeo yake.
Hata hivyo, nimegundua kuwa katika forum hii kuna watu wana akili nzuri na uwezo mkubwa wa kujadili hoja na kuchambua za wenzao. Hawa, hata bila kutaja majina yao wazi, wanatetewa na kazi zao. 'Zinanukia' usomi na uelewa. Na nilipokuja kuwajua, nilikubali kwamba ni watu makini.
Yapo mengi niliyotazama kwa kina katika forum hii. Yapo niliyojifunza, na yapo niliyoyadharau!
Lakini kuna mambo mawili yamenisukuma niingie na kuandika leo.
Kwanza, ni kujitambulisha kwenu, na kuwahamasisha muendelee kuandika MAMBO YA MAANA, na kuyajadili KIUTU UZIMA. Katika hili napenda niwaeleze pia kwamba utambulisho wa mtu una nafasi kubwa katika kazi anayoifanya. Na kazi inayofanyiwa mafichoni inapokelewa kwa mashaka. Watanzania wengi wamezoea kuzungumza mambo ya maana kwenye vikao visivyo rasmi; wakipewa fursa ya kuyasema hayo hadharani au katika vikao rasmi, ama wananyamaza au wanayakana!
Hawa ndio wanaotushangaa sisi tunaoandika makala kali magazetini kuwakosoa na kuwashauri watawala wetu, na tukakubali kuweka majina yetu, 'kusimama na kuhesabiwa.' Wengine wanatulaumu, wanatushangaa. Wanadhani sisi tunaojitambulisha hatuna miili na damu kama wao; hatupumui kama wao...
Hapana! Hoja hapa ni mtu kuamini unachoandika kwamba ni kweli, na ukawa tayari kukisimamia na kukitetea. Vinginevyo, kama wewe hukiamini; kwa nini wengine wakiamini? Kama hujiamini, kwa nini wengine wakuamini? Tulitafakari hilo.
Pili, nimeona baadhi yenu (mnajitambua) hamfanyi utafiti wa kutosha. Yapo mengi ya kudhihirisha hili, lakini nitatoa mfano wa hoja za watu kuhusu Freeman Mbowe, hasa wale wanaombeza kwa sababu wanazozijua. Baadhi yao wamefika mahali pa kutunga uwongo na kuubandika hapa kama sehemu ya propaganda ya kisiasa. Na hii ilikuwa baada ya baadhi yenu kutilia shaka uamuzi wake wa kwenda chuo kikuu. Baada ya kuwa-proved wrong, wakaja na hoja kwamba amefeli mitihani. Baada ya kuwa-proved wrong, sasa wananiingiza na mimi katika kazi zake za chuo na nyingine za magazetini!
Nimeshangaa pia kasi ya baadhi yao kusoma na kuamini uzushi na kuanza kuujadili kama vile wamepata authoritative information! Nimejitokeza kuwasema hao na kuwaumbua hapa! Fanyeni utafiti, hasa mnapokuwa mnazungumzia mambo ambayo yanafahamika kwa wengine.
Huu pia ni ushahidi kwamba baadhi yenu hawawajui vema baadhi ya watu wanaowajadili. Laiti mngejua UWEZO HALISI wa Mbowe, msingethubutu kurusha 'vumbi' na kuliita 'mawe.' Laiti mngejua kwamba mimi mwenyewe nahitaji kujifunza mengi kwake, msingefika mahali pa kudhani mimi naweza kufanya kazi zake. Hata hivyo, mngepaswa kujua kuwa kama ni kuandika makala, Mbowe hajaanza na Tanzania Daima. Ameliandikia sana gazeti la RAI akiwa mbunge, na hoja zake zimekuwa kali kama hizi za leo.
Kitu ambacho mngefanya kikaeleweka, na mkaonekana makini, ni kuzichambua hoja zake moja baada ya nyingine; nasi wasomaji tukaona uwezo wenu.
Zaidi ya hayo, hotuba zake bungeni ni ushahidi mwingine. Nendeni kwenye hansard. Msisahau pia ametoa hotuba nyingi katika mikutano ya hadhara tangu akiwa mbunge na wakati wa kugombea urais 2005. Si mimi niliyekuwa nahutubia. Wala hakuwa anasoma hotuba zilizoandikwa.
Mimi sijawahi kumsindikiza katika mahojiano yake na vyombo vya habari vya ndani na nje alipokuwa akijibu maswali ya hapo kwa papo. Ni uwezo wake; ni karama yake aliyojaliwa na Mungu. Huhitaji kuwa msomi kuyatambua haya na kuyakubali, hata kama huyapendi. Wala huhitaji kufanya utafiti sana kuyajua. Yapo juu juu, lakini watu wanataka kuyapotosha.
Na kila ninaposoma baadhi ya maandishi ya wanaomtukana na kumbeza Mbowe na kumkosoa katika Forum hii, wakituingiza na sisi wengine kwenye mkumbo huo kwa sababu wanazozijua, huku wakijipiga vifua na kushangilia usomi wao, na nikilinganisha uwezo wao (katika maandishi yao) na wa Mbowe, nabaki mdomo wazi kwa viwango hivi wanavyovionyesha na kuvishangilia. Sioni 'quality' wanayoitetea, wanayoilinganisha na ya Mbowe! Naelewa kwa nini hatuendelei.
HITIMISHO: Tafadhari niondoeni kwenye mijadala ya Mbowe. Nina nafasi na nafsi yangu. Inanitosha. Kama mnamtaka Mbowe fanyeji jitihada mmjue kabla ya kumwandika. Kama ni hoja leteni, tutajadiliana. Upuuzi si kazi ya waungwana. Nadhani nimeeleweka. Asanteni.