SoC01 Mbinu Endelevu za Kuwaondoa Ombaomba Mitaani na Kuwafanya Wajitegemee kwa Kipato

Stories of Change - 2021 Competition

Mwadilifu Mdhulumiwa

JF-Expert Member
Jul 22, 2021
418
630
UTANGULIZI:

Kwa muda mrefu kumekuwapo na wimbi la ombaomba katika miji na majiji nchini kwetu. Pamoja na serikali kuchukua hatua mara kadhaa kuwaondo ombaomba hawa lakini tatizo limekuwa likijirudia kila wakati na kubakia kuwa tatizo sugu lililokosa ufumbuzi endelevu. Pengine ni kutokana na mbinu zinazotumika au ni jamii nzima kukosa utashi wa kupambana na tatizo hili.

Katika makala haya nitajadili njia zinazochangia kuzalisha ombaomba, namna ya kuthibiti na pia njia za kuwawezesha ombaomba kuwa wazalishaji na wachangiaji wa ukuaji wa uchumi wetu pasipo kutumia nguvu zozote za kimabavu.

Je nini Kinachangia Kuzalisha Ombaomba?

Kuna sababu za aina mbalimbali zinazochangia ongezeko la ombaomba, miongoni mwa sababu hizi ni pamoja na wananchi wengi kuendelea kuishi kwa mazoea ya kuzaa watoto wengi kupita uwezo wao wa kuwasaidia kuwajengea msingi bora wa maisha na hivyo watoto hawa huingia tu na kukulia mitaani pasipo msaada wa wazazi.

Watoto wa aina hii wengi hutoroka mikoani au vijijini na kukimbilia mijini au miji mikubwa wakiamini kuna nafuu ya maisha lakini hukumbana na hali ngumu na kujikuta wamekosa namna yoyote ya kuingiza kipato zaidi tu ya kuwa ombaomba.

Ombaomba wa kundi hili pia huchangizwa na baadhi ya vijana wa kike na kiume kujiingiza kwenye vitendo vya kihuni kama vile ulevi wa pombe, na matumizi ya madawa ya kulevya amavyo huchochea matendo ya uasherati na kupelekea uzalishaji wa mimba za bila kutarajia huku wakiwa hawana uwezo wa kutunza familia au mtoto. Matokeo yake mtoto hutelekezwa na wazazi kwa bibi au babu asiye na uwezo kiuchumi na kujikuta akijitunza mwenyewe angali mdogo anayehitaji msaada wa malezi na matunzo ya wazazi.

Ulemavu wa aina mbalimbali ni njia nyingine ambayo huchangia ongezeko la ombaomba, huku wengi wao wakiwa ni walemavu wa viungo, ambao hutokea katika familia masikini ambako hukosa misaada ya kupewa elimu na mitaji ya kuanzishia biashara na miradi mbalimbali ya kiuchumi na hivyo hukosa mahala pa kuanzia na hivyo huishia kuwa ombaomba.

Namna Ya Kuwawezesha Ombaomba Kujitegemea Kiuchumi

Ili kuwawezesha ombaomba kuondokana na hali hiyo ni muhimu kwa serikali na wadau kuwekeza vyakutosha katika kufanya tafiti kuhusu chanzo na msingi hasa wa tatizo hili na hivyo kulipatia ufumbuzi wa kudumu.

Mkazo uwekwe katika kubuni miradi rafiki ya kilimo na biashara, pia kutoa elimu na mitaji itakayowawezesha ombaomba wafikie mahala wajiajiri na kujitegemea. Serikali pia ijenga mazingira bora ya kuwezesha ukuwaji na ustawi wa shughuli za ombaomba hawa.

Serikali ihakikishe, shughuli hizi zinakuwa ni zile nyepesi za uzalishaji ambazo ni rahisi kwa watu wa kundi hili kuelewa haraka namna bora ya uendeshaji wake na kupata uzoefu kwa muda mfupi, lakini pia ziwe ni shughuli zinazohitaji mtaji mdogo wa kuanzishia.

Hii itapunguza mzigo wa gharama za mitaji kutokana na ukweli kuwa idadi ya ombaomba walioko nchi nzima ni kubwa ukilinganisha na uwezo wa serikali.

Katika utekelezaji wa mradi huu serikali kwa kushirikiana na watendaji wake wa kuanzia ngazi za serikali za mitaa hadi taifa ifanye uhakiki wa ombaomba waliopo katika kila eneo husika, mfano mkoani Dar es salaam na aina ya kundi la ombaomba kama jinsi yalivyoanishwa hapo juu.

Hii itasaidia kuanisha aina ya shughuli za miradi wanazoweza kuzifanya na kuzalisha bila matatizo.

Nitatolea mifano ya shughuli kwa ombaomba ambao ni walemavu. Katika mifano hii nitawakusanya ombaomba hawa katika makundi mawili kamaifuatavyo:-

Ombaomba Wenye Ulemavu wa Viungo(viwete) na Walemavu wa Masikio (Viziwi)

Hili ni kundi la ombaomba ambalo linajumuisha watu wenye vikwazo vya mawasiliano na usafiri wa kuifikia jamii inayowazunguka, hivyo inahitaji kubuni mradi au biashara ambayo wataifanya katika namna isiyohitaji sana mizunguko mingi kwa viwete au mazunguzo au maelekezo mengi hii ni kwa viziwi.

Hivyo katika mradi husika wanapangwa katika makundi ya uzalishaji kwa kuzingatia aina ya ulemavu wao.

Mfano wa biashara wanazoweza kufanya viziwi na viwete ni kuuza bidhaa kama vile, mikate, maji ya kunywa, mkaa wa vifungashio, matunda, unyowaji wa nywele kwa watu na wannafunzi wa mashuleni n.k.

Katika shughuli kama hizi ombaomba hawa kwa mara ya kwanza wanaweza kukusanywa na kupewa maelekezo kwa kutumia mkalimani na lugha za vitendo, kisha kila mmoja akagawiwa majukumu ya kutekeleza, hapa walemavu wa viungo watafanya kazi ya kupakia bidhaa kwenye vifungashio na kisha viziwi wataanza kuzitembeza kwa wateja.

Kwa mfano katika biashara ya kulangua na kuuza mkaa wa vifungashio, walemavu wa viungo watafanya kazi ya kupakia mkaa katika vifuko vidogovidogo vya bei kati ya Tshs. 500, 1000 hadi 2000, kisha walemavu wa masikio wataanza kupita navyo nyumba hadi nyumba na kwenye migahawa na vijiwe vya wauza chipsi na nyamachoma, huku wale wa viungo nao wakiendelea kuuza kwenye vituo mbalimbali walipotulia.

Wakiendelea na shughuli hii kwa muda hufikia mahala wanapata wateja wa kudumu na hivyo kuwa na soko la uhakika.

Kinachohitajika hapa ni kuendelea kuboresha uwezo wao wa kuwafikia wateja wengi zaidi ili kwa siku moja waweze kuuza junia nyingi zaidi na kuongeza kiwango cha mapato yao. Biashara yao ikifika katika hatua hii hawatahitaji tena usimamizi wa karibu kwani watakuwa tayari wameshapata uzoefu wa kujiendesha wenyewe na hata kuweza kukopa na kurejesha mkopo.



Ombaomba Wenye Ulemavu wa Macho na wenye ulemanavu wa ngozi

Ombaomba wa kundi hili wana vikwazo vya uoni wa vitu mbalimbali, hivyo wanatumia zaidi mguso kutambua vitu vilivyopo katika mazingira yao.

Hivyo basi ili kuweza kuwashirikisha kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali, inahitaji kuwachanganya na ombaomba wanaoona vizuri kama vile walemavu wa masikio au walemavu wa viungo na pia kubuni mradi rafiki kulingana mazingira ya ulemavu wao.

Katika uendeshaji wa mradi wa biashara wao watasaidia katika uchukuzi wa bidhaa kupeleka kwa wateja wakiongozana na wenzao wanaoona vizuri.

Pia kwakuwa wana usikivu mzuri wanaweza kuelekezwa kupakia bidhaa kwenye vifungashio kwa mradi kama huo nilioufafanua hapo juu katika sehemu ya I.

Kwa jinsi hii watafanya upakiaji huku ombaomba walemavu wengine wakiwapa msaada wa hapa na pale kama vile kusogezewa jirani malighafi zote n.k.



NB: Walemavu wa ngozi (Albino), kwakuwa wanaathirika zaidi na jua hivyo miradi rafiki kwa mazingira ya ulemavu wao ni ile ya ndani mfano migahawa ya chakula na saluni za kunyolea nywele,maduka ya vinywaji baridi na matuda. Ingawa ipo miradi ya biashara mingine mingi, lakini hiyo hapo ni baadhi ya miradi isiyohitaji kutumia mtaji mkubwa.

Mfano, zinaweza kuandaliwa flemu tano hadi kumi maeneo yenye watu wengi kwa ajili ya saluni za kunyolea nywele.

Kisha omaomba wa ulemavu wa ngozi wakapewa mafunzo kidogo ya usafi wa miili yao na vyumba vya biashara zao na namna ya kuzitumia mashine na kisha kuwakabidhi wahusika kuendelea na shughuli za mradi chini ya usimamizi na ulinzi wa karibu hadi hapo biashara itakapoonekana kuwa na soko la uhakika.

Ili kupanua soko la mradi huu wahusika wanaweza kubuni namna ya kufanya mobile sharving kwa kuwafuata wateja majumbani kwao na kwenda kushevu watoto. Pia wanaweza kutembelea katika shule za mabweni hasa za wasichana.

Katika nyingi ya shule hizi uongozi wa shule hupiga marufuku wanafunzi kutoka nje ya mipaka au geti la shule muda wote wawapo shuleni hapo. Hivyo ni rahisi kuushawishi uongozi wa shule kuwapa fursa ya kupeleka huduma ya kushevu wanafunzi wa shuleni hapo kila mwisho wa wiki na hivyo kujihakikishia soko la biashara yao.

Katika kuendesha shughuli hizi zote ombaomba hawa watalipa kodi na tozo mbalimbali za serikali, watanunua na kuuza huduma na hivyo kuchangia moja kwa moja katika kuongeza mzunguko wa fedha na mapato ya serikali na ukuwaji wa uchumi.

Jinsi Ya Kuthibiti Ongezeko La Ombaomba

Ili kuweza kukabiliana vyema na wimbi la ombaomba, ni muhimu kuthibiti kwanza mfumo mzima wa vyanzo vyote vinavyochangia kuzalisha ombaomba. Serikali ishirikishe wadau wote kutunga sera na sheria zitakazowezesha mambo yafuatayo:-

  • Kuwepo na mfumo wa kufuatilia malezi na makuzi ya watoto wote wanaozaliwa kila siku nchini kote. Hii itasaidia kuwatambua mapema watoto walio katika hatari ya kuingia katika kundi la ombaomba na hivyo kuchukua hatua za haraka ili kuwaepusha na kundi hilo.
  • Kuwepo na utaratibu endelevu wa kuelimisha jamii juu ya uzazi wa mpango kulingana na uwezo wa mzazi husika na umuhimu wa kuwapatia watoto huduma za malezi bora na elimu.
  • Zitungwe sheria kali dhidi ya wazazi wote wanaotelekeza watoto na familia zao bila kuwapatia huduma stahiki.
  • Serikali kwa kushirikiana na jamii nzima izidishe mapambano dhidi ya uzalishaji,usambazaji na matumizi ya madawa ya kulevya.
  • Kuwepo mpango endelevu wa kuwabaini ombaomba na kuwaunganisha katika makundi mengine ambayo miradi yake tayari imesimama imara.
  • Ombamba wazee watengenewe makambi maalum na watambuliwe na kusaidiwa na mfuko wa TASAF unaosaidia kaya maskini.


Hitimisho


Ili kujenga jamii bora na yenye ustawi, serikali haina budi kuwekeza zaidi katika kuboresha mifumo ya huduma za msingi za kijamii hasa katika maeneo ya vijijini. Pia ni jukumu la kila mmoja wetu kujiona ni mdau muhimu sana katika kusaidia kupambana na ujinga na umaskini ambavyo kimsingi ndio vyanzo vikubwa vya wimbi la ombaomba katika jamii yetu.

Hapa chini nimeweka picha ya Ombaomba walemavu wa viungo na ombaomba watoto wakiwa mtaani.
(Picha zote toka mtandaoni)
NB: Usisahau kupigia kura andiko hili. Asanteni sana!

OMBAOMBA WZEE.jpg


OMBOMBA WATOTO.jpg
 
Karibuni ndugu zangu kwa maoni na mapendekezo ili kushibisha andiko hili na kuleta mapinduzi ya kweli ndani ya jamii yetu katika kupambana na janga hili la ombaomba!
 
Bandiko lako ni zuri na mapendekezo yako ni mazuri,nimekupa kura yangu sema hapo kwa viziwi kuingia mtaani kuuza bidhaa ni ngumu kutekelezeka mkuu, labda wapate mafunzo wafanye kazi labda za kutumia kompyuta ambazo hazihitaji mawasiliano na watu kila siku, nimependa topic yako mkuu
 
Bandiko lako ni zuri na mapendekezo yako ni mazuri,nimekupa kura yangu sema hapo kwa viziwi kuingia mtaani kuuza bidhaa ni ngumu kutekelezeka mkuu, labda wapate mafunzo wafanye kazi labda za kutumia kompyuta ambazo hazihitaji mawasiliano na watu kila siku, nimependa topic yako mkuu
Asante sana, Hata hivyo hilo linawezekana kabisa, unachofanya unampakilia kila mmoja mzigo ambao bei yake inafahamika, mfano unawapakilia vifuko vidogo vya mkaa vya vya TSH 500 au 1000 , usimchanganyie vya bei tofaut mpe vyote viwe vya bei tu. Kwa vile hata huko mtaani wanafahamu bei yake hilo halitampa shida kabisa na mzigo anautoa bila matatizo!
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom